Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Ayatullah Khamenei:

Kumfuata kivitendo Mtume (saw) kunatimia kwa kupambana na ukafiri

Ayatullah Ali Khamenei ambaye alihutubia mkutano huo amesisitiza umuhimu wa maana na madhumuni ya mashairi ya kidini na kusema kuwa, kuwasifu Maimamu watoharifu katika kizazi cha Mtume (saw) na kutaja msaibu yao ni sehemu muhimu ya mashairi ya kidini lakini katika uwanja huu kunapaswa kutumiwa maneno ya mantiki, busara na yanayotokana na mtazamo sahihi na kujiepusha na ufahamu wa kijuujuu na usio ya kisomi au kueleza masuala ya kubuni tu na dhahania.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa, kuungana kwa matukio ya zama za awali za Uislamu na matukio ya kipindi cha sasa ni ujumbe muhimu kwa malenga na washairi wa kidini na kuongeza kuwa: Mtume Muhammad (saw) na Maimamu watoharifu katika kizazi chake walikuwa wakipambana vikali na dhulma, madhalimu, ukafiri, unafiki na ufuska na kwa sababu hiyo waliuawa shahidi na watawala madhalimu na waovu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kuwafuata sawasawa Maimamu maasumu ni kuwafuata kivitendo watukufu hao na kudumisha mapambano dhidi ya ukafiri na unafiki. Ameongeza kuwa: Mapambano dhidi ya ukafiri na unafiki wa kimataifa ni rahisi na jambo linalowezekana katika Jamhuri ya Kiislamu lakini tangazo lolote la kujibari na kujitenga na Marekani chini ya kivuli kiovu cha baadhi ya tawala za eneo la Mashariki ya Kati hufuatiwa na hasira na jibu kali la tawala hizo.
Ayatullah Khamenei amesema, mapambano dhidi ya madhalimu hayahusu tu mapambano ya kutumia silaha na upanga na kwamba hii leo suala la kulingania dini duniani linachukua nafasi ya kwanza na inawezekana kupambana na madhalimu kwa kutumia maneno na mashairi. Amesisitiza kuwa, katika miaka ya hivi karibuni kumeshuhudiwa mifano mizuri sana na ya kutia matumaini katika uwanja huo.
Ameashiria uwezo mkubwa wa sheria na maarifa ya Kiislamu na kutilia mkazo udharura wa kutumiwa ipasavyo maana hizo aali katika mashairi ya kidini. Amesema: Kuna maana kubwa na zenye mafunzo katika dua na minong'ono hususan dua za kitabu cha Sahifa Sajjadiyyah na inawezekana kutumia bahari hiyo kubwa katika mashairi ya kidini.
Suala la mtindo wa maisha na wajibu wa malenga na washairi wa kidini mkabala wake, ni miongoni mwa masuala yaliyoashiriwa na Kiongozi Muadhamu katika mkutano huo. Amesema kuwa: Hii leo barani Ulaya na Marekani kumeanzishwa vituo na taasisi zenye malengo maalumu kwa ajili ya kubadili mtindo wa maisha katika nchi zisizo za Kimagharibi hususan Iran ya Kiislamu.
Ayatullah Khamenei amesema lengo la hujuma inayofanywa dhidi ya mtindo wa maisha wa Kiislamu ni kuanzisha irada, azma na harakati inayoowana na matakwa ya taasisi za Kimagharibi. Ameongeza kuwa, mkabala wa hujuma hiyo, haitoshi kujihami na kujiwekea uzio, bali tunaweza kutekeleza majikumu yetu kwa kubainisha na kuweka wazi mtindo wa maisha wa Kiislamu na kueleza mafundisho na misingi ya kimaadili, kisiasa na kiutamaduni katika kalibu na sura ya mashairi.
Vilevile ameeleza kufurahishwa na maendeleo ya mashairi ya kidini na ongezeko la malenga wanaojituma katika kutunga mashairi ya kidini na kusema kuwa: Shairi zuri huwa na taathira kubwa na kubakia siku zote, na leo hii tunahitajia washairi wenye uzito na daraja kama ya Hafidh, Sa'adi na Saib Tabrizi na lengo hilo linawezekana kwa kufanya juhudi, kutalii, kusoma mashairi ya watu adhimu na kutumia maneno mazuri na ya kuvutia katika mashairi.

     

 

700 /