Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Ayatullah Khamenei:

Maafisa wa serikali waendelee kuwasaidia waathirika wa zilzala

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza kusikitishwa sana na tukio chungu la tetemeko la ardhi lililotokea katika mkoa wa Kermanshah huko magharibi mwa Iran na kuwashukuru viongozi wa serikali waliokwenda kwenye maeneo yaliyoathiriwa na tukio hilo na kuonesha mshikamano wao na wananchi.
Ayatullah Ali Khamenei ameyasema hayo katika kikao na viongozi wa mihimili mitatu ya taifa, yaani vyombo vya Mahakama, Bunge na Serikali kuu. 
Amesisitiza mshikamano wa viongozi kwa wahanga wa tetemeko la ardhi katika ngazi ya utendaji sambamba na kuendelea kutolewa misaada kwa watu hao ili kuweza kupunguza matatizo yao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu sambamba na kubainisha kwamba Wairani wote wanashirikiana katika msiba huu na watu majasiri na walinda mpaka shupavu wa mkoa wa Kermashah, amesema: "Msiba huu na kuondokewa na watu wa karibu ni mchungu sana, lakini natarajia kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu atashusha utulivu na sakina katika mioyo ya watu wa familia zilizoondokewa na wapenzi wao na kutia nuru katika macho yao."
Amesema kutiririka damu ya mahaba na kutoa msaada katika mishipa ya jamii ya Kiislamu ni miongoni mwa athari nzuri za matukio kama haya. Ameongeza kuwa, tukio hilo la tetemeko la ardhi limewafanya watu wote kuingia katika ulingo wa kuwasaidia waathirika na kwamba anatarajia kuwa athari ya mapenzi hayo, udugu na baraka za Mwenyezi Mungu, zitashamili kati ya wakazi wote wa Kermanshah na kwa taifa lote la Iran. 
Ayatullah Ali Khamenei amelitaja tetemeko hilo la ardhi kuwa ni mtihani wa Mwenyezi Mungu na uwanja wa viongozi wa serikali kutekeleza majukumu yao. Ameongeza kuwa, katika siku hizi mbili maafisa wa serikali akiwemo mheshimiwa Rais wa Jamhuri wamekuwa pamoja na wananchi waliopatwa na masaibu na kushirikiana nao katika msiba wao na kwamba anatarajia kwamba, ushirikiano huo utadumishwa kivitendo na katika kuwasaidia wananchi. Vilevile ametoa wito wa kuharakia kupunguza mashaka ya wananchi waliopatwa na masibu hasa kwa kutilia maanani kukaribia kwa msimu wa baridi kali. 
Rais Hassan Rouhani ambaye pia amehudhuria kikao hicho amezungumzia jitihada zinazofanywa na vyombo mbalimbali vya dola kwa ajili ya kutoa misaada, kuokoa na kushughulikia hali za majeruhi na familia zao na kusema: Tukio hili ni mtihani na majaribio. Vilevile Rais Rouhani amezishukuru taasisi zote zinazofanya juhudi katika uwanja huo vikiwemo vikosi vya jeshi ambavyo amesema vimetoa mchango mkubwa.  

700 /