Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Vyuo vikuu na wanavyuo nawapaswa kuwa wanamapinduzi daima

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei alasiri ya leo (Jumamosi) amekutana na wahadhiri wa vyuo vikuu, watu wenye vipaji vya kielimu na watafiti wa vyuo vikuu, vijiji vya sayansi na teknolojia na vituo vya elimu na utafiti ambapo amezungumzia taswira ya malengo ya miaka ishirini ya Mfumo wa Kiislamu kwa ajili ya kufikia kwenye Iran yenye nguvu, izza, huru, yenye kushikamana na dini, tajiri, yenye uadilifu, yenye utawala ya wananchi, safi yenye kupigana jihadi, yenye upendo na wachamungu na kusisitiza kuwa, vyuo vikuu ndiyo msingi na nguzo ya malengo hayo aali. Amesema, kuzidishwa kasi ya ustawi wa kielimu katika vyuo vikuu na vituo vya kielimu, kuanzisha na kuimarisha utambulisho wa kujivunia wa Kiirani - Kiislamu ndani ya nyoyo za vijana na kuhakikisha vyuo vikuu pamoja na wanavyuo wake vinakuwa vya kimapinduzi na uhodari halisi wa makamanda na maafisa wa vita laini ni katika masharti ya kuufanya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kuwa nguvu kubwa ya kielimu na pia kuwa kigezo kizuri cha mfumo wa demokrasia iliyosimama juu ya mafundisho ya Uislamu na masuala ya kiroho duniani. 
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza tena katika mkutano huo kwamba vikao vyake na wahadhii wa vyuo vikuu vinafanyika kwa shabaha ya kuonesha heshimu na kuienzi elimu na walimu wake. Ameashiria mawasiliano yake ya mara kwa mara na watu wa vyuo vikuu, watu wenye vipawa na wanachuo na kusema: Kufanyika kwa vikao hivi mbali na kuwa nembo, kunatoa taswira jumla kuhusu anga ya mazungumzo, ya kielimu na kifikra katika vyuo vikuu. 
Baada ya hapo Ayatullah Khamenei mesema kuwa, mtazamo kuhusu mustakbali wa nchi ni miongoni mwa mambo yanayowatia dukuduku maulama, wasomi na watu wenye vipawa na kuongeza kuwa, kuchora picha na taswira ya mustakbali kuna umuhimu kutokana na kwamba, uongozi wa nchi katika miaka ijayo utakuwa mikononi mwa wanavyuo ambao kwa sasa wanapata elimu na kufanya bidii katika vyuo vikuu.  
Amesema suala hilo linaonesha umuhimu wa nafasi ya wahadhiri na maafisa wa vyuo vikuu na kuongeza kuwa, mnyororo wa elimu na maarifa kuanzia Wizara ya Elimu na Malezi hadi chuo kikuu, una wadhifa na jukumu kuu kwa ajili ya kupatikana mustakbali unaotakikana hapa nchini. 
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameuliza swali kwamba, ni mustakbali upi bora unaotakikana kwa ajili ya Iran ya baada ya miaka 20, na kusema kuwa: Iwapo mustakbali bora tunaotaka ni Iran yenye nguvu, heshima, huru, inayoshikamana na dini, tajiri, yenye uadilifu, yenye utawala wa wananchi, safi, yenye kupigana jihadi, yenye ari na watu wachamungu basi kuna udharura kwa vyuo vikuu kujipamba kwa sifa na vigezo hivi na kulea kizazi cha vijana wenye itikadi na imani na masuala hayo. 
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, iwapo vyuo vikuu havitavipa umuhimu vigeo hivyo, katika siku za usoni tutashuhudia Iran tegemezi, isiyokuwa na mwelekeo katika masuala ya utamaduni, yenye mipasuko ya kijamii, kikaumu, kimadhehebu na kisiasa na yenye utawala wa kibwanyenye. 
Amesema kuwa, matokeo ya mustakbali kama huo ni ni kuwa na nchi ambayo itakuwa katika vilele vya utajiri, lakini wakati huo huo itakuwa na watu maskini kupindukia, wenye shida na matatizo mengi, na mfano wake wa wazi ni jamii ya Marekani au Wall Street ya Kimarekani.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, katika mustakbali kama huo matabaka yote ya jamii hayatakuwa na hali bora ya maisha na kwa hakika nchi itakuwa na Wall Street ya Kiirani. 
Akikamilisha sehemu hii ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Ni kwa sababu hii ndiyo maana daima nimekuwa nikisisitiza sana juu ya umuhimu wa vyuo vikuu, wahadhiri na mawaziri na elimu, kwa sababu ili kufikia mustakbali mwema wa Iran, kunahitajika malezi ya wanadamu wenye elimu, wenye subira, wanaopigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, wajuzi na mashujaa; na watu wa aina hii aghlabu hulelewa katika vyuo vikuu. 
Ayatullah Khamenei ameendelea kwa kueleza masharti ya kulea vijana wa aina hiyo katika vyuo vikuu na kusema: Maendeleo ya kielimu, nidhamu ya kimaadili, ustahamilivu wa kidini, muono wa mbali wa kisiasa na kujenga hisi za kujifaharisha kwa utambulisho wa Kiirani-Kiislamu katika mazingira ya vyuo vikuu ni katika masharti ya kazi hiyo muhimu.
Kuhusu suala la maendeleo ya kielimu, amesisitiza udharura wa kuzidishwa kasi ya ustawi wa kielimu na kusema: Siku zilizopita nilitahadharisha kuhusu suala la kupungua kasi ya ustawi wa kielimu kwa sababu kasi imepungua, na ili kuweza kufidia kubakia nyuma kielimu hatuna budi kuongeza kasi ya ukuaji wa elimu.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria matamshi yanayotolewa na baadhi ya wasomi kuhusu suala la kupungua kasi ya elimu katika nchi za Magharibi na kusema: Iwapo kasi ya elimu imepungua katika nchi za Magharibi basi ni kutokana na kwamba wao wametumia uwezo wao wote, lakini sisi tunalazimika kufidia kubakia kwetu nyuma kwa miaka 60 au 70 kulikosababishwa na serikali saliti na zilizoghafilika ili tuweze kufika kwenye viwango vya juu na kileleni katika mashindano hayo ya kimataifa. 
Ayatullah Khamenei ameashiria nafasi ya wahadhiri wa vyuo vikuu katika kuanzisha na kuimarisha utambulisho wa Kiirani na Kiislamu kati ya wanachuo na kusema: Wahadhiri wanaweza kuamsha hisi ya utambulisho wa kujivunia katika nafsi ya wanafunzi wa vyuo vikuu kwa kueleza maendeleo ya nchi katika nyanja za anga za mbali, nano, nyuklia, bioteknolojia na tiba. 
Vilevile amesisitiza kuwa, hatua yoyote ile ya kujenga hisia za kujiona duni na kuwavunja moyo wanachuo ni usaliti na kuongeza kwamba: Wanafunzi wa vyuo vikuu wanapaswa wakati wote kujivunia na kuona fakhari kuwa kwao Wairani, Waislamu na wanamapinduzi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kwamba: Japokuwa tumebakishwa nyuma kihistoria katika maendeleo ya kielimu, lakini kwa jitihada kubwa na nishati ya vijana wetu wenye vipawa nchini, tunaweza kufidia na kuziba pengo hilo.
Ayatullah Khamenei ameashiria pia ripoti za baadhi ya taasisi za nyaraka na takwimu pamoja na majarida yenye hadhi duniani yaliyothibitisha kupigwa hatua kubwa za maendeleo ya kielimu nchini Iran na kuongeza kuwa: Katika ripoti hizo, taasisi na majarida hayo maarufu na yenye heshima duniani yanapozungumzia maendeleo mbalimbali ya kielimu ya Iran huwa yanatumia maneno kama "maendeleo ya kustaajabisha ya Iran," "Iran nguvu inayochipua yenye nguvu za kielimu," "Iran katika jitihada za kubadilisha uchumi unaotegemea rasilimali kuwa uchumi unaotegemea uzalishaji wa elimu" na "maendeleo ya Iran katika seli shina, sayansi ya teknolojia, anga za mbali, kubadilisha nishati na teknolojia ya mawasiliano." Amesema, uhakika huo unapaswa kufikishwa vizuri kwa kizazi cha vijana nchini ili sambamba na kupata hisia za kupenda utambulisho wao, waweze kujivunia na kuona fakhari kuwa kwao Wairani. 
Amesema, ubunifu mpya wa Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran duniani katika nyuga za demokrasia ni kitu kingine muhimu cha kujivunia na kusisitiza kwamba: Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndio utawala pekee duniani ambao umekuja na demokrasia iliyosimama kwenye msingi wa Uislamu na masuala ya kiroho.
Kiongozi Mudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Demokrasia ya nchi za Magharibi kwa hakika ni utawala wa vyama, na vyama katika nchi za Magharibi badala ya kuwa mtandao ulioenea baina ya wananchi, ni klabu za kisiasa ambazo za baadhi ya wanasiasa na mabepari.  
Ayatullah Udhma Khamenei amekumbusha pia kuwa: Kama uhakika huo wa kujivunia utambulisho wa kitaifa utafikishwa vizuri kwa mwanafunzi wa chuo kikuu, mwanafunzi huyo hatoweza kujiona duni wala kukata tamaa, na hata kama atakwenda nje ya nchi kwa ajili ya kuendelea na masomo, bila ya shaka yoyote atarejea nchini kwake, kwani atakuwa tayari amejengeka vizuri kwa hisia za kujali utambulisho wake na kujifakharisha nao.
Kuhusu suala la kupewa kipaumbele utambulisho wa Kiislamu katika vyuo vikuu nchini amesema kuwa: Viongozi wa vyuo vikuu wana wajibu wa kusimama imara kukabiliana na pia kuzuia hatua au jambo lolote lile lisilokubaliwa na Uislamu kama vile kupigwa kambi zinazowajumuisha pamoja wanachuo wa kike na kiume ambazo zinatia doa utambulisho wa Kiislamu.
Kuwa na muono wa mbali wa kisiasa na siasa katika vyuo vikuu ni jambo jingine la lazima lililososotizwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ili kuweza kuwa na Iran yenye mustakbali unaotakiwa. Amesema: Nimekuwa nikisisitizia mara zote umuhimu wa kujadiliwa masuala ya siasa ndani ya vyuo vikuu na hata katika miaka ya huko nyuma niliwahi kusema kuwa, Mungu awalaani watu waliokunja jamvi la fikra na kazi za kisiasa kwenye vyuo vikuu.
Ayatullah Khamenei ameongeza kwamba: Wakuu wa wakati huo walikasirishwa sana na maneno yangu hayo, lakini itikadi ya viongozi hao ilikuwa ni kupigwa marufuku na kuzuiwa masuala ya siasa ndani ya vyuo vikuu ingawa leo hii watu hao hao wanajitoa kimasomaso na kutoa matamshi tofauti na itikadi zao za huko nyuma kuhusiana na vyuo vikuu.
Amesisitiza kuwa, anga ya vyuo vikuu ni anga ya kupmbnisha mitazamo, mijadala na kutoa changamoto za kila aina na kuongeza kuwa: Kuweko anga hiyo katika kipindi cha vuguvugu la ujana hakuna tatizo lolote, lakini tatizo linakuja pale anga hiyo inapotumika vibaya kwa ajili ya kupiga vita Mapinduzi ya Kiislamu na matukufu ya kimapinduzi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Hakuna tatizo kuweko mitazamo na mirengo tofauti ya kisiasa katika vyuo vikuu, lakini maafisa na viongozi wa vyuo hivyo - iwe ni viongozi wa ngazi za juu au wizara au marais au wahadhiri - kila mmoja ana jukumu la kuielekeza anga hiyo ya mpambano wa hoja katika vyuo vikuu, upande wa kutia nguvu misingi na malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu na kamwe wasiruhusu kuweko mitazamo ya kupinga Mapinduzi ya Kiislamu katika vyuo vikuu.
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa: Vyuo vikuu na wanachuo, wanapaswa kuwa wanapinduzi daima.
Vilevile ameashiria baadhi ya ripoti zinazoonesha kuweko fikra za kuunga mkono mirengo inayopinga mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu katika baadhi ya vyuo vikuu na kuongeza kuwa: Wakuu wa Wizara ya Sayansi na Elimu ya Juu wanapaswa kuwa macho sana, na wasiruhusu vyuo vikuu kugeuzwa kuwa maeneo ya kupotosha na kupiga vita uhakika na matukufu ya Mapinduzi ya Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa: Kuweko anga ya kimapinduzi na ya kushikamana na dini na kupewa nafasi kubwa Imam (Khomeini – Mwenyezi Mungu amrehemu) kwenye vyuo hivyo, ni katika mambo ya lazima ya wazi kabisa kwa vyuo vikuu.
Ayatullah Khamenei ameendelea na hotuba yake kwa kusema: Hata hivyo si sahihi pia kuwepo anga ya kulazimisha na kuteza nguvu katika vyuo vikuu, lakini anga ya vyuo hivyo inapaswa kuwa ya kimapinduzi na kidini, na hilo linapaswa kufanikishwa kwa hekima, kwa utulivu na kwa busara ya hali ya juu.
Kiongozi Mudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea na hotuba yake kwa kutoa nasaha kadhaa kwa maafisa na wakuu wa Wizara ya Sayansi na Elimu ya Juu pamoja na wakuu wa vyuo vikuu nchini.
Kulindwa moyo wa matumaini na nishati na uchangamfu katika maeneo ya kielimu na kiutafiti, kuzipa kipaumbele na umuhimu elimu za kimsingi, kuelekeza makala za kielimu upande wa mahitaji ya nchi, ulazima wa kubainishwa na kutolewa ufafanuzi ramani kuu ya kielimu nchini kwa ajili ya watu wa vyuo vikuu na kuifanya ramani hiyo kuwa ajenda yao na kutiliwa mkazo umuhimu wa kuweko masomo ya Sayansi ya Jamii yaliyosimama kwenye msingi wa dini tukufu ya Kiislamu, ni katika nasaha zilizotolewa na Ayatullah Ali Khamenei kwenye hotuba yake.
Kupewa umuhimu udiplomasia ya kielimu ni nasaha nyingine zilizotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika hotuba yake hiyo na wakati huo huo amesisitiza kwa kusema: Udiplomasia na uhusiano wa kielimu ni jambo muhimu, nami ninaliunga mkono jambo hilo, lakini inabidi tuwe macho tusije tukatekwa na hila za maadui na kugeuzwa uhusiano huo wa kielimu kuwa bwawa la kujipenyeza na kutia doa maadui katika masuala yetu ya usalama kwani adui anatumia kila njia ikiwa ni pamoja na uhusiano na mawasiliano ya kielimu kwa ajili ya kujipenyeza nchini na kwamba jambo hilo limewahi kutokea huko nyuma na madhara yake yanaonekana leo hii katika baadhi ya mambo.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah Khamenei amezungumzia uchumi ngangari na kusema kuwa, uchumi huo utaandaa uwanja wa kupatikana heshima ya kitaifa na kutatua matatizo yote yaliyopo hivi sasa nchini. Ameongeza kuwa: Kuna baadhi ya watu wanasema, vipi utaweza kutatua matatizo na shida za hivi sasa katika jamii kupitia njia ya kusisitizia mara kwa mara suala la kulindwa heshima ya taifa? Majibu ya watu wanaotoa maneno hayo ni kwamba: Utatuzi pekee wa jambo hilo ni kutekelezwa vilivyo na kwa njia sahihi siasa za uchumi ngangari.
Nasaha nyingine zilizotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni umuhimu na kuyafanya kuwa jambo la kimsingi masuala ya kiutamaduni kwenye vyuo vikuu.
Ameongeza kwa kusema: Masuala ya kiutamaduni hayana maana ya kufanya mambo madogo madogo ya pembeni au kupeleka wanafunzi kwenye matamasha ya muziki na tamthilia, bali viongozi wa vyuo vikuu wanapaswa kuwafungulia uwanja wanachuo na wahadhiri wa vyuo hivyo wanaojali mambo ya thamani na ya kiroho ili waweze kufanya kazi zao vizuri na kuzijaza akili na nyoyo za wanafunzi wa vyuo vikuu, utamaduni wa Kiislamu na wa kimapinduzi.
Ayatullah Khamenei vilevile amewalenga moja kwa moja katika maneno yake wahadhiri wanamapinduzi ambao ni makamanda katika vita laini pamoja na wanachuo wanamapinduzi ambao ni maafisa katika vita hivyo laini akiwasisitizia kwa kuwaambia: Jukumu lenu ni kutoa mchango wa kweli na unaotakiwa katika shauri hili kwani ugumu na ukali wa vita laini vinavyoendeshwa na adui hivi sasa ni mkubwa zaidi kwa mara kadhaa ikilinganishwa na miaka ya huko nyuma.
Kutoruhusu kujiingiza na kutumiwa watu wasioaminika katika vyuo vikuu, ni nasaha nyingine zilizotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambaye amesisitiza kuwa: Mtu yeyote ambaye atatumia kisingizio chochote kile kama vile uchaguzi na mfano wake ili kuutia kwenye matatizo mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, mtu huyo haaminiki, na hana sifa za kuweko katika vyuo vikuu, na hilo si jambo jipya kwani hakuna nchi yoyote duniani inayoruhusu mfumo wake wa utawala utiwe katika matatizo.
Mwanzoni mwa mkutano huo, baadhi ya wahadhiri, wanafikra na wataalamu wa taaluma za sayansi ya uhandisi, sayansi ya tiba na sayansi ya jamii wametoa hotuba fupi fupi na kubainisha mitazamo yao kuhusiana na masuala tofauti.
Mabwana:
- Dk Hussein Bolandi, mwenye shahada ya udaktari katika uhandisi wa umeme ambaye pia ni mhadhiri msaidizi katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Ufundi,
- Dk Masoud Derakhshan, mwenye shahada ya udaktari wa uchumi na mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Allama Tabatabai,
- Dk Mostafa Ghanei, daktari bingwa wa mapafu na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba cha Baqiyyatullah,
- Dk Mohammad Reza Pakravan, mwenye shahada ya utaktari wa uhandisi wa umeme na mhadhiri msaidizi katika Chuo Kikuu cha Sharif,
- Dk Hassan Ali Ghobadi mwenye shahada ya udaktari katika fasihi na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tarbiyat Modarres,
- Dk Tavakol Habibzade, mwenye shahada ya udaktari katika sheria za kimataifa na mhadhiri msaidizi katika Chuo Kikuu cha Imam Sadiq AS,
- Dk Ali Akbar Farhangi, mwenye shahada ya udaktari katika masuala ya utawala ambaye pia ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Azadi Islami 
- Dk Hadi Ajili, mwenye shahada ya udaktari katika masuala ya uhusiano wa kimataifa na mhadhiri msaidizi katika Chuo Kikuu cha Allama Tabatabai,
- Na Dk Jaafar Mehrad mtaalamu katika "Systems theory" na mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Shiraza,
Na mabibi:
- Dk Zainab Kadkhoda, daktari bingwa wa upasuaji katika fani ya meno ambaye pia ni mhadhiri msaidizi katika Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba cha Tehran,
- Na Dk Susan Ghahremani, mwenye shahada ya udaktari katika taaluma ya lugha ambaye pia ni mhadhiri msaidizi wa masomo ya lugha ya Kiingereza katika Chuo Kikuu cha al Zahra.
Wamesisitizia mambo yafuatayo:
- Nafasi ya elimu ya anga za juu na teknolojia mpya na uwezo mbalimbali wa Iran katika uga huo,
- Udharura wa kulingana na kuoana sera za Serikali hususan katika sekta ya kuyapa mashirika ya kigeni kazi ya kutafuta na kuchimba mafuta na siasa za uchumi ngangari.
- Umuhimu wa kustawishwa na kutiwa nguvu uchumi unaotegemea elimu za kimsingi katika sekta mbalimbali nchini.
- Mchango na nafasi ya teknolojia ya mawasiliano na mashirika ya teknolojia katika kuzalisha elimu na utajiri.
- Udharura wa kuasisiwa na kuanzishwa kituo kikuu cha kufanya kazi kijihadi kwa ajili ya kutoa huduma za afya na tiba katika maeneo yenye maendeleo madogo.
- Ulazima wa kutumia misingi ya kidini na kifikihi kwa ajili ya kuandaa kalibu na fremu za kinadharia za haki za binadamu za Kiislamu na kutolewa ripoti kila mwaka kuhusu haki za binadamu.
- Umuhimu wa kugundua na kuzijua mbinu na malengo ya siri ya kueneza matumizi ya lugha ya Kiislamu katika nchi mbalimbali dunia na ulazima wa kutumiwa vizuri na kwa njia sahihi ufundishaji wa lugha za kigeni.
- Na udharura wa kuzalishwa upya kifikra na kivitendo fikra ya Mapinduzi ya Kiislamu katika upeo wa aina mbili, wa ndani na nje ya nchi kwa kuzingatia faida na manufaa ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Mwishoni mwa mkutano huo, wahadhiri wa vyuo vikuu wamesalishwa sala za Magharibi na Isha na Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kabla ya kula futari pamoja naye.
 

700 /