Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Iran na Russia zitafanikiwa katika medani nyingine ngumu

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekaribisha pendekezo la Rais Vladmir Putin wa Russia la kupanua zaidi ushirikiano katika nyanja zote na kusema kuwa, kuna udharura wa kutumia tajiriba na uzoefu mkubwa uliopatikana katika miaka ya hivi karibuni kwenye masuala ya kieneo na katika uhusiano wa nchi mbili za Iran na Russia, kuimarisha na kutia nguvu zaidi uhusiano wa pande hizi mbili.
Ayatullah Ali Khamenei amesema hayo jioni ya leo hapa mjini Tehran katika mazungumzo yake na Rais Vladimir Putin wa Russia na kuongeza kuwa, nchi hizi mbili zinaweza pia kuwa na ushirikiano mkubwa katika nyuga nyingine za kiuchumi kama vile usafiri na uchukuzi kwa kutumia bandari za Chabahar ya Iran na ile ya Saint Petersburg ya Russia.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia uzoefu mzuri uliopatikana katika ushirikiano wa nchi hizi mbili katika kadhia ya Syria na kuongeza kuwa, matokeo ya ushirikiano huo yanaonesha kwamba, Tehran na Moscow zinaweza kufanikisha malengo yao mengine muhimu kwenye medani ngumu. 
Amesema, kushindwa muungano wa Marekani unaounga mkono magaidi huko Syria ni uhakika usiokanushika, lakini pamoja na hayo, mabeberu hao wanaendelea kufanya njama mbalimbali, hivyo utatuzi wa kudumu wa suala la Syria unahitajia kuendelea kuwepo ushirikiano madhubuti.
Ayatullah Khamenei vilevile amesisitiza kuwa, kusimama kidete pamoja Iran na Russia katika kukabiliana na magaidi wa kifakfiri wanaoungwa mkono na nchi kadhaa za kigeni kuna matokeo muhimu na kuongeza kuwa: Muundo mzuri sana na kusimama kidete kwa pamoja Tehran na Moscow katika kukabiliana na fitna na ufisadi wa magaidi huko Syria ni jambo lenye thamani kubwa na limeifanya Russia kuwa na taathira katika masuala ya eneo la magharibi mwa Asia.
Ayatullah Khamenei amesisitiza kwamba wananchi wenyewe wa Syria ndio wenye haki ya kuchukua maamuzi kuhusu masuala ya nchi yao na kuongeza kuwa: Kama ulivyosema wewe mwenyewe, kuna ulazima wa masuala yote na njia zote za utatuzi kuhusu serikali ya Syria zitoke ndani ya nchi hiyo, na serikali ya Syria isiwekewe mashinikizo kwa ajili ya kutekeleza mpango wowote ule, na mipango inayowasilishwa inapaswa kuwa na utatuzi kamili na wa pande zote.  
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesifu matamshi ya Rais wa Russia kuhusu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na udharura wa kuheshimiwa makubaliano ya pande mbili na kusema: Inasikitisha kuona kwamba, Wamarekani wanaendeleza uovu wao na kuna ulazima wa kukabiliana nao kwa kutumia akili na njia sahihi. 
Ayatullah Khamenei pia ameunga mkono misimamo ya Putin kuhusu udharura wa kutatuliwa masuala ya kieneo bila ya kuingilia kati nchi ajinabi na kusema kuwa, Wamarekani wanataka kuingilia masuala yote ya Mashariki ya Kati na dunia, na ili kutimiza malengo hayo, wanawatumia viongozi dhaifu katika baadhi ya nchi. 
Amesema umwagaji wa damu unaofanywa na Wasaudia katika baadhi ya nchi zikiwemo jinai na uhalifu wao huko Yemen vinatayarisha uwanja wa kunaswa Saudi Arabia katika kinamasi na matatizo makubwa. Ameongeza kuwa, Wasaudia hawaruhusu hata kupelekwa dawa na misaada kwa watu wanaodhulumiwa wa Yemen ambao wanasumbuliwa na maradhi ya kuambukiza na yanayoua.    
 Kiongozi Muadhamu amezungumzia pia suala la kuongezwa kiwango cha ushirikiano baina ya Iran na Russia katika kukabiliana kwa pamoja na vikwazo vya Marekani dhidi ya nchi hizi mbili na ameunga mkono pendekezo la Rais Vladimir Putin la kuimarishwa ushirikiano wa pande mbili kwenye nyuga zote.
Amesema: Bila ya kujali propaganda chafu zinazofanywa na maadui kwa ajili ya kudhoofisha uhusiano wa nchi mbalimbali, tunaweza kuzima vikwazo vya Wamarekani na kuitenga nchi hiyo kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo ya kufuta matumizi ya sarafu ya dola ya Marekani na badala yake kutumia sarafu ya taifa katika miamala ya kiuchumi ya pande mbili au pande kadhaa.
Amemtaja Rais Putin wa Russia kuwa ni mtu mwenye shakhsia imara na mwenye azma na mchapakazi na kusema: Kwa sababu hiyo inawezekana kuzungumza na kushirikiana na Russia kama nchi kubwa kuhusu kazi kubwa na zinazohitajia azma na juhudi.
Katika mazungumzo hayo yaliyodumu kwa zaidi ya saa moja, Rais Vladimir Putin wa Russia ameelezea kufurahishwa kwake na safari yake hapa nchini na kuonana tena na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusisitiza kuwa, Iran ni mshirika wa kiistratijia na ni jirani mkubwa wa Russia na kwamba haitazembea kutumia fursa yoyote itakayojitokeza kwa ajili ya kuimarisha na kustawisha uhusiano na ushirikiano wake wa pande zote na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Putin ameyataja mazungumzo yake na Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa yalikuwa mazuri sana na kuyataja masuala ya nishati, usafirishaji, teknolojia ya kisasa, kilimo na miradi ya pamoja ya mafuta na gesi kuwa ni miongoni mwa nyanja nzuri kwa ajili ya kupanua zaidi uhusiano wa kiuchumi.
Rais wa Russia amesema kuwa uuzaji wa bidhaa za kilimo za Iran nchini kwake umeongezeka mara saba na kwamba bado kuna nyanja nyingi za kuweza kushirkiana zaidi. 
Vladimir Putin amesisitiza udharura wa kulindwa amani ya eneo la Mashariki ya Kati na kusema: Kwa ushirikiano uliopo nchini Syria tumeweza kupata mafanikio makubwa na inabidi kudumishwe mapambano dhidi ya ugaidi na kuanzisha mchakato unaofaa wa kisiasa nchini humo. 
Rais wa Russia ameita misimamo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuwa ni ya kimantiki na imekuwa na taathira kubwa katika kutimiza malengo ya pamoja huko Syria na kusema: "Tumeuonesha ulimwengu kwamba, tunaweza kutatua matatizo ya eneo hili muhimu sana bila ya kuhitajia nchi ajnabi za nje ya eneo hili."
Rais wa Russia ametangaza uungaji mkono wa Moscow kwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kusema kuwa, anapinga mabadiliko ya aina yoyote ya upande mmoja katika mkataba wa makubaliano ya pande kadhaa na kwamba hatua za kujichukua maamuzi ya upande mmoja zinapingana na kukanyaga sheria za kimataifa. 
Amesema si sahihi kubadilisha misingi mikuu ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki na kwamba, vilevile Russia inapinga suala la kufungamanisha miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia ya Iran na masuala ya kiulinzi. 
Putin amesisitiza kuwa, inawezekana kustawisha zaidi uhusiano wa kiulinzi na kijeshi wa nchi hizi mbili katika fremu ya sheria za kimataifa.
Ameashiria kwamba nchi za nje ya eneo hili zinafanya njama za kuzusha vita na kusema: Marekani inataka kuingilia kati masuala yote ya eneo hili na dunia na katika njia hiyo inapuuza maslahi ya waitifaki wake. 
Rais wa Russia ameashiria uongo wa maafisa wa Marekani kuhusu Russia katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kusema: "Sikudhani hata kidogo kwamba inaweza kufanya jambo kama hilo katika upeo huu wa uhusiano wa kimataifa, lakini sasa miendo kama hii ya Wamarekani limekuwa jambo la kawaida."
Amesema kuwa sera kuu ya nchi yake katika kukabiliana na vikwazo vya Marekani ni kutegemea uwezo wa ndani ya nchi na kusisitiza kuwa: Baadhi ya wazalisha na wamiliki wa viwanda wa Russia wanaomba dua vikwazo vya Marekani viendelee kwa sababu vimekuwa sababu ya kutiliwa maanani na kupewa mazingatio zaidi uwezo wao. 
Putin ameongeza kuwa, tangu mwaka 2014 yaani wakati vilipoanza vikwazo vya Marekani dhidi ya Russia, nchi hiyo imetenga kiwango kikubwa zaidi cha fedha kwa ajili ya maendeleo ya sayansi na teknolojia na imepiga hatua kubwa katika nyanja za bio-teknolojia, IT, kilimo na sekta ya viwanda vya masuala ya anga.
Rais wa Russia amesema kuwa, hivi sasa na tofauti na wasiwasi uliokuwepo hapo awali, tumejua kwamba, kila jambo tunalolitaka tunaweza kulifanya. 
Mwishoni mwa matamshi yake, Rais Vladimir Putin wa Russia amesisitiza kuwa: "Tunafungamana na misimamo yetu ya kimsingi na tutadumisha kazi tulizozianza na upande wowote mwingine."           

700 /