Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Ayatullah Khamenei:

Matatizo ya nchi yatatuliwe kwa moyo na fikra za kimapinduzi

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei leo asubuhi (Jumatano) ambayo imesadifiana na kipindi hiki cha kukaribia tarehe 13 Aban (Novemba 3) ambayo ni Siku ya Mwanafunzi na Siku ya Taifa ya Kupambana na Uistakbari wa Dunia nchini Iran, ameonana na maelfu ya wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu na huku akitahadharisha kuhusiana na baadhi ya harakati hatari za kupotosha ukweli na mantiki ya kusimama imara ya Imam Khomeini (quddisa sirruh) na kusimama kidete taifa la Iran mbele ya Marekani katika fikra za vijana na vilevile kujaribu kupandikiza fikra potofu kuwa njia pekee ya kutatua matatizo ya nchi ni kufanya mazungumzo na kufikia mapatano na Marekani; amesisitiza kuwa: Kitu ambacho kinaweza kutatua matatizo ya nchi ni kuwa na moyo na fikra za kimapinduzi kwa maana ya kutawakali kwa Mwenyezi Mungu, kujiamini, ushujaa katika maamuzi na vitendo, busuri na muono wa mbali, kutekeleza kivitendo nasaha za Imam Khomeini (quddisa sirruh), kuwa wabunifu, kuwa na matumaini mema na mustakbali, kutomwogopa adui na kutosalimu amri wala kumpigia magoti adui.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia uhusiano wa kihistoria wa tarehe 13 Aban katika nyakati tofauti na kusema kuwa, tukio kubwa zaidi lililotokea katika siku kama hiyo ni kutekwa pango la kijasusi la Marekani (uliokuwa ubalozi wa Marekani mjini Tehran) na kuongeza kuwa: Kwa hakika siku hiyo ni siku ya vijana wenye imani thabiti, wanamapinduzi, mashujaa, jasiri, nyamaume na wabunifu ambao kwa hatua yao ya kuliteka pango hilo la kijasusi, walifanikiwa kumbana adui na kumfanya ashindwe kuchukua hatua yoyote ile.
Ayatullah Udhma Khamenei amekumbushia nasaha za Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu awe radhi naye) alipoiita hatua ya kutekwa pango hilo la kijasusi kuwa ni mapinduzi ya pili na kuongeza kuwa: Hatua hiyo ya Imam ya kuipa jina hilo hatua hiyo, ilitokana na njama na ukhabithi wa Marekani kabla na baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu dhidi ya taifa la Iran, kwani serikali ya Marekani haikuacha kuchukua hatua yoyote ile, rasmi na isiyo rasmi, ya kujaribu kuyavunja Mapinduzi ya Kiislamu, hivyo hatua ya vijana wanamapinduzi wa wakati huo ya kuliteka pango hilo la kijasusi, ilivunja njama za Marekani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea na hotuba yake kwa kuashiria mijadala ya wagombea wawili wa uchaguzi wa Marekani na kusema kuwa: Siku hizi wagombea hao wawili wanafichua hadharani na kwa uwazi mambo ya uhakika na majanga makubwa yaliyoko ndani ya Marekani. Kabla ya wagombea hao kutoa fedheha hizo hadharani, kuna baadhi ya watu walikuwa hawaamini kuweko uhakika huo huko Marekani, au walikuwa hawataki kuamini; lakini hivi sasa mambo yanayosemwa na wagombea hao wawili yamezidi kuonesha uhakika wa kukosekana matukufu na thamani za kibinadamu nchini Marekani. 
Ametoa ushahidi wa masuala yaliyozungumzwa katika mijadala ya hivi karibuni ya uchaguzi wa Marekani kuhusiana na ubaguzi wa kizazi na ukata na umaskini nchini Marekani na namna asilimia 90 ya utajiri wa Marekani unavyodhibitiwa na asilimia moja tu ya wananchi wa nchi hiyo na kuongeza kuwa: Kukanyagwa na kupigwa teke thamani za kibinadamu na haki za wanadamu pamoja na ubaguzi na upendeleaji wa kizazi kimoja dhidi ya kingine, ni katika mambo yaliyokita mizizi na kuenea mno hivi sasa katika jamii ya Marekani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kwamba: Kama tunaona kuwa taifa la Iran lilisimama imara kukabiliana na Marekani wakati wa Imam Khomeini (quddisa sirruh) na kama leo hii pia tunaendelea kuona taifa hili linaendelea kutoa nara na shaari za kukabiliana na nchi hiyo, tujue kuwa yote hayo yanatokana na mantiki yenye nguvu na ushahidi madhubuti.

700 /