Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu akihutubia maafisa wa Hija:

Usalama, izza na huduma bora kwa mahujaji vinapaswa kudhaminiwa

Kongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kislamu Ayatullah Ali Khamenei mapema leo amehutubia hadhara ya maafisa wa msafara wa Hija wa Iran waliokwenda kuonana naye na kusema kuwa, ibada ya Hija ni chombo kisichokuwa na kifani cha kiroho na kijamii na eneo bora zaidi kwa ajili ya kueleza itikadi na misimamo ya Umma wa Kiislamu. Amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kamwe haitasahau maafa ya Hija ya mwaka 1394 Hijria Shamsia (mwaka 2015) na kuongeza kuwa: Takwa la siku zote la Jamhuri ya Kiislamu ni kulindwa usalama, heshima na huduma bora kwa mahujaji wote wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu hususan mahujaji wa Iran na usalama wa ibada ya Hija unapaswa kudhaminiwa na nchi inayosimamia Haram mbili tukufu (Makka na Madina).
Ayatullah Khamenei amesema kuwa ibada ya Hija ni faradhi muhimu sana. Ameashiria uwezo mkubwa wa ibada ya Hija kiroho na kimaanawi na kusema kuwa: Vipengee vyote vya faradhi hiyo ikiwemo Swala, twawafu (kuzunguka al Kaaba), Sa'yi (kutembea baina ya Swafa na Marwah), kusimama Arafa na kuhirimu ni nyenzo muhimu na adhimu kwa ajili ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu Muweza na fursa hiyo inapaswa kuthaminiwa.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, sifa nyingine kubwa ya ibada ya Hija ni uwezo wake usio na kifani wa masuala ya kijamii. Amesisitiza kuwa, ibada ya Hija ni dhihirisho la adhama, umoja na mshikamano, na nguvu ya Umma wa Kiislamu linaloonekana kila mwaka bila ya kusita na katika eneo moja maalumu kupitia amali na mazingira makhsusi.
Amekutaja kujuana na kutambuana mahujaji wa mataifa mbalimbali, kukurubisha pamoja nyoyo zao na kupeana mkono wa auni na msaada kuwa ni miongoni mwa sura za kijamii za ibada ya Hija. Amesema kuwa, Hija yenye sifa hizi zote za kiroho na kijamii ndiyo wakati na zama bora zaidi kwa ajili ya kutangaza misimamo ya Umma wa Kiislamu kuhusu masuala muhimu ya ulimwengu wa Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, maudhui ya kujibari na kutangaza msimamo wa kujitenga na washirikina ambayo daima ilikuwa ikitiliwa mkazo sana na hayati Imam Khomeini ni fursa kwa ajili ya kutangaza misimamo kuhusu masuala yanayokubaliwa na Umma wa Kiislamu. Ameongeza kuwa, Moja ya maudhui hizo ni kadhia ya Msikiti wa Al-Aqsa na Quds ambayo katika siku hizi inazungumziwa na kupewa uzito zaidi kutokana na jeuri, utovu wa haya na ukhabithi wa utawala ghasibu na bandia wa Kizayuni. Amesisitiza kuwa moyo wa Umma wa Kiislamu unakwenda mbio kwa kukumbuka Msikiti wa al Aqsa.
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, haifai kwa namna yoyote ile kughafilika na suala la Palestina ambalo ni mhimili mkuu wa masuala ya Ulimwengu wa Kiislamu na akaongezea kwa kusema: Kuna mahali gani bora zaidi kuliko Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu, Makka, Madina, Arafat, Mash'ar na Mina kwa mataifa ya Waislamu kudhihirisha mitazamo yao na kubainisha misimamo yao kuhusu Palestina na Msikiti wa Al-Aqsa?
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, uwepo wenye malengo maovu wa Marekani katika nchi za Kiislamu na eneo la Mashariki ya Kati kwa ujumla na kuanzisha makundi ya kigaidi na kitakfiri, ni maudhui nyingine muhimu ambayo mataifa ya Waislamu yanapaswa kutangaza msimamo wao juu yake katika Hija. Ameongeza kuwa: Utawala wenyewe wa Marekani ni shari kubwa zaidi na khabithi zaidi kuliko hata makundi ya kigaidi uliyoyaanzisha.
Ayatullah Ali Khamenei ameendeleza hotuba yake kwa kuashiria uamuzi uliochukuliwa na viongozi wa nchi kwa ajili kutuma mahujaji katika ardhi tukufu za Makka na Madina na kusema: Kulikuwepo wasiwasi kuhusu suala hilo lakini viongozi wa nchi na Baraza Kuu la Usalama wa Taifa wamedurusu na kuchunguza maudhui hiyo na kuchukua uamuzi kwamba, mahujaji wanapaswa kutumwa kwenye ibada ya Hija.
Amesema, masaibu yaliyoziumiza nyoyo za Wairani kutokana na matukio machungu ya Hija ya mwaka 2015 hayawezi kusahaulika, kwa msingi huo usalama wa mahujaji ni suala lenye umuhimu mkubwa na unapaswa kulindwa ipasavyo.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah Ali Khamenei ameeleza kuwa maudhui ya umoja ni jambo jingine muhimu zaidi na la dharura kwa mataifa ya Waislamu. Amesema: Wakati mabilioni ya dola zinatumika kuzusha mifarakano, hitilafu na uadui baina ya Waislamu, Waislamu wenyewe wanapaswa kujiepusha na mambo yanayosaidia kuzushaji hitilafu, kwa sababu taifa lolote la Waislamu linalosaidia njama hiyo litakuwa mshirika katika athari zake mbaya.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewaasa mahujaji wa Iran kutekeleza ibada ya Swala katika wakati wake wa awali na kushiriki katika Swala za jamaa katika Masjidul Haram na Masjidu Nabii, kusoma Qur’ani ndani ya misikiti hiyo miwili, kuzipa umuhimu makhsusi amali za Siku ya Arafa na kujiepusha na tabia ya kuzurura masokoni. Ameongeza kuwa, mahujaji waheshimiwa wanapaswa kufikiria zaidi suala la kutakasa nafsi na yoyo zao na kufaidika na matukufu ya ibada adhimu ya Hija; kwa sababu faida za kiroho za Hija ni utangulizi wa kupata matunda yake ya kijamii. 
Mwishoni mwa hotuba hiyo Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, mahujaji wote wanapaswa kuwa macho na kutekeleza majukumu yao kwa umakini ili ibada hiyo ya Hija ifanyike kwa ufanisi. 
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Mwakilishi wa Faqihi Mtawala na kiongozi wa msafara wa Iran katika ibada ya Hija, Hujjatul Islamu Qazi Askar amezungumzia tukio chungu la kufa shahidi mahujaji wa Kiirani katika ibada ya Hija ya mwaka 2015 na kusema kuwa: “Japokuwa hadi sasa hakujatolewa ripoti ya mwisho kuhusu tukio hilo na dia na fidia bado haijatolewa kwa ndugu na jamaa wa mahujaji walioaga dunia katika tukio hilo, lakini tutatendelea kufuatilia maudhui hii hadi kutakapopatikana natija ya mwisho”.
Bwana Qazi Askar amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kamwe haitaki kusimamisha ibada ya Hija na kuongeza kuwa: Baada ya duru kadhaa za mazungumzo ya mwaka huu na kukubaliwa masharti ya Jamhuri ya Kiislamu, kumeandaliwa uwanja wa kufanyika Hija itakayoambatana na heshima na izza. Amesema kwamba, kama mwaka jana wangekubali masharti ya Jamhuri ya Kiislamu hapana shaka kwamba, wahujaji wa Iran wangekwenda Hija. 
Vilevile Mkuu wa Jumuiya ya Hija ya Ziara ya Iran Bwana Muhammadi ametoa ripoti kuhusu shughuli zilizofanywa na jumuiya hiyo na kusema: Baada ya mwaliko wa Wizara ya Hija ya Saudi Arabia na uamuzi wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa na vilevile sisitizo la viongozi wakuu wa dini, kulifanyika mazungumzo kuhusu ibada ya Hija mbayo yalijikita zaidi katika matakwa ya Jamhuri ya Kiislamu hususan suala la kudhaminiwa usalama, heshima na utukufu wa mahujaji, na vilevile suala la haki za mashahidi waliouliwa Mina mwaka 2015. Ameongeza kuwa, baada ya kupewa dhamana ya kutimizwa matakwa ya Iran, Baraza Kuu la Usalama wa Taifa liliafiki suala la kutuma mahujaji huko Saudi Arabia kwa ajili ya ibada ya Hija. 
Bwana Muhammadi amesema kuwa, juhudi kubwa zimefanyika kwa ajili ya kuandaa Hija yenye ufanisi na kwamba katika uwanja huo kiwango cha huduma na suhula zilizotayarishwa kwa ajili ya mahujaji mwaka huu ni cha juu na bora zaidi kuliko miaka iliyopita.
 

700 /