Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Ayatullah Khamenei:

Hija ni fursa bora zaidi kwa ajili ya kuzima propaganda za maadui

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuna kambi kubwa ya kimataifa ya propaganda dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusisitiza kwamba: Fursa ya Hija ni minbari bora kabisa ya tablighi kwa ajili ya kujenga mawasiliano na walimwengu na kuzima propaganda za upande wa pili.

Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo leo katika mkutano na kiongozi wa msafara wa mahujaji wa Iran, maafisa wahusika na wasimamizi wa Hija ya mwaka huu.
Ameashiria kuwepo kambi hatari sana, amilifu na iliyojizatiti kwa anuwai za nyenzo na suhula za propaganda ya kukabiliana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kueleza kwamba: Mfumo wa Kiislamu una uwezo na nyenzo nyingi sana za kuuwezesha kusimama kidete kujihami na kuiandama kambi hiyo; na njia ya kukabiliana na kambi hiyo hatari ni utaalamishaji na kufanya tablighi amilifu na ya ushambuliaji; na Hija ni moja ya vituo vikuu na vya msingi vya kutekelezea hatua hiyo.
Ayatullah Khamenei amewashukuru maafisa wanaosimamia ibada ya Hija na kusema: "Kurejea nchini salama mahujaji huwa kama siku ya idi na sikuu kwetu sisi".
Amesema kulindwa usalama, izza na heshima ya mahujaji ni miongoni mwa mambo yanayomtia wasiwasi na akaongezea kwa kusema: Kwa mujibu wa ripoti ya wakuu husika, wameridhishwa na Hija ya mwaka huu katika masuala mengi yanayohusiana na kulindwa heshima na izza, japokuwa yameripotiwa baadhi ya matukio ya ukiukaji misingi hiyo ambayo inapasa yafuatiliwe.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria kuwa kuzifunga au kuziwekea mipaka njia za mawasiliano kati ya Iran na mahujaji wa mataifa mengine, kama dua ya Kumeili, mkusanyiko wa kujibari na washirikina pamoja na mijumuiko na makongamano ya tablighi ni mbinu inayotumiwa na serikali ya Saudi Arabia dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na akafafanua kwamba: Leo katika Ulimwengu wa Kiislamu kuna wasomi na wenye vipawa wengi ambao wana hamu ya kusikia ukweli na hakika ya mambo kupitia Jamhuri ya Kiislamu; kwa hivyo inapasa zitumike nyenzo mpya na za kisasa za tablighi na lugha athirifu, maneno mazuri na hoja madhubuti kuwafikishia wakusudiwa ujumbe wa masuala muhimu kama kupambana na Uistikbari, kufichua utambulisho halisi wa Magharibi, kujibari na maadui wa Uislamu pamoja na madhumuni na makusudio aali na ya kina yaliyomo kwenye dua ya Kumeili.
Ayatullah Khamenei ameeleza pia kwamba ni jambo la kawaida kuwepo shaka na utata katika fikra za wakusudiwa kutokana na athari za wimbi kubwa la propaganda hasi zinazofanywa dhidi ya Iran na akabainisha kuwa: wakati wa msimu wa Hija, viongozi wa Saudia walijitokeza bila aibu wala haya katika televisheni na kuzungumza dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran; na ni kawaida kwamba maneno hayo yatazusha shaka na utata kwa watu wa kawaida katika nchi nyengnezo, lakini kinachopasa kufanywa ni kuwa na mawasiliano na watu ili kuondoa shaka na utata na kuuvunja mzingiro uliowekwa na upande wa pili.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ametilia mkazo suala la kupelekwa bidhaa za matumizi ya kila siku ya mahujaji kutoka hapa nchini kadiri inavyowezekana. Kuhusu suala la kupungua tabia ya baadhi ya mahujaji kuzurura masokoni wanapokuwa katika ardhi tukufu za Makka na Madina, Ayatullah Khamenei amesema: Kama ripoti hiyo itakuwa imefanyika kwa kutegemea uchunguzi makini na wa kina basi hilo litakuwa jambo la kufurahisha.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatul-Islam Walmuslimin Sayyid Ali Qazi Askar, Mwakilishi wa Faqihi Mtawala na kiongozi wa msafara wa mahujaji wa Iran na Hamid Mohammadi, Mkuu wa Shirika la Hija na Ziara la Iran walitoa ripoti kuhusu harakati mbalimbali zilizofanywa katika Hija ya mwaka huu.
 

700 /