Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Mudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Iran yenye maendeleo inahitajia vijana wasomi na wanamapinduzi

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei leo asubuhi (Jumatano) ameonana na zaidi ya vijana elfu moja wenye vipaji na vipawa mbalimbali vya kielimu na kusema kuwa, vijana hao ni zawadi yenye thamani kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu na ni amana mikononi mwa viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Vilevile amewasisitizia wajibu wa kutodharau hata kwa sekunde moja kuilinda na kuihami jamii ya watu wenye elimu na wenye vipawa nchini na kusema: Kwa kutegemea watu wenye hekima na wenye vipaji chini ya kivuli cha kulea kizazi cha vijana wenye jitihada kubwa, taifa kubwa la Iran litakuwa nchi yenye maendeleo makubwa, yenye nguvu, yenye heshima, azizi na yenye kupeperusha juu bendera ya ustaarabu mpya wa Kiislamu. 
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, jukumu la viongozi wa Iran mbele ya zawadi hii yenye thamani kubwa iliyotoka kwa Mwenyezi Mungu, ni kuwalinda watu hao wenye vipaji na kufanya juhudi za kivigundua na kuvilea kwa njia sahihi vipaji mbalimbali vilivyopo nchini.
Aidha amesema: Watu wenye vipaji nao wana jukumu mbele ya neema hiyo waliyopewa na Mwenyezi Mungu na wanapaswa kuwa na hisia za kutekeleza vizuri majukumu yao na kutumia vipaji na uwezo wao katika mambo sahihi kama njia ya kuonesha shukrani zao kwa Mwenyezi Mungu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, sababu kuu inayomfanya asisitizie mara kwa mara umuhimu wa kuthamini uwepo wa vijana wenye vipaji na wajibu wa kuwahami na kuwaunga mkono ni kutilia nguvu imani ya "sisi tunaweza" katika jamii.
Amesisitiza kwa kusema: Ni jambo la kusikitisha kuona kuwa, katika kipindi kirefu cha wafalme wa Qajar na Pahlavi nchini Iran, jeni ya kujiona duni, kuhisi sisi hatuwezi kufanya chochote na kuwa tegemezi wakati wote, ilipandikizwa baina ya watu na vijana wetu na matokeo yake ni kuwa, nchi kubwa ya Iran yenye vyanzo muhimu na nguvu kazi kubwa, yenye utajiri wa kutosha na historia kongwe, ikawa inaonekana dhalili mbele ya madola ya Magharibi.
Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yameleta mabadiliko adhimu nchini na kwa hakika, Mapinduzi ya Kiislamu yameleta kujiamini na kujitegemea na yametangaza vita na fikra ya kuwa tegemezi.
Amesema, ingawa vita vya kujihami kutakatifu (vita vya miaka minane vilivyoanzishwa na utawala wa zamani wa Iraq dhidi mfumo mchanga wakati huo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran) vilikuwa ni tukio chungu, gumu na lililosababisha hasara, lakini vilimthibitishia kijana wa Kiirani kwamba anaweza kwa kutawakali kwa Mwenyezi Mungu na kwa kutegemea vipaji na uwezo wao wa ndani, kumshinda adui ambaye alikuwa akiungwa mkono na madola yote makubwa ya dunia.
Ayatullah Khamenei ameongeza kwamba: Ijapokuwa Mapinduzi ya Kiislamu yamefufua moyo wa "sisi tunaweza" mbele ya fikra ya kujiona tegemezi na kueneza fikra ya kujiamini katika jamii, lakini upande wa pili kama ilivyotegemewa wameamua kuanzisha vita vikali ambavyo leo hii vinaitwa vita laini kukabiliana na Mapinduzi ya Kiislamu. Maadui wanaendesha vita hivyo kupitia njia ya kuzalisha upya utamaduni mbovu wa kujiona duni na wa kuwa tegemezi kwa kutumia mbinu mpya ambazo kijuujuu zinaonekana za kuvutia.
Amegusia suala la utandawazi na mwito wa Wamarekani na madola ya Ulaya wa kujiunga Iran eti na "familia ya kimataifa" na kusema kuwa, huo ni mfano wa wazi wa kuzalisha upya utamaduni tegemezi nchini Iran. Amesema: Upinzani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran dhidi ya kujiunga na kile madola ya Magharibi yanachodai ni jamii ya kimataifa, hauna maana ya kukataa kuwa na uhusiano na nchi za nje bali kuna maana ya kusimama kidete kukabiliana na utamaduni wa kutwishwa wa madola ya kibeberu yenye hamu kubwa ya kudhibiti uchumi, siasa na usalama wa Iran. 
Vilevile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia matatizo yaliyomkumba mwanadamu leo hii na jinsi fikra za kimaada zilivyomkwamisha mwanadamu katika kila kitu na kuongeza kuwa, dunia inahitajia fikra na mambo mapya ya kuweza kutatua matatizo ya mwanadamu na masuala ya kimataifa. Amesema, kampeni za uchaguzi nchini Marekani na jinsi wagombea wawili wanavyotumia mbinu chafu za kuchafuliana jina ni mfano wa wazi wa madhara ya kukosekana umaanawi na imani kwa watu wenye madaraka.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, katika wiki chache zijazo, mmoja wa wagombea hao wawili atakuwa rais wa Marekani lakini sote tunaona maneno yasiyo laiki wanayoyatoa na tunayaona wazi maadili yao bali hatari zaidi ni kwamba mmoja wa wagombea hao wenye maadili kama hayo, atakuwa rais wa nchi ambayo ina nguvu, utajiri, idadi kubwa ya silaha angamizi za atomoki na vyombo vikubwa vya habari duniani.
Ayatullah Khamenei ameendelea na hotuba yake kwa kusema kuwa, ili mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu uweze kufikia kwenye malengo yake hayo makuu, inahitaji kuwa na kizazi cha watu mashujaa, walioimarika kwa imani, wasomi, wabunifu, walioko mstari wa mbele katika kila kitu, wanaojiamini, wenye ghera, amilifu na wenye misukumo mingi ya hali ya juu. Amesisitiza kuwa: Kizazi cha namna hiyo ndicho hasa kinachoitwa kizazi cha Mapinduzi ya Kiislamu licha ya kuweko propaganda nyingi dhidi yake na ni kizazi cha namna hiyo ndicho ambacho kitatumia uwezo na nguvu zake zote kwa ajili ya kuiletea maendeleo Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Kuna baadhi ya watu unapotaja tu neno "adui" wanakasirika lakini kurudia rudia neno na tahadhari hiyo ni kama vile ilivyofanya Qur'ani Tukufu kurudia mara nyingi neno "shetani" kwa shabaha ya kuleta mwamko na tahadhari wakati wote na kwa hakika kukariri neno hilo adui mara kwa mara ndiko kuzitambua vyema njama za adui. 
Amesema, lengo kuu la adui ni kukwamisha harakati ya kielimu ya Iran na pale anapoona ameshindwa, hufanya njama za kupotosha njia ya harakati hiyo na akiona ameshindwa hukimbilia kwenye kuipaka matope, hivyo watu wote wanapaswa kuwa macho na wasifanye mambo kiuwanagenzi wakawa sababu ya kusaidia kufanikishwa njama hizo za maadui.
Vilevile Ayatullah Khamenei amezungumzia uadui wa madola ya kishetani dhidi ya kila harakati inayopinga ubeberu wao na kusema kuwa: Siku chache zilizopita, kiongozi mmoja wa Marekani alisema kuwa maadamu Iran inaendelea kuunga mkono muqawama na mapambano ya wananchi kama wa Palestina, tusitarajie kabisa kuwa vikwazo vitaondolewa dhidi yake, na huo kwa hakika ndio uhalisia wa mambo ambao nimekuwa nikiwakumbusha na kuwasisitizia viongozi nchini mara chungu nzima.
Vilevile amegusia jinsi viongozi wa Marekani wanavyolalamika kuwa, Kiongozi Muadhamu hana mtazamo mzuri kabisa kuhusiana na Marekani na kuhoji kwa kusema: Wakati maneno ya viongozi wa nchi hiyo ni kama hayo niliyoyanukuu hivi punde, inawezekana kweli kuwa na mtazamo mzuri na Marekani?
Aidha amesema: Mara chungu nzima nimekuwa nikiwaambia viongozi humu nchini katika vikao vya wazi na vya faragha kwamba, kama mtalegeza kamba katika kadhia ya nyuklia, jueni kuwa maadui watazusha suala la makombora, na kama mtalegeza kamba katika hilo, watazusha suala la kuunga mkono muqawama na kama katika hilo pia mtalegeza kamba, watazusha suala la haki za binadamu na kama misimamo na siasa zetu hazitakubaliana na vipimo vyao wao, watakimbilia kwenye kufutwa kabisa vigezo vya kidini katika utawala, alimradi hakuna siku watakinaika au kuachana na uadui wao dhidi yetu.
Vilevile amegusia tamko la hivi karibuni la Umoja wa Ulaya ambalo ndani yake limezungumzia uwezo adhimu wa Iran na kusema: Wakati tunaposema kuwa Iran ina suhula nyingi za maendeleo na nguvu kazi madhubuti pamoja na utajiri mkubwa wa maliasili, huwa hatuongezi chumvi, bali ni uhakika ambao hata Wamagharibi nao wanaukiri. 
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Bila ya shaka yoyote, Wamarekani wanaipiga vita Iran yenye uwezo huo mkubwa wa maendeleo na yenye utawala uliosimama juu ya msingi wa dini tukufu ya Kiislamu na ni wakati vijana wenye vipaji nchini Iran watakapougundua uhakika huo ndipo watakapoweza kutekeleza vizuri majukumu yao ya kihistoria.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah Khamenei amesema kuwa, tukio la Ashura ni jua lisilozama na kuongeza kwamba: Tukio la Ashura ni taswira ya kweli ya mapambano ya nuru dhidi ya giza, na vita vya heshima dhidi ya uovu ambapo Bibi Zaynabul Kubra (Salamullahi Alayha) na Imam Sajjad (Alayhis Salaam) ndio walioikamilisha harakati hiyo adhimu.
Vilevile amewashukuru wote walioongoza na kusimamia maombolezo ya Ashura mwaka huu na kusema, kushiriki wimbi kubwa la vijana kwenye kumbukumbu hizo, hotuba nzuri zenye mambo mengi mazuri na baadhi ya mashairi yenye maana pana ni katika mambo yaliyosaidia mno kufanyika maombolezo hayo kwa ufanisi.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Dk Sattari, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya Sayansi na Teknolojia ambaye pia ni mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Watu Wenye Vipaji nchini Iran, ametoa ripoti fupi kuhusiana na kazi na ratiba za baadaye za taasisi hiyo. 
Aidha wawakilishi kadhaa wa watu wenye vipaji nchini wametoa mitazamo, mapendekezo na fikra zao kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
 

700 /