Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Utawala wa Kizayuni wa Israel utaangamizwa kwa hima ya Waislamu

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei mapema leo amehutubia hadhara ya Baraza la Idi iliyohudhuriwa na maafisa wa serikali, makamanda wa jeshi, mabalozi wa nchi za Kiislamu na wananchi wa matabaka mbalimbali na kusema kuwa, sababu muhimu zaidi za kupelekea kuheshimiwa jamii za Kiislamu duniani ni umoja na kutatua hitilafu zilizopo. 
Ayatullah Khamenei amesema kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel ndiyo sababu kuu ya hitilafu zilizopo katika eneo la Mashariki na Kati na kati ya nchi za Waislamu na kuongeza kuwa: "Tatizo la utawala wa Kizayuni ni kutokuwa kwake halali na ni utawala ulioanzishwa kwa misingi batili na isiyo sahihi; hivyo kwa taufiki yake Mwenyezi Mungu na hima ya mataifa ya Waislamu, utawala huo utaangamizwa na kutoweka kabisa."
Amesema kuwa, siasa za sasa za mabeberu ni kuzusha hitilafu na migawanyiko kati ya Waislamu, na njia pekee ya kukabiliana na siasa hizo za Marekani mtenda jinai na Wazayuni ni kutambua vyema mipango na njama za adui na kusimama kidete kukabiliana nayo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema nchi za Waislamu, viongozi wa kisiasa, kidini na kiutamaduni katika Umma wa Kislamu wana jukumu zito la kuyasaidia mataifa kukabiliana na siasa za madola ya kibeberu. Ameashiria malengo ya kuundwa utawala bandia wa Israel katika eneo la Mashariki ya Kati na kusema: "Moja ya malengo asili ya kuasisiwa utawala huo ni kuzusha hitilafu baina ya mataifa ya Waislamu." Ameongeza kuwa: Hata hivyo uzoefu wa kihistoria unaonyesha kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel unaokabiliawa na mgogoro wa utambulisha na kutokuwa halali hautaendelea kuwepo.
Kiongozi Muadhamu amesisitiza kuwa hatua ya baadhi ya tawala zenye mitazamo dhaifu ya kuanzisha uhusiano wa siri na wa wazi wa kidiplomasia na utawala wa Kizayuni pamoja na hatua ya Marekani kuhamishia ubalozi wake katika mji wa Quds haiwezi kuondoa tatizo la utawala wa Kizayuni. Amesema utawala huo wa Kizayuni wa Israel umejengeka katika msingi wa kutumia mabavu, vitisho na mauaji pamoja na kulifukuza taifa katika ardhi yake na kwa msingi huo, suala la kukosa uhalali utawala huo limechorwa katika nyoyo za mataifa ya Kiislamu; hivyo haiwezekani kuifuta ramani ya Palestina katika kumbukumbu ya kihistoria ya jiografia ya dunia.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa mara nyingine amesisitiza ulazima wa kufanyika kura ya maoni itakayohusisha Wapalestina halisi, wakiwemo Waislamu, Wakristo na Mayahudi ili kuamua mfumo wa utawala wa Palestina na kuongeza kuwa: "Kufanyika kura kama hii ya maoni na kuundwa serikali ya Palestina kwa kutegemea kura za Wapalestina kwa hakika kuna maana ya kuangamizwa utawala bandia wa Israel na kwa yakini jambo hili litatimia katika mustakabali usio mbali."
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, kuangamizwa kwa utawala wa Kizayuni kutaleta umoja na izza katika Umma wa Kiislamu.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Rais Hassan Rouhani ametoa hotuba fupi akisema kuwa kuna haja kubwa zaidi ya kuimarishwa anga ya kiroho, umoja, kujiamini na kuwa na matumaini ya mustakbali mwema. Amesisitiza kuwa, serikali inahitajia msaada wa asasi zote hususan wananchi. 
Rais Rouhani amesema kwa sasa adui hana uzoefu wala mantiki na kuongeza kuwa: Adui amechukua uamuzi wa kukanyaga na kupuuza majukumu yake si mbele ya taifa la Iran pekee bali hata majukumu yake ya kikanda na kimataifa. 
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, inashangaza kuona dola ambalo mikono yake imejaa damu za watu wa eneo hili kuanzia Afghanistan, Iraq, Syria, Yemen na maeneo mengine amevaa nikabu ya kudai amani na kuzungumzia suala la amani.
Rais Rouhani amesema hii leo watu na nchi mbalimbali duniani, washirika wa kibiashara wa Iran, Ulaya, Russia, China, nchi jirani, Waislamu na mataifa mengine yanapaswa kusimama kidete kukabiliana na ubabe wa watawala wa White House.    
 

700 /