Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Marekani ni ile ile ya siku zote, Iran itasimama imara

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei, leo asubuhi (Jumatano) ameonana na maelfu ya wananchi wa Isfahan na kusema kuwa, mkoa wa Isfahan ni mkoa wa watu walioko mstari wa mbele kwa ajili ya kujitolea kufa shahidi katika njia ya haki, watu wa istikama na kusimama kidete, watu wa elimu na utamaduni, watu wa dini na kushikamana na Wilaya na watu wabunifu wa wanachapa kazi.
Vilevile amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haiwezi kusema chochote kuhusiana na uchaguzi wa Rais wa Marekani kwani muda wote imekuwa ikifanyiwa uadui wa kila namna na vyama vyote viwili vya nchi hiyo na kuongeza kuwa: Mahitaji muhimu zaidi leo hii nchini hususan kwa watu wenye vipaji na viongozi wa Iran ni kuwa na busuri na muono wa mbali wa kisiasa na kutoghafilika hata chembe na njama za adui.
Vilevile amesema mahitaji mengine muhimu kwa viongozi na watu wenye vipaji nchini ni kuwa na moyo na misimamo ya kimapinduzi, kuchukua hatua za kivitendo katika uchumi wa kimuqawama, kuendeleza kasi ya maendeleo na ustawi wa kielimu nchini, kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa na kulinda uimara wa kiroho na wa ndani ya watu binafsi na wa jamii kiujumla.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesema katika mkutano huo uliofanyika katika siku za kukumbuka hamasa ya wananchi wa Isfahan ya kuzika mashahidi 370 wa mkoa huo waliouawa shahidi katika opereseheni ya Muharram tarehe 25 Aban mwaka 1361 Hijria Shamsia (Novemba 16, 1982) kwamba, moja ya sifa za kipekee na za wazi za wananchi wa mkoa wa Isfahan ni moyo wao wa kuwa tayari kufa shahidi katika njia ya haki na kusimama kwao imara.
Aidha amesisitizia wajibu wa kuzijua njama za adui katika kila kipindi na zama na kutositasita katika kukabiliana na adui na kuongeza kuwa: Kusimama imara juu ya misingi na usuli za Mapinduzi ya Kiislamu, ni moja ya mahitaji muhimu sana ya hivi sasa na kwamba usuli za Mapinduzi ya Kiislamu ni ile misingi na vielelezo vilivyomo katika miongozo ya Imam Khomeini (quddisa sirruh) na wasia wake. 
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa nasaha kwa mara nyingine tena kwa vijana, wasome na watalii miongozo na wasia wa Imam Khomeini (quddisa sirruh) na kujua kuwa huo ndio muongozo wa harakati ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Amesisitiza kwa kusema: Imam ambaye aliitikisa duniani, ni kielelezo cha wazi cha matamshi yake na wasia huo na hatuwezi kumuangalia Imam (Rahmatullahi Alayh) kinyume na wasia na matamshi yake hayo na kujaribu kupindua matamshi na miongozo yake.
Amesema, njia pekee ya kuweza kutatua matatizo yaliyopo na kuziba pengo la kubakishwa nyuma kimaendeleo na hatimaye kufikia kwenye heshima ya kweli, ustawi na maendeleo ya kimaada na kimaanawi na ya kimaadili na kiutamaduni, ni kusimama imara juu ya usuli na misingi ya Mapinduzi ya Kiislamu. Ameongeza kuwa, katika upande wa kielimu pia, lazima tujiimarishe ndani ya nchi hususan katika utendaji wa viongozi serikalini na kusimamia vizuri uchumi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesema, adui ameulenga moja kwa moja uchumi wa Iran katika mashambulizi yake na kusisitiza kuwa, sababu ya yeye kuuita mwaka huu (wa Kiirani wa 1395 Hijria Shamsia) kwa jina la Mwaka wa Uchumi Ngangari na wa Kimuqawama, Hatua na Vitendo ni kutaka kuona athari za hatua na vitendo vya viongozi nchini katika uchumi huo zinaonekana wazi mbele ya wananchi.
Amma kuhusiana na matatizo ya ndani ya jamii ya Marekani na ambayo yalifichuliwa wazi na wagombea wakati wa kampeni za hivi karibuni za uchaguzi, Ayatullah Udhma Khamenei amesema: Wakati wa kampeni za uchaguzi huo, mtu ambaye hatimaye amechaguliwa kuwa Rais wa Marekani alisema, kama fedha zilizotumika kwenye vita katika miaka ya hivi karibuni zingelitumika kwa maendeleo ya ndani ya Marekani, basi nchi hiyo ingelijengwa mara mbili; je, wale watu waliopumbazwa na nukta hiyo ya kufikirika wameelewa maana ya maneno hayo?
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia maneno yaliyozungumzwa wakati wa kampeni za uchaguzi nchini Marekani yaliyofichua kiwango kikubwa cha umaskini, uharibifu na matatizo mengine mengine nchini humo na kuongeza kuwa: Katika miaka ya hivi karibuni, Marekani imetumia fedha za wananchi kwenye masuala ya vita na matokeo yake ni kuuawa mamia ya raia na kuangamizwa miundombinu ya nchi za Afghanistan, Iraq, Syria, Libya na Yemen. 
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa, mambo yote hayo yaliyofichuliwa na wagombea urais nchini Marekani yalikuwa yakizungumzwa kwa miaka mingi lakini kuna baadhi ya watu walikuwa hawataki kukubali na hapa ndipo linapokuja suala la wajibu wa kuwa na busuri na muono wa mbali kuhusiana na masuala mbalimbali yanayojiri duniani kila leo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea kuzungumzia matokeo ya uchaguzi wa hivi karibuni wa rais nchini Marekani na kusema kuwa, sisi hatuwezi kusema lolote kuhusu uchaguzi huo kwani Marekani ni ile ile na hakuna chochote kilichobadilika na kwamba katika kipindi cha miaka 37 iliyopita, kila chama kilichoingia madarakani kati ya vyama viwili (vya Republican na Democrats) hakuna chochote kilichokuwa na kheri kwa Iran, bali muda wote shari zao zimekuwa zikielekezwa kwa taifa la Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa, tofauti na baadhi ya watu duniani ambao wako miongoni mwao wanaomboleza na wengine wanafurahia matokeo ya uchaguzi wa Marekani, sisi hatuombolezi na wala hatufurahii, kwani hakuna tofauti yoyote kwetu sisi kama ambavyo pia hatuna wasiwasi wowote na kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu tuko tayari kukabiliana na tukio lolote linaloweza kutokea.
Amesema lililo muhimu kwa Iran hivi sasa ni kuzingatia njia za kutatua matatizo yaliyopo na yajayo nchini na njia pekee ya kuweza kufanikisha jambo hilo ni kulinda ustawi na uimara wa ndani ya nchi.

700 /