Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Utawala wa Kizayuni unataka kuunda Israel mpya katika eneo hili

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo usiku ameonana na Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki na ujumbe alioandamana nao hapa mjini Tehran na kusisitiza kwamba kuna ulazima wa kuzidishwa kiwango cha ushirikiano wa kiuchumi wa nchi mbili. Vilevile amesisitiza kuwa ni jambo muhimu na lenye taathira kuwepo maafikiano na ushirikiano kati ya Iran na Uturuki katika masuala muhimu ya ulimwengu wa Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia manufaa ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel katika kuitishwa kura ya maoni iliyofanywa na baadhi ya viongozi wa eneo la Kurdistan la Iraq na kuongeza kuwa: Marekani na madola ya kibeberu hayana mwamana hata kidogo na hivi sasa yanafanya njama za kuanzisha Israel mpya katika eneo hili.
Ayatullah Khamene amegusia pia matatizo mapya ya ulimwengu wa Kiislamu kuanzia mashariki mwa Asia na Mynamar hadi kaskazini mwa Afrika na kuongeza kuwa, kama Iran na Uturuki zitakuwa na kauli moja katika kukabiliana na matatizo hayo, hapana shaka kuwa makubaliano yao hayo yatafanikiwa na manufaa yake yatakuwa ni kwa nchi zote hizi mbili na kwa ulimwengu mzima wa Kiislamu.
Vilevile amesisitizia ulazima wa kuzidishwa kiwango cha ushirikiano wa kiuchumi baina ya nchi mbili na kuongeza kuwa: Inasikitisha kuona kwamba, licha ya kuweko nafasi nyingi sana, lakini kiwango cha ushirikiano wa kiuchumi katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita baina ya nchi hizo mbili hakikuongezeka hata kidogo, hivyo kuna haja ya kufanyika juhudi kubwa zaidi za kunyanyua kiwango cha ushirikiano wa nchi hizi mbili katika uwanja huo.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza kufurahishwa kwake na ushirikiano mzuri wa Iran na Uturuki katika kikao cha Astana na mwenendo unaoboreka kila uchao kuhusu kadhia ya Syria kutokana na ushirikiano huo na kuongeza kuwa: Hata hivyo masuala ya Daesh na matakfiri hayawezi kumalizika na kutatuliwa kwa njia hii, na utatuzi wake unahitaji mipango ya muda mefu na ya kweli.  
Amesema kura ya moni iliyofanyika katika eneo la Kurdistan huko Iraq ni usaliti kwa eneo hili na tishio kwa mustakbali wake. Vilevile ameashiria taathira mbaya za kipindi kirefu za hatua hiyo kwa nchi jirani na kusisitiza kuwa: Iran na Uturuki zinapaswa kuchukua hatua zote zinazowezekana kukabiliana na tukio hilo na serikali ya Iraq inapaswa kuchukua maamuzi na hatua madhubuti kuhusu kadhia hiyo.
Ayatullah Khamenei amesema ushirikiano, fikra za pamoja na maamuzi ya aina moja na muhimu ya kisiasa na kiuchumi ya Iran na Uturuki katika kukabiliana na kadhia hiyo ni jambo lenye umuhimu mkubwa. Ameongeza kuwa: Mtazamo wa Marekani na nchi za Ulaya kuhusu suala hilo unatofautiana kikamilifu na mtazamo wa Iran na Uturuki, na Marekani daima inataka kuwa na sababu ya kuzisumbua na kuziudhi Iran na Uturuki; hivyo haifai kabisa kuwaamini Wamarekani na watu wa Ulaya na misimamo yao kwa hali yoyote ile. 
Ayatullah Khamenei amemwambia Rais wa Uturuki kwamba: "Kama ulivyoashiria wewe, utawala wa Kizayuni wa Israel katika daraja ya kwanza na baadaye Wamarekani ndio wanaofaidika na matukio ya sasa".
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria njama zinazofanywa na maadui kwa ajili ya kuzishughulisha Iran na uturuki na kuziweka mbali na masuala muhimu ya eneo la Mashariki ya Kati na kusema kuwa: Madola a kibeberu hususan utawala wa Kizayuni yanataka kuanzisha "Israel mpya" katika eneo hili na kubuni wenzo wa kuzusha hitilafu na mivutano.
Amesisitiza kuwa, kuna udharura wa kuchukua maamuzi madhubuti na ya haraka kwa kutumia mtazamo wa muda mrefu na wa kistratijia kwa masuala ya sasa, na kukabiliana na suala hilo kwa hatua za pamoja. 
Kwa upande wake, Rais Recep Tayyid Erdogan wa Uturuki amesisitiza katika mazungumzo hayo ambayo pia yamehudhuriwa na Rais Hassan Rouhani kuhusu udharura wa kuanzishwa umoja wenye nguvu na madhubuti baina ya Iran na Uturuki katika eneo hili na kusema kuwa, katika mazungumzo yake na Rais wa Jamhuri ya Kiislamu pande hizo mbili zimefikia mtazamo wa pamoja kuhusu Syria na Iraq.
Rais wa Uturuki ameashiria ulazima wa kuchukuliwa hatua za pamoja kati ya Iran, Uturuki na Iraq kuhusu kadhia ya Kurdistan huko Iraq na kusema kuwa: "Kuna nyaraka na ushahidi ambao hauwezi kukanushwa kwamba, Marekani na Israel zimefikia mapatano jumla kuhusu suala la kurdistan, na Masud Barzani (rais wa eneo la Kurdistan, Iraq) amefanya kosa ambalo haliwezi kusameheka kwa kuitisha kura ya maoni. 
Bwana Erdogan amesema ghairi ya Israel hakuna upande wowote mwingine uliotambua kujitenga eneo la Kurdistan na Iraq. Amesisitiza kuwa, nchi zinazopakana na Iraq kamwe haziwezi kukubaliana na jambo hilo; kwa msingi huo maafisa wa eneo la Kurdistan huko Iraq tangu sasa hawawezi kupiga hatua yoyote na hawatakuwa na njia ya kuokoka.
Rais wa Uturuki ameeleza kwamba, Marekani, Ufaransa na Israel zinataka kuzigawa nchi za Mashariki ya Kati na kufaidika na hali hiyo kwa maslahi yao. Ameongeza kuwa, pande hizo pia zimepanga njama kama hiyo dhidi ya Syria, na ni muhimu sana kwa Iran na Uturuki kuwa na umoja na maamuzi ya aina moja katika uwanja huo.
Recep Tayyep Erdogan amesisitiza udharura wa kuzidishwa ushirikiano wa kiuchumi wa nchi hizo mbili hadi kufikia kiwango cha dola bilioni 30 kwa mwaka na kusema: Kuna kazi nyingi tunazoweza kufanya kwa kushirikiana japokuwa baadhi hawatafurahishwa na kupanuka ushirikiano huo na watafanya jitihada za kukwamisha hatua hizo chanya.
 

700 /