Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi akutana na wanachuo

Nasaha 12 za Kiongozi kuhusu majukumu ya jumuiya za wanachuo

Jumamosi alasiri Julai 2, wanachuo zaidi ya elfu moja wakiwemo wawakilishi wa jumuiya tofauti za wanachuo wamekuwa na mkutano wa kirafiki wa karibu masaa matano na Ayatullah Ali Khamenei Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ambapo wametoa madukuduku yao ya kiutamaduni, kijamii, kisiasa, na kiuchumi kuhusiana na kizazi cha vijana na kupata kusikia mitazamo ya Kiongozi Muadhamu kuhusiana na masuala ya wanachuo, vyuo vikuu, majukumu muhimu ya wanachuo katika mkondo wa mapambano ya taifa na masuala mengine muhimu ya siku. Kiongozi Muadhamu amesisistiza kuwa kukutana na wanachuo katika siku tukufu za mwezi wa Ramadhani ni jambo la kuvutia sana na linalofaa na kuongeza kuwa masuala tofauti yaliyopendekezwa na kujadiliwa katika kikao hicho ni mazuri na ya kuvutia sana, ambayo yanaashiria kuboreka kwa kiwango cha fikra na matakwa ya tabaka la wanachuo. Amesema jambo hilo linaonyesha kwamba kwa kupita wakati, mielekeo ya kimapinduzi, fikra pevu na hoja za nguvu zimeongeza pakubwa miongoni mwa wanachuo. Amewanasihi wanachuo kuzingatia na kufarijika zaidi na Qur’ani Tukufu pamoja na dua na kusema: ‘Msingi wa matamshi yangu kwa wanachuo ni kuimarisha imani kwa sababu ni kupitia imani thabiti tu ndipo tunaweza kupambana vilivyo na matatizo na mashinikizo. Kiongozi Muadhamu amesema kwamba hali maalumu na nyeti ya hivi sasa nchini inashabihiana sana na ile ya zama za vita vya Ahzab (makundi) katika zama za Mtume Muhammad (saw) na kuongeza: ‘Leo pia wanaoabudu dunia na wenye kiburi ulimwenguni wamesimama dhidi ya Jamuri ya Kiislamu ya Iran na kuihujumu kutokea kila upande’. Ayatullah Khamenei amesema katika hali kama hiyo watu walio na imani dhaifu na pengine kuvutiwa kwa ndani na adui huwa wanakata tamaa, kupoteza matumaini na kujiona kuwa duni lakini watu walio na imani thabiti husimama imara wakiwa na izma na irada thabiti, hali iwe ngumu itakavyokuwa. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kwamba kama tunataka kusimama imara mbele ya kambi ya uistikbari na kufikia utukufu na heshima inayofaa ya Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tunapasa kulinda na kuimarisha takwa katika mienendo yetu ya mtu binafsi na ya kijamii. Ametolea hoja baadhi ya aya za Qur’ani tukufu kuhusiana na kuporomoka kwa baadhi ya vizazi vya mataifa yaliyokuwa na imani na kusema, kupuuza swala na kufuata matamanio ni masuala mawili ya msingi yanayoporomosha na kudhoofisha ukakamavu na mapambano. Ayatullah Khamenei amesema: ‘Hii ndiyo sababu ya mimi kuwasisitizia mara kwa mara wakuu (wa vyuo) juu ya ulazima wa kuzuia safari za mchanganyiko za wanachuo (wa kike na kiume). Hii ni kwa sababu kutozingatiwa mipaka ya kidini hudhoofisha imani ya ndani.’ Baada ya kubainisha nafasi ya imani katika mapambano, Kiongozi Muadhamu amezungumzia mapambano muhimu na yasiyoepukika ya taifa la Iran na kambi ya uistikbari na kusema: ‘Mapambano hayo yalianza pale taifa la Iran lilipoamua kujitawala na kuwa na maendeleo jambo ambalo lilipingana na maslahi ya madola yanayoudhibiti ulimwengu.’ Ayatullah Khamenei amesema kwamba matamshi ya baadhi ya watu wanaodai kwamba Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu unatafuta visingizio vya kutoshirikiana na madola muhimu ya dunia ni ya kiuwanagenzi na yasiyo na msingi wowote. Amesema mapambano haya hayahitajii kisingizio chochote kwa sababu madamu taifa la Iran litaendelea kusimama kwenye msingi wa heshima na uzoefu wa Mapinduzi ya Kiislamu, mapambano hayo yataendelea kuwepo na kwamba kuna njia mbili tu za kuyamaliza, ima Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ifikie nguvu na uwezo mkubwa ambao utaufanya upande wa pili kutothubutu kuichokoza au Jamhuri ya Kiislamu ipoteze utambulisho wake wa asili na kugeuka kuwa mfumo mtupu usiokuwa na utambulisho wowote. Huku akisisitiza kwamba njia ya kwanza yaani ya kuwa na nguvu kubwa ndiyo iliyochaguliwa na taifa la Iran kwa ajili ya kumalizika mapambano hayo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: ‘Ni wazi kuwa huenda leo siasa za Marekani zina maslahi katika kutaka kuwagawa viongozi wa Mfumo wa Kiislamu katika makundi mawili ya viongozi wabaya na wazuri, lakini Wamarekani wakipata uwezo watawaita viongozi haohao wanaowataja kuwa ni wazuri kuwa wabaya.’ Ayatullah Khamenei amesema utambulisho wa Mfumo wa Kiislamu ndiyo sababu kuu ya maadui kukabiliana na taifa la Iran na kuongeza kuwa makusudio ya Mfumo wa Kiislamu ni mjumuiko wa muundo wa Mfumo, thamani  na malengo yake kama vile uadilifu, maendeleo ya kielimu, maadili, demokrasia, kuheshimiwa sheria na kuwa na malengo matukufu. Huku akisisitiza kwamba kwenye mapambano haya kuna matatizo makubwa ambayo yanaweza kutatuliwa kupitia mapambano na mipango mizuri, Ayatullah Khamenei amesema kwamba wanachuo wakiwa ndio kiini cha uwezo wa taifa wana nafasi maalumu katika mapambano na njia hii utatuzi wa matatizo hayo.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema matakwa ya wanachuo yana umuhimu mkubwa na kusisitiza kwamba utatuzi wa matatizo muhimu ya nchi unawahusu viongozi wa ngazi za juu serikalini na kwamba iwapo matakwa ya wanachuo yatachunguzwa kwa makini kwa kutegemea habari na maelezo sahihi bila shaka jambo hilo litaandaa mazingira ya viongozi kufanya juhudi zaidi za kutatua matatizo yaliyopo. Ayatullah Khamenei ameashiria baadhi ya matakwa ya wanachuo katika kikao hicho likiwemo suala la mikataba mipya ya mafuta na kusema: ‘Kama marekebisho ya lazima hayatafanyika katika mikataba hiyo kwa ajili ya kulinda maslahi ya nchi, bila shaka mikataba hiyo haitatiwa saini.’ Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria ukosoaji wa wanachuo kuhusiana na maamuzi yaliyochukuliwa katika baadhi ya idara nchini na kusema: ‘Kwa mujibu wa sheria na mantiki, Kiongozi (Muadhamu) hawezi kuingilia kati maamuzi madogo madogo  na ya kiutendaji ya idara za serikali na iwapo viongozi watendaji watafanya makosa, Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge) inapasa kutumia vyombo (uwezo) vyake vya usimamizi kama vile vya kusaili au rais wa nchi aingilie kati na kuzuia utekelezwaji wa uamuzi huo wa kimakosa.’ Ameendelea kusema kwamba ni wazi kuwa Kiongozi Muadhamu anaweza kuingilia kati hata kwenye masuala madogo madogo na kuzuia utekelezwaji wake iwapo atahisi kwamba yanaweza kuufanya Mfumo utoke kwenye njia yake ya asili. Ayatullah Khamenei ameashiria matatizo yanayotokana na mapambano na kusimama imara nchi na kusema kwamba baadhi ya masuala yakiwemo ya kuimarisha uchumi na uwezo wa kiulinzi wa nchi ni miongoni mwa masuala muhimu ya taifa ambayo kuthibiti na kutatuliwa kwake ni jukumu la viongozi. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza: ‘Baadhi ya matatizo yanahusiana na ndani ya nchi ambapo jumuiya za wanafunzi zinapasa kuwasilisha njia za utatuzi na hivyo kuwasaidia viongozi kuyatatua.’ Amesema kujiepusha kukata tamaa na uzembe ni siri ya utatuzi wa matatizo na kuziambia jumuiya za wanafunzi kwamba iwapo zitasimama imara na kuzishawishi fikra za watu kupitia mazungumzo ya umma ni wazi kuwa viongozi pia watalazimika kujibu matakwa yao. Akiashiria matamshi ya mmoja wa wanachuo kuhusiana na athari mbaya za kutolewa matamshi ambayo yanakwenda kinyume na maneno ya Kiongozi, Ayatullah Khamenei amesema kuwa amesema mara nyingi kwamba kutamka maneno yanayopingana   ya Kiongozi sio uhalifu wala pingamizi dhidi yake. Akiendelea na hotuba yake Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kwamba wanachuo ni fursa kubwa, utajiri mkubwa  na moja ya nukta za nguvu za Mfumo wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusisitiza ya umuhimu wa kuzingatiwa kwa njia maalumu tabaka hili muhimu na viongozi katika upangaji wa miapnago yao. Amesema wanafunzi wa sasa wakilinganishwa kiviwango na ubora na wa mwanzoni mwa Mapinduzi ya Kiislamu,  wako juu zaidi na kwamba wana uelewa na fikra za kina zaidi kuhusiana na Mapinduzi na Uislamu. Ayatullah Khamenei ameongeza kwamba wanachuo wengi wa kimapinduzi na walio na hamu kubwa wa mwanzoni mwa Mapinduzi hii leo ni miongoni mwa watafiti na wasomi wakubwa nchini na kwa hivyo hakuna pingamizi yoyote kati ya kuwa mwanamapinduzi na kusoma. Amewanasihi wanchuo kusoma vizuri sambamba na kuimarisha imani na umaanawi wao na kuongeza: ‘Wanachuo pia wanapasa kuwa na mwamko na wakiwa katika mazingira ya uanachuo, kuyatazama kwa macho yaliyo wazi, masuala na matukio ya nchi, ya kieneo na kimataifa.’ Kiongozi wa Mapiduzi ya Kiislamu amesisitiza kwamba iwapo mwanachuo hatakuwa na mwamko na macho yaliyo wazi huenda akafanya makaso katika mahesabu ya kumjua rafiki na adui yake au katika kuchambua masuala ya kieneo na kimataifa. Amewasihi wanachuo wote kuwa na dhana mbaya na vyombo vya habari vya maadui na kusema: ‘Kwa kutumia ghama kubwa maadui wameanzisha harakati kubwa na isiyofahamika vyema ya vyombo vya habari dhidi ya Mfumo wa Mapinduzi ya Kiislamu lengo lake halisi likiwa ni kufunika mafanikio ya Jamhuri ya Kiislamu na kupanua kuliko kiasi baadhi ya nukta zake za udhaifu ili kuchochea ukataji tamaa na kutokuwa na matumaini miongoni mwa wananchi na vijana.’ Kiongozi wa Mapinduzi amesema kutoakisiwa pakubwa au kutoakisiwa kabisa maandamano makubwa ya Siku ya Kimataifa ya Quds na vyombo vya habari vya kigeni ni mfano mmoja wa utendaji mbaya wa vyombo hivyo vya adui kuhusiana na Iran na kusisitiza: ‘Maandamano ya Siku ya Quds katika siku ya Ijumaa na katika joto kali na katika hali ya kufunga Saumu kwa hakika ni tukio kubwa lakini tukio hilo la nadra halikuakisiwa inavyopasa katika vyombo vya habari vya kigeni. Hii ni katika hali ambayo ikiwa kuna nukta ya udhaifu vyombo hivyo huifanya nukta hiyo kuwa kubwa mara mia moja zaidi.’ Huku akiendelea na hotuba yake, Kiongozi Muadhamu amesema kwamba majukumu ya wanachuo wanachama wa jumuiya za wanachuo ni makubwa zaidi kuliko ya wanachuo wengine wa kawaida na huku akiashiria utata wa masuala ya hivi sasa ya kisiasa nchini ameongeza kwamba katika muongo wa kwanza wa Mapinduzi na katika kipindi cha vita vya kujitetea kutakatifu, kupambana na adui ni jukumu lilikokuwa wazi na kufahamika na kila mtu lakini leo kuchanganyika mambo tofauti ya kiutamaduni, kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiusalama ni mambo ambayo yamefanya hali ya mambo kuwa ya utata mkubwa na inayoandamana na majukumu makubwa na mazito, ambayo utatuzi wake unahitajia macho yaliyo wazi, umakini mkubwa, akili na busara. Ayatullah Khamenei baada ya kufafanua utata na pande kadhaa za mazingira ya hivi sasa amebainisha nasaha 12 katika kuweka wazi majukumu ya jumuiya za wanachuo. Nasaha yake ya kwanza kwa wanachuo wanaharakati ilikuwa ni kuwepo kwao kifikra katika masuala muhimu ya nchi na kuhudhuria kimwili katika matukio ya lazima. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kwamba kutangazwa misimamo ya jumuiya za wanachuo katika masuala muhimu ya nchi ni jambo lililo na umuhimu mkubwa na kusema: ‘Iwapo misimamo hiyo madhubuti na ya msingi itatangazwa kwa njia nzuri na iliyo wazi, bila shaka marafiki wa Mapinduzi watapata nguzu zaidi na maadui wa nchi wakiwemo Wamarekani kufahamu kwamba hawapasi kufurahia ripoti zilizopotoshwa na bandia kuhusiana na vijana wa Kiirani.’ Ayatullah Khamanei amesema, mapatano ya nyuklia na madola sita makubwa ya dunia mashuhuri kwa jina la JCPOA, uhusiano na Marekani, uchumi ngangari na mustakbali wa nchi ni miongoni mwa masuala muhimu ya nchi ambapo amesema jumuiya za wanachuo ni mfano wa maafisa wa vita laini ambapo wanatakiwa kubainisha kwa dalili madhubuti na za kukinaisha, misimamo ya Mapinduzi. Amesema jumuiya za wanachuo zinapasa kuchukua misimamo kwa msingi wa habari madhubuti, sahihi, zenye hoja na kwa wakati na misimamo hiyo kuakisiwa vizui katika majarida, magazeti na vitabu vinavyochapishwa na wanachuo. Amesema misimamo hiyo pia inaweza kuakisiwa kwenye jamii kwa njia nyingine zikiwemo za wawakilishi wa jumuiya za wanachuo kupewa fursa ya kutoa hotuba zao kabla ya hotuba za swala ya Ijumaa katika miji mikubwa nchini. Kiongozi Muadhamu amesema kuwa mara nyingine mahudhurio ya kimwili ya wanachuo huwa ya lazima katika baadhi ya sehemu lakini kwa njia sahihi zinazoruhusiwa kisheria. Huki akisisitiza upinzani wake wa daima kuhusiana na hatua ya kuvurugwa kila mikusanyiko na vikao, Ayatullah Khamenei amesema kuwa jambo hilo lina madhara au kwa uchache halina faida na kwamba ikibidi vikao vingine vinapaswa kuitishwa kando ya vikao kama hivyo vya upinzani ili kubainisha mambo kwa sababu anachokitaka mwanachuo ni kupata kusikia ukweli. Kuhusiana na suala hilo Kiongozi Muadhamu amewataka viongozi wa wizara za elimu na afya na vilevile wa vyuo vikuu kuzisaidia jumuiya za kimapinduzi. Amesema licha ya kuwa ni wazi kuwa jumuiya zote zina haki sawa za umma lakini ni jambo la wazi na kimantiki kuwa viongozi wa vyuo vikuu wanapasa kuunga mkono na kuzitetea jumuiya za kimapinduzi na kidini ili kuziwezesha zaidi jumuiya hizo.
Kukinai nyoyo ni nasaha ya pili aliyotoa Kiongozi Muadhamu kwa jumuiya za wanachuo. Amesisitiza kwamba kwa mtazamo wa fikra ya Kiislamu, kukinai na kuvutia nyoyo ni msingi muhimu na kwamba jumuiya za wanachuo zinapasa kuwabainishia wanachuo na wananchi misimamo yao kwa kutomia hoja za nguvu na zilizo wazi. Ayatullah Khamenei amesema masuala kama vile uchumi ngangari, maendeleo ya kielimu, maisha ya kawaida na uhusiano na Marekani ni miongoni mwa mambo ambayo jumuiya za wanachuo zinapasa kubainisha misimamo yao kuhusiana nayo. Kuhusu uhusiano na Marekani Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: ‘Jumuiya za wanachuo zinapasa kuzingatia kwa makini baadhi ya misimamo ya Kiongozi kwa mfano kuhusiana na kupinga kwake kuanzishwa uhusiano na Marekani na mazungumzo na nchi hiyo isipokuwa katika baadhi ya masuala maalumu, na huku zikiwa na ufahamu mzuri wa hoja madhubuti zilizotumika katika kupinga suala hilo, ziwabainishie wanachuo na wasiokuwa wanachuo hoja hizo kwa njia bora zaidi na za dalili zenye nguvu.’ Amesema kudumu na kubainishwa kwa njia sahihi, za wazi na zenye hoja misimamo ya jumuiya za kimapinduzi za wanachuo ni jambo lenye taathira na la dharura katika kuianishwa matakwa ya umma na muelekeo wa nchi katika njia sahihi.
Kuboreshwa kiwango cha uelewa wa kisiasa na kidini ni nasaha ya tatu aliyoitoa Kiongozi Muadhamu kwa jumuiya za wanachuo. Ayatullah Khamanei pia amesema kupanuliwa kiwango cha idadi ya watu wanaohutubiwa na wanachuo ni miongoni mwa makujumu mengine ya jumuiya za wanachuo na kuongeza kuwa maadili, subira, kuvumilia kusikiliza maneneo ya upande wa upinzani na kuyadhibiti vyema mambo yaliyowasilishwa ni mambo yanayohitajika kabla ya kutekelezwa majukumu hayo. Nasaha ya tatu ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa jumuiya za wanachuo ilikuwa ni kutetea waziwazi na bila ya kufanya takiya Mfumo wa Kiislamu. Amesema kwa kutegemea uhaba, kasoro na makosa adui anataka kuonyesha kuwa Mapinduzi yana thamani ndogo na hivyo kupuuza maendeleo na mafanikio ya Mfumo ambapo Jumuiya za kimapinduzi zinapasa kuvunja mlingano huo usiokuwa sawa. Ayatullah Khamanei ameendelea kusema kuwa kusimama imara kwa muda wa miaka 37 mbele ya uadui wa kambi kubwa ya madola ya kimaada yaliyozatiti barabara ni mafanikio muhimu zaidi ya Mfumo bora na wenye fahari wa Mapinduzi ya Kiislamu na hasa katika mazingira haya ambapo kukasirishwa kudogo tu kwa madola hayo hupelekea utawala fulani wa kifalme unaojigamba, kunyenyekea na kusalimu amri. Amesema wingi na ubora wa uchangamfu wa wanachuo wa kimapinduzi ni alama ya kuwa hai, utayarifu na uwezo wa dhati wa Mapinduzi na kuongeza: ‘Ni wazi kuwa makusudio ya kutetea Mfumo sio kumtetea Kiongozi bali ni kutetea mjumuiko wa thamani zinazofungamana ambazo zinategemewa na Mapinduzi katika kuendelea kustawi na kukua.
Kudumishwa na kuimarishwa kambi (vituo) za jihadi katika maeneo ya vijijini na ya watu masikini ni nasaha ya sita aliyotoa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi kwa jumuiya za wanachuo katika kikao hicho. Amesema kambi za vijijini ni mfano wa ujenzi wa dhati, huduma na pia kuelewa hali halisi ya nchi. Huku akiashiria msimamo wake wa daima kuikumbusha serikali ya hivi sasa na nyingine zote zilizopita, kuhusiana na udharura wa kuyashughulikia maeneo ya vijijini, Ayatullah Khamenei amesema: ‘Kuthibiti kwa jambo hili kuna njia zilizo wazi ambapo kuanzishwa kwa viwanda vidogo vidogo na vya kubadili bidhaa ni miongoni mwa njia hizo. Bika shaka kutekelezwa ushauri huu wa daina kunahitaji jitihada.’
Kuzingatiwa kifikra na kimatendo maisha ya kawaida ya Kiirani na kiislamu na kuimarishwa mijadala mikuu ya Mapinduzi ukiwemo uadilifu, uchumi ngangari uliosimama juu ya msingi wa elimu, maendeleo ya Kiislamu na Kiirani na kasi ya elimu, ni nasaha za saba na nane alizozitoa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa jumuiya za wanachuo. Kuhusiana na suala hilo alisema: ‘Mimi sikubali hata kidogo ustawi wa Magharibi kwa sababu misingi na nguzo zake ni makosa na ndio maana nikawasilisha pendekezo la ‘mjadala wa maendeleo ya Kiislamu Kiirani.’ Kuhusu Uchumi ngangari, Kiongozi wa Mapinduzi pia amesema: ‘Kwa mujibu wa ripoti zilizonifikia, kazi nzuri zinafanyika kwa sharti kuwa ziendelee kufanyika.’ Katika nasaha yake ya tisa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa wito wa kubuniwa mrengo mmoja ulio dhidi ya Marekani na uzayuni katika kiwango cha wanachuo wa ulimwengu wa Kiislamu. Amesema kwa kutegemea vyombo vya kisasa vya mawasiliano na intaneti, kampeni za umma za wananchuo wa Kiislamu zinaweza kuanzishwa kwa msingi wa upinzani dhidi ya siasa za Marekani na utawala wa Kizayuni ili inapobidi mamilioni ya wanachuo wa Kiislamu wabainishe misimamo yao na hivyo kuweza kubuni harakati kubwa katika Ulimwengu wa Kiislamu.
Kuepuka kuwatuhumu watu kuwa sio wa kimapinduzi ni nasaha ya kumi aliyoitoa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi kwa wanachuo katika kikao hicho. Amewaambia wanachuo: ‘Umapinduzi una viwango na vipimo maalumu, kwa hivyo msiwatuhumu wale watu ambao wana mitazamo tofauti na yenu lakini wakawa wana vipimo hivyo kuwa sio wanamapinduzi.’
Kuimarishana na kukamilishana jumuiya za kimapinduzi katika vyuo vikuu kwa kutegemea nukta za pamoja kati yao ilikuwa nasaha ya kumi na moja ya Kiongozi Muadhamu kwa jumuiya za wanachuo. Amesema kwamba hitilafu hazipasi kubadilishwa kuwa mvutano na kwamba jumuiya za kimapinduzi zinapasa kutenda kazi kwa namna ambayo itaeneza utamaduni wa kuwavumilia wapinzani katika mazingira ya vyuo vikuu.
Kutazamwa Mapinduzi kwa mtazamo wa kistratijia na kutafakari kuhusu mustakbali ni nasaha ya mwisho aliyowapa Kiongozi Muadhamu wanachuo waliokutana naye leo. Aliwaambia: ‘Marais wa miongo ya baadaye wa nchi, wabunge na wakuu wa baadaye wa nchi watachaguliwa kutoka miongoni mwenu wapendwa. Kwa hivyo kuweni na matumaini makubwa na yaliyojaa uchangamfu na mchore  picha ya ruwaza ya nchi ya miaka 20 au 30 ijayo na kuanzisha harakati yenu hii leo kwa msingi wa upeo huo unaong’ara.’
Katika sehemu ya mwisho ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu alibainisha masuala kadhaa kuhusiana na mambo yanayoendelea ndani ya nchi. Amekosa baadhi ya watu ambao licha ya kudai kuunga mkono Mfumo, Imam (MA) na Mapinduzi lakini bado hawajaweka wazi misimamo yao kuhusiana na fitina iliyozuka nchini mwaka wa Kiirani wa 1388 (2009). Amesema: ‘Msimamo wangu kuhusu fitina ya 88 uko wazi kabisa na ninalipa uzito mkubwa suala hili na kipimo pia ni kutowaunga mkono waliokuwa wakiongoza fitina na kuitumia vibaya na hadi sasa bado hawajatangaza kujitenga nayo.’ Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kwamba ugawaji wa watu katika makundi kama vile wafuasi wa misingi na wapenda mageuzi au wapenda mageuzi wa kisasa na wafuasi wa misingi wa jadi si muhimu hata kidogo bali suala lililo na umuhimu ni uzito wa maudhui. Ayatullah Khamenei pia amezungumzia masuala yanayojadiliwa nchini kuhusu udharura wa kuzingatiwa busara na mantiki na kusema, siku hizi kuna masuala mengi yanayojadiliwa kuhusiana na udharura wa majadiliano kati ya mirengo ya kisiasa kufanyika kwa msingi wa akili na busara ambapo asili ya suala la kutumika akili ni jambo zuri sana na linaloungwa mkono na Uislamu, Qur’ani ambapo Imam Khomeini (MA) pia alikuwa miongoni mwa watu wenye busara kubwa duniani. Aliyataja Mapinduzi ya Kiislamu kuwa mapinduzi ya watu wenye busara na kuongeza: ‘Kwa msingi wa busara, tunapasa kusema kuwa wale watu wanaoamini kwamba tunapasa kukimbilia Magharibi kwa ajili ya kufikia maendeleo kwamba wamepoteza akili zao kwa sababu akili inatwambia kwamba tunapasa kujifunza kutokana na uzoefu.’ Huku akiashiria uzoefu mbaya wa taifa la Iran kuhusu Magharibi kukiwemo kulazimishwa udikteta wa Kipahlawi, kupinduliwa kwa serikali ya taifa na kuasisiwa chombo cha ukandamizaji na unyama cha Sawak, Kiongozi Muadhamu amesema: ‘Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu pia, vikwazo vya kwanza, hiana, ujasusi, hujuma kubwa ya kipropaganda, uungaji mkono kwa makundi yaliyo dhidi ya Mapinduzi, ulazimishaji wa vita vya miaka minane, uungaji mkono wa pande zote kwa Saddam, kutunguliwa ndege ya abiria hadi uvunjwaji ahadi na kuvurugwa mapatano ya JCPOA yote hayo yamefanywa na Wamagharibi na hasa Marekani.’ Huku akiashiria rekodi mbaya ya Ufaransa na Marekani kuhusiana na kadhia ya JCPOA Kiongozi Muadhamu amasema: ‘Imethibiti kuhusu kadhia ya JCPOA kwamba Wamarekani iwe ni Konresi au serikali bado wanafanya uadui dhidi ya taifa la Iran.’ Amesisitiza kwamba mantiki inahukumu kwamba katika kuamiliana na adui kama huyu, tunapasa kuchukua tahadhari  na kutumia busara ya hali ya juu ili tusije tukahadaika  na kuingia kwenye uwanja aliotuandalia adui. Huku akiashiria madai ya Wamarekani kwamba wana hamu ya kufanya mazungumzo na uratibu na Iran kuhusu masuala ya kieneo yakiwemo ya Syria, Ayatullah Khamanei amesema: ‘Sisi hatutaki uratibu wa aina hii kwa sababu lengo lao kuu ni kukata uwepo wa Iran katika eneo.’ Amesisitiza kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataka Marekani isikuwepo wala kuingilia kabisa masuala ya eneo la Mashariki ya Kati na kuongeze kuwa misimamo hiyo ya Mfumo wa Kiislamu kuhusiana na masuala ya eneo inachukuliwa katika fremu ya busara. Ayatullah Khamenei amesisitiza: ‘Mimi, kwa msingi wa  majukumu ya kidini, kisheria na kimaadili na madamu nitaendelea kuwa hai, nitasimama ngangari na pia ninawaamini wananchi kama ambavyo pia nina yakini kuhusiana na matokeo ya kusimama ngangari, yaani ushindi.’
Amesema kwamba miongoni mwa wasomi nchini na hasa wahadhiri na wanachuo kuna watu wengi sana pia ambao ni waumini na wanaamini kusimama ngangari kiasi cha kuwatia moyo hata wale waliokata tamaa.
Mwanzoni mwa kikao hicho, wawakilishi wanane wa jumuiya za wanachuo Mabwana:
- Ihsan Ibrahimi - mwakilishi wa Basij ya Wanachuo
- Muhammad Hussein Qaid Sharif – mwakilishi wa Muungano wa Tahkime Wahdat
- Mujtaba Raisi – mwakilishi wa Harakati ya Uadilifu ya Wanachuo
- Muhammad Ahangaran – mwakilishi wa Makundi ya Jihadi
- Aliridha Ahmadi – mwakilishi wa Jumuiya ya Kiislamu ya Wanachuo Huru
- Muhammad Ali Kamfirouzi - mwakilishi wa Wakuregenzi Watendaji wa Machapisho ya Wanachuo
- Hussein Zeinaliyan Burujeni – mwakilishi wa Jumuiya ya Jamii ya Kiislamu ya Wanachuo
Na Bi Fatemeh Sadat Dharabi – Mwakilishi wa Muungano wa Asasi za Chuo Kikuu Huru, walitumia zaidi ya masaa mawili kubainisha mitazamo na dugudugu za jamii ya wanachuo. Kwa ufupi masuala muhimu yaliyozungumzwa na wawakilishi hao wa wanachuo ni kama ifuatavyo:
-    Kubainishwa wasiwasi wa hatari ya kusambaratika kwa ndani (Mfumo) kutokana na watu na makundi ambayo hayana imani thabiti kuhusiana na misingi ya  Mapinduzi wala Imam Khomeini (MA)
-    Udharura wa kubainishwa njia za kufikiwa matakwa ya wanachuo kuhusu matatizo na kasoro zilizopo
-    Kukosolewa kupachikwa nembo za kisiasa matakwa na ufuatiliaji wa manachuo kutoka kwa wakuu
-    Kubainishiwa wazi wananchi na vijana misigi ya ulinzi wa nchi na sababu ya kuungwa mkono harakati za mapambano ya Kiislamu katika eneo la Mashariki ya Kati
-    Kukosolewa kuenea ubwanyenye miongoni mwa baadhi ya viongozi
-    Kukosolewa kutozingatia baadhi ya wakuu wa Wizara ya Elimu masuala ya utamaduni
-    Kuandaliwa misaada inayofaa ya kuwezesha kufanyika kirahisi ndoa za wanachuo
-    Kukosolewa uandaliwaji wa mazingira ya kupenya wageni kwenye vyuo vikuu kwa kisingizio cha udiplomasia wa kielimu
-    Kubainishwa wasiwasi kuhusu upenyaji wa kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na kimafunzo wa wageni kwa kisingizio cha utandawazi
-    Kukosolewa kwa juhudi zinazofanywa na baadhi ya watu za kutekelezwa mfano wa JCPOA kuhusiana na masuala ya kieneo, kiulinzi na haki za binadamu
-    Jinsi ya kukabiliana na mirengo isiyo ya kimapinduzi ndani ya Mfumo kwa njia ambayo haitazua kambi mbili.
-    Kukosolewa maneno matupu na ya nara tu ya baadhi ya viongozi kuhusiana na suala la uchumi ngangari
-    Kukosolewa mameya wa miji mikuu kutokana na kuenea bila mipaka kwa vituo vya kibiashara na athari zake mbaya za kiutamadui na kijamii
-    Udharura wa vijana kuandaliwa nafasi za uongozi nchini
-    Kukosolewa kwa baadhi ya miamala ya vyombo vya mahakama kuhusu machapisho (majarida/magazeti) ya jumuiya na vyama vya wanachuo
-    Udharura wa kubainishwa njia za kuamiliana na wakosoaji wa Mfumo, ambao wana mitazamo tofauti
-    Kubainishwa wasiwasi kuhusiana na kuondolewa malengo matukufu ya Mapinduzi ya Kiislamu katika siasa za nje
-    Kukoselewa utendaji wa baadhi ya viongozi wa vyombo vya mahakama na kutotangazwa wazi hukumu zinazotolewa na mahakama
-    Kukosolewa kunyamaziwa kimya mswada wa kusimamiwa utendaji wa wabunge
-    Malalamiko kuhusiana na utendaji wa baadhi ya viongozi katika kuhalalisha uadui wa Marekani na juhudi za kuifanya nchi hiyo kuonekana kuwa kubwa mno
-    Kukosolewa vikali kutochukuliwa hatua Marekani kutokana na uvurugaji na  uvunjaji wa nchi hiyo makubaliano ya JCPOA
-    Udharura wa kubuni sera za ngazi za juu kwa ajili ya maendeleo ya vijijini na kuenezwa shughuli za makundi ya kijihadi katika maeneo ya watu masikini na
-    Umuhimu wa mpango wa maendeleo wa miaka 20 wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na mwenendo usiofaa wa hivi sasa katika kufikia malengo yake.
Katika kikao hicho wanachuo waliswali pamoja swala ya Maghrib na Isha kwa uimamu wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na baadaye kufuturu pamoja naye.

 

700 /