Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Ayatullah Khamenei:

Taasisi zote ziharakie kuwasaidia watu waliokumbwa na maafa

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ujumbe maalumu kufuatia tetemeko la ardhi lililotokea magharibi mwa Iran na kusababisha vifo vya mamia ya watu na wengine wengi kujeruhiwa.
Ayatullah Ali Khamenei ametoa mkono wa pole kwa taifa la Iran hususan watu wa mkoa wa Kermanshah na kuvitaka vyombo vyote vya dola na jeshi kuharakia kuwasaidia watu walioathiriwa na tetemeko hilo. 
Matini kamili ya ujumbe wa Kiongozi Muadhamu ni hii ifuatayo: 
Kwa jina la Allah, Mwingi wa rehma, Mwenye kurehemu.
Nimepokea kwa masikitiko na huzuni kubwa habari ya tetemeko la ardhi lililotokea magharibi mwa nchi ambalo limesababisha vifo vya wananchi wapenzi na kujeruhiwa wengine wengi pamoja na kusababisha hasara kubwa.
Jukumu la viongozi ni kuhakikisha kuwa, kwa uwezo wao wote wanafanya hima kwa kuharakisha katika muda huu huu wa tukio kuwasaidia waathirika hususan waliokwama chini ya vifusi na kutumia kwa haraka suhula zote zilizopo ili kuepusha ongezeko la maafa.
Kwa kasi na nidhamu maalumu, vikosi vya Jeshi la Taifa, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) pamoja na jeshi la kujitolea la wananchi la Basij yasaidie kuondoa kifusi na kuhamisha majeruhi; navyo vyombo vya serikali vikiwemo vya kijeshi na vya kiraia vichukue hatua kwa uwezo wao wote kuwasaidia waathirika na familia zao.
Binafsi, ninatoa salamu za dhati za rambirambi na mkono wa pole kwa wananchi wa Iran hususan watu azizi wa mkoa wa Kermanshah na hasahasa familia zilizofikwa na msiba wa tukio hili chungu na ninamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa unyenyekevu ayafanye masaibu na machungu haya sababu ya kupata rehema na fadhila zake na kuwazidishia subira na ustahamilivu wananchi wetu wapenzi.
Vilevile nawaomba watu wote wenye uwezo waharakie kuwasaidia watu walioathiriwa na mtetemeko huu kwa kuwapunguzia masaibu na kufidia hasara zake. 
Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh
Sayyid Ali Khamenei
22 Aban 1396 (13 Novemba 2017)

700 /