Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Muungano wa Magharibi dhidi ya ugaidi si wa kweli, ni hadaa

Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo alasiri (Jumanne) ameonana na Bakir Izetbegović, Mwenyekiti wa Baraza la Urais la Bosnia Herzegovina na huku akitilia mkazo ulazima wa kukabiliana na siasa za kupenda vita na za kulea ugaidi za baadhi ya nchi za Magharibi amesema: Nchi huru duniani zinapaswa kuimarisha uhusiano wao na zisikubai kuathiriwa na siasa za madola ya kibeberu bali ziungane kuzima moto wa mizozo na mapigano.
Ayatullah Khamenei ameashiria pia wimbi la makundi ya kitakfiri na kigaidi ambayo leo hii yamefika pia barani Ulaya na kuna uwezekano hali ya bara hilo ikawa mbaya zaidi na kusema: Chimbuko la wimbi hilo ambalo kijuujuu linaonekana ni la eneo la nchi za Kiarabu, kwa hakika ni Marekani na baadhi ya tawala za nchi Ulaya ndizo hasa zilizozusha wimbi hilo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea kusema, muungano wa kijeshi wa nchi za Magharibi dhidi ya ugaidi si wa kweli na kuongeza kwamba: Ijapokuwa kuna uwezekano baadhi ya wakati muungano huo ukaingia vitani dhidi ya magaidi lakini hauna lengo kabisa la kung'oa mizizi ya ugaidi si Iraq na wala si Syria bali siasa mbaya na za kishari za madola hayo zinaongeza matatizo kadiri siku zinavyopita.
Amesema, utatuzi wa hali hiyo umo katika kufahamu chanzo cha kuzuka matatizo yaliyopo na kuwa na nia ya kweli ya kuyatatua. Vilevile ameashiria moja ya sababu za kuzuka ugaidi kwa kusema: Kudhalilishwa vijana wa Kiislamu katika baadhi ya nchi tajiri na zenye nguvu za barani Ulaya kumeandaa mazingira ya kujiunga vijana hao na makundi ya kigaidi yenye fikra mgando kama Daesh (ISIS) na wakati vijana hao wa Kiislamu wanaodhalilishwa wanaporejea barani Ulaya, huamua kujiripua na kufanya mauaji.
Ayatullah Khamenei amezungumzia pia historia ndefu ya uhusiano wa kirafiki baina ya Iran na Bosnia Herzegovina hususan katika kile kipindi kigumu cha vita walivyotwishwa wananchi wa nchi hiyo na kusema: Utulivu na usalama ni mambo mawili ya lazima kwa ajili ya kufanikisha nguzo zote za maisha ya taifa fulani na kwa ajili ya kukuwa na kustawi taifa hilo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbushia safari yake ya kuitembelea Bosnia Herzegovina wakati akiwa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na mapokezi mazuri sana aliyopata kutoka kwa wananchi wa nchi hiyo na vilevile amemuenzi rais wa zamani wa nchi hiyo hayati Ali Izetbegović na kusema: Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kikamilifu kupanua wigo wa ushirikiano na mawasiliano baina yake na serikali ya Bosnia Herzegovina katika nyuga tofauti.
Katika mazungumzo hayo ambayo yamehudhuriwa pia na Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Bw. Bakir Izetbegović, Mwenyekiti wa Baraza la Urais la Bosnia Herzegovina ameelezea kufurahishwa kwake na safari yake ya mjini Tehran na kusema kuwa, mazungumzo yake na viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yalikuwa ya mafanikio. Aidha ameelezea matumaini yake kuwa, uhusiano wa kiurafiki baina ya nchi hizi mbili utazidi kunawiri na kunawirisha pia ushirikiano mzuri wa kiuchumi kwa manufaa ya pande zote mbili.
Vilevile amesema, siasa za Bosnia Herzegovina zimesimama katika msingi wa kuimarisha na kutia nguvu uhusiano wake na nchi zote za Waislamu na huku akigusia ulazima wa kuweko ushirikiano wa kweli wa kupambana na hatari ya ugaidi amesema: Maradhi hayo hatari, yamefikia hadi ya kusababisha kushambuliwa misikiti na kuuliwa watu wasio na hatia, lakini huko Bosnia Herzegovina, shakhsia wote wakubwa wamesimama imara kupinga fikra za kitakfiri na pia wametangaza kujibari na kuwa mbali kikamilifu na fikra hizo.
Mwenyekiti wa Baraza la Urais la Bosnia Herzegovina ameelezea kusikitishwa kwake na vita na mapigano katika jamii za Waislamu na kusema kuwa, umoja na mshikamano ni jukumu la Waislamu wote na kwamba mizozo na mifarakano itapelekea kudhoofika tu jamii za Waislamu.

700 /