Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Matatizo yote ya Mashariki ya Kati yanasababishwa na Marekani

Ayatullah Khamenei amesema kiwango cha sasa cha uhusiano wa Iran na Sweden kiko chini ya uwezo wa nchi mbili hizi na kuongeza kuwa: Taifa la Iran lina mtazamo chanya kwa Sweden kutokana na mahusiano ya muda mrefu ya nchi hiyo na Iran, suala ambalo linaandaa mazingira mwafaka kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano. 
Ameashiria pia safari za mara kwa mara na mazungumzo ya baadhi ya serikali za Ulaya na Tehran katika mwaka mmoja na nusu uliopita na kutotekelezwa kivitendo aghlabu ya makubaliano yaliyofikiwa kati ya pande mbili na kumwambia Waziri Mkuu wa Sweden kwamba: Kutokana na maarifa niliyonayo kuhusu wewe mheshimiwa, ni kwamba ni mtu wa vitendo na mchapakazi; hivyo inatarajiwa kuwa, utahakikisha kwamba, makubaliano ya pande mbili hayabakii kwenye makaratasi.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, nguvu muhimu zaidi ya Iran ni vijana walioelimika na wenye nishati, walio tayari kuchapakazi na taifa lenye irada na azma imara. Ameashiria maandamano makubwa ya tarehe 22 Bahram (10 Februari mwaka huu) na kusema: Maadhimisho ya mapinduzi mbalimbali duniani hufanyika kwa sherehe rasmi za gwaride la jeshi na kuhudhuriwa na idadi kadhaa ya watu mashuhuri na wanasiasa, lakini hapa Iran sherehe za ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni sherehe halisi zinazofanywa na wananchi wenyewe na kuhudhuriwa na matabaka yote ya wananchi.
Amesema kuwa, mahudhurio hayo makubwa ya wananchi na ya kupigiwa mfano ni mfano wa kustaajabisha na usio na kifani wa nishati na utayarifu wa taifa la Iran na kuongeza kuwa: Wachambuzi wanaotoa hukumu kutokea mbali kuhusu Iran hawawezi kuelewa vyema adhama hiyo. 
Ayatullah Khamenei ameashiria kura ya Iran ya kuunga mkono suala la Sweden kupewa uanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kusema: Baraza la Usalama ni uwezo muhimu lakini inasikitisha kuwa, sasa limekuwa mfungwa na mateka wa baadhi ya madola makubwa; hata hivyo inawezekana kutumia taasisi hiyo kwa ajili ya kutoa mchango muhimu ili kuzuia misimamo ya kindumakuwili.
Katika sehemu nyingine ya matamshi yake Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema, matatizo yote ya eneo la Mashariki ya Kati yanatokana na uingiliaji wa baadhi ya madola makubwa katika masuala ya ndani ya eneo hili. Ameongeza kuwa, Marekani na madola mengi ya Ulaya yamehusika moja kwa moja katika matukio machungu ya syria na Iraq na kwamba wananchi wa eneo hili wamekasirishwa mno na uingiliaji wa madola hayo ya kibeberu. 
Amesema kuwa utatuzi wa matatizo ya eneo hili uko katika eneo hili hili la Mashariki ya Kati. Ameashiria hali inayoboreka nchini Iraq na kusema, mgogoro wa Syria nao unaweza kutatuliwa kwa njia hiyo hiyo na hilo litawezekana iwapo tu wanaowaunga mkono magaidi wataacha kufanya hivyo. 
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, kitendo cha baadhi ya mabalozi wa nchi za Magharibi cha kushirikiana na wapinzani wa serikali ya Syria na kuwapa silaha waziwazi mwanzoni mwa mgogoro wa nchi hiyo ni mfano wa wazi wa uingiliaji wa madola ya kibeberu katika masuala ya ndani ya nchi hiyo. Amesema, ili kuweza kutatua mgogoro huo kuna wajibu wa kujua kwanza chanzo chake na kisha zichukuliwe hatua za kuutatua.
Katika mazungumzo hayo yaliyohudhuriwa pia na Rais Hasssan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu, Waziri Mkuu wa Sweden, Stefan Löfven ameitaja safari yake mjini Tehran kuwa ni muhimu na ya kihistoria. Amepongeza mazungumzo ya pande mbili na kusema kuwa: Tumefanya mazungumzo kuhusu uhusiano wa kiuchumi na masuala muhimu ya kikanda na tutafanya juhudi za kutekeleza kivitendo makubaliano yaliyofikiwa.
Waziri Mkuu wa Sweden amesema kuwa, nchi yake ilikubali uanachama katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kutekeleza majukumu yenye taathira na tofauti, na kwa msingi huo tumetetea nafasi ya nchi wanachama katika Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote.
Bwana Stefan Lofven ametilia mkazo umuhimu wa nafasi ya mataifa na vijana wenye elimu na watanashati na kusema jamii kijana ya Iran ni mtaji na utajiri wenye thamani kubwa.  
 
 

700 /