Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Ayatullah Khamenei:

Nchi za Kiislamu zichukue hatua dhidi ya serikali ya Myanmar

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei amekosoa kimya na kutochukua hatua jumuiya za kimataifa na wanaojigamba kuwa watetezi wa haki za binadamu kuhusiana na matukio ya maafa yanayojiri Myanmar na kusisitiza kwamba: Njia ya utatuzi wa kadhia hii ni kuchukuliwa hatua za kivitendo na nchi za Kiislamu na kuishinikiza kisiasa na kiuchumi serikali isiyo na huruma ya Myanmar.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameyasema hayo asubuhi ya leo wakati wa kuanza darsa ya fiqhi na kusisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapaswa kutangaza waziwazi na kwa ushujaa msimamo wake dhidi ya dhulma popote pale inapofanyika duniani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza pia kwamba, si sahihi kuyahafifisha maafa ya Myanmar kwa kuyataja kuwa ni mapigano ya kidini tu baina ya Waislamu na Mabudha na akaongezea kwa kusema: Inawezekana taasubi na chuki za kidini nazo pia zikawa na taathira katika kadhia hii, lakini hii ni kadhia ya kisiasa kwa sababu mtendaji wake ni serikali ya Myanmar na katika nafasi ya juu kabisa ya serikali hiyo kuna mwanamke asiye na huruma ambaye ni mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobeli; na ukweli ni kwamba matukio yanayojiri huko Myanmar ni sawa na kifo cha Tuzo ya Amani ya Nobeli.
Amesema kuwa, maafa haya yanafanywa na serikali ya kikatili ya Myanmar mbele ya macho ya nchi na serikali za Kiislamu, jumuiya za kimataifa na serikali za kiria na kidhabi zinazodai kutetea haki za binadamu.
 Ayatullah Khamenei vilevile amemkosoa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa kutosheka na kutoa tamko la kulaani tu jinai za Myanmar na akaeleza kwamba: Wanaojigamba kuwa watetezi wa haki za binadamu ambao baadhi ya wakati huzusha zogo na makelele wakati inapotokea mhalifu mmoja akahukumiwa katika nchi fulani, hawaonyeshi radiamali wala jibu lolote kwa mauaji na kufanywa wakimbizi makumi ya maelfu ya watu nchini Myanmar.
Ayatullah Khamenei ametilia mkazo ulazima wa nchi za Kiislamu kuchukua hatua za kivitendo na kusema: Tab'an madhumuni ya kuchukua hatua za kivitendo si kupeleka majeshi bali zinapaswa kuzidisha mashinikizo ya kisiasa, kiuchumi na kibiashara kwa serikali ya Myanmar na kupaza sauti zao dhidi ya jinai hizi katika jumuiya za kimataifa.
Ayatullah Khamenei amebainisha kuwa kuna udharura kwa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kuitisha mkutano wa kuzungumzia maafa ya Myanmar na kuongeza kwamba: Dunia ya leo ni dunia ya dhulma na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapaswa kudumisha sifa yake hii ya kujivunia ya kutangaza kinagaubaga na kwa ushujaa msimamo wake dhidi ya dhulma inayofanyika sehemu yoyote ile duniani, iwe ni katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni, Yemen, Bahrain au Myanmar.

 

700 /