Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi akutana na wabunge wa bunge la kumi

Ayatullah Khamenei awataka wabunge wazingatie uchumi

Ayatullah Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo asubuhi (Jumapili) amekutana na spika pamoja na wabunge wa Majlisi ya 10 ya Ushauri ya Kiislamu ambapo amesisitiza juu ya udharura wa kulindwa nguvu, hadhi na nafasi ya bunge kuwa kwenye kilele cha mambo yote nchini. Wakati huohuo ameashiria umuhimu wa wabunge kuzingatia misingi ya kubuni sheria nzuri kwenye Majlisi ambapo pia amegusia vipaumbele vinavyopasa kutiliwa maanani na wabunge hao katika nyanja za uchumi ngangari, utamaduni, siasa za ndani ya nchi, kieneo na kimataifa na kusema: ‘Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu inapasa kupuliza moyo wa utulivu nchini, kuwa ya kimapinduzi, na kuchukua hatua za kimapinduzi katika kubuni sheria, kutoa radiamali dhidi ya misimamo ya kiuadui na kibaguzi ya Marekani na kusimama imara mkabala na siasa za uistikbari. Mwanzoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu amewapongeza wabunge wa Majlisi ya kumi kwa kupata taufiki ya kuhudumu kwenye bunge na kusema kuwa nafasi ya bunge ni ya juu mno. Amesema: ‘Jukumu la kubuni sheria katika bunge ni muhimu sana na kwa hakika ni uwekaji reli kwa ajili ya serikali kutembea juu yake.’ Huku akisisitiza kuwa jukumu la bunge kusimamia mambo nchini haligongani na suala la kushirikiana na serikali, Ayatullah Khamenei amesema kuwa ushirikiano huu hauna maana ya bunge kupuuza haki zake na kwamba wabunge wanapasa kutumia uwezo wao wa kisheria kama vile kuhakiki na kuchunguza ili kufuatilia utekelezwaji sahihi wa sheria. Ameashiria kiapo cha wabunge cha kulinda misingi ya Uislamu na matunda ya Mapinduzi na kusema: ‘Hakika bunge linapasa kuwa katika kilele cha masuala yote, na kulindwa kwa nafasi na hadhi halisi ya bunge ni jukumu la wabunge.’
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa moja ya dhamana za kulindwa nafasi ya juu ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ni kwa majlisi hiyo yenyewe kujichunguza, na kuashiria suala la utungaji sheria nzuri na kufungamana nazo. Amesema: ‘Sheria zinapasa kuwa na ubora, imara, za pande zote, za wazi, zisizogongana na sheria nyingine, zilizo dhidi ya ufisadi, zinazofungamana na siasa (maamuzi) za mamlaka ya juu, zinazotokana na mitazamo ya kitaalamu ndani na nje ya serikali na zinazozingatia maslahi ya kitaifa badala ya maslahi ya kieneo.’ Ayatullaha Khamenei ameashiria mswada wa Mpango wa Sita (wa ustawi wa kiuchumi) kuwa moja ya ajenda zenye umuhimu mkubwa za bunge hili jipya na kuongeza: ‘Mazingira ya hivi sasa ya nchi ni mazingira maalumu. Kwa hivyo Mpango wa Sita unapaswa kuchunguzwa kwa makini na bila kufanyika ulegevu wala upuuzaji wowote na kisha kupasishwa.’ Pia ameashiria kuwepo kwa idadi kubwa ya wabunge wapya katika bunge la kumi na kusema: ‘Mimi ninalichukulia jambo hili kuwa fursa kwa sababu kuwepo kwa wabunge hawa wapya kando ya wabunge walio na uzoefu kunaandaa uwanja wa kuwepo bunge lililo na uchangamfu na motisha na ambalo litanufaika na wabunge walio na uzoefu.’ Kiongozi Muadhamu kisha amezungumzia suala la vipaumbele vya bunge la kumi na kusisitiza kwamba uchumi ni suala la msingi. Amesema wabunge wana taathira kubwa katika kutekelezwa kwa uchumi ngangari kwa sababu wanaweza kuweka hatua za uchumi ngangari za serikali kwenye njia ya uchumi ngangari na wakati huohuo kuiwajibisha serikali kuhusu suala hilo. Huku akiashiria juhudi za adui za kutumia chombo cha uchumi kwa lengo la kutoa pigo dhidi ya Mfumo wa Kiislamu, Ayatullah Khamenei amesema kwamba hata kama baadhi ya hatua zisizo za kiuzoefu zimechukuliwa, na baadhi ya misimamo na maneno yasiyo ya busara kumshajiisha adui kutumia chombo cha vikwazo, lakini matatizo ya uchumi na hasa kuhusiana na mdororo na nafasi za ajira yanapaswa kutatuliwa na kwamba maneno matupu hayana faida yoyote. Amesema kutatuliwa suala la mdororo na ajira kupitia uimarishwaji wa uzalishaji wa ndani ni vipaumbele vya msingi na muhimu mno katika sekta ya uchumi na kuongeza kuwa aibu unayoipata Mfumo kuhusiana na suala la ajira ni kubwa zaidi kuliko aibu anayoipta kijana asiyekuwa na kazi mbele ya familia yake. Hivyo amesema juhudi kubwa zinapasa kufanyika ili kutatua suala hili. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kupambana na magendo ya bidhaa ni kipaumbele kingine cha Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu kuhusu suala la uchumi na kuongeza: ‘Magendo ni mfano wa kisu kinachodungwa Mfumo wa Kiislamu kutokea mgongoni ambapo kupambana nayo pia si jambo rahisi lakini serikali inapasa kupambana vilivyo na tatizo hilo la kikorofi nayo Mjlisi kuiunga mkono katika hilo.’ Katika kuendelea na hotuba yake Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia suala la utamaduni kama mojawapo ya vipaumbele vya ajenda ya Majlisi ya kumi na kusema; ‘Suala la uchumi ni kipaumbele cha haraka na cha hivi sasa cha nchi lakini utamaduni katika kipindi cha muda mrefu ni muhimu zaidi kuliko hata uchumi.’ Ameongeza kuwa kuna aina fulani ya upuuzaji na kutojali kunakoonekana katika vyombo vya utamaduni kuhusiana na suala la utamaduni kwa sababu kuna uzembe ambao umefanyika katika uzalishaji wa bidhaa za utamaduni zenye manufaa na kuzuia uzalishaji wa bidhaa hizo zilizo na madhara.
Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa baadhi ya wakati sisitizo linalowekewa bidhaa zenye madhara zisizo za kiutamaduni kama vile baadhi ya vyakula ni mkubwa zaidi kuliko sisitizo linalowekewa bidhaa zenye madhara za kiutamaduni katika hali ambayo madhara ya bidhaa hizo kwa wananchi ni hatari na makubwa zaidi. Amesema baadhi ya wakati hakuna hatua zozote zinazochukuliwa kuzuia uzalishaji au uingizwaji ndani ya nchi wa bidhaa zenye madhara za utamaduni kutokana na hofu ya kutuhumiwa kuzuia mkondo wa uhuru wa habari. Huku akiashiria hatua kali zinazochukuliwa katika nchi za Ulaya na Marekani katika kudhibiti habari, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: ‘Sisi tonahofia kukabiliwa na tuhuma zao zisizo na msingi kuhusiana na suala la kuzuia uhuru wa habari katika hali ambayo udhibiti wetu haufikii hata moja ya kumi ya misimamo yao mikali kuhusu suala hilo.’ Nasaha nyingine ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa wabunge wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ilikuwa ni, ‘kuwa wanamapinduzi, kubakia wanamapinduzi na kutenda kazi kimapinduzi.’ Ayatullah Khamanei amesema Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ni taasisi ya kimapinduzi iliyotokana na mapinduzi na kuwasisitizia wabunge kwa kuwaambia: ‘Tekelezeni mambo kimapinduzi katika kubuni sheria, utekelezaji wa majukumu yenu ya kibunge na katika matamshi na misimamo yenu.’ Amesema misimamo mikuu ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu kuhusu masuala makuu ya nchi ni muhimu sana na huku akipongeza rekodi nzuri ya utendaji wa bunge la tisa kuhusiana na suala hilo amesema, bunge linapasa kuchukua msimamo thabiti na wa wazi katika kukabiliana na makundi ya upinzani wa kisiasa dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria tabia ya uadui wa moja kwa moja ya serikali na kongresi ya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema: ‘Katika kukabiliana na ujeuri wa maadui tunapasa kuingia kwenye medani na kufunga midomo yao kwa jibu kali. Hii ni kwa sababu katika uwanja wa siasa adui huzingatia sana radiamali ya upande wa pili na anapohisi kuwa upande huo ni wa kuzembea na kuwa uko tayari kurudi nyuma, huwa halegezi msimamo wake bali hutoa madai ya ziada.’ Kuhusu jambo hilo Ayatullah Khamanei ameashiria kadhia ya mazungumzo ya nyuklia na kusema kwamba Wamarekani ikiwa ni pamoja na serikali, kongresi na wagombea wa kiti cha urais wa nchi hiyo wote wanendelea kutoa madai ya ziada na vitisho. Amesema misimamo na vitisho vyao hivyo katika mazingira ya hivi sasa ni sawa na kama ilivyokuwa kabla ya kufikiwa mapatano ya nyuklia na kwamba haipasi kunyamazia ujeuri huo. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amefafanua njama zinazofanywa na adui ndani ya nchi kwa kuzipa nguvu nyufa za ndani na kuongeza: ‘Adui anafanya juhudi za kuhuisha nyufa za kikabila, kiitikadi na kimirengo na kuzibadilisha kuwa zilzala. Kwa msingi huo, wabunge wanapasa kufanya juhudi za kufanya njama hiyo isifikie natija.’ Ayatullah Khamenei amesema: ‘Mwakilishi wa bunge anaweza kutoa maoni yake kwa msingi wa mtazamo wake wa kisiasa na kutoa mtazamo au kukosoa suala fulani, lakini kwa vyovyote vile hapasi kuwa kama ilivyokuwa katika baadhi ya vipindi vilivyopita vya bunge ambapo kulizuka hitilafu, msuguano wa maneno, kushikana mashati na mvutano.’ Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kudhihiri mvutano bungeni huenea hadi kwenye jamii ambapo huzua mvutano na athari hasi za kisaikolojia kwenye jamii. Amesema: ‘Utulivu unapasa kutawala bungeni ambapo bila shaka utulivu huo pia utaakisiwa kwenye jamii.’ Ayatullah Khamenei kisha amefafanua njama za adui katika upeo wa eneo na kusema kwamba adui ana mipango maalumu kwa ajili ya eneo muhimu na nyeti la magharibi mwa Asia na kwamba ana lengo la kuzima na kuzuia siasa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambazo ni kikwazo cha kuthibiti mipango hiyo. Huku akiashiria baadhi ya sifa maalumu za eneo la magharibi mwa Asia, kiongozi Muadhamu amesema kwamba, kuwepo Uislamu na Waislamu, utajiri mkubwa wa maliasili na njia za baharini na utawala wa Kizayuni kumelifanya eneo hili kuwa na umuhimu mkubwa kwa adui na kwamba njama yao kwa ajili ya eneo hili ni lile lile jambo walilolitaja miaka kadhaa iliyopita kwa anwani ya ‘Mashariki ya Kati Mpya’ na ‘Mashariki ya Kati Kubwa.’ Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria kutothibiti kwa njama za Marekani katika eneo zikiwemo nchi za Iraq, Syria, Lebanon na Palestina kutokana na kusimama imara Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusisitiza: ‘Inapasa kusimama imara mbele ya siasa hizo za kibeberu na kufichua uso wa uistikbari.’ Ameashiria udharura wa kujiepusha kuchukua misimamo na tabia inayopendelewa na adui na kusisitiza: ‘Bainisheni hakika na ukweli wa uistikbari na mfumo wa ubeberu katika misimamo na matamshi yenu na mchunge maneno na vitendo vyenu visije vikaisaidia Marekani na utawala wa Kizayuni.’ Mwishoni mwa hotuba yake Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kwamba adui katika ngazi tatu za kimataifa, kieneo na ndani ya nchi ana mipango (njama) kwa ajili ya Jamhuri ya Kiislamu ambapo katika ngazi ya kimataifa anaendeleza tuhuma, kuondoa vizuizi vinavyozuia mipango yake katika ngazi ya kieneo na kuhuisha nyufa katika ngazi ya ndani ya nchi. Amesema kwa kuzingatia masuala hayo, mihimili na viongozi wote na hasa wabunge wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu wanapasa kuwa macho mbele ya mipango (njama) hii. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu vilevile ameashiria kukaribia kwa mwezi wa ugeni kwa Mwenyezi Mungu na kusema kuwa mwezi wa Ramadhani ni fursa nzuri kwa ajili ya kuomba dua, kujijenga kimaanawi na kuteda mambo mema. Amesema: ‘Fursa ya uwakilishi bungeni pia ambayo mmepewa nyinyi wapendwa ni fursa na nafasi inayopita kwa haraka ambapo inapasa kuthaminiwa na mumuombe msaada Mwenyezi Mungu katika utekelezaji wa majukumu yenu ya kisheria.’
Kabla ya hotubaya Kiongozi Muadhamu, Bwana Larijani, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu alimuenzi hayati Imam Khomeini na kubainisha vipaumbele vya mipango ya Majlisi ya kumi ya Ushauri ya Kiislamu. Amesema: ‘Tuna majukumu mazito katika kulinda ngome ya Mapinduzi, na kile ambacho kinaweza kuelekeza mazingira yaliyojaa mvutano ya eneo kwenye utulivu, kudhamini usalama wa kudumu na kuthabiti usalama wa Iran ni kuwa na mtazamo wa kimapinduzi na kuutekeleza.’ Amesema kuwa ya kimapinduzi (majlisi) ni nukta ya kitivo ya Majlisi ya Ushauri ya kiislamu na kwamba majlisi hii ya kumi itafuatilia kwa karibu matukio ya kieneo kwa jicho la usalama wa hali ya juu. Huku akisema kuwa uchochezi wa hivi karibuni wa Marekani baada ya kufikiwa mapatano ya nyuklia ni ishara ya wazi kwamba uistikbari una lengo la kutoa pigo dhidi ya maslahi ya taifa la Iran, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu amesisitiza kwamba wawakilishi wa taifa la Iran wanalichukulia kuwa jukumu lao suala la kulifanya bunge kuwa ngome ya kulinda haki za taifa dhidi ya wageni. Bwana Larijani amesema kwamba ushirikiano wa mihilimi mitatu ya dola na pia wananchi na serikali katika mazingira ya hivi sasa ni jambo la dharura na kuongeza kuwa hatua za haraka na za makini zinapasa kuchukuliwa ili kuvuka mdororo wa uchumi. Amesema bunge litalipa kipaumbele cha kwanza na kuzingatia sana suala la kuthibiti uchumi ngangari na uimarishwaji wa uzalishaji bidhaa katika kamisheni zake zote na kufuatilia kwa karibu mipango na miswada ya lazima pamoja na kusimamia juhudi za kuthibiti uchumi ngangari nchini.

 

700 /