Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Usalama ni nguzo muhimu ya maendeleo ya nchi

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei  leo adhuhuri (Jumanne) ameonana na makamanda na maafisa wa Jeshi la Polisi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mnasaba wa siku ya jeshi hilo na kusema kuwa, usalama ni moja ya nguzo kuu na za kimsingi za maendeleo ya nchi. Amesisitiza nafasi muhimu ya jeshi la polisi katika kuleta na kudumisha amani na kuongeza kuwa, kuna ulazima wa kuongezwa siku baada ya siku uwezo na utayarifu wa jeshi la polisi na azma na imani ya wafanyakazi wake.
Katika mkutano huo, Ayatullah Khamenei amesema pia kuwa, usalama una maana ya utulivu wa kisaikolojia wa watu mmoja mmoja na wa jamii nzima na kuongeza kuwa: Wakati usalama unapokosekana, uwezekano wa kufanyika harakati mbalimbali za kiuchumi, kiutamaduni, kisiasa na utoaji huduma nao hupoteka hata kama kutakuwa na uwezo na ari kati ya watu wa jamii hiyo.
Akitoa ushahidi wa aya za Qur'ani Tukufu kuthibitisha kuwa usalama huwa sababu ya kuongezeka imani ya waumini, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Amesema: Jeshi la polisi ni miongoni mwa nguzo muhimu zaidi za usalama nchini. Amesema, ni jambo lisilo na shaka kwamba, nguzo hiyo kubwa ya usalama ina nguvukazi ya watu ambao wengi wao ni makini, watu wema na wanaofanya kazi kwa ikhlasi na bidii kubwa, na inabidi nia, imani, ari na moyo huo ulindwe daima kwenye jeshi hilo.
Vilevile amegusia huduma kubwa zinazotolewa na jeshi la polisi nchini Iran na kutilia mkazo udharura wa kupewa mazingatio maalumu nafasi ya vituo vya polisi kutokana na kazi yao ya kuwajihiana moja kwa moja na watu wa aina mbalimbali katika jamii.
Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria pia mabadiliko ya haraka yanayotokea katika sekta mbalimbali kama vile sekta ya maendeleo ya sayansi na teknolojia, na kusisitzia ulazima wa kuongeza utayarifu na kusasisha uwezo wa jeshi hilo, kuelewa majukumu na kuyatekeleza kikamilifu pamoja na kutumia vyombo vya habari kubainisha kwa umakini na kwa kina kazi na huduma zinazotolewa na Jeshi la Polisi kwa wananchi, kwa ajili ya kudhamini na kuimarisha usalama nchini.
Kabla ya mkutano huo, hadhirina wamesalishwa Sala za Adhuhuri na Laasiri na Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

700 /