Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Msiwaamini Wamarekani, wanawinda fursa ya kutoa dharuba

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei alasiri ya leo amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Iraq aliyemtembelea ofisi kwake hapa mjini Tehran. Amepongeza umoja na mshikamano wa makundi yote ya kisiasa na kidini ya Iraq katika kupambana na kundi la Daesh (ISIS) na kuyataja makundi ya kujitolea ya wananchi kuwa ni jambo muhimu na lililobarikiwa na sababu ya nguvu ya Iraq. Ametilia mkazo suala la umoja wa ardhi yote ya Iraq na kusema kuwa: Kuna ulazima wa kuwa macho na makini mbele ya Wamarekani na kutowaamini kamwe, kwa sababu Marekani na vibaraka wake wanapinga suala la kujitawala, utambulisho na umoja wa Iraq.
Ameashiria jinsi kundi la kigaidi la Daesh, wakati mmoja, lilipokaribia mji wa Baghdad na kusema: Sasa Daesh wanakimbia na kuondoka nchini Iraq na mafanikio haya ya kusifiwa ni matokeo ya umoja na mshikamano wa ndani ya Iraq, na vilevile siasa sahihi za serikali ya Iraq za kuwategemea vijana wenye imani na mahudhurio yao katika medani za vita. 
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia pia upinzani wa Marekani na vibaraka wake dhidi ya al Hasdu Shaabi yaani makundi ya kujitolea ya wananchi (yanayopambana na Daesh) na kusema: Sababu ya upinzani wa Wamarekani dhidi ya makundi hayo ni kutaka kuona Iraq ikipoteza moja kati ya nguzo muhimu za nguvu zake.
Ayatullah Ali Khamenei amesema kumwambia Waziri Mkuu wa Iraq kwamba: Msiwaamini Wamarekani kwa namna yoyote, kwa sababu wanasubiri fursa kwa ajili ya kutoa pigo. 
Amesema hitilafu na migawanyiko nchini Iraq itaipa Marekani fursa ya kutoa dharuba na pigo kwa taifa la Iraq na kuongeza kuwa: Wamerekani wasipewe fursa hiyo, na vilevile kuna ulazima wa kuzuia askari wa Marekani kuingia Iraq kwa kisingizio cha kutoa mafunzo na masuala mengine.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kile kinachodaiwa kuwa ni upinzani wa Marekani dhidi ya Daesh (ISIS) si kweli na kuongeza kuwa: Wamarekani na vibaraka wao katika Mashariki ya Kati hawataki kuliangamiza kundi la Daesh kwa sababu kundi hilo lilianzishwa kwa uungaji mkono na fedha zao na wanataka kuwepo Daesh wanayoweza kuidhibiti nchini Iraq.
Ayatullah Ali Khamenei amepongeza hatua ya jeshi la Iraq ya kufika katika mpaka wa nchi hiyo na Syria na kusema, hiyo ni harakati ya kistratijia na kubwa. Ametilia mkazo udharura wa kulindwa harakati hiyo.
Amesisitiza ulazima wa kulindwa umoja wa ardhi yote ya Iraq na kusema: Jamhuri ya Kiislamu ikiwa nchi jirani, inapinga mikakati ya kutaka kuitisha kura ya maoni ya kujitenga eneo moja la Iraq na inawatambua watu wanaofanya mikakati hiyo kuwa wanapinga kujitawala na utambulisho wa Iraq.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria utajiri wa kimaada, kibinadamu na kihistoria wa Iraq na kusisitiza kuwa, Iraq yenye ustaarabu wa kihistoria, kiutamaduni na kibinadamu kama huo inapaswa kuendelea kuwa moja, na ni haki ya nchi kama hiyo kusimama kidete na kupambana kwa nguvu zote na wale wanaotaka kukabiliana nayo.
Ayatullah Khamenei amesema, anatarajia kwamba serikali ya Iraq itafanikiwa kushinda vizuizi vyote na amelitakia taifa la Iraq mustakbali mwema na bora zaidi. Amesema kuwa, serikali ya Iraq inapaswa kuimarishwa katika pande zote na kwamba ni wajibu wa makundi na mirengo yote ya kisiasa na kidini nchini humo kuisaidia serikali.
Kuhusu uhusiano wa pande mbili za Iran na Iraq, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza udharura wa kupanuliwa zaidi uhusiano huo katika nyanja mbalimbali na kusema: Kuna ulazima wa kuvuka baadhi ya matatizo ya kiidara yaliyopo katika njia ya kustawisha zaidi uhusiano, na kiwango cha ushirikiano kinapaswa kustawishwa zaidi kadiri inavyowezekana.
Katika mkutano huo ambao pia umehudhuriwa na Makamu wa Rais Bwana Is’haq Jahangiri, Waziri Mkuu wa Iraq, Haidar al Abadi ameishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa misaada yake katika mapambano dhidi ya magaidi wa Daesh na kusema kuwa, lengo la safari yake nchini Iran ni kufanya mazungumzo juu ya njia za kustawisha zaidi uhusiano wa pande mbili katika nyanja mbalimbali. Ameongeza kuwa, hii leo Iraq imeungana kwa ajili ya kupambana na Daesh na kwamba, makundi na mirengo yote ya kisiasa na kidini inaafikiana kuhusu ulazima wa kupambana na Daesh hadi mizizi ya kundi hilo itakapong’olewa kikamilifu. 
Amesema ni jambo linalowezekana kuangamizwa kabisa kundi la Daesh na ametoa wito wa kudumishwa misaada ya Iran. Waziri Mkuu wa Iraq amesisitiza kuwa, nchi hiyo inahitaji misaada ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kipindi hiki cha kupambana na Daesh na kipindi cha baada ya Daesh ambacho ni kipindi cha utulivu na ujenzi mpya wa nchi.
Waziri Mkuu wa Iraq ameashiria pia misingi ya kihistoria, kiutamaduni na kijamii ya uhusiano wa mataifa mawili ya Iran na Iraq na kusema: Baghdad inataka kupanua zaidi uhusiano wake na Tehran katika nyanja zote ikiwa ni pamoja na kuzidisha huduma kwa Wairani wanaokwenda kuzuru maeneo matakatifu nchini Iraq. Amesema taifa la Iraq linaona fahari kuwahudumia Wairani wanaokwenda kufanya ziara nchini humo.    

700 /