Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Ayatullah Khamenei:

Hauza inapaswa kubuni mpango wa mabadiliko

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei leo asubuhi (Jumapili) ameonana na kuzungumza na wajumbe wa Baraza Kuu la Hawza (vyuo vikuu vya kidini) ambapo amesisitiza kuwa, Hawza haziwezi kutenganishwa kabisa na masuala ya serikali ya Kiislamu. Ameongeza kuwa, serikali ya Kiislamu inaihitajia Hawza yenye watu makini, walioiva kielimu, wasafi, wabunifu na wanaojua mahitaji ya zama kwa ajili ya kueneza mafundisho na sheria za Kiislamu katika pande zote maisha ya mwanadamu na kuingia ndani kabisa ya jamii. Amesema: Miongoni mwa mahitaji makuu na muhimu ya Hawza kwa sasa ni kubuni mpango wa mabadiliko katika vyuo vikuu vya kidini na kuweka mipango ya muda mrefu, makini na ya kufanyika katika muda maalumu kulingana na mpango huo wa mabadiliko na malengo yaliyokusudiwa.
Amesisitiza kuwa, kuweka mipangilio mizuri katika Hawza kwenye vitengo mbalimbali hususan kitendo cha masomo, utekelezaji na masuala ya kiutawala inabidi yote yafanywe kwa ajili ya kusaidia kutajirisha uhusiano na serikali ya Kiislamu. Ameongeza kuwa: Hawza na vyuo vikuu vya kidini ni nguzo ya kusimamisha sheria na hukumu za Kiislamu, hivyo kama serikali ya Kiislamu itakuwa inatekeleza vilivyo sheria na hukumu za Kiislamu, jukumu la Hawza ni kuiunga mkono serikali hiyo kwa nguvu zake zote na kuionya serikali pale inapofanya makosa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, ni jambo la dharura mno kwa Hawza kuwa na mipango ya muda mrefu na kusisitiza kuwa: Katika mipango hiyo, inabidi malengo yawekwe wazi kikamilifu na yawe yana sifa ya ya kutekelezeka; yawe na muda maalumu wa kutekelezwa kwa namna ambayo mipango hiyo iweze kutathminiwa vizuri na kufanyiwa mabadiliko kila inapohitajika.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa, mipango ya muda mrefu ya Hawza inabidi isimame juu ya mpango wa mabadiliko makuu ya Hawza na kuongeza kuwa: Inabidi kuanzishwe kituo kikuu cha utafiti wa kiistratijia kitakachoundwa na watu muhimu na walioiva katika Hawza; na ndani ya kituo hicho kufanyike mipango ya mabadiliko na mipango mingine mbalimbali ya kiistratijia.
Mwishoni mwa hotuba yake, Ayatullah Ali Khamenei ametoa nasaha kadhaa akisema: Kujiepusha na mifumo ya kiutawala inayofanana na serikali, kuweko vikao na mazungumzo baina ya wakuu wa Hawza na wanafunzi, kujenga anga ya kuwa karibu mno na Qur'ani Tukufu kati ya wanafunzi, kugundua vipaji bora na kuvilea ipasavyo, kueneza tabia ya kutalii na kusoma hususan katika nyuga za historia ya elimu za hauza na tafsiri ya Qur'ani, kulea wafanya tablighi kwa njia ya kalamu, hotuba na tablighi kwa kutumia Intaneti ni miongoni mwa nukta ambazo zinapaswa kupewa umuhimu mkubwa katika Hawza na vyuo vikuu vya kidini.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ustadi, Katibu wa Baraza Kuu la Hawza, ametoa ripoti fupi kuhusu mipango na kazi za baraza hilo na changamoto zilizoko mbele yake.
Vilevile Hujjatul Islam Walmuslimin A'rafi, mkuu wa Hawza ametoa ufafanuzi kuhusu hatua muhimu mno zilizochukliwa katika miaka ya hivi karibuni katika vitengo mbalimbali vya taasisi hiyo.
 

700 /