Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Mti habithi uliolaaniwa wa Aal Saud haustahiki kusimamia Hija

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei leo asubuhi (Jumatano) ameonana na familia za mashahidi wa Mina na wa Msikiti Mtakatifu wa Makka na kusema kuwa, kutokuwa na uwezo wa kusimamia Hija kwa ukoo wa Aal Saud kulikopelekea kutokea tukio hilo, kwa mara nyingine tena kumethibitisha namna mti huo habithi uliolaaniwa usivyo na ustahiki wa kusimamia na kuendesha Haram Mbili Tukufu za Makka na Madina. Amesisitiza kuwa: Kama Aal Saud wanasema kweli ya kwamba hawakuwa na makosa katika tukio hilo, basi waruhusu kuundwe tume ya kutafuta ukweli ya Kiislamu na kimataifa, ili iweze kuchunguza kwa karibu jambo hilo na kuwaonesha walimwengu uhakika wake.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa, kuonana na familia za mashahidi wa Mina na wa Masjidul Haram kunakumbushia tukio chungu la mwaka jana na kuongeza kuwa: Tukio la Mina lililopelekea kupoteza maisha mahujaji wengi wakiwemo wa Kiirani wakiwa katika ibada na katika midomo yenye kiu, chini ya jua kali, ni tukio la kusikitisha mno ambalo si rahisi kusahaulika. Ameongeza kuwa, tukio hilo lina vipengee mbalimbali vya kuweza kutumiwa kuwaamsha watu kisiasa, kijamii, kimaadili na kidini na inabidi vipengee hivyo visisahauliwe.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Lilikuwa jambo zito sana kwa familia za mahujaji kusikia habari ya kufariki dunia wapendwa wao na kupokea maiti za jamaa zao mwaka jana, lakini katika upande wa pili wa msiba huo, kuna jambo jingine nalo ni kujua kwamba, wapendwa hao ni sawa na mashahidi walioko chini ya kivuli cha maghufira, rehema na neema za Mwenyezi Mungu na hilo linazipa utulivu na kuzifariji nyoyo za wafiwa.
Baada ya hapo, Ayatullah Khamenei ameashiria kufa shahidi karibu mahujaji elfu saba mwaka jana katika maafa ya Mina na kutoa lawama kali akisema, kwa nini nchi na tawala zilizopoteza watu wao katika tukio hilo, hazichukui hatua yoyote?
Amesema, kunyamazia kimya kwa viongozi wa nchi na maulamaa na wanaharakati wa kisiasa na wasomi na watu wenye vipawa katika ulimwengu wa Kiislamu mbele ya tukio la kufa shahidi mahujaji elfu saba wasio na hatia, ni mtihani mkubwa kwa Umma wa Kiislamu na kuongeza kuwa: Kutoguswa na kutoonesha hisia zozote mbele ya maafa mazito na yaliyosababisha huzuni kubwa kama ya Mina, ni msiba mkubwa katika ulimwengu wa Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, kitendo cha watawala wa Saudi Arabia cha kukataa hata kuomba radhi kwa maneno tu ni jeuri iliyopindukia mipaka na ni kukosa kwao haya na kuongeza kuwa: Hata kama tujaalie tukio hilo halikufanyika kwa makusudi, lakini wa kulaumiwa kwa kosa hilo ni kundi la watawala wa kisiasa wa nchi hiyo ambao wameshindwa kuweka mipango madhubuti ya kusimamia vizuri ibada ya Hija.
Ayatullah Khamenei ameendelea na hotuba yake mbele ya familia zenye majonzi za mashahidi wa Mina kwa kuuliza swali muhimu akisema: Wakati utawala fulani unaposhindwa hata kuwasimamia wageni wa Mwenyezi Mungu ambao kwenda kwao Hija kuna pato zuri kwa utawala huo, kuna dhamana gani ya kutojikariri maafa kama ya Mina inapotokezea hali kama ya huko nyuma?
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Taifa la Iran limesimama kishujaa kukabiliana na ujahili na upotofu wa ukoo wa Aal Saud na linaendelea kubainisha kwa uwazi misimamo yake ya haki inayotiwa nguvu na mafundisho ya Qur'ani Tukufu na inabidi mataifa na nchi nyingine duniani zisimame kishujaa kukabiliana na ukoo huo wa Aal Saud.
Amesema, kushindwa Wasaudia kusimamia vizuri amali ya Hija na ukosefu wa usalama wanaobebeshwa mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Allah kwa hakika ni jambo linaloonesha kuwa, utawala huo wa Aal Saud haustahiki kusimamia Haram Mbili Tukufu (za Makka na Madina) na inabidi uhakika huo uenezwe na kubainishwa vilivyo katika ulimwengu wa Kiislamu.
Ayatullah Khamenei amesema, kipengee kingine kinachohusiana na tukio la Mina, ni kimya cha kutisha kilichoonesha na watu wanaodai kulinda haki za binadamu duniani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia makelele ya kisiasa na kipropaganda ya mashirika yanayodai kutetea haki za binadamu kuhusiana na utekelezaji wa baadhi ya maamuzi ya mahakama katika baadhi ya nchi na kuongeza kuwa: Kunyamazia kimya tena vibaya sana uzembe wa utawala fulani ulioshindwa kutekeleza vizuri majukumu yake na kupelekea watu elfu saba kufa kidhulma tena bila ya hatia, kunazidi kuthibitisha uongo wa watu hao wanaodai kutetea haki za binadamu duniani na kwamba, wale watu ambao wana tamaa na mashirika ya kimataifa kama hayo, wanapaswa kupata funzo kutoka katika tukio hilo chungu.
Ayatullah Khamenei amesema, kuundwa tume ya kutafuta ukweli ni miongoni mwa kazi za wajibu na za dharura zinazopaswa kufanywa na nchi za Kiislamu na wale wanaodai kutetea haki za binadamu duniani. Ameongeza kuwa, baada ya kupita mwaka mzima tangu lilipotokea tukio hilo la kuhuzunisha mno, utafiti uliofanywa kuhusu nyaraka na ushahidi mbalimbali wa video, sauti na maandishi, umefichua kwa kiwango kikubwa uhakika wa tukio hilo.
Vilevile amewahimiza viongozi wa Iran kulipa uzito mkubwa suala kufuatilia suala la kundwa kamati ya kutafuta ukweli na kuongeza kuwa: Kama Aal Saud wana yakini na madai kuwa hawana makosa katika tukio la Mina, basi wasifumbe midomo ya watu kwa kuwahonga fedha, na waruhusu kuundwe tume ya kutafuta ukweli ili kulichunguza kwa uhuru na kwa karibu suala hilo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema katika sehemu nyingine ya hotuba yake kwamba, wanaouunga mkono utawala wa Aal Saud ni washiriki wa jinai za utawala huo katika maafa ya Mina na kuongeza kuwa: Utawala usio na huruma wa Aal Saud kwa uungaji mkono wa Marekani, umesimama kukabiliana na Waislamu kwa jeuri kubwa na unamwaga damu za Waislamu katika nchi za Yemen, Syria, Iraq na Bahrain; hivyo Marekani na waungaji mkono wote wa Riyadh ni washiriki wa jinai za Aal Saud.
Ayatullah Khamenei ameashiria pia namna mashirika ya kipropaganda ya vibaraka wa Saudia yanayofanya kila njia kujaribu kuzihusisha jinai za Mina na hitilafu na mivutano baina ya Waislamu wa Kishia na Kisuni au ugomvi baina ya Waarabu na wasio Waarabu na kuongeza kuwa: Wanaowasaidia kipropaganda watawala wa Saudi Arabia wanakariri-kariri na kurudia-rudia madai ya uongo wakati ambapo wengi wa mahujaji elfu saba waliouawa shahidi huko Mina, ni Waislamu wa Kisuni licha ya kuweko pia mahujaji wengi wa Iran waliouawa shahidi kwenye maafa hayo.
Amesema: Ukoo wa Aal Saud na magenge ya magaidi makatili yalioanzishwa na kutiwa nguvu na wao wenyewe yanawaua kwa umati Waarabu katika nchi za Yemen, Syria na Iraq; hivyo tofauti na propaganda za kikhabithi zinazoenezwa na Wamagharibi, Wasaudia si watetezi na wala si walinzi wa Waarabu na kwamba tukio la Mina halina uhusiano wowote na mvutano wa kupandikiza unaodaiwa kuwepo baina ya Waarabu na wasio Waarabu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Uhakika wa jambo hilo ni kwamba, Wasaudia wanaochukiza, ni kundi ndani ya ulimwengu wa Kiislamu ambalo baadhi yao kwa kujua na baadhi yao kwa kutojua, wanawafanyia vitendo vya kiadui Waislamu na kwamba ulimwengu wa Kiislamu una wajibu wa kusimama kidete kukabiliana nao na vilevile utangaze kujibari na kuwa mbali kwake na mabwana wa Wasaudia yaani Marekani na Uingereza makhabithi.
Mwishoni mwa hotuba yake, Ayatullah Ali Khamenei amezitaka taasisi na vyombo mbalimbali nchini Iran ikiwemo Wizara ya Mambo ya Nje, Taasisi ya Biitha, Taasisi ya Hija na Taasisi ya Mashahidi, zitekeleze vilivyo na zifuatilie kwa uzito mkubwa majukumu yao kuhusiana na tukio kubwa la Mina.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatul Islam Walmuslimin Qadhi Askar, mwakilishi wa Fakihi Mtawala (Waliyyul Faqih) katika Masuala ya Hija na Ziara ametoa mkono wa pole kwa mnasaba wa kuwakumbuka mashahidi wa Septemba 8, 1978, na pia mashahidi wa Ijumaa ya umwagaji damu huko Makka iliyotokea mwaka 1366 Hijria Shamsia (Agosti 2, 1987) na mashahidi wa Hija ya mwaka jana na kusema kuwa, maafa mawili makubwa ya Mina na lile la ndani ya Masjidul Haram, yaliigeuza furaha ya Hija kuwa msiba na kuwatumbukiza watu na familia zao kwenye majonzi makubwa.
Hujjatul Islam Walmuslimin Qadhi Askar amegusia pia namna Wasaudia wanavyokwamisha juhudi za kuundwa kamati ya kutafuta ukweli kuhusu maafa hayo na kusema kuwa, Taasisi ya Biitha ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na Taasisi ya Hija ya Iran zimekusanya ushahidi mbalimbali uliotolewa kuhusiana na maafa hayo na kwamba imeshirikiana na wanasheria kugundua njia za kulifuatilia jambo hilo katika taasisi za kisheria za kimataifa na kamwe hazitaruhusu suala la Mina lisahauliwe.
Naye Hujjatul Islam Walmuslimin Shahidi Mahallati, mwakilishi wa Fakihi Mtawala ambaye pia ni mkuu wa Taasisi ya Mashahidi na Masuala ya Kujitolea katika Njia ya Haki ametoa ripoti fupi kuhusiana na kazi na hatua zilizochukuliwa na taasisi hiyo kuhusu matukio ya Mina na Masjidul Haram na kusema: Maafa ya kutisha na kutia majonzi ya Mina yametokea kutokana na uendeshaji mbaya na uanagenzi wa ukoo wa Aal Saud.

700 /