Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Ayatullah Khamenei:

Ndoto kwamba Marekani haishindwi ni makosa makubwa

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei amefnya mazungumzo na Rais Nicolas Maduro wa Venezuela na huku akiashiria namna zilivyoshindwa njama na siasa za Marekani katika eneo la magharibi mwa Asia, amesema kuwa, suala la kupunguza bei ya mafuta ni wenzo unaotumiwa na Marekani kwa ajili ya kuzishinikiza nchi huru duniani. Amesisitiza pia kuwa: Bila ya shaka yoyote ushindi ndiyo matunda ya mapambano na kusimama imara kwa hekima na tadibiri mbele ya mashinikizo.
Ayatullah Khamenei ameashiria pia namna silaha ya mafuta inavyotumika kuzibebesha matatizo ziliyo nayo hivi sasa nchi huru duniani na kuongeza kuwa: Huko nyuma, wakati baadhi ya nchi za Kiislamu zilipoamua kuususia utawala wa Kizayuni wa Israel na kukataa kuuzia mafuta yao, Wamagharibi walizusha makelele mengi na kudai kuwa si sahihi kutumia mafuta kwa malengo ya kisiasa, lakini cha kusikitisha ni kuona kuwa, leo hii, nchi hizo hizo za Magharibi kwa msaada wa baadhi ya wanachama wa Opec na baadhi ya nchi za eneo hili (la Mashariki ya Kati) ambazo zenyewe zinapata madhara kutokana na siasa hizo, zote zinashiriki kikamilifu katika kufanikisha siasa za Marekani za kutumia mafuta kama silaha ya kuzishinikiza nchi nyingine. 
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Njama hizo na uadui huu uliopo hivi sasa unaweza kufelishwa kwa kutumia siasa za busara na kuongeza ushirikiano baina ya nchi huru duniani.
Vilevile ameashiria jinsi Marekani ilivyofeli katika siasa zake kwenye eneo la magharibi mwa Asia licha ya kutumia fedha nyingi mno kutoka mfukoni mwake na mifukoni mwa baadhi ya nchi za eneo hili na kusisitiza kwamba: Kuna baadhi ya watu wana fikra zisizo sahihi kuwa Marekani haishindiki wakati jambo hilo ni kosa kubwa na kwamba makosa ya mara kwa mara yaliyofanywa na Wamarekani katika kipindi cha miaka 15 iliyopita, yamewatumbukiza kwenye kinamasi na kuwakwamisha kikamilifu katika eneo hili hivi sasa.
Ayatullah Khamenei amegusia pia nafasi muhimu ya Venezuela katika harakati za kupambana na uistikbari kwenye eneo la Amerika ya Latini na kusisitizia ulazima wa kutumia vizuri fursa ya uenyekiti wa nchi hiyo katika harakati ya NAM (Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote). Ameongeza kuwa, Wamagharibi hawafurahishwi kuona harakati za NAM zinapata mafanikio na zinaongezeka, hivyo nchi huru duniani zinapaswa kuwa na msimamo unaokinzana kikamilifu na msimamo huo wa nchi za Magharibi, na kama zitafanya hivyo, basi mustakbali wake bila ya shaka yoyote utakuwa bora zaidi kuliko huko nyuma. 
Vilevile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina nia ya kweli ya kuongeza ushirikiano wake na Venezuela na kusisitizia wajibu wa viongozi na mawaziri wa nchi hizi mbili kulipa umuhimu mkubwa suala hilo na kufuatilia kwa kina utekelezaji wa maafikiano yanayofikiwa baina ya pande mbili.
Katika mazungumzo hayo ambayo yamehudhuriwa pia na Bw. Jahangiri, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Rais Nicolas Maduro wa Venezuela ameelezea kufurahishwa kwake na kupata fursa nyingine ya kutembela Iran na kuonana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusema: Hayati Hugo Chavez, rais wa zamani wa Venezuela aliitambua vizuri Iran na nafasi yake muhimu na muda wote alikuwa akisema kuwa Iran ni dola lenye nguvu.
Aidha amelisifu sana taifa la Iran kwa kusimama imara kukabiliana na uadui wa Marekani na kusema kuwa: Taifa la Iran linaishi katika utulivu na usalama kamili katika hali ambayo kwa masikitiko nchi nyingine za eneo hili zilizoizunguka Iran zimezama katika vita, mifarakano na udhaifu mkubwa.
Rais wa Venezuela ameashiria pia suala la kuporomoka bei ya mafuta katika kipindi cha miaka miwili iliyopita na kusema kuwa: Ubeberu wa Marekani unaingilia mambo ya ndani ya Venezuela na kulifanyia uadui mkubwa taifa hilo, lakini wananchi wa nchi hiyo wamesimama imara kukabiliana na vita hivyo vya kiuchumi na hivi sasa nchi hiyo imeanza kutoka pole pole kwenye mgogoro wa kiuchumi.
Rais Maduro amegusia pia kampeni za Uchaguzi wa Rais nchini Marekani na kusema kuwa: Mgombea yeyote kati ya wagombea hao wawili wakuu atakayeshinda kwenye uchaguzi huo, ataipeleka Marekani kwenye maporomoko, na hilo ni jambo la hatari sana kwa mustkbali wa dunia.
Rais wa Venezuela pia amesema, mazungumzo yake na viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yamekuwa ya mafanikio na kuongeza kwamba: Inabidi jitihada zote zifanyike kuhakikisha kuwa makubaliano yote yanayofikiwa yanatekelezwa kivitendo na kiufanisi.
 

700 /