Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Vijana wenye imani wameipigisha magoti Marekani

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema mapema leo katika hadhara ya maelfu ya wapiganaji wa kujitolea wa jeshi la Basiji waliokwenda kuonana naye kutoka maeneo mbalimbali ya Iran kwamba Basiji ni tukio la aina yake, linalotatua mambo mengi na miongoni mwa mambo ya kijifaharisha ya hayati Imam Ruhullah Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu). Ayatullah Ali Khamenei ametilia mkazo udharura wa kupanuliwa zaidi moyo wa kibasiji kwa maana ya kuwa na ari, shauku na kufanya jitihada zaidi za kutimiza malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu na maendeleo ya Iran na kusema: Adui amezidisha uhasama wake kwa shabaha ya kuangamiza muqawama na mapambano yaliyoanzishwa na fikra ya kimapinduzi na Kiislamu katika eneo la Mashariki ya Kati, lakini vijana na waumini wenye istiqama wamewapigisha magoti maadui na kuthibitisha tena kivitendo kaulimbiu ya "Sisi Tunaweza" kwa kuliangamiza tezi la sarati na kitakfiri la Daesh.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja jeshi la kujitolea la Basiji kuwa lina maana ya kukusanya na kutumia nguvu na uwezo wa wananchi wote na nguvukazi amilifu, ya wanajihadi na wabunifu na kusema kuwa: Kama Mapinduzi ya Kiislamu yasingekuwa na Basiji basi yangekabiliwa na mapungufu makubwa. Ameongeza kuwa, Taasisi ya Muqawama ya Basiji ni nembo ya mkusanyiko wa wananchi wenye nyadhifa muhimu na nyeti sana. 
Ayatullah Khamenei ameashiria ujumbe mpya ulioletwa na Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kwa wanadamu na kusema: Ujumbe mpya wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kuwa jamii ya mwanadamu inaweza kupata maendeleo ya kimaada na ya kisayansi sambamba na kulinda radhi za Mwenyezi Mungu na thamani za mbinguni.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, kujenga jamii kama hiyo na kupata maendeleo ya kimaada sambamba na kufikia malengo aali ya kiroho kunalazimu kujiepusha na dhulma, udikteka, tofauti za kimatabaka, ufisadi wa kimatendo na kifikra na kughariki katika matamanio ya kinafsi kwa upande mmoja, na kuwa na ikhlasi, kubeba na kutekeleza majukumu, kufanya jitihada na jihadi, kuchapakazi na kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu katika upande mwingine.
Ayatullah Khamenei amesema, mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndio ulioweza kukusanya mambo hayo mawili. 
Amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa msaada na mwongozo wa Mwenyezi Mungu na kutokana na mwamko na kuwa makini kwa Imam Khomeini na jihadi ya taifa, imeweza kuhuisha Uislamu uliokuwa ukitarajiwa na Waislamu katika kalibu ya mfumo wa kisiasa na kuweka jiwe lake la msingi.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Hata hivyo mfumo huu wa kisiasa bado una safari ndefu ili kufikia malengo yake aali, lakini inawezekana kufikia malengo hayo kwa kuwa katika medani na kwa kutegemea watumishi wenye irada na azma kubwa.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria njama zinazoendelea kufanywa bila kusita na maadui na kuwakosoa wale wanaokasirika kwa kusikia neno "adui". Amesema kuwa, watu hawa wanaghafilika kwamba, kama adui atapata fursa hatasita kutoa dhuruba na pigo; kwa msingi huo kwa mujibu wa kanuni ya akili na mantiki, hatupasi kufanya jambo au kutoa maneno na kuonesha hali itakayomuwezesha adui kuingia katika safu za Wairani akidhani kuwa ni wadhaifu na kumhamasisha kutoa pigo na kufanya uhasama.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria aya za Qur'ani tukufu zinazoonesha kuwa, istiqama na kusimama kidete katika njia ya Mwenyezi Mungu kuna thawabu za Akhera na ujira wa hapa duniani yaani izza, nguvu na maendeleo na kusema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikikabiliana na uhasama wa mabeberu, uzayuni na madola yenye fikra mgando kwa kipindi cha miaka 38 sasa lakini hii leo imepiga hatua kubwa za maendeleo na kuwa na nguvu kubwa mara mamia au hata maelfu zaidi ya ilivyokuwa mwanzoni mwa Mapinduzi ya Kiislamu, na haya ndiyo malipo ya dunia ya kusimama kidete na kuwa na istiqama. 
Kiongozi Mudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametilia mkazo udhaura wa kuchambua hali halisi ya nchi kwa njia sahihi na kusema: Si sahihi kutasawari kwamba, Mfumo wa Kiislamu umedhoofika kutokana na mapungufu ya kiitikadi na kutojali kwa baadhi ya watu, kwa sababu masuala kama hayo yalikuwepo tangu mwanzoni mwa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. Amesisitiza kuwa, hata hivyo harakati nzuri na iliyobarikiwa ya vijana wenye imani ni hakika inaong’aa zaidi kuliko hapo awali.
Ayatullah Khamenei ameitaja taathira kubwa ya kizazi cha vijana wenye imani wa Iran katika eneo la Mashariki ya Kati licha ya kwamba vijana hao hawakuona kipindi cha Mapinduzi ya Kiislamu wala Imam Khomeini na kipindi cha vita vya kujitetea kutakatifu kuwa ni miongoni mwa miujiza ya Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini.  Amesema: "Ninyi vijana mumeweza kuipigisha magoti Marekani beberu na kuishinda".
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema sababu halisi ya kuangamizwa na kushindwa tezi la saratani la Daesh ni moyo wa kujitolea na wa kibasiji na kuongeza kuwa, maadui walifanya jitihada za kutumia kundi hilo la kitakfiri na lisilo na ubinadamu kukwamisha harakati ya mapambano lakini vijana wenye imani, shauku na ari waliingia katika medani ya jihadi na kumpigisha magoti adui.
Ayatullah Khamenei amewakosoa wale wanaovunja moyo na kuwakatisha tamaa wananchi mbele ya madola ya kibeberu na kusisitiza kuwa, njama kadhaa na za mara kwa mara za Marekani, uzayuni na vibaraka wao katika eneo la Mashariki ya Kati zimezimwa kwa nguvu na uwezo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na miongoni mwa mifano hai ni kuangamizwa kundi la Daesh. Amehoji kwamba, je hii si ithibati tosha kwamba “sisi tunawezza”? 
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kutokomezwa kundi hilo la kitakfiri na lisilo na ubinadamu kutokana na hima kubwa ya vijana na wanaume wenye imani na jitihada za watu wanaokubali muqawama na mapambano ni kazi kubwa sana na kuongeza kuwa: Baadhi ya watu katika nchi jirani hawakuamini kuwa wanaweza kuliangamiza kundi la Daesh, lakini walipoingia katika medani ya mapambano walishuhudia ushindi kwa macho yao na kuamini ujumbe wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran unaosema: "Sisi Tunaweza."  
Ayatullah Khamenei amesema moyo wa kibasiji yaani ari, shauku na juhudi kubwa ni suala linalohitajika katika nyanja zote za kielimu, kiuchumi, kiviwanda na kiutamaduni. Ameongeza kuwa, mamilioni ya watu hapa nchini si wanachama rasmi wa Jumuiya ya Basiji lakini kwa hakika wao ni Basiji, na uwezo huu wa aina yake unapaswa kutumiwa vizuri kwa ajili ya kutekeleza kazi nyingi katika nyanja mbalimbali. 
Amesema kuwa sharti la kulindwa Basiji ni kulinda sifa zake ikiwa ni pamoja na kuona mbali na kumjua adui na kusisitiza kuwa: Vijana wanapaswa kuzima njama mbalimbali za adui kwa kujua vyema mbinu tofauti anazozitumi katika nyanya za mtu binafsi, familia na jamii. 
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema moja kati ya mbinu zinazotumiwa na wageni ni kuwavunja moyo vijana na kuwafanya waamini kwamba “sisi hatuwezi”. Ameongeza kuwa, inasikitisha kuona kwamba, baadhi ya watu hapa nchini wamekuwa vipaza sauti vya maadui na wanapuuza mifano mingi ya vielelezo cha uwezo wa taifa na utawala wa Kiislamu.
Ayatullah Khamenei amekutaja kupinduliwa utawala wa kidikteta na tegemezi wa Shah, kutengeneza sababu na nyezo za maendeleo na nguvu ya Mfumo wa Kiislamu na uwezo wa kuathiri fikra za mataifa mengine kuwa ni kati ya mifano mingi ya uwezo wa taifa la Iran. Ameongeza kuwa, tangu sasa pia na kwa taufiki yake Mwenyezi Mungu, Mapinduzi ya Kiislamu yatadumisha harakati ya kutimiza malengo yake yote kwa kutegemea kizazi cha vijana na waumini.
Amekumbushia tajiriba inayokariri mara kwa mara ya taifa la Iran ya kutimiza kivitendo kaulimbiu ya “sisi tunaweza” na kusema: Kaulimbiu ya “sisi tunaweza” si suala la kiitikadi tu, bali taifa la Iran limeiona na kuishuhudia mara kadhaa kwa macho.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja jihadi, kufanya jitihada kubwa na kusimama kidete kuwa ni miongoni mwa masharti muhimu zaidi ya maendeleo na kusema: Inabidi mlinde istikama na kusimama imara ndani ya nafsi zenu ili ahadi ya Mwenyezi Mungu ya kupata ushindi iweze kutimia.
Ayatullah Ali Khamenei ameashiria malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu katika nyanja mbalimbali za uchumi, jamii, elimu, siasa na utamaduni na kusisitiza kuwa: Kwa Baraka zake Mwenyezi Mungu, Iran itafikia malengo hayo yote katika mustakbali si wa mbali na kizazi cha vijana kitatatua matatizo ya kiuchumi, kuzidisha mafanikio na maendeleo ya kielimu na kutimiza malengo ya kiutamaduni na ya Qur’ani. 
Kwa mara nyingine tena Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametilia mkazo udharura wa kuwa macho mbele ya maadui na kusema: Makundi ya wananchi wavumbuzi na wenye imani yanapaswa kuwa tayari kwa ajili ya kukabiliana na mbinu mpya za maadui na kutekeleza majukumu yao vyema kwa kuzuia na kujibu mapigo.
Mwishoni mwa hotuba yake, Ayatullah Khamenei amewaombea dua mashahidi watukufu walioingia kwa imani katika medani za vita huko Iraq na Syria na kumtaradhia Mwenyezi Mungu awafufue na Mawalii Wake.       
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah), Meja Jenerali Muhammad Ali Ja’fari amezungumzia tukio la kuangamizwa magaidi wa kitakfiri wa kundi la Daesh, kuwekwa kando Marekani katika matukio ya sasa ya Mashariki ya Kati na kubakia nyuma tawala tegemezi na vibraka na kusema: Hii leo rafiki na adui wanajua vyema kwamba, utawala wa Kizayuni wa Israel si lolote si chochote na kwamba vita vingine katika eneo hili vitapelekea kufutwa kabisa utawala huo katika jiografia ya kisiasa.
Kamanda wa jeshi la Sepah amesema kuwa, kipaumbele cha sasa cha jeshi la Basiji ni kuwasaidia wananchi kwa ajili ya kutatua mtatizo ya kimaisha na kuongeza kuwa, kushiriki ipasavyo katika operesheni za kutoa misaada na kuokoa wananchi waliokumbwa na migogoro na kuzidisha usalama wa kikanda na maeneo mbalimbali ni miongoni mwa vipaumbele muhimu vya Basiji. 
 

700 /