Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Zidisheni uwezo wa jeshi ili madhalimu watishike

Husainia ya Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu) mjini Tehran leo (Jumatano) ilikuwa mwenyeji wa maonyesho ya mafanikio ya sekta ya ulinzi ya Wizara ya Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ayatullah Ali Khamenei ambaye ni Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Iran ametembelea maonyesho hayo kwa muda wa zaidi ya masaa mawili na kuona kwa karibu teknolojia za kisasa na za ndani ya Iran za taasisi za elimu za kimsingi ambayo ni matunda ya jitihada, ubunifu, maarifa na utafiti wa wataalamu wa ndani ya nchi na ambayo yana taathira ya moja kwa moja katika kuzidisha uwezo wa kijeshi wa vikosi vya ulinzi vya Iran.
Katika maonyesho hayo kumeoneshwa matunda yaliyopatikana katika kubuni na utengenezaji wa mifumo ya aina mbalimbali ya kiulinzi na zana za kisasa katika nyuga za makombora, rada, vifaa vya baharini, magari ya deraya, ndege zisizo na rubani na vituo vya mawasiliano.
Kiongozi Muadhamu pia amepewa ripoti kuhusu utengenezaji wa aina mbalimbali za zana za kijeshi zilizoonyeshwa katika maonyesho hayo.
Baada ya kutembelea maonyesho hayo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa hotuba mbele ya Waziri, maafisa, watafiti na wataalamu wa Wizara ya Ulinzi na kusema kuwa ni haki iliyo wazi ya Iran kuwa na nguvu za kiulinzi na za kimashambulizi. Amesisitiza udharura wa kudumishwa njia ya kuzidisha uwezo wa kiulinzi wa taifa na kusema: Katika dunia hii inayotawaliwa na madola ya kidhalimu, kibeberu, yenye kiwango cha chini kabisa cha maadili, utu na ubinadamu na yasiyosita hata kidogo kuzivamia nchi nyingine na kuua watu wasio na hatia, ni jambo la kawaida kwa nchi kuimarisha viwanda vyake vya kutengeneza zana za kiulinzi na kimashambulizi, kwani nchi haiwezi kupata usalama iwapo madola hayo ya kibeberu hatahisi nguvu kubwa za kijeshi za nchi yetu. 
Ayatullah Khamenei amesema anafurahishwa na kuvutiwa sana kutembelea maonyesho ya maendeleo ya viwanda vya ulinzi na kuongeza kuwa: "Jambo linalonifurahisha zaidi ni kuona kuwa, mbali na kuona uwezo wa aina mbalimbali wa kiulinzi, ambao una nafasi kubwa sana katika kukuza na kuimarisha nguvu na uwezo wa kiulinzi wa nchi, ninashuhudia nguvu kazi ya wasomi, watafiti, wataalamu na watu wenye fikra nzuri na wenye imani thabiti, suala ambalo  linanifurahisha mno.
Amesema: Kuwepo nguvu kazi kama hii katika sekta za ulinzi nchini, ni mfano wa kuwa na kito chenye thamani kubwa ambacho haiwezekani kukikadiria thamani yake.
Akibainisha sababu zinazomfanya asisitize mno suala la kuongeza na kuimarisha uwezo wa kiulinzi na viwanda vya zana za kijihami nchini, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Wakati tunapoona kuwa madola ya kibeberu yamefungua "mwavuli" wa nguvu zao na hayana hata chembe ya huruma, bali yanashambulia waziwazi sherehe za harusi na mahospitali kwa madai ya eti kupambana na ugaidi na kuua kikatili mamia ya watu wasio na hatia na hakuna taasisi wala chombo chochote kinachoyazuia na kuyaambia chochote, lazima na sisi tuzidishe uwezo na nguvu zetu za kijeshi kadiri tunavyoweza ili kuyatia woga madola ya kibeberu na yasithubutu kutushambulia. 
Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: "Pamoja na hayo tunajiwekea mipaka katika kuimarisha sekta yetu ya zana za kiulinzi na kwa mujibu wa itikadi zetu za kidini, haifai kutengeneza silaha za mauaji ya umati kama vile silaha za kemikali na silaha za nyuklia".
Amesisitiza kuwa: Marufuku ya kutengeneza silaha za kemikali ni katika upande wa silaha za kushambulia tu, kwani kumiliki zana za kiulinzi za kujilinda na kujihami mbele ya mashambulizi ya kemikali, ni jambo ambalo halina tatizo lolote.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesema: Ghairi ya mipaka hiyo, hakuna mipaka mingine yoyote katika kuimarisha nguvu zetu za kijeshi, bali ni jukumu letu kupiga hatua za maendeleo katika nyuga mbalimbali.
Ayatullah Ali Khamenei ameashiria nafasi ya kiistratijia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na umuhimu mkubwa wa eneo la magharibi mwa Asia na jinsi madola ya kibeberu yanavyoliangalia kwa tamaa eneo hili na kuongeza kuwa: Ni wajibu kuongeza na kuimarisha uwezo wa mashambulizi sambamba na uwezo wa kujilinda na kujihami kama njia ya kudhamini usalama wa taifa, wa nchi na mustakbali bora.
Vilevile ameashiria jinsi madola ya kibeberu yanavyokasirishwa na suala la Iran kununua zana za kijeshi kutoka kwa baadhi ya nchi na kusema: Madola hayo yanayodai kuwa yana akili na insafu na  yanazungumzia ni nchi ipi yenye ustahiki wa kimaadili wa kumiliki au kutomiliki baadhi ya zama za kijihami, yenyewe madola hayo, hayaheshimu wala kushikamana na msingi wowote wa kimaadili.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesema: Serikali ya Marekani haina ustahiki wowote wa kimaadili wa kuifanya iwe na haki ya kusema lolote kuhusiana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Amesema: Hakuna chama chochote kinachoingia madarakani huko Marekani kati ya vyama viwili (vya Republican na Democrat) chenye ustahiki wa kufanya hivyo, iwe ni chama cha serikali iliyoko madarakani hivi sasa au chama cha upinzani, kwani vyama vyote hivyo viwili vimetenda jinai na kusababisha maafa ya aina mbalimbali duniani.
Ayatullah Khamenei amesema, dhambi kubwa iliyofanywa na chama kilichoko madarakani hivi sasa nchini Marekani, ni kuanzisha mitandao hatari mno ya kigaidi na kusisitiza kwamba, serikali hiyo ya Marekani inajifanya kulishambulia kidhahiri  kundi moja la kigaidi na kuliacha kundi jingine la kigaidi, jambo ambalo linaonesha jinsi siasa zinavyotawala maadili.
Ameongeza kuwa: Serikali iliyopita ya Marekani ndiyo iliyofanya jinai na kusababisha maafa makubwa katika nchi za Iraq na Afghanistan kiasi kwamba, mamilioni ya watu wasio na hatia wameuawa na hata maelfu ya wasomi na wanasayansi wa Iraq walisakwa na genge la mauaji la Black Water na kuuliwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Kwa kuzingatia hayo tutaona kuwa hakuna chama chochote kati ya vyama hivyo viwili huko Marekani ambacho kina ustahiki wa kimaadili. 
Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: Tunakabiliana na tawala za namna hii huko Marekani, hivyo ni kosa kudhani kuwa, tunaweza kufikia maelewano na Marekani kupitia mazungumzo.
Amesisitiza kwamba: Hilo ndilo linalonifanya nisitizie mara kwa mara wajibu wa kutofanya mazungumzo yoyote na Marekani kwani uzoefu umethibitisha kuwa, badala ya kutafuta maafikiano, siku zote Wamarekani wanataka kuwatwisha wengine misimamo na maamuzi yao, na mfano wa wazi ni matukio yaliyotokea hivi karibuni.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake Amirijeshi Mkuu wa Iran ameipongeza Wizara ya Ulinzi na watafiti na wataalamu wa taasisi mbalimbali za jeshi la ulinzi na kusema: Miongoni mwa sababu kuu za maendeleo ya viwanda vya zana za kujihami hapa nchini ni mawasiliano baina ya sekta ya zana za kijihami na vyuo vikuu na makampuni ya elimu msingi.
Ameashiria maagizo yake ya mara kwa mara juu ya kuwepo ushirikiano kati ya viwanda vya zana za kujihami na vyuo vikuu na kusema, ushirikiano huo una faida kwa pande zote mbili na mfano wake wa wazi unonekana sasa katika Wizara ya Ulinzi.
Amesema kuwa maendeleo ya sasa ni mtunda ya harakati kubwa ya kielimu hapa nchini katika kipindi cha miaka 12 iliyopita na kusisitiza kuwa: Harakati ya kielimu ambayo sasa imekuwa mjadala wa nchi nzima na wasomi wetu vijana waliofanikiwa kuvuka mistari myekundu ya elimu ya sayansi vinapaswa kudumishwa; kwa sababu maendeleo katika uwanja wowote ule yanaanda uwanja mzuri wa maendeleo mapya katika sekta nyingine. 
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Brigedia Jenerali Dehqan. Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa ripoti fupi kuhusu kazi zilizofanyika katika viwanda vya ulinzi, kuanzisha kanali ya wafanyakazi wa wizara ya ulinzi na kuanzisha mawasiliano mazuri na ya kuendelea baina ya viwanda vya ulinzi na vyuo vikuu pamoja na mashirika ya elimu za kimsingi. Amesema, Leo hii sekta ya ulinzi nchini Iran kutokana na kustafidi vizuri na miundombinu ya kiufundi na elimu za kimsingi, ina uwezo wa kudhamini mahitaji yote yanayotakiwa na vikosi vya ulinzi nchini.
 

700 /