Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi katika marasimu ya Chuo cha Imam Hussein (as)

Jukumu la wote katika kukabiliana na upenyaji ni ubainishaji

Sambamba na kuwadia tarehe 3 Khordad sawa na tarehe 23 Mei ambayo ni tarehe ya kukumbukwa operesheni ya kifahari ya Beitul Muqaddas ambayo ilipelekea kukombolewa kwa mji wa Khorramshahr, leo asubuhi (Jumatatu) sherehe za kuhitimu masomo ya makadeti wa Chuo Kikuu cha kijeshi cha Imam Hussein (as) zimefanyika katika uwanja wa chuo kikuu hicho na kuhudhuriwa na Ayatullah Ai Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi yote ya Iran. Mara tu baada ya kuingia kwenye uwanja wa chuo hicho, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyazuru makaburi ya mashihidi wasiojulikana utambulisho wao na kuwasomea Fatiha. Pia amewaenzi mashahidi wa vita vya kujitetea kutakatifu vya Iraq dhidi ya Iran na kumwomba Mwenyezi Mungu awapandishe daraja ya kimaanawi. Kiongozi Muadhamu kisha amekagua gwaride la vikosi vya wanajeshi waliokuwa wamejipanga vyema uwanjani. Ayatullah Khamanei pia amekutana na majeruhi na mashujaa wa vita wakiwemo majeruhi wa vita vya kujitolea vya kulinda haramu tukufu za kidini huko Syria waliokuwa uwanjani hapo pamoja na baadhi ya familia zao.
Akizungumza katika sherehe hizo, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa hotuba muhimu ambapo amebainisha mantiki ya Qur’ani Tukufu na ya Uislamu na kusema kuwa maana ya Jihadi kubwa ni kusimama imara na kutofuata mrengo wa Uistikbari na mifungamano yake katika Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Huku akiashiria juhudi na mipango mikubwa inayofanywa na kambi ya uistikbari kwa madhumuni ya kupenya na kuubadilisha utambulisho wa Mfumo wa Kiislamu, Ayatullah Khamenei amesema kuwa jukumu muhimu zaidi la hivi sasa la vyuo vikuu na vya kidini, watu na vijana waumini na wa kimapinduzi na vilevile  Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ni kuchukua hatua za busara na erevu kwa ajili ya kubainisha na kufafanua kina na undani wa nara za Mapinduzi ya Kiislamu na kujiepusha na hatua za juu juu tu, kuandaa watu wanaofaa kwa ajili ya mustakbali na kukusanya kielimu uzoefu mkubwa uliorundikana na wa kushangaza wa Mapinduziya Kiislamu katika kipindi cha miaka 38 iliyopita. Ayatullah Khamanei ametoa mkono wa fanaka na pongezi kwa mnasaba wa kuzaliwa Mwakozi wa Ulimwengu, Imam wa Zana Imam Mahadi (AF) na maadhimisho ya tarehe 3 Khordad (tarehe 23 Mei) ambayo ni siku ya kukombolewa mji wa Khorramshahr na kusema kuwa siku hiyo ni moja ya siku muhimu ambazo haziwezi kusahaulika katika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu na kuitaja kuwa nembo ya nguvu za Mwenyezi Mungu. Amesema kuna mambo mengi ya kina kuhusiana na operesheni ya kuukomboa mji huo na operesheni nyinginezo za kujitetea kutakatifu ambayo huenda watu wengi na hasa kizazi cha vijana, hawayajui na kwa msingi huo ameshauri vitabu vinavyohusiana na operesheni hizo bila shaka vipate kusomwa. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha moja ya nukta muhimu katika operesheni  ya ukombozi wa mji wa Khorramshahr kwa msaada na nguvu za Mwenyezi Mungu na kusema: ‘Imam mpendwa, mtu huyo wa Mwenyezi Mungu na hakimu halisi wa Allah alisema kwamba Mwenyezi Mungu ndiye aliyeukomboa mji wa Khorramshahr.’ Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: ‘Katika mantiki hiyo, wakati ambapo kila juhudi na jitihada zimefanywa na uwezo wote kuletwa kwenye medani na hatimaye kumtegemea Mwenyezi Mungu, mkono Wake, ambao ni mfano wa himaya madhubuti na imara, utafika na matokeo yake kuwa ukombozi wa mji wa Khorramshahr ambao ulikuwa umetekwa na adui aliyekuwa amejizatiti vilivyo na kwa pande zote kwa suhula na zana.’ Kiongozi Muadhamu amesema kwa mantiki hii dunia nzima inaweza kukombolewa kutoka kwenye udhibiti wa uistikbari, Palestina kukombolewa na kutoachwa hata taifa moja linalonyongeshwa duniani. Amesisitiza kwamba kila taifa linalokuwa na mantiki hii na kufanya juhudi zake zote huku likimtegemea Mwenyezi Mungu bila shaka halitatishwa na nguvu ya kijeshi, kifedha, kipopagada wala kisiasa ya madola makubwa duniani. Huku akiashiria kushindwa kwa juhudi za kambi ya uistikbari katika kipindi cha miaka 38 iliyopita kwa ajili ya kuuangusha Mfumo wa Kiislamu licha ya kutumia vyombo na njama tofauti, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa huo ni mfano wa wazi wa kufuatwa mantiki hii ya kufanya jitihada na kusimama imara huku Mwenyezi Mungu akitegemewa na kusisitiza: ‘Taifa la Iran lingali lipo kwenye medani na kuna vijana wengi sana ambao wako tayari kutoa roho zao kwa ajili ya Mapinduzi, na hili ndilo jambo litakalovutia nguvu ya Mwenyezi Mungu.’ Kiongozi Muadhamu ameita aina hii ya makabiliano na kambi ya uistikbari kuwa ni ‘vita visivyo na uwiano’ na kuongeza kwamba katika vita hivyo visivyo na uwiano na kwa maneno mengine, mlingano sawa, pande zote mbili huwa hazina uwezo wa kijeshi wala chanzo cha nguvu kama ulivyonao upande wa pili. Amesema chanzo cha nguvu za Mfumo wa Kiislamu ni kutegemea na kutawakali kwa nguvu za Mwenyezi Mungu, kuamini ushindi na nguvu za irada ya watu walio na imani ya sawa. Huku akisisitiza kuwa vita visivyo na mlingano ni vita vya irada, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, iwapo katika medani ya vita hivi irada ya upande mmoja itadhoofika bila shaka upande huo utashindwa, na kwa hivyo uangalifu mkubwa unapasa kufanyika ili adui asije akaathiri irada zetu madhubuti kupitia tashwishi na propaganda zake. Kiongozi Muadhamu amesema vita hivyo ni vikubwa kuliko vita vya kijeshi na kuwa ni aina moja ya Jihadi na kuongeza: ‘Hii leo kuna uwezekano mdogo sana wa kutokea vita vya kawaida (vya kutumia silaha) lakini Jihadi ingalipo na Jihadi hii ambayo ina mantiki ya Qur’ani na Uislamu ni Jihadi kubwa ambayo ina maana ya kusimama imara, kupambana na kutowafuata makafiri na washirikina.’ Ayatullah Khamenei amesisitiza kwamba Jihadi kubwa pia inadhihirika katika nyanja za kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kisanii na kuongeza kuwa badala ya kufuata kambi ya makafiri na washirikina katika nyanja hizi, mpango wa utendaji kazi wa Uislamu na Qur’ani ndio unaopasa kufuatwa. Amesema suala muhimu lililopo kati ya Jamhuri ya Kiislamu na kambi ya uistikari ni suala la ‘ufuataji’ na kuongeza kuwa wao hii leo wanatumia kila chombo, mashinikizo na juhudi za kiutamaduni, kiuchumi, kisiasa na kipropaganda na wakati huohuo kuwatumia vibaraka wao wahaini ili kuupigisha magoti Mfumo wa Kiislamu na kuulazimisha kuwafuata lakini jambo linaloufanya uitsikbari ulichukie sana taifa la Iran ni kwamba wananchi wa nchi hii kwa kuwa ni Waislamu wanaozingatia dini yao hawako tayari kuufuata uistikbari huo.
Kongozi Muadhamu amesema kuwa madai ya masuala kama vile nishati ya nyuklia, nguvu ya makombora ya Iran na haki za binadamu ni visingizio tu vinavyotumiwa na maadui dhidi ya Iran na kusisitiza kuwa sababu kuu ya uadui huo wote na visingizio ni kutoufuata uistikbari, kwa sababu kama taifa la Iran lingekuwa tayari kuufuata, bila shaka madola hayo ya kiistikbari yangefumbia macho nguvu za makombora ya Iran na nishati yake ya nyuklia na wala suala la haki za binadamu halingezungumzwa kabisa. Ayatullah Khamenei ameashiria nukta moja muhimu kuhusiana na suala la makombora na kusisitiza: ‘Hivi Karibuni wamezua vurugu nyingi kuhusiana na nguvu ya makombora ya Iran lakini waelewe kwamba makelele hayo hayatakuwa na athari yoyote na wala hawawezi kufanya lolote.’
Katika kuendelea kubainisha sababu hasa ya kudumishwa uadui wa uistikbari dhidi ya Mfumo wa Kiislamu, Kiongozi Muadhamu amesema: ‘Wamarekani wanafanya juhudi kubwa za kutozungumzia sababu halisi ya uadui huo lakini wakati mwingine huteleza na kufichua sababu hiyo. Kama ambavyo hivi majuzi afisa mmoja wa Marekani baada ya kukariri tuhuma za kila siku dhidi ya Iran aliashiria bila kutarajia suala la ‘aidiolojia’ yaani fikra ya Kiislamu, ambayo inalifanya taifa la Iran lisikubali kuwa chini ya udhibiti wa kambi ya uistikbari.’
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kusimama imara, kutomfuata adui na kulinda utambulisho wa kimapinduzi na Kiislamu ni masuala muhimu yanayoupa nguvu Mfumo wa Kiislamu na taifa la Iran na kuongeza kuwa Marekani na madola mengine yenye nguvu duniani yanakerwa sana na maudhui hiyo. Amesema pamoja na hayo lakini madola hayo hayana budi na ndipo yamekuwa yakifanya juhudi kubwa za kujaribu kupenya na kudhibiti vituo vya uchukuaji maamuzi na ubunifu wa maamuzi nchini lakini yameshindwa kabisa kufikia lengo hilo na kwamba kwa taufiki na uwezo wa Mwenyezi Mungu hayatafanikiwa kufikia kengo hilo. Kiongizo Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema jukumu la msingi la Jeshi la Walinda Mapinduzi ni kuchunga na kulinda Mapinduzi na kwa msingi huo Jihadi kubwa, inapasa kuwa ndio msingi wa mipango ya jeshi hilo la walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Ameashiria wimbi la hujuma na tuhuma nyingi zinazoelekezwa kwa jeshi hilo na kusema sababu kuu ya chuki hiyo ni kusimama imara jeshi hilo katika njia ya Mapinduzi na kulinda muelekeo na moyo wa kimapinduzi na Kiislamu. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amewahutubu vijana nchini pamoja na wanachuo waliohudhuria sherehe hizo na kusema: ‘Mustakbali wa Mapinduzi ni wenu na ni nyinyi ndio mnaopasa kuilinda historia hii kwa utukufu na mfahamu kwamba kuna Khorramshahr nyingine zinazokuja huko mbele. Hata hivyo sio katika medani ya vita vya kijeshi bali ni katika medani ambayo haina uharibifu kama ule unaosababishwa na vita vya kijeshi, na kinyume chake ina maendeleo pia, lakini vita hivyo ni vugumu zaidi kuliko vita vya kijeshi.’ Kuhusu suala hilo Ayatullah Khamanei amefafanua pande tofauti za Jihadi kubwa katika nyanja za kiuchumi, kiutamaduni na kijamii na na kusema: ‘Sisitizo la kutekelezwa uchumi ngangari ni sekta ya kiuchumi ya jihadi hiyo, sisitizo juu ya suala hili kuwa vijana waumini,wa Kihizbullah na kimapinduzi wanapasa kujituma katika kudumisha kwa nguvu zao zote kazi za kiutamaduni na vyombo vya utamaduni pia kuelekea upande huo, ni sekta ya utamaduni ya jihadi hiyo, na sisitizo la kutumiwa uwezo na vipawa (talanta) vyote nchini katika njia ya ustawi ni sekta muhimu ya kijamii ya jihadi hii kubwa.’ Huku akiashiria tuhuma zisizo na msingi za baadhi ya watu wanaopinga harakati hii na madai yao kwamba kutumiwa uwezo wa ndani kuna maana ya kukata uhusiano na dunia, Ayatullah Khamanei amesema: ‘Sisi hatuamini hata kidogo kukatwa uhusiano na dunia na kujibana kwa ndani, bali tunasema tuwe na uhusiano wa kisiasa na mabadilishano ya kiuchumi lakini msisahau utambulisho na shakhsia yenu ya asili. Mnapotaka kuzungumza au kutia saini mikataba, yafanyeni hayo kama wawakilishi wa Iran ya Kiislamu na Uislamu na kuketi kwenye meza ya mikataba na kufanya mambo kwa uangalifu.’ Huku akisisitiza kwamba Jihadi kubwa inahitajia umakini na ikhlasi, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria juhudi na matumaini ya adui kwa ajili ya kupenya katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema: ‘Hii leo adui amekata tamaa ya kutoa pigo kubwa dhidi ya Mfumo wa Kiislamu lakini anatumia vyombo tofauti na visivyofahamika kirahisi kwa lengo la kupenya na kubadilisha utambulisho wa vijana wa Iran ili wawe na utambulisho unaoupendelewa na Marekani na uistikbari. Hii ni kwa sababu iwapo hili litathibiti basi hatakabiliwa na matatizo wala kutoa gharama katika kufikia malengo na kutekeleza njama zake nchini.’ Ayatullah Khamanei amesema kuwa ufahamu uliojaa makosa na kasoro wa Marekani na kambi ya uistikbari kuhusu taifa la Iran ndicho chanzo cha mahesabu yao yaliyojaa makosa na kuongeza: ‘Bila shaka wao hawajakata tama kuhusu upenyeji nchini na kwa msinggi huo jukumu kubwa liko kwenye mabega ya wale wote wanaojali taifa na Mfumo wa Kiislamu likiwemo Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu.’ Huku akisisitiza kwamba jeshi hilo daima linapasa kulinda utayarifu wake wa kijeshi katika hali bora zaidi ya ubunifu, Kiongozi Muadhamu amesema: ‘Ama wadhifa wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi (Sepah) sio vita tu katika medani ya kijeshi bali katika hali ya hivi sasa moja ya majukumu muhimu ya wale wote wanaojali na manaopenda Mapinduzi likiwemo jeshi la Sepah, ni kuweka wazi mambo na kuzifahamisha fikra undani na kina cha hakika na nara za Mapinduzi.’ Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza sana juu ya watu wote kuzingatia suala la ubainishaji, ufafanuzi na undani wa kazi na kuongeza: ‘Ubainishaji wa nara za Mapinduzi na ufafanuzi wa undani wa nara hizo ni miongoni mwa mambo ya lazima katika kuthibiti Jihadi kubwa kwa sababu nara za Mapinduzi ni mfano wa alama na viasharia vinavyoelekeza kwenye njia sahihi ya Mapinduzi na njia iliyonyooka.’ Ayatullah Khamenei amesema ushabiki na kubainisha hisia ni muhimu katika kufuatilia hakika na nara za Mapinduzi lakini kwamba jambo hilo pekee halitoshi na kusisitiza: ‘Iwapo jambo hilo litabainishwa kwa mtazamo wa kina na wa ndani bila shaka imani na itikadi ya watu kuhusiana na nara hizo haitatengana nao na itaendelea kuwa nao daima.’
Kiongozi Muadhamu amesema kwamba sababu kuu ya baadhi ya watu kubadilika kwa digrii 180 katika vipindi tofauti vya Mapinduzi ni kutokuwa kwao na undani na kuyatazama mambo kijuu juu tu na kuongeza kwamba, masuala ya kimsingi na nara za Kiislamu zinapaswa kutazamwa kwa fikra ya kina na kunufaika na miongozo ya walimu na wahadhiri wema. Kiongozi wa Mapinduzi amesema mafunzo na malezi ya nguvukazi nzuri kwa ajili ya baadaye na ukusanyaji wa kielimu wa uzoefu mkubwa na uliorundikana wa miaka 38 ya Mapinduzi ya Kiislamu katika njia panda na za mteremko za kushangaza, ni mambo mengine ya lazima katika Jihadi kubwa na kuongeza kuwa vituo vyote vya elimu ya juu ikiwa ni pamoja na vyuo vikuu na vya kidini, na hasa Chuo Kikuu cha kijeshi cha Imam Hussein (as) vina majukumu kuhusu suala hilo. Huku akibainisha udharura wa kuchukuliwa hatua za kina, Ayatullah Khamenei amekosoa baadhi ya hatua zisizo za kimantiki na kusema: ‘Wakati mwingine baadhi ya vijana ambao huenda ni wema na pia waumini, kutokana tu na hoja ya kuwa wanampinga mtu fulani au kikao fulani cha hotuba, huamua kuzua makelele na fujo na mwishowe kukivuruga kikao hicho. Hii ni katika hali ambayo tokea zamani mimi sijawahi kuafikiana na wala siafikiani na vitendo hivi ambavyo havina faida yoyote. Ninaamini kwamba faida iko kwenye ubainishaji na kazi bora na erevu.’ Amewataka vijana waumini na wa kimapinduzi kuwa waangalifu na kusema: ‘Bila shaka wakati mwingine baadhi ya watu huamua kufanya vitendo hivi visivyo sahihi kwa malengo maalumu na kisha kujaribu kuonyesha kuwa vimefanywa na watu wa Kihizbullah na waumini. Kwa hivyo uangalifu mkubwa unahitajika.’ Kiongozi Muadhamu amesema kuwa mwamko wa kina na hatua sahihi na erevu ni katika majukumu ya msingi na kusisitiza kwamba hatua zote hizi zitakuwa na taathira iwapo tu Mwenyezi Mungu atategemewa na kutawasaliwa.
Mwishoni mwa hotuba yake Ayatullah Khamenei amesema kuwa sharti la kuimarisha uhusiano wa kiroho na Mwenyezi Mungu ni kufarijika zaidi na Qur’ani na kutafakari aya za Mwenyezi Mungu, kuzingatia swala na kuitekeleza kwa unyenyekevu na mazingatio ya moyo na kunufaika na fursa za miezi ya Shaaban na Ramadhan.
Katika sherehe hizo Brigedia Jenerali Mohammad-Ali Ja’fari, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, amesema kuwa sababu kuu ya nguvu ya Mfumo wa Kiislamu ni kusimama imara mbele ya matakwa ya ziada na chokochoko za Marekani. Amesema ili kuzima njama za maadui, jeshi hilo linazingatia stratijia kama vile kuzalisha nguvu za kulinda Mapinduzi, kutazama upya muundo na njia ya Mapinduzi ya Kiislamu pamoja na kutekeleza miongozo na maagizo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi katika ngazi za operesheni. Kamanda Mkuu wa  Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria vita vya niaba vya Marekani vinavyotekelezwa na tawala vibaraka wake katika eneo na kusema: ‘Mwamko na mapambano ya Kiislamu yangali yanaendelea na wala juhudi za mfumo wa ubeberu haziwezi kuzuia kuendelea kwa Mapinduzi ya Kiislamu na mwamko wa Kiislamu.’ Brigedia Jenerali Mohammad-Ali Ja’fari amesema kwamba hii leo walinzi vijana wa jeshi la Sepah wako tayari kuingia kwenye medani ngumu na tata ya vita katika siku zijazo kwa ajili ya kutetea kwa ushujaa na nguvu zao zote Mapinduzi na utukufu wa Mfumo wa Kiislamu. Naibu Admeri Morteza Saffari, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Imam Hussein (as) pia ametoa ripoti kuhusu hatua na mipingo inayotekelezwa kielimu, kiutamaduni na pia mafunzo na uimarishwaji wa nguvu za kivita katika chuo kikuu hicho. Katika sherehe hizo, idadi ya makamanda, wakurugenzi, watafiti, wabunifu, na wawakilishi wa wahitimu na wanachuo bora wa Chuo Kikuu cha Imam Hussein (as) walipokea zawadi zao kutoka kwa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Iran. Mwakilishi wa wanachuo wa Chuo Kikuu cha Imam Hussein (as) pia alipata fahari ya kupewa mapurendi.
Miongozi mwa ratiba zilizotekelezwa na wanachuo wa Chuo Kikuu cha Imam Hussein (as) katika sherehe za leo kwa ajili ya kuthibitisha kwamba wako tayari kulinda Mapinduzi ya Kiislamu ni ratiba ya ‘Ibadiya as-Swalihun.’ Katika sherehe hizo vikosi vilivyokuwa kwenye medani vilipiga gwaride mbele ya Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Iran.

 

700 /