Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Maadui wanapanga njama za kuharibu uwezo wa Jamhuri ya Kiislamu

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei alasiri ya leo amehutubia hadhara ya viongozi wa mihimili mitatu ya dola, maafisa na wafanyakazi wa Mfumo wa Kiislamu, wakurugenzi wa taasisi mbalimbali na wanaharakati wa masuala ya siasa, jamii na utamaduni akisema kuwa, kuzidishwa uwezo wa nchi kutalinda na kulipa nguvu taifa na nchi. Ameongeza kuwa: Kuweka mipango na kuainisha vipaumbele katika kutatua matatizo mawili muhimu ya mdororo wa kiuchumi na ukosefu wa kazi kutazidisha kasi ya harakati ya kuelekea kwenye uchumi ngangari.
Mwanzoni mwa hotuba yake, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amewausia viongozi wa Mfumo wa Kiislamu kutumia vyema anga ya kiroho na kimaanawi ya mwezi mtukufu wa Ramadhani na kuashiria baadhi ya dua zinazosomwa katika mwezi huu. Amesema kuwa: Katika baadhi ya dua za mwezi wa Ramadhani kumetolewa ombi la kuokolewa na madhambi ambayo iwapo viongozi wa nchi watakumbwa nayo (Mwenyezi Mungu atuepushe na jambo hilo) basi madhara yake yataikumba jamii na nchi nzima.
Ayatullah Khamenei amesema, kutokuwa na ari, kughafilika, kuwa na roho ya kutu, kutojali na ghururi ni miongoni mwa madhambi hayo. Ameongeza kuwa, iwapo viongozi wa nchi hawatakuwa macho na wakatumbukia katika madhambi haya, awamu za baadaye na hatari zaidi ni kuwa dhaifu katika vipindi vya hofu na misukosuko, kupatwa na maradhi ya unafiki na kukana neema za Mwenyezi Mungu.
Amesema njia pekee ya kujikomboa na madhambi na kuteleza huko ni kuwa na taqwa na kujichunga.
Baada ya hapo Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia masuala ya sasa na ya kipindi hiki. Ametilia mkazo kwamba, kwa sasa nchi iko katika kipindi nyeti na makhsusi na kusema: Miongoni mwa sifa za kipindi cha sasa ni kuwa, viongozi wa nchi wanaelewa vyema uwezo mkubwa na suhula za nchi hii, tofauti na ilivyokuwa katika zama za mwanzoni mwa Mapinduzi ya Kiislamu.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa, sifa nyingine ya kipindi cha sasa ambayo inakifanya kiwe nyeti na muhimu ni kuwapo uadui makhsusi wa wazi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ambao ni zaidi ya hitilafu za kawaida kati ya nchi mbalimbali.
Akibainisha sababu kuu ya uadui huo makhsusi, amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ni tukio lisilo na kifani na kuongeza kuwa: Mfumo wa Kiislamu wa Iran unapinga ubeberu, dhulma, ubaguzi na siasa za kutumia mabavu kwa kutegemea misingi ya kifikra na kimatendo ya Kiislamu, na nguvu na ushawishi wake umepanuka na kukita mizizi zaidi katika eneo hili na duniani licha ya kuwepo mashinikizo ya aina mbalimbali. Ameongeza kuwa Iran, kama nguvu mpya inayojitokeza, inatoa changamoto kwa maslahi ya kidhalimu ya madola ya kibeberu.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kuna ulazima wa kutambua vyema njama na mipango ya adui na kubuni mipango kabambe ya kujilinda na kukabiliana na njama hizo. Amesisitiza kuwa mipango ya utekelezaji pia itapata maana katika fremu ya mipango hiyo kabambe.  
Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa, njama na mipango ya adui ni kuvunja na kuharibu uwezo wa Jamhuri ya Kiislamu na kama hataweza basi atafanya njama za kuzuia ustawi wa uwezo huo. Amesema kuwa, njia pekee ya kukabiliana na mipango na njama za adui ni kutumia vyema na kwa njia sahihi uwezo uliopo na kuzidisha nguvu ya nchi hii siku baada ya siku. Baada ya hapo amebainisha uwezo mkubwa wa nchi hii.
"Njia pekee ya kukabiliana na mipango na njama za adui ni kutumia vyema na kwa njia sahihi uwezo uliopo na kuzidisha nguvu ya nchi hii."
"Imani ya Kiislamu" ni nguvu na uwezo wa kwanza ulioashiriwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu. Amesema kuwa upande tunaokabiliana nao unatumia uwezo wake wote hususan intaneti kwa ajili ya kuteteresha na kuyumbisha imani ya kizazi cha vijana na kizazi cha baadaye; kwa msingi huo tunapaswa kulipa umuhimu makhsusi suala la kulinda na kuimarisha zaidi imani ya Kiislamu katika jamii ambayo ni miongoni mwa nyanja za uwezo na nguvu (zetu).
Ayatullah Ali Khamenei ameyataja maendeleo ya kielimu kuwa nguvu na uwezo wa pili mkubwa wa nchi. Amesisitiza kuwa, upande wa pili unapinga sana maendeleo ya kielimu na kisayansi ya Iran na unatumia hata njia ya mauaji ya kigaidi dhidi ya wasomi wa Iran kwa shabaha ya kusimamisha maendeleo hayo. Ameongeza kuwa, ili kukabiliana na maendeleo ya kisayansi ya Iran, maadui wametumia hata nyezo chafu na zilizopigwa marufuku kama virusi vya intaneti, na tungeweza kuwaburuta katika mahakama za kimataifa kutokana na uhalifu huo lakini inasikitisha kwamba, hilo halikufanyika.
"Tungeweza kuwaburuta katika mahakama za kimataifa kutokana na uhalifu huo lakini inasikitisha kwamba, hilo halikufanyika".
Amesema kuwa moja kati ya sababu kuu za mashinikizo ya adui dhidi ya sekta ya nyuklia ya Iran ni upinzani wake dhidi ya maendeleo ya kielimu ya nchi hii na wao wenyewe wanaelewa vyema kwamba, madai kwamba Iran inafanya jitihada za kupata bomu la nyuklia ni uongo wa wazi.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu mesema kuwa uwezo wa kiuchumi na uwezo wa kujilinda ni miongoni mwa sababu za nguvu za nchi hii. Amesisitiza udharura wa kuzidishwa uwezo huo na kusema: Nguvu ya kisiasa ya taifa kwa maana ya umoja na mshikamano wa kitaifa, inapaswa kulindwa, na hakupasi kuwepo hitilafu katika misingi ya harakati ya Mfumo wa Kiislamu baina ya wananchi licha ya kuwepo hitilafu na mitazamo mbalimbali ya kisiasa, jambo ambalo si tatizo.
Ayatullah Khamenei amesema, kwa baraka zake Mwenyezi Mungu, hii leo kuna umoja na mshikamano huo wa kitaifa kuhusu misingi ya Mfumo wa Kiislamu, na wananchi wote wanapenda Mapinduzi, vielelezo vya Mapinduzi, turathi za Mapinduzi na jina la Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu.
Amesema kuwa "jamii kijana ya Iran" ni miongoni mwa nguvu na uwezo mkubwa wa nchi hii. Ameongeza kuwa, jamii kijana ni neema kubwa sana na muhimu, na viongozi wa serikali wanapaswa kufanya harakati za kuzidisha jamii kijana hapa nchini kwa kutumia mipango na ratiba sahihi.
Baada ya kutilia mkazo udharura wa kuzidishwa uwezo wa kimsingi wa nchi kwa ajili ya kukabiliana na mipango ya adui, Ayatullah Khamenei amesema kuwa, adui ni 'mtandao wa ubeberu' unaoongozwa na serikali ya Marekani na 'kanali ya Kizayuni' ambayo kielelezo chake ni utawala bandia wa Israel.
Ameashiria kuwa upande wa pili haufichi uadui wake na kusema: Matamshi yaliyotolewa siku chache zilizopita na Waziri wa Mambo ya Nje katika kikao cha wazi cha Bunge akisema kuwa dhati na hakika ya Marekani haijabadilika, ni matamshi sahihi kabisa; hakika ya Marekani ya sasa ni ile ile ya kipindi cha (Ronald) Reagan na hakuna tofauti yoyote baina ya Wademokrati na Warepublican.
"Matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje kuwa hakika ya Marekani haijabadili ni sahihi kabisa"
Ayatullah Khamenei ameashiria fikra isiyo sahihi kuhusu Marekani na kusema: Baadhi ya watu wanadhani kuwa, tunaweza kupatana na Marekani na kumaliza matatizo yetu, hii ni fikra isiyo sahihi na njozi tupu.
Amesisitizia kuwa, katika mtazano wa mantiki, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kamwe haitapendwa na Marekani. Ameongeza kuwa: Mwenendo wa Wamarekani daima umekuwa wa kihabithi na unaoambatana na inadi; kwa msingi huo dhana kwamba masuala ya Iran na Marekani ni suutafahamu na yanaweza kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo na kwa mbinu ya 50 kwa 50, ni dhana isiyo ya kweli na isiyo sahihi.  
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Tatizo kuu la Wamarekani ni uwepo wa Jamhuri ya Kiislamu, suala mbalo haliwezi kutatuliwa kwa mazungumzo na uhusiano, kwa sababu nguvu na kujitawala kunakotokana na Uislamu hakukubaliwi na ubeberu.
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, katika mtazamo wa Marekani mapatano yana maana ya kutupilia mbali misimamo ya misingi (yetu). Ameongeza kuwa, kuachana huko na misimamo na misingi hakuna mwisho, na kama ambavyo kwa sasa baada ya maudhui ya nyuklia wamezusha suala la makombora, baada ya makombora itakuja zamu ya haki za binadamu na baada ya haki za binadamu watajadili suala la Baraza la Walinzi wa Katiba, kisha Utawala wa Faqihi na hatimaye Katiba na utawala wa Kiislamu hapa nchini; kwa msingi huo dhana kwamba Jamhuri ya Kiislamu inaweza kupatana na Marekani ni dhana isiyo sahihi.
"Kuachana na misimamo na misingi mkabala wa Marekani hakuna mwisho, na baadaye watazusha suala la makombora, haki za binadamu, Baraza la Walinzi wa Katiba, kisha Utawala wa Faqihi, Katiba na utawala wa Kiislamu hapa nchini"
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria dhana nyingine isiyo sahihi na kusema: Baadhi wanadhani kuwa sababu ya uhasama wa Marekani na Iran ni uchochezi wa Jamhuri ya Kiislamu, ilhali wao (Wamarekani) ndio ambao tangu mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu walijenga msingi wa uadui na uhasama kwa kutoa matamshi mabaya, vikwazo na kumpa hifadhi adui wa taifa la Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema dawa mujarabu ya uadui wote wa mabeberu ni kuimarisha kinga na uwezo wa nchi na kusisitiza kuwa: Kwa mujibu wa amri ya wazi ya Qur'ni, tunalazimika kuzidisha uwezo wetu wa kiimani, kiuchumi, kiulinzi, kielimu, kisiasa na kijamii kadiri tunavyoweza.  
Ayatullah Khamenei amewataka viongozi wote wa taasisi mbalimbali hapa nchini kutekeleza kikamilifu nyadhifa na majukumu yao katika fremu ya kuzidisha uwezo na kinga ya taifa na amewausia maafisa wa wizara mbalimbali na taasisi zinazohusika na masuala ya kielimu ya nchi kujiweka mbali na masuala yasiyo ya msingi.
Ayatullah Khamenei ametilia mkazo udharura wa kulindwa vijana wenye imani na wanamapinduzi ambao ni miongoni mwa nguvu na uwezo wa nchi na kusema: "Kama ambavyo nimekuwa nikisema waziwazi, ninawaunga mkono vijana wenye imani na wanamapinduzi na ninawapenda".  
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea kuhutubia hadhara ya viongozi na wakurugenzi wakuu wa Mfumo wa Kiislamu kwa kutaja masuala kadhaa muhimu katika uwanja wa uchumi na mapatano ya nyuklia.
Amesema kuwa mdororo wa uchumi na ukosefu wa kazi ni matatizo makuu ya nchi na kuongeza kuwa: Matatizo haya yanatokana zaidi na sera na mipango ya serikali ya sasa, serikali iliyopita na ile ya kabla yake kuliko sula la vikwazo.
Ayatullah Khamenei ameeleza baadhi ya njia za kutatua matatizo hayo mawili na kusema, kuna udharura wa kutiliwa maanani viwanda vidogo na vya kati. Ameongeza kuwa, kuhuishwa kwa viwanda hivyo ni miongoni mwa nguzo za uchumi ngangari na kunaweza kwa kiasi kikubwa kuleta harakati ya kiuchumi na kuanzisha nafasi za ajira.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa suala la kuainisha vipaumbele katika kazi lina umuhimu mkubwa. Ameongeza kuwa, ni jambo la kawaida kwa kila waziri kuyatambua matatizo yake kuwa ndiyo muhimu zaidi na kufanya jitihada za kupata bajeti zaidi, hata hivyo serikali inawajibika kuzidisha kasi ya harakati ya kiuchumi kwa kuainisha vipaumbele halisi.
Ameeleza matumaini ya kuonekana matokeo ya shughuli za seikali katika medani ya uchumi ngangari na kusema kuwa, kuunga mkono makampuni ya elimu msingi kunapaswa kupewa kipaumbele kikamilifu na kuna taathira katika kutatua matatizo mawili makuu ya mdororo na ukosefu wa kazi.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa, suala la kuvutia na kuelekeza rasilimali na vitegauchumi vya kigeni katika maeneo husika pia lina umuhimu. Amesema kuwa, katika uwanja huu pia kuna udharura wa kuainishwa vipaumbele.
Miongoni mwa mambo yaliyotiliwa mkazo na Kiongozi wa Mapinduzi ni pamoja na kuzuia uagizaji kutoka nje wa bidhaa zinazoshabihiyana na zile zinazozalishwa ndani ya nchi au zisizohitajiwa hapa nchini, kubadilisha zana zilizochakaa za viwanda, kutiliwa maanani kikamilifu sekta ya kilimo na kuzingatia na kuwekeza katika uzalishaji na uuzaji nje bidhaa zinazotokana na mafuta ya petroli badala ya kuuza petroli ghafi.
Amesema kuwa, suala la kuzidisha uzalishaji na uuzaji nje wa mafuta ya petroli ni haja muhimu ya nchi lakini inatupasa kuelewa kuw, nchi yenye akiba kubwa zaidi ya mafuta na gesi duniani haipasi kuagiza mafuta kutoka nje; hivyo maafisa wa serikali wanapaswa kupanga ratiba na kuweka mipango ya kutatua tatizo hili.
" Nchi yenye akiba kubwa zaidi ya mafuta na gesi duniani haipasi kuagiza mafuta kutoka nje".
Ayatullah Khamenei amekosoa mtazamo unaoamini kuwa, hakuna rasilimali za kutosha kwa ajili ya kutekeleza sera za uchumi ngangari na kusema: Akiba ya fedha za kigeni na za riale za wananchi katika mabenki ni kubwa sana, hivyo rasilimali hii inaweza kutumiwa kwa ajili ya kuzidisha kasi katika mchakato wa uchumi ngangari kwa kuzidisha suhula na vihamasishi vya kisheria.
Suala la mapatano ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1 (JCPOA) na tathmini ya kiwango cha kufungamana pande husika na utekelezaji wake lilikuwa sehemu ya mwisho ya hotuba muhimu ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika hadhara ya viongozi wa nchi.
Ayatullah Khamenei amesema mitazamo ya pande zote mbili za waungaji mkono na wapinzani wa mapatano hayo imetiwa chumvi. Amesema kuwa, watu wanaosifu mapatano hayo ya nyuklia na wale wanaoyapinga na wakosoaji wanatia chumvi katika kueleza mitazamo yao ilhali makubliano hayo yana mambo chanya na mazuri na nukta za udhaifu na nakisi.
"Makubaliano ya nyuklia ya Iran na 5+1 yana mambo chanya na mazuri na nukta za udhaifu na nakisi”.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, mambo chanya ya JCPOA ndiyo yaliyoihamasisha Jamhuri ya Kiislamu kuingia katika mazungumzo lakini mengi kati ya mambo hayo mazuri hayakudhaminiwa.  
Ameashiria nakisi na mapungufu ya JCPOA na kusema: Nakisi hizo ni yale mambo ambayo daima tumekuwa na wasiwasi nayo na tumekuwa tukikariri kwamba upande wa pili unakengeuka ahadi, si mwema na hauheshimu makubaliano.
Ameongeza kuwa, katika makubaliano hayo ya nyuklia kuna myanya ambayo iwapo ingefungwa basi nakisi zingekuwa chache au zingeondolewa kabisa.
"Myanya iliyopo katika JCPOA iwapo ingefungwa nakisi zingepungua au kuondolewa."
Ayatullah Khamenei amepongeza kazi na juhudi kubwa za timu ya Iran katika mazungumzo ya nyuklia na kusema: Tunayosema kuhusu JCPOA hayahusu jitihada za ndugu hawa wapendwa bali ni tathmini kuhusu utendaji wa upande wa pili.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria vipengee vyenye utata katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ambavyo vinatayarisha uwanja wa kutumwia vibaya na upande wa pili na kusisitiza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu haitakuwa ya kwanza kukiuka makubaliano hayo kwa sababu kutekeleza ahadi na makubaliano ni amri ya Qur'ani, lakini iwapo vitisho vinavyotolewa na wagombea urais wa Marekani kwamba watararua makubaliano hayo vitatekelezwa basi Jamhuri ya Kiislamu itayachoma moto, suala ambalo pia ni amri ya Qur'ani mkabla wa wakiukaji wa ahadi na makubaliano.
Ayatullah Khamenei ameendeleza hotuba yake kwa kueleza vielelezo vya ukiukaji wa makubaliano wa Marekani na kusema: Wajibu wa upande wa pili (katika mazungumzo ya nyuklia) ulikuwa kuondoa vikwazo lakini upande huo haukutekeleza wajibu wake na baadhi ya vikwazo vimeondolewa kwa namna fulani lakini vikwazo hivyo bado vipo kivitendo.
"Vikwazo havijaondolewa kivitendo".
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, Wamarekani wameendeleza vikwazo vya awali kikamilifu suala ambalo lina taathira pia katika vikwazo vya awamu ya pili ambavyo ilipangwa kuwa viondolewe.
Ayatullah Ali Khamenei amesema maafisa husika wanapaswa kulitilia maanani suala hilo na kuwa makini, na wasikariri kusema kuwa vikwazo vimeondolewa.
Vilevile ameashiria tatizo na miamala na benki za kigeni na kusema: Maafisa wa serikali ya Marekani wanasema kwa ndimi na katika nyaraka kwamba hakuna kizuizi chochote cha miamala ya kibenki na Iran lakini kivitendo wanazizuia benki za kigeni kuamiliana na Iran.
Ayatullah Khamenei amesema matamshi yaliyotolewa hivi karibuni na afisa mmoja mwandamizi wa Marekani akisema: "Hatutaruhusu Iran kuwa na hali bora", ni mfano wa mienendo hiyo ya kindumakuwili. Ameongeza kuwa, Wamarekani wamefanya kosa hilo kubwa la kuzuia miamala ya benki za kigeni na Iran na mtu yeyote hapasi kutetea mwenendo huo wa Wamarekani.
'Bima ya meli zinazobeba mafuta ya petroli' ni maudhui nyingine muhimu ambayo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameizungumzia akibainisha vielelezo vya ukiukaji wa makubaliano na ahadi wa Marekani. Amesema wamekubali bima hiyo kwa kiwango fulani lakini muundo mkubwa wa bima hiyo haukuwekwa katika maudhui hii kwa sababu Wamarekani ni wanachama katika muundo huo na wanawekwa vizuizi.
Ameashiria jinsi Jamhuri ya Kiislamu ilivyotekeleza kikamilifu ahadi zake na kusema kuwa, masharti na makubaliano yetu yote yametekelezwa na urutubishaji wa urani kwa kiwango cha asilimia 20 umesitishwa na taasisi za nyuklia za Fordo na Arak zimesimamishwa, lakini upande wa pili bado unataka makubwa zaidi.
"Msikubali kabisa matakwa yao kuhusu nyuzi kaboni (carbon fiber) ambazo zinatumika katika utengenezaji wa mashinepewa (centrifuge) na upimaji wa kilo 300 za mada za nyuklia".  
Ayatullah Khamenei amemwambia Mkuu wa Taasisi ya Atomiki ya Iran kwamba: Msikubali kabisa matarajio ya upande wa pili katika medani ya nyuzi kaboni (carbon fiber) ambazo zinatumika katika utengenezaji wa mashinepewa (centrifuge) na upimaji wa kilo 300 za mada za nyuklia wala msisalimu amri mbele yao.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia pia fedha za Iran zinazozuiliwa nje ya nchi na kusema: Hii leo ni vigumu kupata fedha za mafuta za Iran zinazoko nje ya nchi na kazi hiyo ina gharama kubwa, na fedha tulizonazo katika benki za nchi nyingine hazijarejeshwa katika Jamhuri ya Kiislamu kwa sababu fedha hizo ziko kwenye sarafu ya dola na zimezuiliwa kurejeshwa nchini kutokana na uhasama wa ukiukaji wa makubaliano wa Marekani.
Ayatullah Khamenei amesema sekta ya nyuklia bi sekta ya kistratijia na inapaswa kudumishwa na kustawishwa zaidi bila ya tatizo lolote.
Ameashiria taathira kubwa za sekta ya nyuklia katika kutoa kinga na kuzidisha usalama wa nchi na kusema: Uwezo wa sekta hiyo, nguvu kazi yake hodari na uwezekano wa kufikia hali yake ya hapo kabla vinapaswa kuchungwa na kulindwa.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kwa bahati nzuri uwezo wa kurejea kwenye hali ya hapo awali umelindwa na ikilazimu tunaweza kupata SWU laki moja kwa kutumia kizazi kipya cha mashinepewa katika kipindi cha chini ya mwaka mmoja na nusu; hivyo upande wa pili usidhani kwamba mikono yetu imefingwa.
"Uwezo wa kurejea kwenye hali ya hapo kabla ulehifadhiwa na kulindwa".
Ayatullah Khamenei ametilia mkazo udharura wa kukabiliana ipasavyo na aina yoyote ya vizingiti vya Marekani na amewaambia viongozi hapa nchini kwamba: Haki inachukuliwa hususan kwa mbwamwitu kama Marekani ambaye lazima umnyang'anye haki yako kutoka mdomoni mwake.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza kufurahishwa na matamshi ya Rais na Waziri wa Mambo ya Nje yanayosisitiza udharura wa kukabiliana na vizingiti vya Marekani na kusema: Tunapaswa kulinda uwezo wetu kwa ajili ya kukabiliana na uhaini na hatua za upande wa pili.
Amesema kuwa kuzalisha urani iliyorutubishwa kwa daraja ya asilimia 20 na kutengeneza mashinepewa za kisasa ndiyo sababu kuu iliyoilazimisha Marekani kukubali baadhi ya ahadi ilizotoa na kusisitiza kuwa, kama si uwezo wa kielimu na kiteknolojia wa Iran basi bila shaka Wamarekani wasingekubali hata hali hii ya sasa; hivyo basi uwezo huo unapaswa kustawishwa zaidi.   
Katika matamshi yake ya mwisho kwenye hadhara ya viongozi wa nchi kuhusu masuala ya nyuklia, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Tunatarajia kwamba jopo linalosimamia utekelezaji wa JCPOA litasimama imara na kuwa makini na macho zaidi na kutetea maslahi ya taifa katika eneo lolote upande wa pili unapofanya visivyo au unapofikiria kufanya hiana.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiisalmu, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Hujjatul Islam Walmusilimin Hassan Rouhani ametoa hotuba fupi akiutaja mwezi wa Ramadhani kuwa ni mwezi wa rehma za Mwenyezi Mungu. Ameashiria hali ya nchi hii wakati serikali ya awamu ya 11 iliposhika usukani na kusema: Serikali ililipa kipaumbele suala la kudhibiti na kukomesha mfumuko wa bei na tumeweza kupunguza kiwango cha mfumuko wa bei kutoka asilimia 40.1 mwaka 1392 (Hijria Shamsia) hadi asilimia 11.9 mwaka 1394 na katika mwezi ujao kiwango hicho kitakwenda chini ya asilimia 10.
Rais Rouhani amesema kuwa, kudhibiti soko la fedha za kigeni, ustawi wa kiuchumi na kuondoka katika mdororo ni miongoni mwa matunda ya serikali ya sasa.
"Rais Rouhani: Mwezi ujao mfumuko wa bei utafiki chini ya asilimia 10".
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake Rais wa Jamhuri ya Kiislamu amezungumzia hatua zilizochukuliwa na serikali katika sekta ya kilimo na kusema: Kuanzia mwaka 1392 hadi 1394 uzalishaji wa bidhaa za kilimo uliongezeka kutoka tani milioni 97 hadi tani milioni 112. Ameongeza kuwa katika uwanja wa chakula cha kistratijia kama ngano na mchele, akiba imeongezeka mara tatu katika mwaka 1394 ikilinganiswha na mwaka 1392 na inatazamiwa kuwa uzalishaji wa ngano katika mwaka huu utafikia tani milioni 10 ambazo ni karibu sawa na mahitaji ya nchi.
Ameashiria pia maendeleo yaliyopatikana katika sekta ya mafuta ya petroli ma kusema kuwa, awamu za 12, 15, 16 na 17 za mradi wa Pars Kusini zimefunguliwa na awamu nyingine tatu hadi nne za mradi huo zitafunguliwa hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu.
Rais Rouhani amesema kuwa uzalishaji wa gesi nchini pia umeongezeka katika kipindi hicho kwa mita za ujazo milioni 150 kwa mwaka.
Vilevile ameashiria ongezeko la njia za reli nchini na kusema: Kwa kuzidishwa kilomita 475 za njia za reli na mipango ya kuongeza kilomita nyingine 700 za njia za reli, kutashuhudiwa mabadiliko makubwa katika uwanja wa reli na usafirishaji hapa nchini.
Rais Rouhani amesema kuwa, katika biashara ya nje kumepatikana mabadiliko chanya. Amesisitiza kuwa, mwaka uliopita na baada ya kipindi cha miaka 60 Iran imefanikiwa kwa mara ya kwanza kuuza nje bidhaa nyingi zaidi zisizo za mafuta kuliko bidhaa zisizo za mafuta zinazoagizwa kutoka nje ya nchi.
Ameongeza kuwa kwa wastani katika kipindi cha miaka 8 iliyopita urari wa biashara ya nchi ulikuwa hasi kwa dola bilioni 25 lakini kwa mara ya kwanza urari huo wa kibiashara umekuwa chanya.
Ameashiria pia mazungumzo ya nyuklia na kusema: Katika mazungumzo hayo tumethibitisha haki za nyuklia za taifa la Iran na maazimio ya kidhalimu yamefutwa.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hatua ya kwanza baada ya kuondolewa vikwazo ilikuwa kufika kwenye masoko ya mafuta ya petroli na kuongeza kuwa, katika uwanja huo tumekaribia hali iliyokuwepo kabla ya vikwazo.  
Dakta Rouhani amesema kuwa uzalishaji wa gesi umeongeza kutoka mapipa laki tatu na 70 elfu hadi laki 3 na 90 elfu katika miezi ya hivi karibuni. Ameongeza kuwa uuzaji nje wa mafuta ghafi ya petroli hii leo umeongezeka na kufikia mapipa milioni 2 na uzalishaji wa mafuta hayo umeongezeka kutoka mapipa milioni 2.7 hadi milioni 3.8 kwa siku.
Rais Rouhani amesema kuwa: Hii leo tunahitjia umoja na mshikamano kwa ajili ya kufikia malengo yetu. Ametaja changamoto kubwa zaidi inayoikabili nchi kuwa ni suala la ajira. Amesema moja kati ya fahari za serikali ya awamu ya 11 ni kuanzisha nafasi mpya milioni 1 na laki 3 na arubaini elfu za kazi katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita. Amesema kwa mujibu wa Kituo cha Takwimu nchini, kwa sasa watu milioni 22 wanafanyakazi hapa nchini.
Amesema kuwa miongoni mwa matatizo ynayokwamisha juhudi za ustawi wa kiuchumi ni uchache wa mahitaji. Ameongeza kuwa hatuwezi kufikia ustawi unaohitajika wa kiuchumi bila ya kupatikana soko jipya; kwa msinghi huo tunalazimika kutafuta soko jipya la ndani na nje na vilevile vitegauchumi vya kigeni.                         

700 /