Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi akutana na familia za mashahidi wa 7 Tir

Kulaaniwa uchokozi dhidi ya Sheikh Isa Qassim

Ayatullah Ali Khamenei Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu leo alasiri (Jumamosi) amekutana na familia za mashahidi zikiwemo za mashahidi wa tarehe 7 Tir sawa na tarehe 27 Juni na vilevile mashahidi wa kulinda haram takatifu za Watu wa Nyumba ya Mtume (saw). Huku akisifu imani, mapambano, ushujaa na utambuzi wa hali ya juu wa mashaidi na subira pamoja na ukakamavu wa familia zao, Kiongozi Muadhamu amesema kuwa mashahidi hao na familia zao ni misingi ya nguvu na uwezo wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema kuwa njia pekee ya kufikiwa maendeleo ya Iran ya Kiislamu ni kuhuishwa moyo wa mapinduzi na mapambano. Mwanzoni mwa hotuba yake Kiongozi Muadhamu ametoa mkono wa pole kwa mnasaba wa kukumbukwa siku ya kuuawa shahidi Imam Ali (as) na kusema kuwa mtukufu huyo ni shahidi mkubwa zaidi katika historia ya mwanadamu, shahidi wa mihrabu na njia ya haki, ukakamavu na mapambano. Kisha ameashiria kupita miaka 35 tokea kujiri kwa tukio la kigaidi la kulipuliwa ofisi ya Chama cha Jamhuri hapo tarehe 7 Tir mwaka 1360 Hijiria Shamsia ambayo inasadifiana na tarehe 27 Juni 1981 na kusema kwamba watekelezaji wa jinai hiyo ambalo ni kundi la kigaidi, khabithi na lisilo na huruma, baada ya kukimbia nchi walipewa hifadhi na nchi za Ulaya na Marekani ambako wamekuwa wakiishi kwa miaka mingi sasa, nchi ambazo zinadai kuongoza mapamano dhidi ya ugaidi na kuunga mkono haki za binadamu. Kiongozi Muadhamu amesema suala hilo ni kashfa kubwa ya kihistoria kwa nchi za Ulaya na Marekani na kuongeza: ‘Kundi hilo la kigaidi ni la watu ambao mwanzoni waliingia kwenye mapambano kwa madai ya kutetea haki za wananchi na hata za Uislamu, lakini baada ya hapo walitenda jinai kama vile ya Tir 7 na kuua kigaidi raia wa kawaida. Hatimaye walisimama pembeni ya mtu kama Saddam na hivi sasa pia wako chini ya mwavuli wa uungaji mkono wa Marekani.’ Ayatullah Khamenei amesema tukio la Tir 7, 1360 Hijiria Shamsia ni tukio kubwa sana ambalo lina mafunzo na ibra nyingi. Huku akielezea malalamiko yake kutokana na kutofanyika kazi ya kutosha kwa ajili ya kuarifisha matukio muhimu ya Mapinduzi ya Kiislamu na mashahidi kwa kizazi cha sasa, Kiongozi Muadhamu amesema licha ya kupita miaka 35 lakini hadi sasa hakuna filamu, mchezo wa kuigiza wala riwaya iliyoandikwa kuhusiana na tukio la Hafte Tir (Tir 7), Shahid Beheshti na mashahidi wengiene wa tukio hilo la jinai na kwamba tukio hilo limeendelea kukumbukwa tu kutokana na kuwepo moyo wa kimapinduzi wa wananchi. Ameashiria kuandikwa vitabu vinavyohusiana na operesheni na mashahidi wa vita vya kujitetea kutakatifu na kuwashauri watu wote na hasa vijana kusoma kwa makini vitabu hivyo. Hata hivyo Kiongozi Muadhamu amesema kuwa licha ya kuandikwa vitabu vingi katika uwanja huo, lakini bado kuna uwanja wa kuandikwa vitabu zaidi kuhusiana na pande tofauti za vita hivyo vitakatifu na mashahidi watukufu wa vita hivyo. Amesema hii ni kutokana na kuwa tabia, maneno na namna ya harakati za kila mmoja wa mashahidi hao ni dirisha na mwanya wa kuelekea kwenye ulimwengu wa maarifa. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema moja ya sifa maalumu za kipindi cha vita vita vitakatifu ni kuingia kwenye medani ya vita wananchi wa kawaida waliokuwa na moyo thabiti na pia matabaka mbalimbali ya wanachi na hivyo vita kutoka katika mkondo wake wa kawaida wa kuhusisha tu askari rasmi. Amesisitiza: ‘Hii leo pia ushauri wetu kwa viongozi wa serikali ni kuwa wanapasa kunufaika na uwezo wa wananchi katika nyanja tofauti na hasa katika sekta ya uchumi na hivyo kuufanya uchumi kuwa wa wananchi (unaoendeshwa na wananchi). Ayatullah Khamenei ameendelea na hotuba yake kwa kuashiria suala la kulindwa Haram za Ahlul Beit wa Mtume (saw) na mashahidi wa kulindwa haram hizo na kusema: ‘Suala hili ni miongoni mwa mambo ya ajabu na ya kushangaza kihistoria ambapo vijana walio na imani na azma thabiti wa Iran na wa nchi zingine za dunia huwaacha kirahisi wake na watoto wao wachanga pamoja na maisha yao na kuendesha mapambano katika  njia ya Mwenyezi Mungu katika nchi ya kigeni na kuuawa shahidi katika njia hiyo.’ Amesema imani ya juu ya mashahidi wanaolinda Haram za Watu wa Nyumba ya Mtume (saw) na subira ya familia zao ni sehemu ya maudhui hiyo ya kushangaza na kuongeza: ‘Upande mwingine wa suala hili unahusiana na sifa za nguvu za Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo imesimama kwenye msingi wa imani na azma pamoja na irada ya watu wenye imani, mapambano na mashahidi.’ Huku akisisitiza kwamba maadui wa Mfumo wa Kiislamu hawana uwezo hata kidogo wa kudiriki na kufahamu misingi ya nguvu na uwezo wa mfumo huu, Kiongozi wa Mapindizi ya Kiislamu amesema: ‘Mashahidi na familia zao ni nguzo za mwamba za Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na ndio maana daima ukawa unazishinda changamoto tofauti ambazo umekuwa ukikabiliwa nazo.’ Ayatullah Khamenei ameongeza: ‘Kila mara mbapo tumekuwa tukiegemea Mapinduzi na moyo wa kimapinduzi tumekuwa na maendeleo na kila mara ambapo tumepuuza thamani na kuona haya katika kubainisha misimamo ya kimapinduzi kwa ajili ya kuwaridha Waistikbari, tumebaki nyuma na kupata hasara.’
Huku akisisitiza kuwa maadui wa Kiistikbari wanapasa kukabiliwa kwa moyo wa kimapinduzi, Kiongozi Muadhamu amesema kwamba kumwamini Mwenyezi Mungu, kuamini Jihadi na motisha imara wa vijana walio na imani na wanamapinduzi ni vyanzo vya nguvu ya Mfumo wa Kiislamu katika vita visivyo na mlingano na kambi ya uistikbari. Amesema licha ya maadui hao kuona athari za vyanzo hivyo vya nguvu lakini wameshindwa kuchambua hakika yavyo na hivyo kuamua kutumia mbinu za mabavu na zisizo na huruma. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema mpango wa kutumiwa makundi ya kigaidi na kitakfiri kama Daesh ni miongoni mwa mbinu hizo za mabavu kwa ajili ya kukabiliana na Mfumo wa Kiislamu na kuongeza: ‘Lengo kuu la kuanzishwa kwa makundi ya kigaidi na kitakfiri na vitendo vyao nchini Iraq na Syria lilikuwa ni kuishambulia Iran lakini kutokana na nguvu ya Mfumo wa Kiislamu, wamekwama katika nchi hizo zenyewe.’ Amesema kuwa makundi ya kigaidi na kitakfiri hayatenganishi kati ya Mashia na Masuni na kwamba humlenga Mwislamu yoyote ambaye anaunga mkono Mapinduzi ya Kiislamu na kuichukia Marekani. Ameashiria matukio ya Bahrain na kusema: ‘Nchini Bahrain pia suala si la Ushia na Usuni, bali suala la msingi ni utawala wa kidhalimu wa kundi dogo lenye kiburi na ubinafsi dhidi ya waliowengi.’
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kwamba uchokozi wa watawala hao wa Bahrain dhidi ya mwanazuoni mwanamapambano, Sheikh Isa Qassim ni alama ya ujinga wao. Amesisitiza kwamba Sheikh Isa ni mtu ambaye kila mara ambapo amekuwa akipata fursa ya kuzungumza na wananchi wa Bahrain amekuwa akiwakataza kutumia njia za nguvu na silaha lakini watawala wa Bahrain hawafahamu kuwa kumchokoza mwanazuoni huyo mwanamapambano kuna maana ya kuondoa kizuizi  mbele ya vijana walio na hamasa na hamu kubwa wa nchi hiyo kuchukua hatua yoyote dhidi ya serikali. Huku akisisitiza kuwa madola ya kiistikbari na vibaraka wao daima hushindwa kutambua nguvu ya wananchi na imani ya jamii na hivyo kufanya makosa makubwa katika mahesabu yao, Ayatullah Khamenei ameongeza: ‘Njia sahihi ni kutembea kwenye nji ya Uislamu na kumtegemea Mwenyezi Mungu Mtukufu na ni taifa lililo na imani na linalopambana na kuwa na azma thabiti tu ndilo linaloweza kuvuka vizuizi na kuendelea.’ Kiongozi Muadhamu amewahusia watu wote kufanya juhudi za kunufaika zaidi na nyusiku hizi za Leilatul Qadr na siku za mwisho za mwezi huu mtukufu wa Ramadhani na kusema kwamba katika nyusiku na nyakati hizi za daku ambao ni wakati wa kutawasali na kuomba dua, tunapasa kuomba msaada wa nyoyo tukufu zikiwemo za mashahidi na kutawasali nao kwa unyenyekevu na kuomba dua kwa namna ambayo itamfanya Mwenyezi Mungu Mtukufu atuzingatie.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatul Islam wal Muslimeen, Mohammad Ali Shahidi, Mwakilishi wa Kiongozi Muadhamu na Mkuu wa Taasisi ya Mashahidi na Masuala ya Mashujaa wa Vita amezungumzia umuhimu wa kizazi cha vijana kufahamishwa kujitolea na hamasa ya wapiganaji wa Kiislamu na kuongeza kuwa kubuniwa na kuanza kufanya kazi kwa sekretarieti ya Baraza Kuu la Kueneza na Kusambaza Utamaduni wa Kujitolea na Ushahidi, kuanzishwa kwa mrengo wa intaneti, kuenezwa kwa vitengo vya kujitolea, kutekelezwa mpango wa shukrani na kubuniwa kitengo cha uchumi ngangari kwa ajili ya kuimarisha uwezeshaji katika jamii inayojitolea, ni miongoni mwa mambo muhimu ambayo yametekelezwa na taasisi hiyo.

 

700 /