Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu:

Wizara ya Usalama ni handaki na jicho la Jamhuri ya Kiislamu

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei leo jioni ameonana na Waziri na manaibu na wakurugenzi wa Wizara ya Usalama wa Taifa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema kuwa, wizara hiyo ni ngao muhimu mno na nyeti na ni jicho linaloangalia mbali na lililomacho la mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Amesisitiza kuwa: Wizara ya Usalama wa Taifa ya Iran ni tabaka lililoundwa na mfumo wa Kiislamu na haipasi kuruhusiwa lipatwe na madhara ya aina yoyote.
Ayatullah Khamenei ameishukuru Wizara ya Usalama wa Taifa kutokana na kazi kubwa za usiku na mchana zinazofanyika kwa moyo wa imani thabiti ya kidini katika nyuga tofauti ndani ya wizara hiyo na kusema kuwa, ushindi na kuweza kubakia na kudumu Mapinduzi ya Kiislamu kunatokana na kulindwa imani hiyo thabiti ya kidini. Ameongeza kuwa: Kushindwa kwa ubeberu wa kimataifa kukabiliana na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu licha ya kuweko wimbi kubwa la njama na hila za aina mbalimbali za adui huyo tangu mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hadi leo hii, ni jambo ambalo lisingeliwezekana bila ya kuwepo silaha ya imani thabiti.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesema, hatua yoyote ile ya kujaribu kudhoofisha imani ya wananchi na viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni usaliti. Ameongeza kuwa: Nguvu madhubuti ya kiulinzi ambayo imekuwa nayo Iran kwa miaka yote hii ni nguvu yake ya kiimani na kama silaha hii yenye nguvu na muhimu sana itadhoofishwa, basi kutatokea madhara makubwa sana.
Ametumia fursa hiyo kuihimiza Wizara ya Usalama wa Taifa ya Iran kujiimarisha kiroho na kiimani na kusisitiza kuwa: Wizara ya Usalama wa Taifa ya Iran ni tabaka lililoundwa na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na haipasi kuruhusu ipate madhara ya namna yoyote ile, hivyo suala la kuimarishwa mambo muhimu ndani ya wizara hiyo kama vile imani na masuala ya kiroho inabidi lipewe hima kubwa zaidi kuliko katika taasisi nyingine yoyote.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia nafasi kubwa ya Wizara ya Usalama wa Taifa ya Iran ya kuweza kupata nguvukazi ya vijana wanamapinduzi walioimarika kiimani na kusisitiza kuwa: Kizazi kipya ndani ya Wizara ya Usalama wa Taifa kinapaswa kukuzwa na kuimarishwa kimapinduzi na kiroho kama ilivyokwua huko nyuma.
Ayatullah Khamenei ameitaja Wizara ya Usalama wa Taifa kuwa ni jicho linaloona mbali na lililomacho la mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kuongeza kuwa, misingi na misimamo ya Mapinduzi ya Kiislamu inabidi ichungwe na ilindwe kikamilifu ndani ya Wizara ya Usalama wa Taifa.
Amesema, misingi ya Mapinduzi ya Kiislamu inapatikana kwa uwazi kabisa katika athari na miongozo ya Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu) na kusisitiza kwamba: Wajibu wa viongozi na wananchi wa Iran wa kuweka mpaka ulio wazi baina yao na kinara wa mrengo wa ubeberu yaani Marekani ni miongoni mwa misingi mikuu na isiyotetereka ya Imam wetu mtukufu na suala hili si la kuzembewa wala kudharauliwa hata kidogo.
Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: Wizara ya Usalama wa Taifa ina wajibu wa kuweka kambi sehemu yoyote inayoweza kwa ajili ya kumchunguza na kufuatilia nyendo za adui mwenye nia ya kutoa pigo kwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Inabidi wizara hiyo iweko sehemu zote hizo na kuzifanya kuwa ni katika maeneo ya kuyafanyia kazi. 
Mchango wa Wizara ya Usalama wa Taifa katika kufanikisha uchumi wa ngangari ni nukta nyingine iliyosisitiziwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika hotuba yake hiyo. Amesema: Utatuzi wa matatizo yaliyopo nchini ni uchumi ngangari, na tayari kazi za kufanikisha uchumi huo zimeanza katika baadhi ya sekta, lakini lililo muhimu ni kuonekana wazi matunda ya kazi hizo.
Vilevile amesisitizia wajibu wa Wizara ya Usalama wa Taifa kutoa mchango unaotakiwa katika vita dhidi ya ufisadi wa kiuchumi.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatul Islam Walmuslimin Alavi, Waziri wa Usalama wa Taifa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa ripoti fupi na jumla kuhusiana na ratiba na kazi za wizara hiyo.
 

700 /