Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Serikali izidishe misaada kwa waathiriwa wa tetemeko la ardhi

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei mapema leo ameelekea mkoani Kermanshah katika safari ya ghafla ya kukagua maeneo yaliyokumbwa na tetemeko la ardhi pamoja na kuonana na wananchi walioathiriwa na janga hilo la kimaumbile.
Mara baada ya kuwasili mkoani Kermanshah, Ayatullah Khamenei alielekea kwenye mji wa Sarpol-e-Zahab na kukagua maeneo yaliyoharibiwa na mtetemeko huo.
Baada ya kukagua maeneo hayo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alionana na wananchi wa mji huo na kuhutubia hadhara ya wananchi wenye huzuni na majonzi waliofikwa na masaibu hayo.
Ayatullah Khamenei amesema: "Nilitarajia kutembelea mji wenu nyinyi wananchi wakarimu na waaminifu katika kipindi cha furaha na ukwasi wa maisha na si katika mazingira na kipindi hiki mkiwa katika msiba, balaa na masaibu makubwa."
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza masikitiko yake makubwa na mshikamano wake na wananchi wote waliopatwa na masaibu wa mijini na vijijini na akasema: "Masaibu yenu yamezitia ghamu na masikitiko makubwa nyoyo zetu na kuzishughulisha sana fikra zetu." 
Ameashiria kujitolea na kusimama imara kwa watu wa mkoa wa Kermanshah katika kipindi cha vita vya kujitetea kutakatifu (wakati Saddam Hussein alipoivamia ardhi ya Iran) na kusema: Hii si mara ya kwanza kwa mji wenu nyinyi wananchi wenye subira na wakarimu na miji ya kandokando yake kupatwa na matatizo kama haya na katika kipindi cha vita vya kulazimishwa pia mlisimama imara, kiume na kishujaa mbele ya mashaka na matatizo yote, na hii leo pia mtafanya hivyo. 
Ayatullah Khamenei amesema, watu adhimu na mashujaa husimama kidete mbele ya matukio ya aina mbalimbali na kuyashinda, hivyo basi japokuwa mtetemeko wa ardhi ni balaa na tatizo kubwa ambalo huwatia msibani watu wote kutokana na uharibifu wake, lakini zilzala hiyo hiyo inaweza kuwa neema kutokana na kusimama ngangari kwa wananchi na juhudi zao za kuanza maisha na ujenzi mpya. 
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, inawezekana kusimama imara mbele ya matatizo na kutumia uwezo mkubwa wa taifa kwa ajili ya kukabiliana na majanga ya kimaumbile na ya kutwishwa na kuongeza kuwa, tukio hili limetia harakati katika taifa la Iran, na watu kote nchini wametekeleza wajibu wao wa kutoa misaada kadiri ya uwezo wao wakihisi kwamba, nyoyo zao ziko Kermanshah na kwamba wana deni kwa Kermanshah.
Amesema kuwa maafisa wa serikali hususan katika baadhi ya taasisi wamefanya vizuri sana katika tukio hili na tangu saa za mwanzoni tu baada ya tetemeko la ardhi, Jeshi la Taifa lilielekea katika maeneo ya mijini na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah) likaelekea katika maeneo ya vijijini kutoa msaada kwa wananchi na kuokoa waliokuwa chini ya vifusi. Hata hivyio amesisitiza kwa kusema: "Mimi binafsi sijatosheka na jitihada zilizofanywa, kwa msingi huo maafisa wa sekta mbalimbali wanapaswa kuzidisha mara dufu jitihada na juhudi zao." 
Ayatullah Khamenei ametawaka wananchi kufanya juhudi za kustawisha eneo hilo na kuliboresha zaidi na kusema: Tegemeeni zaidi nguvu, juhudi na uwezo wenu na tengenezeni maisha yenye furaha kwa kutumia ghera na ari mliyopewa na Mwenyezi Mungu. 
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu anaendelea kutembelea maeneo mengine yaliyoathiriwa na mtetemeko wa ardhi katika eneo la Sarpol-e-Zahab.
Tetemeko kubwa la ardhi lenye ukubwa wa 7.3 kwa kipimo cha Rishta lilitokea Jumapili usiku wa tarehe 12 Novemba magharibi mwa Iran. Watu 437 wamefariki dunia na wengine wapatao 10,203 wamejeruhiwa kutokana na zilzala hiyo.
     
 

700 /