Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Ayatullah Khamenei:

Vijana wetu wengi ni waumini na wako taayari kwa jihadi

Sambamba na maadhimisho ya sikukuu ya Ghadir, idi ya Uimamu na Wilaya, na sikukuu kubwa zaidi ya Mwenyezi Mungu, leo asubuhi (Jumanne), Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei ameonana na kuhutubia maelfu ya wananchi wa matabaka tofauti katika Husainia ya Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu mjini Tehran.
Katika mkutano huo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa mkono wa baraka kwa mnasaba wa sikukuu ya Ghadir na kusema kuwa, ujumbe muhimu zaidi unaopatikana katika tukio la Ghadir ni kuainishwa Uimamu kuwa ndio msingi na kielelelezo cha utawala katika Uislamu. Vilevile amegusia sifa za kipekee za Imam Ali (as) hususan namna alivyokuwa ametimiza sifa zote za kuongoza dola ya Kiislamu na amewausia hadhirina ulazima wa kushikamana na Wilaya na utawala wa Amirul Muminin, Imam Ali bin Abi Twalib (as) kupitia kutekeleza ipasavyo miongozo na nasaha za shakhsia huyo mkubwa na wa aina yake.
Vilevile amegusia baadhi ya maneno yanayotumika kuitambulisha sikukuu ya Ghadir kama vile kuiita idi kubwa ya Mwenyezi Mungu na kusema kuwa, sababu ya kuweko majina hayo, ni tukio muhimu sana ambalo lilitokea katika Ghadir, nalo ni kuainishwa kigezo na kielelezo cha utawala ndani ya dola ya Kiislamu.
Ameongeza kuwa: Kielelezo na kigezo hicho ni Uimamu na Wilaya katika jamii ya Kiislamu ambayo ni amri kutoka kwa Mwenyezi Mungu iliyotangazwa na Bwana Mtume Muhammad SAW.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Mbali na kuainisha kigezo na kielelezo, Imam Ali (as) alitangazwa rasmi kuwa ni Imam akiwa ni shakhsia mkubwa, mtukufu, aliyejaa nuru na ambaye si rahisi kumtia doa.
Ameongeza kuwa: Hakuna mtu yeyote aliyeweza kufikia kilele alichofikia Imam Ali bin Abi Twalib (as) katika upande wa Uimamu na kuongoza jamii ya Kiislamu baada ya Bwana Mtume SAW. Shakhsia wengine wakubwa wa kielimu na uchaji Mungu wamekuja katika historia ya Uislamu, kama vile Imam wetu mtukufu (Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu), lakini wote hao ni tone tu mbele ya miale iliyojaa nuru ya Amirul Muminin Imam Ali (as).
Baada ya hapo ametoa muhtasari wa maelezo yake kwa kusema: Tukio la Ghadir liliweka msingi wa kigezo na kielelezo cha utawala katika jamii ya Kiislamu na kusisitiza kwa kusema: Ukitoa kigezo cha Uimamu na Wilaya, Uislamu haukubaliani na tawala nyinginezo zozote, za kisultani, za watu binafsi, za kibeberu, za watu wanaopenda kujilimbikizia kila kitu upande wao, za watu wenye viburi na za watu wanaofuata matamanio ya nafsi, anasa na ubwanyenye.
Vilevile amebainisha umuhimu wa kadhia ya Ghadir ambayo Mwenyezi Mungu alimwamrisha Mtume Wake aitangaze na kwamba risala aliyotumwa kuifikisha hatakuwa ameifikisha kama hakutanga Uimamu na kuongeza kuwa: Itikadi hiyo ya Kiislamu imesimama juu ya msingi madhubuti wenye hoja zisizokanushika, lakini pamoja na hayo, kushikamana na kuitangaza itikadi hiyo, hakupasi kuandamana na uchochezi wa hisia za Waislamu wa Kisuni, kwani kufanya hivyo ni kinyume na sira ya Maimamu maasumu (as).
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza tena umuhimu wa umoja na mshikamano katika ulimwengu wa Kiislamu na kusema kwamba, kusema maneno yoyote yale mabaya dhidi ya shakhsia wakubwa na viongozi wa Waislamu wa madhehebu mengine, kwa hakika ni kuzuia kusikika misingi ya kimantiki na yenye hoja madhubuti za itikadi ya Uimamu. Amesisitiza kuwa, kitendo chochote kile cha kuchochea hisia za watu wa madhehebu mengine ya Kiislamu kwa jina la Ushia, kwa hakika huo si Ushia halisi, bali huo ni Ushia wa Kiingereza na matokeo yake ni kujitokeza magenge khabithi na mamluki wa Marekani na wa shirika la kijasusi la Uingereza kama vile Daesh na Jabhatun Nusra ambayo yanafanya jinai na kusababisha hasara kubwa kwa ulimwengu wa Kiislamu.
Ayatullah Khamenei ameendelea na hotuba yake kwa kuashiria sifa za kimaanawi na kiutu za Imam Ali (as) kama vile kuwa na imani kubwa sana, kuwa wa mwanzo kukubali Uislamu, kujitolea kikamilifu katika njia ya Uislamu, ikhlasi, elimu, maarifa ya Allah, ushujaa, huruma, kujitolea na kusamehe na kuongeza kuwa: Sehemu nyingine ya sifa za aina yake za mtukufu huyo inahusiana na mbinu alizotumia katika kuongoza dola ya Kiislamu. Miongoni mwa sifa hizo ni uadilifu, insafu na kuwaweka daraja sawa wananchi wote, kujiweka mbali na anasa za kidunia, tadibiri, kutochelewesha hata kidogo utekelezaji wa majukumu, uwazi, kuiongoza jamii kuelekea kwenye taqwa na uchamungu, na kutoogopa lolote wakati wa kutenda haki na uadilifu.
Kuhusiana na jinsi Imam Ali bin Abi Twalib (as) alivyojiepusha na anasa za dunia au kutumia utawala katika mambo yake binafsi Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kwamba: Vishawishi vinavyompata mwanadamu kwa ajili ya kutumia vibaya vyanzo vya fedha vilivyo mikononi mwake kwa ajili ya kujinufaisha binafsi, ni miongoni mwa mabalaa ambayo yanazitesa tawala zisizo za Mwenyezi Mungu, lakini utawala ambao kigezo na kielelezo chake ni Uimamu na Wilaya, unapinga vikali mambo kama hayo na unapiga marufuku kutumia mali ya umma kwa mambo ya watu binafsi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesema: Imam Ali (as) alikuwa akifanya tadibiri sana katika kumjua rafiki na adui na katika kuwaainisha maadui na hayo yanaonekana wazi katika hatua zilizochukuliwa na mtukufu huyo kwenye vita vitatu alivyopigana na maadui baada ya kuwa kiongozi wa dola ya Kiislamu; hatua hizo zinatofautiana kulingana na mazingira ya kila vita.
Amesema, Amirul Muminin Imam Ali (as) alikuwa shakhsia aliyekusanya sifa za kila upande, alikuwa shakhsia adhimu na ambaye ni vigumu kuzungumzia ipasavyo wasifu wake. Amesema, jukumu letu sisi ni kujitahidi kupiga hatua kuelekea kwenye kilele hicho na kustafidi ipasavyo na sifa zake hizo kwa kadiri ya uwezo na kiwango cha imani yetu.
Ayatullah Khamenei amegusia pia ulazima wa kujipamba Mashia kwa tabia na maadili ya Ahlul Bait AS na kusema: Mtu ambaye anapokea rushwa au anatumia "Baitul Maal" (hazina ya dola na mali ya umma) kwa manufaa yake binafsi au anayekodolea macho maovu bila ya kuwa na hisia zozote mbele ya wajibu wa kuiongoza vizuri jamii, mtu huyo si fakhari wala si pambo kwa Jamhuri ya Kiislamu wala kwa jamii ya Kiislamu, bali ni aibu kwa Shia.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesema, sisi kamwe hatuwezi kuishi kama alivyokuwa akiishi Imam Ali (as) kwa uchaji mkubwa mno wa Mwenyezi Mungu, lakini pamoja na hayo tunaweza kuingia kwenye mkondo wa njia hiyo iliyojaa nuru kwa kujiweka mbali na israfu na kuchupa mipaka. Amesema: Inasikitisha kuona kuwa, jamii yetu imekumbwa na jambo la aibu la israfu, ambayo ina sura nyingi na miongoni mwake ni israfu katika maisha binafsi ya mwanadamu.
Ayatullah Khamenei amesema, miongoni mwa madhara ya israfu katika jamii, ni kuharibu uchumi wa nchi. Ameongeza kuwa: Kama jamii inataka kuwa na nguvu za ndani za kiuchumi na kufikia daraja ya juu inayotakiwa, basi jamii hiyo haina njia nyingine ila kupambana na israfu.
Kiongozi Mudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, jukumu la kwanza kabisa la wananchi ni kupambana na israfu. Amesisitiza kuwa kushikamana na Wilaya na Uimamu wa Imam Ali (as) inabidi kuonekane kivitendo na kusema: Moja ya njia zinazotumiwa na adui kutoa pigo, ni kutumia udhaifu wa jamii, hivyo kuna wajibu wa kurekebishwa udhaifu wowote unaojitokeza.
Ayatullah Khamenei aidha amesema, lengo kuu la adui hivi sasa ni kuvuruga uchumi wa Iran. Amekumbusha namna ambavyo amekuwa akisisitizia mara kwa mara suala la kushikamana na uchumi wa kimuqawama na kusema: Anachopigania adui ni kuharibu uchumi wa wananchi ili hatimaye wananchi hao wauchukuie Uislamu na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. 
Amesisitiza kuwa: Kwa kuzingatia hali hiyo, ni jukumu la Serikali, Bunge na maafisa wa sekta nyingine za wananchi kuwa na mipango mizuri ya kukabiliana na njama hizo za adui.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amemshukuru Mwenyezi Mungu kutokana na harakati nzuri za vijana wa Iran katika kuuhuisha Uislamu na kusimamisha dini na kusema, vijana hao kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu watampigisha magoti adui yeyote yule ikiwemo Marekani na utawala wa Kizayuni. 
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa: Sababu inayonifanya nisisitize mno katika maneno yangu kwamba nina mtazamo mzuri na matumaini ya mustakbali mwema ni kuweko vijana kama hawa na uhakika kama huu ambao unao uwezo wa kuifanya nchi isonge mbele.
Vilevile amesema, vijana walio imara kiimani, wenye msukumo wa hali ya juu na walio tayari wakati wote kuingia katika medani za jihadi na kulinda nchi, ni wengi nchini Iran. Amesisitiza kuwa: Huu ndio huo msukumo ambao utaweza kuiokoa nchi, hivyo kuna wajibu wa kuuimarisha na kuutia nguvu msukumo huo.

700 /