Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Ujumbe wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa mahujaji:

Kulinda Palestina na kuikomboa ni wajibu halisi wa Kiislamu

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei leo ametoa ujumbe kwa mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu ambapo ameashiria siasa za mfumo wa kibeberu za kuzusha mifarakano kati ya Waislamu na kusema kuwa, ni wajibu wa viongozi wa nchi za Kiislamu, wasomi na wanafikra katika ulimwengu wa Kiislamu kuimarisha umoja, kuyazindua mataifa mbalimbali na kusitisha mara moja maafa machungu katika nchi za Waislamu. Amesema: Kutetea Palestina na kuwa bega kwa bega na taifa ambalo linapambana kwa kipindi cha karibu miaka 70 sasa kwa ajili ya kukomboa nchi yake iliyoghusubiwa ndiyo wajibu mkubwa zaidi kwetu sote. 
Ujumbe kamili wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambao umesomwa hivi punde na mwakilishi wa Faqihi Mtawala, Hujjatul Islam Walmuslimin Qazi Askar kwa mahujaji katika jangwa la Arafat ni huu ufuatao:
Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehma, Mwenye kurehemu.
Hamdu zote ni za Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu. Na Swala na salamu zimshukie Bwana wetu Muhammad, Mtume wa Mwisho, Aal zake watoharifu na Masahaba zake wema.
Ninamshukuru Mwenyezi Mungu Mkubwa ambaye mwaka huu pia amewapa waumini kutoka maeneo mbalimbali ya dunia, saada na ufanisi wa kutekeleza ibada ya Hija ili wafaidike na chemchemi hiyo yenye maji matamu na yanayotiririka, na kufanya itikafu na kuwa kandokando ya Nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu katika nyakati za ibada, khushui, dhikri na kujikurubisha kwake katika siku na nyusiku zinazohesabika kuwa ni fursa adhimu na yenye baraka ambazo saa zake ni mithili ya mada inayofanya muujiza unaoweza kubadilisha nyoyo na kutakasa na kuzipamba nafsi na roho zao.
Hija ni ibada yenye siri nyingi, na nyumba tukufu (ya al Kaaba) ni eneo lenye baraka tele za Mwenyezi Mungu na ni dhihirisho la aya na ishara zake za wazi. Ibada ya Hija inaweza kumfikisha mja mwenye imani, khushui, unyenyekevu na mazingatio katika nafasi za juu za kiroho na kumfanya kuwa mwandamu aali na mwenye nuru. Vilevile inaweza kumfanya mtu mwenye kuona mbali, shujaa, jasiri na mwanajihadi. Pande zote mbili za masuala ya kiroho na kisiasa, kibinafsi na kijamii zinaonekana waziwazi katika faradhi na ibada hii isiyo na kifani, na jamii ya Waislamu hii leo inahitajia pande hizo zote mbili. 
Katika upande mmoja uchawi wa fikra za kimaada unaotumia zana za kisasa unafanya kazi ya hadaa na upotoshaji. Na katika upande mwingine siasa za kambi ya ubeberu zinaeneza fitina na moto wa vita baina ya Waislamu na kuzifanya nchi za Waislamu kuwa Jahannam ya ukosefu wa amani na hitilafu nyingi. Hija inaweza kuwa dawa ya kuponya mabalaa hayo mawili makubwa ya Umma wa Kiislamu, kwa kusafisha na kuondoa kutu katika nyoyo na kuzipamba kwa nuru ya taqwa na maarifa, na vilevile kufungua macho mbele ya machungu ya Ulimwengu wa Kiislamu, kuimarisha azma ya kukabiliana na machungu hayo, kuthabitisha hatua na kutayarisha mikono na akili kwa ajili ya harakati na kuchukua hatua. 
Hii leo Ulimwengu wa Kiislamu umekumbwa na hali ya ukosefu wa amani; ukosefu wa amani ya kimaadili na kimaanawi na ukosefu wa amani ya kisiasa. Sababu kubwa zaidi ya hali hiyo ni kughafilika kwetu na hujuma ya kikatili ya maadui. Hatukutekeleza wajibu wetu wa kidini na kiakili mbele ya hujuma ya adui muovu. Tumesahau اَشِّدآءُ عَلَی الکُفّار kwa maana kwamba, Waumini ni imara mbele ya makafiri, na vilevile tumetupilia mbali «رُحَمآءُ بَینَهُم» kwa maana kwamba, ni wenye kurehemeana na kuoneana huruma baina yao. Matokeo yake ni kwamba, adui Mzayuni anafanya kazi ya kueneza fitina katika kitovu cha jiografia ya Ulimwengu wa Kiislamu huku sisi tukighafilika na wajibu wetu halisi wa kuikomboa Palestina na tunashughulishwa na vita vya ndani huko Syria, Iraq, Yemen, Libya na Bahrain na kupambana na ugaidi huko Afghanistan , Pakistan na kadhalika. 
Marais wa nchi za Kiislamu, wasomi na shakhsia wa kisiasa, kidini na kiutamaduni katika Ulimwengu wa Kiislamu wanabeba majukumu mazito; majukumu ya kujenga umoja na kuwatahadharisha Waislamu wote kuhusu hatari za vita na mapigano ya kikaumu na kimadhehebu, wadhifa wa kuyazindua mataifa kuhusu mbinu zinazotumiwa na adui na usaliti wa mabeberu na Uzayuni, wadhifa wa kujiandaa Waislamu wote kwa ajili ya kukabiliana na adui katika medani mbalimbali za vita laini na vita vya silaha (Soft and Hard War), wajibu wa kusitisha mara moja maafa yanayotokea kati ya nchi za Kiislamu ambayo hii leo mfano wake mchungu ni yale yanayotokea Yemen, yanayowasikitisha walimwengu na kuwafanya walalamike ya kuyapinga, wadhifa wa kuwatetea kwa nguvu zote Waislamu waliowachache wanaodhulimwa kama watu madhlumu wa Myanmar na kadhalika, na muhimu zaidi, wajibu wa kuitetea Palestina, kushirikiana na kuwa bega kwa bega na taifa ambalo kwa kipindi cha karibu miaka 70 sasa linapambana kwa ajili ya kukomboa nchi yake iliyoghusubiwa.
Haya ni majukumu muhimu yaliyoko kwenye mabega yetu sote. Mataifa yanapaswa kuzitaka serikali na tawala kutekeleza majukumu hayo, na wasomi na shakhsia mbalimbali wanalazimika kufanya juhudi kubwa kwa azma thabiti na nia yenye ikhlasi za kuhakikisha majukumu hayo yanatekelezwa. Kazi hizi ni kielelezo halisi cha kuinusuru dini ya Mwenyezi Mungu ambayo hapana shaka kuwa, kutaambatana na nusra na msaada wa Mwenyezi Mungu kama alivyoahidi Mola Mwenyewe. 
Hizi ni baadhi ya darsa za ibada ya Hija na ninatarajia kwamba tutazielewa na kuzifanyia kazi.
Ninawatakia nyote Hija yenye kutakabaliwa na ninawakumbuka mashahidi wa Mina na Masjidul Haram na kumuomba Mwenyezi Mungu Rahimu na Karimu awape daraja za juu peponi.
 Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh
Sayyid Ali Khamenei
7 Shahrivar 1396
7 Dhulhija 1438    
 

700 /