Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Mauaji ya Saudia dhidi ya Wayemen ndio aina mbaya zaidi ya ugaidi

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa ugaidi ni miongoni mwa masaibu yanayoiumiza sana jamii ya mwanadamu.
Ayatullah Khamenei aliyasema hayo jana jioni katika mazungumzo yake na Rais Sauli Niinistö wa Finland hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, mauaji ya halaiki kama yale yanayofanywa na serikali ya Saudi Arabia dhidi ya watu wa Yemen ndio aina mbaya zaidi ya ugaidi. Amesisitiza kuwa, mapambano dhidi ya ugaidi yanahitaji azma kubwa ya wale wote wenye ushawishi ndani ya mamlaka ya kimataifa, na kwamba watu wenye busara, nchi mbalimbali na wale wenye nguvu na sharafu duniani wanapaswa kutafakari na kuchukua hatua za kuondoa uovu huo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, Marekani na baadhi ya nchi hazina azma thabiti ya kupambana na ugaidi na kuongeza kuwa, nchi hizo zinayahesabu masuala yote kwa mujibu wa maslahi yao na hazifikirii kabisa suala la kutokomeza maradhi ya ugaidi iwe ni huko Iraq au Syria.
Akitoa mfano wa hali ya kutokuwepo azma ya kupambana na ugaidi, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria mauaji yanayofanywa dhidi ya watu wa Yemen na kusema: Ugaidi hauna maana na vitendo vya kigaidi vinavyofanywa na makundi yasiyo rasmi pekee, bali mauaji ya halaiki yanayofanywa na nchi mbalimbali kama mashambulizi  yaliyofanywa na Saudi Arabia dhidi ya majlisi ya maombolezo nchini Yemen na kuua mamia ya watu na kujeruhi wemgine ni aina mbaya zaidi ya ugaidi; na licha ya kupita mwaka mmoja na miezi saba sasa tangu kuanza kwa mauaji kama hayo hakuonekani azma ya kweli ya kukabiliana nayo. 
Vilevile Ayatullah Khamenei amesema msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu utatuzi wa kadhia ya Syria ni wa kimantiki na unaotetea taifa na serikali halali ya nchi hiyo. Ameongeza kuwa, Marekani na baadhi ya nchi nyingine zinasisitiza suala la kuondolewa madarakani serikali ya Syria ilhali ni lazima kwanza kuainishwa aliyeanzisha na kuchochea vita kwa ajili ya kukomesha vita hivyo.
Amesema kuwa hatua ya Umoja wa Mataifa ya kutotilia maanani upande ulioanzisha vita na hujuma katika vita vya Saddam Hussein na Iran ni miongoni mwa sababu zilizopelekea kurefuka kwa vita hivyo. Ameongeza kuwa, miaka kadhaa baada ya kumalizika vita hivyo vya kulazimishwa Katibu Mkuu wa wakati huo wa Umoja wa Mataifa ambaye alikuwa mtu wenye dhamira safi na shujaa, alimuarifisha Saddam Hussein kuwa ndiye aliyeanzisha vita. 
Katika uwanja huo Ayatullah Khamenei amekosoa misimamo ya Katibu Mkuu wa sasa wa Umoja wa Mataifa na kusema: Katibu Mkuu wa umoja huo amesema waziwazi kwamba kutokana na taasisi hiyo kutegemea fedha za Saudi Arabia hakuna uwezekano wa kulaaniwa mauaji yanayofanywa na nchi hiyo dhidi ya watoto wa Yemen, suala ambalo linadhihirisha hali ya kusikitisha ya kimaadili ya wanasiasa katika uongozi wa jumuiya za kimataifa. Amesisitiza kuwa, anatajia Katibu Mkuu ajaye wa Umoja wa Mataifa atalinda kujitawala kwa taasisi hiyo ya kimataifa.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amekaribisha suala la kuzidishwa kiwango cha ushirikiano wa Iran na serikali ya Finland na akasema kuwa: Makubaliano yaliyotiwa saini baina ya pande mbili yanapaswa kutekelezwa kivitendo na kutotekelezwa kwake kutakuwa na taathira mbaya katika fikra za wananchi.
Kwa upande wake Rais Sauli Niinistِ wa Finland ameeleza kuridhishwa na mazungumzo yake hapa mjini Tehran na na kusema: Leo kumetiwa saini hati nne za maelewano katika nyanja mbalimbali na hatua nzuri zimehukuliwa katika mazungumzo ya wajumbe wa biashara wa nchi hizi mbili. 
Rais wa Finland amesema ana matumaini kwamba, hati hizo hazitabakia kwenye karatasi na kwamba zitatekelezwa kivitendo na kuwa na matokeo mazuri. Amesisitiza kuwa jumuiya ya wafanyabiashara wa Finland ina azma kubwa ya kushirikiana na Iran. 
Rais Sauli Niinistِ wa Finland amegusia pia matukio ya miaka kumi ya hivi karibuni duniani na kushamiri kwa ugaidi na akasema, hali ya sasa ya dunia unatawaliwa na machafuko. Amesema ugaidi umechukua mwelekeo mpya na mkubwa zaidi na kuwalazimisha watu wengi kuwa wakimbizi. Amesisitiza kuwa, inasikitisha kuona kuwa, hii leo watoto na akina mama wengi wanauawa katika nchi za Syria, Iraq na Yemen. 
Vilevile ameunga mkono mtazamo wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu ugaidi. Amesema katika kikao hicho kilichohudhuriwa pia na Rais Hassan Rouhani kuwa, nchi mbalimbali na Umoja wa Mataifa zimefeli katika suala la kudhibiti na kupambana na ugaidi.
Amezungumzia pia nafasi na ushawishi wa Iran katika eneo la Mashariki ya Kati na mchango wake mkubwa katika kupambana na ugaidi na kasema kuwa, Iran imefanya jitihada kubwa katika suala la kung'oa mizizi ya ugaidi na kwamba hapana shaka kuwa kazi hiyo itadumishwa.
 

700 /