Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi katika kikao cha Qur’ani

Nguvu na heshima vinapatika katika Qur'ani Tukufu

Leo alasiri (Jumanne 2016/06/07) ikiwa ni siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, mwezi wa kuteremka kitabu kitakatifu cha Qur’ani, kikao cha kufarijika na Qur’ani kimefanyika kwa muda wa zaidi ya masaa matatu ambapo Ayatullah Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amehudhuria. Katika kikao hicho cha nuru kilichojaa uturi na umanawi wa Qur’ani, mahafidh, makarii na maustadhi wa Qur’ani wanane kutoka pembe zote za nchi walisoma baadhi ya aya za kitabu hicho kitakatifu na pia makundi ya vijana kuimba kasida za kusifu na kumuhimidi Mwenyezi Mungu. Katika marasimu hayo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema kuwa lafudhi na maneno ya kuvitia ya Qur’ani Tukufu ni mujiza na mwanya unaovutia katika mafundisho aali na ya kina. Huku akisisitiza umuhimu wa kuenezwa vikao kama hivyo vya Qur’ani katika nchi nzima, Kiongozi Muadhamu ameashiria suala la dunia nzima kuhitajia sana mafundisho ya kitabu hiki kitakatifu katika mazingira ya hivi sasa na kusema: ‘Iwapo wanadamu watabainishiwa mafundisho ya kina ya Qur’ani kwa lugha wanayoifahamu na ya kisasa, bila shaka yatakuwa na taathira kubwa na hivyo kuwaandalia uwanja wa kupata maendeleo ya kweli. Hii ni kwa sababu heshima, nguvu, maisha bora ya kimaada, ustawi wa kimaanawi, kuimarishwa fikra na itikadi, uchangamfu na utulivu wa kiroho, yote haya yanapatikana katika kutekelezwa mafundisho ya Qur’ani.’
Mwanzoni mwa hotuba yake hiyo fupi, Ayatullah Khamenei alikumbuka na kuwaenzi makarii wa Qur’ani na Mahujaji waliopoteza maisha yao mwaka uliopita katika maafa ya Mina huko Saudi Arabia. Ameelezea kufurahishwa kwake na kuimarika na kupanuka kwa duara la wasomaji Qur’ani na hasa tabaka la vijana nchini na kuongeza kwamba hata kama lafudhi na maneno ya Qur’ani ni ya kuvutia lakini lengo la maneno hayo ya kuvutia ni kufunguliwa mwanya wa kufikiwa anga iliyojaa baraka na ya kuvutia ya mafundisho ya Qur’ani. Kiongozi Muadhamu amesisitiza: ‘Ikiwa mafundisho hayo ya kina ya Qur’ani na taathira zake yatazingatiwa kwa kina, bila shaka yatafahamika na kueleweka vyema zaidi katika dunia ya leo yenye utata, tufani na iliyojaa matatizo.’
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa kiwango cha sasa cha kuenea na kuimarika vikao vya Qur’ani Tukufu nchini hakiwezi kulinganishwa kwa vyovyote vile na kiwango kilichokuwepo kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na hata miaka ya mwanzoni mwa mapinduzi hayo na kuongeza kuwa, moja ya mambo ya lazima yanayopasa kutekelezwa nchini ni kueneza vikao vya kusoma na kusikiliza kwa makini Qur’ani Tukufu. Ayatullah Khamenei ameongeza: ‘Kama ambavyo vikao vya maombolezo au vya furaha vya Ahlul Beit (as) hufanyika, vikao vya Qur’ani pia vinapasa kuenea ili kasi ya kufahamika mafundisho ya Qur’ani pia iongezeke.’
Huku akiashiria pengo la utambulisho wa kifikra na kiimani lililopo katika dunia ya leo na mahitajio ya wanadamu kwa mafundisho ya Qur’ani. Ayatullah Khamenei amesema kwamba tunapasa kuimarisha misingi ya imani zetu na kujifunza lugha za kufikisha ujumbe wa Qur’ani kwa wanadamu ili tupate kuufikishia ulimwengu ujumbe huu.’ Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kwamba iwapo ujumbe huu utafikishwa kwa njia sahihi, bila shaka Qur’ani Tukufu  itakuwa ndiyo yenye taathira kuu ulimwenguni na wala madola makubwa na silaha zao pamoja na utawala wa Kizayuni, hayatakuwa na uwezo wa kufanya upuuzi wowote.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa utulivu wa kiroho na kidini ni moja ya baraka za kufahamu vyema ujumbe wa mafundisho ya Qur’ani na kumalizia kwa kusema kuwa utulivu huo bila shaka utaandaa uwanja wa mwanadamu kuimarisha imani yake kwa Mwenyezi Mungu na nguvu Zake.

 

700 /