Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Ujumbe kwa Mahujaji wa Nyumba tukufu ya Allah

Ujumbe kwa Mahujaji wa Nyumba tukufu ya Allah

Katika kuwadia msimu wa ibada tukufu ya Hija, Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ujumbu muhimu kwa mnasaba huu kwa Waislamu wote duniani na hasa kwa Mahujaji wanaozuru Nyumba ya Mwenyezi Mungu, al-Kaaba  huko katika mji mtakatifu wa Makka. Amesema Hija ya Nabii Ibrahim (as) ni dhihirisho la izza na utukufu wa Umma wa Kiislamu katika kukabiliana na madhalimu wa kimataifa. Huku akiashiria matukio machungu ya maafa ya Mina mwaka uliopita, amezihutubu  serikali na mataifa ya Kiislamu kwa kusisitiza kuwa ulimwengu wa Kiislamu zikiwemo serikali na mataifa ya Waislamu unapasa kuwafahamu vyema watawala wa Saudia na kuwawajibisha kutokana na jinai ambazo wamezieneza katika ulimwengu wa Kiislamu, na wakati huohuo kufikiria juu ya njia za msingi za kusimamia Haram Mbili Takatifu na suala zima la Hija. Ufuatao ni ujumbe kamili wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Kwa jina la Allah, Mwingi wa rehma Mwenye kurehemu

Na hamdu zote ni za Allah Mola wa viumbe wote. Na rehma na amani zimshukie bwana wetu Muhammad na Aali zake watukufu na masahaba zake wema na wote waliowafuata wao kwa mema mpaka Siku ya Malipo

 

Kina kaka na kina dada Waislamu wa ulimwenguni kote!

Msimu wa Hija kwa Waislamu ni msimu wa kujivunia na wa adhama mbele ya macho ya viumbe; na ni msimu wa kunawirisha nyoyo na kudhihirisha khushuu na unyenyekevu mbele ya Muumba. Hija, ni faradhi takatifu, ya kidunia, ya Kiungu na ya watu. Upande mmoja ni amri ya فَاذْكُرُواْ اللَّهَ كَذِكْرِكُمْ آبَاءَكُمْ أَوْ أَشَدَّ ذِكْرًا

 Basi mtajeni Mwenyezi Mungu kama mlivyo kuwa mkiwataja baba zenu au mtajeni zaidi; na وَاذْكُرُواْ اللَّهَ فِي أَيَّامٍ مَّعْدُودَاتٍ yaani Na mtajeni Mwenyezi Mungu katika zile siku zinazo hisabiwa.

Na upande mwingine tunahutubiwa:الَّذِي جَعَلْنَاهُ لِلنَّاسِ سَوَاء الْعَاكِفُ فِيهِ وَالْبَادِ  Ambao tumeufanya kwa ajili ya watu wote sawasawa, kwa wakaao humo na wageni. Haya yanaweka wazi kabisa upeo mpana usio na kikomo na wa hali tofauti wa Hija.

  Katika faradhi hii isiyo na mfano, amani ya mahala na wakati inazipa nyoyo za watu utulivu mithili ya nyota ing'arayo na kumweka mbali Hujaji na mzingiro wa mambo yanayovuruga amani, yanayosababishwa na mabeberu madhalimu; na ambayo daima yamekuwa tishio kwa wanadamu wote; na kumfanya Hujaji aonje ladha ya amani katika muda maalumu.

Hija ya Kiibrahim ambayo Uislamu umewatunukia Waislamu ni dhihirisho la izza, umaanawi, umoja na adhama; adhama ya Umma wa Kiislamu na kutegemea kwao Waislamu nguvu isiyo na mwisho ya Mwenyezi Mungu wanayojivunia mbele ya maadui na wanaowatakia mabaya; ambayo inazidi kuwaweka mbali zaidi na uchafu wa ufisadi, udunishwaji na udhoofishwaji ambao wababe na watumiaji mabavu wa kimataifa wanazitwisha jamii za wanadamu. Hija ya Kiislamu na Kitauhidi ni dhihirisho la   أَشِدَّاء عَلَى الْكُفَّارِ رُحَمَاء بَيْنَهُمْ wana nguvu mbele ya makafiri, na wanahurumiana wao kwa wao. Ni mahala pa kujibari na washirikina na kujenga upendo na umoja na waumini.

 Wale walioishusha hadhi ya Hija kuwa safari ya kimatembezi na kitalii na wakaficha nyuma ya madai ya "Kuingiza siasa katika Hija" chuki na uadui wao dhidi ya taifa la waumini na la kimapinduzi la Iran, ni mashetani duni na dhalili ambao wanatetemeka wao kutokana na kuhatarika maslahi ya kitamaa ya Shetani Mkubwa Marekani. Watawala wa Kisaudi, ambao mwaka huu wamewazuilia na kuwafungia njia ya Mwenyezi Mungu na Msikiti Mtukufu Mahujaji wenye ghera na waumini wa Iran ili wasiifikie Nyumba ya mahabubu wao, ni wapotofu waliohasirika wanaoamimi kwamba kubaki kwao kwenye hatamu za madaraka ya kidhalimu kunategemea jinsi watakavyowatetea waistikbari wa dunia na kushirikiana na Uzayuni na Marekani na kufanya kila jitihada za kukidhi matakwa yao. Na hawaachi kufanya uhaini na usaliti wowote ule katika kulifanikisha hilo.

Sasa ni karibu mwaka mmoja umepita tangu matukio ya kutisha ya Mina, ambapo maelfu kadhaa ya watu walifariki wakiwa madhulumu katika Siku ya Idi, wakiwa wamevaa vazi la Ihramu huku wakipigwa na jua na wameshikwa na kiu. Muda mfupi kabla ya tukio hilo, katika Msikiti Mtukufu watu kadhaa pia waliuawa wakiwa wanafanya ibada, wakitufu na kusali. Watawala wa Kisaudi ndio wenye makosa katika matukio yote mawili; hivi ndivyo wanavyokubaliana kwa kauli moja wote walioshuhudia, waliofuatilia na waliohakiki kitaalamu matukio hayo; na kuna baadhi ya wajuzi wa mambo pia wanaozungumzia uwezekano wa kuwa ni tukio lililofanywa makusudi. Ni jambo la wazi kabisa kwamba kulikuwa na uzembe na ucheleweshaji katika kuwaokoa majeruhi waliokuwa bado hawajakata roho, ambao roho zao zenye shauku na nyoyo zao zenye hamu katika Siku ya Idi ya Kuchinja ziliambatana na ndimi zao zilizokuwa zikidhukuru na kusoma aya za maneno ya Mwenyezi Mungu. Wasaudi watenda jinai na wenye nyoyo kavu na ngumu waliwachukua majeruhi hao na kuwafungia kwenye makontena pamoja na waliofariki. Na badala ya kuwapatia matibabu na kuwasaidia au hata kuwafikishia maji kwa kiu walizokuwa nazo, waliwaua shahidi. Maelfu ya familia kutoka nchi mbalimbali zilipoteza wapendwa wao na mataifa yao yakapatwa na msiba.

Mahujaji kutoka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kulikuwa na watu karibu 500 miongoni mwa Mashahidi. Nyoyo za familia zingali zimehuzunika na kupatwa na machungu ilihali taifa lingali limehuzunika na kukasirika.

Ama watawala wa Saudia badala ya kuomba msamaha na kusikitishwa na tukio hilo pamoja na kuwafuatilia kisheria wahusika wa moja kwa moja wa tukio hilo la kutisha, wameonyesha upeo wa kutojali na ukhabithi wao kwa kukwepa kuchukua hatua hata ya kubuni tu tume ya uhakiki wa kimataifa ya Kiislamu. Badala ya kusimama kweye kizimba cha mtuhumiwa imesimama kwenye kizimba cha mtuhumu na kudhihirisha kwa njia khabithi na ya upumbavu mkubwa uadui wake mkongwe kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kwa kila bendera ya Uislamu inayopeperushwa mkabala na kufri na uistikbari.

 Vyombo vyao vya propaganda wawe ni wanasiasa wao ambao vitendo na tabia zao kuhusiana na Wazayuni na Marekani ni fedheha kubwa kwa ulimwengu wa Kiislamu, mamufti wao wasiomwogopa Mwenyezi Mungu na wanaokula haramu ambao daima hutoa fatwa zinazokwenda kinyume na Kitabu pamoja na Suna au Vyombo vyao vya habari vilivyofeli ambavyo hata mipaka ya maadili ya uandishi haivizuii kusema uongo, vinafanya juhudi kubwa za kujaribu kuonyesha kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndiyo iliyopelekea MahujajI wa Iran wasihiji mwaka huu. Watawala wa fitina ambao wamebuni na kuyapa silaha makundi ya kitakfiri na ya shari na hivyo kuufanya ulimwengu wa Kiislamu kukumbwa na vita vya ndani, mauaji na kujeruhiwa watu wasio na hatia, kumwaga damu katika nchi za Yemen, Iraq, Sham, Libya na nchi nyinginezo, wachezajisiasa wasiomtambua Mwenyezi Mungu ambao wanaupa mkono wa urafiki utawala ghasibu wa Kizayuni na kufumbia macho machungu na misiba ya kusikitisha ya Wapalestia, kueneza dhulma na khiana katika miji na vijiji vyote vya Bahrain, watawala wasio na dini wala utu ambao wamesababisha maafa makubwa ya Mina na ambao wanadai kuwa wahudumu wa Haram mbili Tukufu na kuvuruga kabisa utukufu na amani ya Haram hizo za Mwenyezi Mungu pamoja na kuwachinja wageni wa Mwenyezi Mungu Mrehemevu katika siku ya Idi huko Mina na kabla ya hapo kwenye Masjidul Haram, hivi sasa wanazungumzia kutofanywa siasa kwenye Hija na kuwatuhumu wengine kuhusika na dhambi kubwa ambazo wao wenyewe wamezitenda au kuzisababisha. Wao ni mfano wa wazi wa aya za 205 na 206 za Surat an-Baqarah katika Qur’ani Tukufu ziazosema: وَإِذَا تَوَلَّى سَعَى فِي الأَرْضِ لِيُفْسِدَ فِيهَا

 وَيُهْلِكَ الْحَرْثَ وَالنَّسْلَ وَاللَّهُ لاَ يُحِبُّ الْفَسَادَ

وَإِذَا قِيلَ لَهُ اتَّقِ اللَّهَ أَخَذَتْهُ الْعِزَّةُ بِالإِثْمِ فَحَسْبُهُ جَهَنَّمُ وَلَبِئْسَ الْمِهَادُ

Na anapotawala hufanya juhudi katika ardhi kufanya ufisadi humo, na huangamiza mimea na viumbe. Na Mwenyezi Mungu hapendi ufisadi. Na akiambiwa: Mche Mwenyezi Mungu, hupandwa na mori wa kutenda madhambi. Basi huyo inamtosha Jahannam, nayo ni makao mabaya mno.

Mwaka huu pia kwa mujibu wa ripoti, mbali  na Mahujaji wa Kiirani na wa mataifa mengine, Mahujaji wa nchi nyingine wanapitia vidhibiti ambavyo si vya kawaida ambapo Wasaudia kwa kushirikiana na vyombo vya ujasusi vya Marekani na utawala wa Kizayuni wameifanya Nyumba ya Amani ya Mwenyezi Mungu kutokuwa ya amani tena kwa mtu yoyote.  Ulimwengu wa Kiislamu zikiwemo serikali na mataifa ya Kiislamu yanapasa kuwafahamu vyema watawala wa Saudia, ukweli wao wa kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu, kutokuwa kwao na imani na utegemezi na mfungamano wao na masuala ya kimaada, kuwawajibisha kutokana na jinai ambazo wamezieneza katika ulimwengu wa Kiislamu, dhulma waliyowafayia wageni wa Mwenyezi Mungu na kufikiria kimsingi jinsi ya kuendesha na kusimamia Haram mbili Tiukufu pamoja na suala zima la Hija. Kuzembea katika kutekeleza jukumu hilo bila shaka kutaufanya mustakbali wa Kiislamu ukabiliwe na matatizo makubwa zaidi.

Ndugu Waislamu! Licha ya kuwa mwaka huu Mahujaji waliokuwa na hamu kubwa ya kufanya Hija na hasa Mahujaji wa Kiirani hawakufanikiwa kufanya hivyo, lakini wako pamoja na Mahujaji kutoka nchi mbalimbali za dunia kwa nyoyo zao na wanahofia hali zao, na wanaomba dua kwamba mti uliolaaniwa wa mataghuti usije ukawadhuru. Waombeeni ndugu zenu wa Kiirani na muwakumbuke kwenye ibada na dua zenu na pia muombe dua kwa ajili ya kuondokewa na matatizo jamii za Kiislamu na kukatwa mikono ya Waistikbari na Wazayuni pamoja na vibaraka wao katika Umma wa Kiislamu.

Ninawakumbuka na kuwaenzi mashahidi wa Mina na Masjidul Haram wa mwaka uliopita na Mashahidi wa Makka mwaka 1366 (tarehe 31Julai, 1987) na ninamwomba Mwenyezi Mungu aweze kuwaghufiria, kuwarehemu na kuwapandisha daraja. Ninatoa salamu zangu kwa Imam wa Zama (AF) (roho yangu iwe fidia kwake) na kumwomba Mtukufu huyo auombee dua utukufu wa Umma wa Kiislamu na kuepuka Waislamu na fitina na shari ya maadui.

Na Taufiki ni ya Mwenyezi Mungu naye ni Mbora wa kutegemewa.

Sayyid Ali Khamanei

Mwishoni mwa Dhil Qaada 1437

12/06/95 (Septemba, 2016)

700 /