Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Ayatullah Khamenei:

Idara ya Mahakama inabeba bendera ya kutetea haki na uhuru

Ayatullah Khamenei amesisitiza umuhimu wa kuwepo mtazamo wa kimabadiliko na kijihadi katika kupanga ratiba na kuchukua hatua ndani ya Idara ya Mahakama. Ameashiria nafasi ya juu ya kisheria ya chombo hicho na taathira zake kubwa katika mihimili mingine miwili ya dola katika masuala ya umma na kusema: Katiba inasema waziwazi kwamba, ni jukumu la Idara ya Mahakama kusimamia utekelezaji mzuri wa sheria na masuala ya nchi, na Mahakama ya Masuala ya Kidara na Taasisi ya Ukaguzi Mkuu wa Taifa ambazo ni mbawa mbili za Idara ya Mahakama, ndizo zinazosimamia masuala hayo mawili.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, Idara ya Mahakama inapasa kutumia uwezo wake na kuongeza kuwa, kuhuisha haki za umma na kulinda uhuru halali wa wananchi ni katika nyadhifa muhimu za chombo hicho. Amesema kuwa, idara hiyo inapaswa kubeba bendera ya kutetea mambo hayo na kukabiliana na wapinzani wote wa haki za umma katika nafasi yoyote wanapokuwa.
Ametaja masuala kama ya uchaguzi, kimbunga cha mchanga na msaada wa nafasi za masomo unaotolewa na serikali kuwa ni mfano wa nyanja ambako Idara ya Mahakama inapasa kutetea haki za umma na kusema: Maudhui ya msaada wa nafasi za masomo haikufuatiliwa ipasavyo na kazi iliyopaswa kufanyika haikufanyika.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwepo Mkuu wa Idara ya Mahakama katika taasisi kama Baraza Kuu la Usalama wa Taifa, Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni na Baraza Kuu la Masuala ya Mtandao wa Intaneti ni miongoni mwa mambo yanayoipa nguvu zaidi za kisheria Idara ya Mahakama. Ameongeza kuwa: Kutokana na shakhsia yake kubwa na uwezo wake wa kielimu, Ayatullah Amoli Larijani anaweza kuwa na taathira kubwa katika taasisi hizo.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa, ni suala lenye umuhimu mkubwa kufuatilia kisheria masuala ya kimataifa na kusisitiza kuwa: Idara ya Mahakama ya Iran inapaswa kuingia kisheria katika masuala kama ya vikwazo, hatua ya Wamarekani ya kutwaa mali za Iran, ugaidi, kuwatetea watu wanaodhulumiwa duniani kama Sheikh Ibrahim Zakzaky au kuwatetea Waislamu wa Myanmar na Kashmir na kutangaza uungaji mkono au upinzani wake ili uakisiwe kote duniani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, sharti la maendeleo katika kazi za Idara ya Mahakama na kutambuliwa na wananchi kuwa ni chombo cha uokozi, kinachotia matumaini na kuwapa utulivu ni kukabiliana ipasavyo na wahalifu. Amepongeza kazi ya kutuma wakaguzi wa siri katika miji mbalimbali kwa shabaha ya kuchunguza na kukabiliana na uhalifu na akasema: Zidisheni ukaguzi kadiri mnavyoweza na fanyeni mageuzi katika Idara ya Mahakama.
Ayatullah Khamenei ametilia mkazo udharura wa kukabiliana na kuwaadhibu wahalifu na wakati huo huo kulinda heshima na hadhi ya jamaa na familia zao na kusema: Hata hivyo pale hadhi na heshima ya utawala wa Kiislamu hapa nchini inapokuwa hatarini, basi hapana budi kutangulizwa mbele na kuipa umuhimu zaidi heshima ya Mfumo wa Kiislamu, kwa sababu wananchi wanaona na wanaelewa, na lazima kuwa makini isije ikaonekana kuwa, Idara ya Mahakama haikabiliani na wahalifu ndani ya chombo hicho.
Amesisitiza kuwa, kuwapongeza majaji waadilifu na wanaochapa kazi ipasavyo kunakamilisha kazi ya kuwaadhibu na kukabiliana na wahalifu, na amewaambia maafisa wa Idara ya Mahakama kwamba: Majaji waadilifu, shujaa, madhubuti, wenye insafu na wachapakazi, wanaomcha sana Mwenyezi Mungu, wajuzi na wanaohukumu kwa haki bila ya kujali lolote, watangazwe na kuarifishwa kwa jamii.
Suala jingine lililozungumziwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni haki za wanaoamrisha mema na kukataza maovu. Amesema kuwa, baadhi ya watu wamekuwa wakisema mara kwa mara kwamba, baadhi ya vipengee vya Katiba ya nchi havitekelezwi; hata hivyo inaonekana kuwa watu hawa hawakitambui kifungu nambari 8 cha Katiba kinachohusiana na suala la kuamrisha mema na kukataza maovu kuwa ni sehemu ya Katiba na wala hawatilii maanani suala hilo la wajibu. 
Ameashiria himaya na uungaji mkono wake ya kimatamshi na kivitendo kwa watu wanoamrisha mema na kukataza maovu na kusisitiza kuwa, suala hilo pia ni wadhifa na jukumu la Idara ya Mahakama.
Vilevile Ayatullah Ali Khamenei ametilia mkazo suala la kutoa mafunzo kwa umma na kutumia mbinu za kuvutia katika kuwafunza wananchi haki zao. 
Amesema ni jambo la dharura kuchunga na kuwa makini kuhusu neema za Mwenyezi Mungu na kuongeza kuwa: Neema ya vijana, neema ya Jamhuri ya Kiislamu, neema ya Idara ya Mahakama na uwezo wake mkubwa, neema ya wananchi kuunga mkono, kupenda na kuutii Mfumo na Mapinduzi ya Kiislamu ni miongoni mwa neema kubwa za Mwenyezi Mungu na kwamba, wananchi wote wanapaswa kuwa makini ili neema hizo zisije zikapuuzwa na wazitumie vizuri kadiri inavyowezekana. 
Mwanzoni mwa mkutano huo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesifu shakhsia ya Shahidi Ayatullah Muhammad Beheshti akimtaja kuwa alikuwa mhandisi wa Idara ya Mahakama ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Amesema: Jina la Shahidi Beheshti limefungamana na idara hiyo, kwa sababu shakhsia huyo aliingia katika chombo hicho kwa nia yenye ikhlasi na fikra za kistratijia akiwa na fikra ya kuanzisha msingi mpya wa Idara ya Mahakama katika Jamhuri ya Kiislamu, na akatoa huduma kubwa katika kipindi kifupi kwa kutumia ujuzi na mtazamo wa magezi.
Ayatullah Khamenei ameashiria suala la kuwepo shakhsia wakubwa katika uongozi wa Idara ya Mahakama katika kipindi chote cha baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kumtaja mkuu wa sasa wa chombo hicho, Ayatullah Amoli Larijani kuwa ni shakhsia mkubwa mwenye uwezo na sifa nzuri za kielimu, kimatendo, kiroho na kifikra. Amesifu huduma kubwa zinazotolewa na shakhsia huyo na maafisa wengine wa Idara ya Mahakama na kusema: Katika miaka ya hivi karibuni kumefanyika kazi muhimu na zenye thamani kubwa katika idara hiyo na kwamba kazi hizo zinapaswa kutangazwa kwa umma kwa kutumia mbinu za kisasa. 
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, mkuu wa Idara ya Mahakama ametoa ripoti kuhusu huduma na kazi zilizofanywa na chombo hicho. Ayatullah Amoli Larijani ameashiria maagizo ya Kiongozi Muadhamu kwa maafisa wa idara hiyo mwaka uliopita na kusema: Miongoni mwa kazi zilizofanywa na chombo hicho katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita ni pamoja na kupambana na maovu na uhalifu ndani ya Idara ya Mahakama na usimamizi mkubwa wa kazi za majaji, kuwasilisha ratiba na mpango wa nne wa ustawi wa mahakama, kutangazwa hati ya marekebisho yanayohusiana na wafungwa na kupunguza asilimia 5 ya mahabusu, kutayarisha wataalamu, kutangaza kazi na shughuli za chombo hicho, kutoa mafunzo ya kisheri na kuhusu haki za wananchi kwa umma, kueleza mafanikio ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nyanja za haki za binadamu na kufanya juhudi za kuhuisha haki za binadamu za Kiislamu.             
  

700 /