Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Kupambana na utawala wa Kizayuni ni kupambana na ubeberu

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alasiri ya jana alizungumza na mamia ya wahadhiri wa vyuo vikuu, wanachama wa jumbe za kielimu, watafiti na wasomi wa vyuo vikuu katika kikao kilichoendelea kwa kipindi cha zaidi ya masaa mawili. Katika Kikao hicho Ayatullah Khamenei ameeleza mchango usio na mbadala wa wahadhiri wa vyuo vikuu katika kulea wanafunzi na kutengeneza nafasi ya Iran katika dunia yenye changamoto na mabadiliko mengi na kusisitiza kuwa, Siku ya Kimataifa ya Quds ni tukio lenye umuhimu mkubwa. Amesema kuwa, siku hiyo si siku ya kutangaza uungaji mkono kwa taifa linalodhulumiwa tu bali pia ni nembo ya mapambano dhidi ya ubeberu na mabeberu wa kimataifa.

Ayatullah Khamenei ameashiria maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds na kusema: Kuadhimisha Siku ya Quds hakuna maana ya kutetea taifa linalodhulumiwa na ambalo limefukuzwa katika ardhi yake tu, bali hii leo kuitetea Palestina ni kutetea hakika pana zaidi kuliko kadhia ya Palestina.

Amesisitiza kuwa, kupambana na utawala wa Kizayuni wa Israel ni kupambana na ubeberu na mfumo wa kibeberu na kwa sababu hiyo wanasiasa wa Marekani wanahisi pigo kutokana na harakati hiyo na wanaifanyia uadui.

Baada ya hapo Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja maudhui kuu ya hotuba yake kuwa ni "majukumu ya ualimu" na kuongeza kuwa: Mwalimu na mhadhiri anayekuwa na fikra chanya, mwenye kushikamana na sheria, mwenye matumaini, mwenye imani na misingi ya kidini, thamani za kitaifa na masuala ya kimapinduzi na mwenye kuwajibika, mwenye azma kubwa na nia ya kutenda majukumu yake anaweza kuwa na mchango usio na kifani katika kumlazimisha mwanafunzi kufikiria na kufanya harakati.

Ayatullah Khamenei amesema, mkabala wake, iwapo mtazamo wa mhadhiri na mwalimu utakuwa ni wa nje ya nchi na hatakuwa na itikadi na imani na nchi yake wala fikra zilizopo zinazounda utambulisho wa taifa, basi atalea wanafunzi wenye mitazamo ileile mibovu, na uzoefu huo ulijitokeza katika kipindi cha utawala wa kifalme hapa nchini. Amesema: Mapinduzi ya Kiislamu kwa hakika yaliiokoa nchi kuongozwa na kizazi ambacho hakikuwa na thamani na utambulisho wa kidini na kitaifa.

Amesema kuwa, vyuo vikuu hapa nchini katika kipindi cha sasa ni vituo vya elimu, ubunifu na taathira katika jamii. Ameongeza kuwa, tangu kilipoanzishwa chuo kikuu nchini Iran vibaraka wa ubeberu walifanya jitihada za kuzuia kuwepo harakati ya kielimu inayonasibiana na kwenda sawa na vipawa vya Kiirani na ubunifu, na vilevile walidhibiti taathira ya vyuo vikuu katika jamii kupitia vyombo vya usalama na utamaduni tegemezi. 

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kuzuia uingizaji wa elimu na sayansi mpya nchini ilikuwa miongoni mwa mipango na sera za mabeberu kwa ajili ya kudhoofisha vyuo vikuu nchini Iran. Amaongeza kuwa: Katika kipindi kirefu cha utawala wa Kipahlavi, Wamagharibi hawakuleta maendeleo muhimu ya kisayansi na elimu ya kisasa katika vyuo vikuu hapa nchini na walizuia ubunifu wa aina yoyote katika vyuo hivyo kupitia njia ya kuvibadili na kuvifanya mahala pa kueneza thamani na maadili ya kimagharibi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria hatua muhimu ya wanafunzi wa vyuo vikuu na vyuo hivyo ya kuitikia wito wa harakati ya Imam Khomeini na kusema: Licha ya kwamba vyuo vikuu vilikuwa vikisumbuliwa na matatizo ya kimsingi na masuala mawili yaliyokuwa yakipinga fikra za Kiislamu, yaani mielekeo ya kimaxi na popaganda zilizokuwa zikiharibu na kuvuruga maadili mema, lakini vyuo vikuu vilijiunga katika safu za taifa na harakati ya Kiislamu, na baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu pia vilikuwa na nafasi ya kwanza katika kuunda tasisi za kimapinduzi kama taasisi ya Jihadi ya Ujenzi na Jeshi la Sepah. Amesisitiza kuwa, ukweli huo unaonesha mchango wa vyuo vikuu katika kuelekeza watu kwenye Uislamu na Mapinduzi, na hiyo ilihesabiwa kuwa fusra muhimu sana kwa ajili ya maendeleo Mapinduzi ya Kiislamu na Iran.

Ayatullah Khamenei amesema kuwa: "Kuokoa vyuo vikuu na kuviondoa katika mkondo wa upotovu", "kueleweka umuhimu wa elimu na ubunivu wa kisayansi katika vituo vya vyuo vikuu" na "kuanzisha harakati ndani ya vyuo vikuu" ni miongoni mwa baraka za Mapinduzi ya Kiislamu. Ameongeza kuwa, wanafunzi wengi wa kipindi hicho wamekuwa walimu na wahadhiri na sasa na wanaweza kuwa na mchango mkubwa katika kustawisha vyuo vikuu na kulinda thamani na maadili ya Kiislamu.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ametaja njia mbili makhsusi na zinazokamilishana kwa ajili ya kutimizwa malengo hayo. Kwanza ni kulea wanafunzi na taathira ya wahadhiri kwa wanafunzi hao, na pili ni taathira yao katika mazingira ya nje ya vyuo vikuu. Ameashiria pia mabadiliko yanayotokea haraka haraka duniani na kusema kuwa, miongo ijayo itakuwa na changamoto nyingi. Amewataka wahadhiri na vyuo vikuu kulea na kutayarisha vijana watakaokuwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto hizo.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, iwapo tutalea nguvu kazi ya vijana wenye kushikamana na dini, wanamapinduzi, wenye ujuzi na azma wataweza kuvunja mzingiro wa kihistoria wa kuwa tegemezi na kuiweka Iran katika nafasi yake halisi.

Ametahadharisha kwamba, kinyume chake, nchi itarejea katika kipindi cha giza, kudhalilishwa kwa muda mrefu na kuwa tegemezi kama kile cha kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu.

Ayatullah Khamenei amesema kuwa, utegemezi katika fikra na matendo ni jambo hasi na baya sana na kuongeza kuwa: Kijana wa sasa anapaswa kuwa mjuzi, hodari, mchapakazi anayejiamini na mwenye moyo wa mapambano, na mbali na kujifaharisha kwa utambulisho wake wa kitaifa, aelewe kwamba, maslahi halisi ya taifa ni yale yasiyopingana au kutofautiana na utambulisho wa kitaifa.

Amesema kuzaliwa na kulelewa vijana wa leo katika Iran isiyokuwa tegemezi kwa madola ya kibeberu kunawafanya wasielewe umuhimu na thamani ya kijitawala na amewataka wahadhiri wa vyuo vikuu kutayarisha vijana wanaotambua thamani ya kujitawala na kutokuwa tegemezi.

Baada ya kueleza umuhimu wa mchango wa wahadhiri wa vyuo vikuu katika kulea vijana, amebainisha medani nyingine ya harakati za walimu wa vyuo vikuu yaani taathira yao nje ya vyuo hivyo.

Ameashiria matamshi yaliyotolewa na wahadhiri kadhaa katika mkutano huo na kusema: Kuna umuhimu kwa fikra na mitazamo kama hii kufikishwa kwenye vituo vya kuchukua maamuzi na kuwa na taathira katika uchukuaji wa maamuzi sahihi. 

Ayatullah Khamenei amesema kuwa, kutambua na kutafuta ufumbuzi wa shughuli na jitihada ambazo hazikuweza kuzaa matunda katika upeo wa kitaifa ni miongoni mwa mambo yanayopaswa kushughulikiwa na wahadhiri wa vyuo vikuu. Ametaja mifano kadhaa katika uwanja huo na kusisitiza kuwa, fikra ya uchumi ngangari inaungwa mkono na wote na kumeundwa kamisheni na kamati kwa ajili ya suala hilo, lakini hakuna kilichotendeka katika uwanja huo, suala ambalo ni ishara kwamba kuna tatizo la kielimu; kazi ya kutambua na kutatua tatizo hilo ni jukumu la wahadhiri wa vyuo vikuu.

Miongoni mwa mambo ambayo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewataka wahadhiri wa vyuo vikuu kuyashugulikia ni lile la kutozaa matunda juhudi za kutayarisha nafasi za ajira katika serikali ya sasa na ya kabla yake, kutokuwepo maendeleo ya kutosha katika utekelezaji wa kufungu nambari 44 cha katiba, uchunguzi juu ya sababu za kutotumiwa rasilimali kubwa za nchi katika uzalishaji na maendeleo, matatizo ya mfumo wa benki na juhudi zisizoridhisha za kuimarisha uadilifu wa kijamii.

Vilevile Ayatullah Khamenei amewataka wahadhiri wa vyuo vikuu kusaidia usimamizi wa masuala ya nchi na kusema: Kupatwa na virusi vya maadui kwa sekta ya usimamizi wa masuala ya taifa ni miongoni mwa masuala yanayoweza kuvuruga kazi zote na ili kuweza kuzua tatizo kama hilo kuna ulazima wa kutumia uwezo wa wadau wa vyuo vikuu.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amewataka wahadhiri wa vyuo vikuu kuweka wazi mambo mbalimbali. Amemshukuu mmoja kati ya waliozungumza katika kikao hicho kuhusu taathira za waraka wa mwaka 2030 na kusema: Suala hilo lina umuhimu mkubwa, na ni hatari sana kuona baadhi ya watu wanaketi katika vikao vya taasisi mbalimbali za Umoja wa Mataifa ikiwemo UNESCO na kufanya mikakati ya kubuni mfumo wa kifikra, kielimu, kiutamaduni na kivitendo kwa ajili ya mataifa yote ili walimwengu wote wafikirie na kutenda kama watakavyo wao.

Ayatullah Khamenei amesema kuwa: Waraka wa 2030 ni miongoni mwa nyaraka kuu za Umoja wa Mataifa yaani waraka wa maendeleo endelevu ambao unatumiwa na mabeberu wa dunia katika harakati yao iliyojaa makosa, kwa ajili ya kuyadhibiti mataifa mbalimbali. Amehoji kwamba, wana haki gani ya kuchukua maamuzi kuhusu itikadi, mila na tamaduni za mataifa mengine? Amesisitiza kuwa: Haya ni masuala ambayo wahadhiri wa vyuo vikuu hapa nchini wanapaswa kuyaeleza na kuyatolea ufafanuzi katika jamii.

Amewakosoa wale wanaosema kuwa waraka huo hauilazimisha nchi kufanya lolote akisisitiza kuwa, huo ni mtazamo wa kijuujuu kwa sababu vipengee vyote vya waraka huo  ni lazima kutekelezwa la sivyo kutotekezwa kwake kutakabiliwa na radimali ya nchi hizo.

Ayatullah Khamenei amekamilisha sehemu hii ya hotuba yake kwa kuhoji kuwa, kimsingi kuna ulazima gani wa kukubali waraka huu na kuwakubali Wamagharibi kuwa ruwaza na kigezo chetu cha kufuata katika matendo?

Amesema ni miaka kadhaa sasa ambapo tumekuwa tukijadili suala la kigezo cha maendeleo cha Kiislamu nchini Iran, sasa kigezo hicho kinapaswa kutayarishwa kimaandishi kwa juhudi za wahadhiri wa vyuo vikuu na kufunga kabisa njia ya kuwafanya Wamagharibi kuwa kigezo cha kuigwa hapa nchini.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbusha taathira za kusimama kidete taifa na utawala wa Kiislamu hapa nchini katika kupeleka mbele malengo ya Uislamu na Mapinduzi na kusisitiza kuwa Taifa la Iran litadumisha njia hiyo iliyojaa fahari na hatimaye litapata ushindi kwa baraka zake Mwenyezi Mungu.

Ayatullah Khamenei amewausia watu wote hususan walimu na wahadhiri wa vyuo vikuu kutumia ipasavyo siku za mwishoni za mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa ajili ya kujikurubisha zaidi kwa Mola Muumba. Ameongeza kuwa: Hii leo nchi hii inakabiliana na masuala na matatizo mengi na matatizo hayo yanaweza kutatuliwa kwa hima ya wananchi na kwa kuimarisha uhusiano wetu na Mwenyezi Mungu mtukufu, kwa sababu kujikurubisha zaidi kwa Mwenyezi Mungu ndiyo sababu ya kuwa na nguvu, matumaini na kutatuliwa mishkeli na matatizo.

Mwanzoni mwa mkutano huo, wahadhiri kadhaa wa vyuo vikuu hapa nchini walihutubia hadhirina wakieleza dukuduku na mitazamo yao kuhusu masuala mbalimbali yanayohusiana na masuala ya elimu, vyuo vikuu, uchumi na kadhalika.   

700 /