Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Wajibu wa Umma wa kutetea Palestina utaonekana Siku ya Quds

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei alasiri ya leo (Jumatano) amekutana na kuhutubia hadhara iliyojumuisha Mkuu wa Idara ya Vyombo vya Mahakama nchini Iran na maafisa na wafanyakazi wa idara hiyo ambako amesisitiza kuwa usafi wa chombo hicho na juhudi za siku zote za kuwaridhisha wananchi ni wadhifa muhimu na lengo kuu la Idara ya Vyombo vya Mahakama. Ameashiria suala la kukaribia Siku ya Kimataifa ya Quds na kusisitiza kuwa: Kwa Baraka zake Mwenyezi Mungu, siku ya Ijumaa nchini Iran na duniani kote itasikika tena sauti moja ya kuwatetea watu wanaodhulumiwa wa Palestina, na Umma wa Kiislamu utatekeleza faradhi muhimu ya kuwatetea watu wanaodhulumiwa. 
Mwanzoni mwa mkutano huo Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amemkumbuka na kumtaja kwa wema marehemu shahidi Ayatullah Muhammad Beheshti, mwasisi wa Idara ya Vyombo vya Mahakama nchini Iran na kumtaja kuwa alikuwa mudiri mwenye fikra nzuri, imara, mwenye tadbiri na mfuatiliaji. Vilevile amewashukuru maafisa waandamizi, wakurugenzi na wafanyakazi wa Idara ya Vyombo vya Vyombo vya Mahakama hapa nchini kwa jitihada zao kubwa.
Ayatullah Khamenei pia amemsifu Mkuu wa Idara ya Vyombo vya Mahakama akimtaja kuwa ni msomi mwenye hikima na kamili na kusema kuwa, Idara ya Vyombo vya Mahakama ina umuhimu mkubwa sana kutokana na majukumu yake kama kusimamia utekelezaji wa sheria, kuzuia uhalifu na kutokana na kuwepo mkuu wa idara hiyo katika mabaraza ya juu na asili ya utawala wa Kiislamu hapa nchini.
Ayatullah Khamenei amesema, kutokana na umuhimu huo mkubwa na wa aina yake, hatua na utendaji wa Idara ya Vyombo vya Mahakama daima umekuwa na unyeti makhsusi, na idara hiyo imekuwa ikilengwa kwa hujuma na propaganda nyingi mbaya.
Amesema propaganda chafu za vyombo vya habari vya kigeni na hujuma dhidi ya Idara ya Vyombo vya Mahakama hapa nchini zimeongezeka sana katika kipindi cha sasa na sababu yake ni misimamo ya kimapinduzi, ya thamani na ya wazi ya mkuu wa idara hii na maafisa wake wa ngazi za juu.
Ayatullah Khamenei ametilia mkazo umuhimu wa suala la kuwaridhisha wananchi akisema kuwa, ni wadhifa wa Kiislamu na lengo la kimsingi. Amesema, kulinda usafi wa Idara ya Vyombo vya Mahakama ndiyo sababu kuu ya kuwaridhisha wananchi. Amesisitiza kuwa: Kuna ulazima wa kupambana ipasavyo na kwa nguvu zote na watu wahalifu na mafisadi ndani ya Idara ya Vyombo vya Mahakama katika mikoa na miji yote, na mbinu hiyo inapasa kudumishwa. 
Amewaambia viongozi wa chombo hicho kwamba: "Lipeni umuhimu wa daraja la kwanza suala la usafi wa Idara ya Vyombo vya Mahakama na mulitambue kuwa ni kazi muhimu na ya msingi". 
Ayatullah Khamenei pia ametilia mkazo udharura wa kuuelimisha umma kuhusu jinsi idara hiyo inavyopambana na wahalifu ndani ya chombo hicho. 
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, watu wachache wanaofanya ufisadi na vitendo vilivyo kinyume na sharia ndani ya Idara ya Vyombo vya Mahakama, mbali na kwamba wanawasaliti wakurugenzi na wafanyakazi wanaotoa huduma kwa bidii na kwa mashaka wa chombo hicho, wanawadhulumu pia wananchi. 
Ayatullah Khamenei amesema kuwa, miongoni mwa masharti ya ufanisi wa Idara ya Vyombo vya Mahakama ni kuwa na ratiba kabambe na ya kipindi maalumu kwa ajili ya utekelezaji wa mipango, kuzuia uhalifu na kufanya marekebisho ya sheria. Amesisitiza tena ulazima wa kupunguzwa adhabu ya kifungo na kusema: Kuna ulazima wa kutumiwa weledi na wataalamu waliobobea kwa ajili ya kubuni adhabu mbadala wa kifungo jela.
Kuhusu suala la kuzuia uhalifu, amesema kuwa, suala hilo lina umuhimu mkubwa sana na linavihusu vyombo na mihimili yote ya dola na linahitaji fikra, ujuzi na tajiriba. 
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, miongoni mwa kazi za dharura sana za Idara ya Vyombo vya Mahakama ni kuakisi habari kuhusu huduma zake na kuwapa wananchi taarifa kuhusu huduma hizo. Ameongeza kuwa, kuna ulazima wa kutumiwa mbinu za kisasa na za kuvutia za upashaji habari kwa ajili ya kuakisi kiwango kikubwa cha kazi zinazofanywa na Idara ya Vyombo vya Mahakama hapa nchini. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kutoa mafunzo ya kuvutia ya masuala ya sheria na mahakama kwa wananchi kutapelekea kupungua idadi ya watu wanaokwenda mahakamani na amewausia maafisa wa Idara ya Vyombo vya Mahakama walipe uzito na umuhimu mkubwa suala la kuandaa uwanja mzuri wa wananchi kuweza kutumia ushauri kuhusu masuala ya sheria na mahakama kwa masaa 24 kwa siku. 
Vilevile amesisitiza udharura wa Idara ya Vyombo vya Mahakama hapa nchini kufuatilia kisheria masuala ya kimataifa na kuongeza kuwa: Ufuatiliaji wa haki zilizokanyagwa za taifa la Iran kutokana na vikwazo unapaswa kuwekwa kwenye ajenda ya Idara ya Vyombo vya Mahakama.
Ayatullah Khamenei ameashiria hukumu iliyotolewa na mahakama ya Marekani kwa ajili ya kupora mali za taifa la Iran kwa kutumia visingizio na tuhuma zisizo na msingi na kusema kuwa: Kukanyagwa kwa haki za taifa la Iran kupitia njia ya vikwazo ni uhakika ambao unapaswa kufuatiliwa kisheria katika upeo wa kimataifa.
Miongoni mwa mambo yaliyousiwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa maafisa wa Idara ya Vyombo vya Mahakama hapa nchini ni kufuatilia haki za maelfu ya wahanga wa ugaidi nchini Iran, kufungua mashtaka dhidi ya nchi zinazowasaidia na kuwaunga mkono waziwazi na kwa siri wauaji wa wahanga hao na kuwatetea kisheria shakhsia wa Kiislamu wanaodhulumiwa kote dunia.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa, miongoni mwa nyadhifa za Idara ya Vyombo vya Mahakama hapa nchini ni kuhuisha haki za binadamu za Kiislamu katika upeo wa kimataifa. Amesema: Haki za binadamu zinazotajwa na Magharibi zimebuniwa kwa kutumia misingi isiyo sahihi na kuna ulazima wa kubainishwa na kufuatiliwa haki za binadamu za Kiislamu katika fikra za watu duniani na kwenye duru za sheria kwa kutumia misingi imara na kimantiki.
Amesema tangazo rasmi la Umoja wa Mataifa la kufumbia jicho jinai zinazofanyika sasa na mauaji ya watoto nchini Yemen mkabala wa kupokea fedha kutoka kwa baadhi ya nchi ni fedheha na aibu kwa wanadamu na kuongeza kuwa: Fedheha hii ni dhidi ya haki halisi za binadamu na tunapaswa kuifanyia kazi ya kisheria na katika vyombo vya mahakama katika upeo wa kimataifa.
Mwishoni mwa hotuba yake Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, Idara ya Vyombo vya Mahakama hapa nchini inapaswa kuwa ya kimapinduzi mia kwa mia na ifanye kazi kimapinduzi. Ameongeza kuwa: Umapinduzi unaokusudiwa hapa, tofauti na mitazamo na propaganda chafu za baadhi, si kuwa na misimamo ya kuchupa mipaka, bali una maana ya kutenda kazi kwa uadilifu, kwa mantiki, kwa umakini, kwa huruma, kwa insafu, kwa umadhubuti na bila ya kumuonea haya mtu yeyote. 
Kabla ya hotuba ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Mkuu wa Idara ya Vyombo vya Mahakama nchini Ayatullah Sadiq Amoli Larijani alitoa ripoti kuhusu hatua na kazi muhimu zaidi zilizofanywa na idara hiyo.
Ayatullah Larijani amesema kuwa, huduma za Idara ya Vyombo vya Mahakama ni kubwa na pana sana na katika uwanja huo ameashiria mwenendo wa kushughulikiwa zaidi ya mafaili milioni 14 katika mahakama na mabaraza ya kutatua hitilafu na huduma zaidi ya milioni 70 za usajili wa masuala mbalimbali katika mwaka ulipota.
Mkuu wa Idara ya Vyombo vya Mahakama amesema kuwa, kuzidisha usimamizi juu ya utendaji wa majaji na wafanyakazi na kupambana ipasavyo na ufisadi kwa shabaha ya kudhamini usafi wa hahakama ni miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na idara hiyo. Ameongeza kuwa: Kukabiliana bila ya kujali lolote na kwa nguvu zote na mafisadi wa kichumi wakiwemo wale wa faili la watuhumiwa wa kesi ya mafuta ya petroli na kushughulikia mafaili ya kucheleshwa kwa kiwango kikubwa cha mikopo ya benki na vilevile kutayarisha mazingira salama na ya amani ya kiuchumi kwa ajili ya uzalishaji na uwekezaji ni miongoni mwa sera na hatua muhimu zilizochukuliwa na Idara ya Vyombo vya Mahakama.
Ayatullah Amoli Larijani ameashiria sisitizo la Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu la kupunguzwa idadi ya wafungwa na kusema: Katika uwanja huo kumebuniwa mpango kamili na makini na sasa tunafuatilia adhabu mbadala ya kifungo. Ameongeza kuwa, kiwango cha wafungwa wanaohukumiwa vifungo jela pia kimepungua kwa asilimia 20.
Mkuu wa Idara ya Vyombo vya Mahakama nchini pia ameashiria kazi zilizofanyika katika kuzuia uhalifu, marekebisho ya sheria na kadhalika na kusema kuwa upungufu wa bajeti na nguvu kazi ni miongoni mwa matatizo yanayoikabili idara hiyo.        
 

700 /