Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Ujumbe wa Kiongozi Muadhamu kwa Mahujaji

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema katika ujumbe wake uliosomwa leo kwa Mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu kwamba sera za Marekani ni kuchochea vita baina ya Waislamu na akasisitiza kwamba: inapasa kuzizima sera hizo za kishetani kwa umakini na kuwa macho na kwamba Hija na kujibari na washirikina vinawezesha kupatikana umakini huo.
Vilevile amewataka Mahujaji kuthamini taufiki ya kuwa katika ugeni wa Allah na kuitumia kwa ajili ya kujisafisha na kupata masurufu kwa ajili ya muda uliobakia katika umri wao.
Matini kamili ya ujumbe wa Ayatullah Ali Khamenei ni hii ifuatayo: 
Bismillahir Rahmanir Rahiim
Hamdu zote zinamstahikia Allah na sala na salamu zimshukie Mtume wake al Mustafa na Aali zake watoharifu, na maswahaba zake wema. Mwenyezi Mungu SW anasema: Na watangazie watu Hija; watakujia kwa miguu na juu ya kila ngamia aliyekonda, wakija kutoka katika kila njia ya mbali. Ili washuhudie manufaa yao na walitaje jina la Mwenyezi Mungu katika siku maalumu….

Tangu karne zilizopita na vipindi mbalimbali, wito huo wa mbinguni ungali unaziita nyoyo na kuwataka wanadamu wakusanyike pamoja katika duara la Tauhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu. Wanadamu wote wanalengwa na wito huu na wanajifaharisha nao, japokuwa masikio yao hayausikii na nyoyo zilizogubikwa na pazia la mgafala na ujahili zinashindwa kuupokea, na japokuwa wako watu ambao hawana ustahiki wa kuingia katika ugeni huo wa kimataifa na wa kudumu au hawakupata taufiki ya kuwa katika ugeni huo kwa sababu moja au nyingine.

Nyinyi, mahujaji, mumefanikiwa kupata hiba hiyo na kuingia katika ugeni wa Mwenyezi Mungu. Arafa, Mash'ar, Mina, Safa, Marwa, Masjidul Haram na Masjidunnabi maeneo haya yote ya ibada ya Hija ni sehemu ya mnyororo wa masuala ya kiroho na ngazi ya kukwea katika masuala ya kimaanawi wakati wa Hija; hivyo mnapaswa kuthamini taufiki hiyo na kuitumia kwa ajili ya kujisafisha na kupata masurufu kwa ajili ya muda uliobakia katika umri wenu.

Jambo muhimu linalomfanya kila mtu mwenye fikra atake kudadisi ni suala la kuainishwa sehemu ya kudumu kwa ajili ya watu wote na vizazi vyote na katika myaka yote katika eneo moja maalumu na zama na wakati mmoja. Umoja huu wa zama na eneo ni miongoni mwa siri kuu za ibada ya Hija. Hapana shaka kuwa, moja kati ya vielelezo vikubwa zaidi vya sehemu ya aya ya Qur'ani inayosema: "Ili washuhudie manufaa yao.." ni mkutano huu wa kila mwaka wa Umma wa Kiislamu kandokando ya Nyumba ya Mwenyezi Mungu. Hii ndiyo siri ya umoja wa Kiislamu na nembo inayojenga umma wa Uislamu ambayo inapaswa kuwa chini ya kivuli cha Nyumba ya Mwenyezi Mungu. Nyumba hii ya Mwenyezi Mungu ni ya watu wote, "Msikiti mtakatifu ambao tumeufanya kwa ajili ya watu wote sawa sawa kwa wakaao humo na wageni…"

Hija katika eneo hili na katika kipindi hiki maalumu; daima na katika miaka yote; inawalingania Waislamu umoja na mshikamano kwa lugha bayana na kwa mantiki iliyo wazi. Na kinyume na jambo hilo ndicho kitu kinachotakiwa na maadui wa Uislamu katika vipindi vyote na hasa katika kipindi cha hivi sasa. Maadui walikuwa na wanaendelea kuwachochea Waislamu kupigana na kugombana wao kwa wao. Angalieni vitendo vya hivi sasa vya kiistikbari vya Marekani. Siasa zake kuu mbele ya Uislamu na Waislamu ni kuzusha vita. Matakwa na njama zake za kikhabithi ni kuwafanya Waislamu wauane wao kwa wao. Kuwachochea madhalimu wawakandamize wadhulumiwa, kuunga mkono mirengo ya madhalimu, kukandamizwa kikatili mrengo wa wadhulumiwa na kuzidi daima kuchochea moto wa fitna hiyo hatari mno; (yote hayo ni katika njama za kikhabithi za Marekani). Waislamu wanapaswa kuwa macho ili waweze kuvunja siasa hizo za kishetani. Hija ni fursa nzuri ya kupatikana mwamko huo wa Waislamu na hii kwa hakika ndiyo falsafa ya kujibari na kutangaza kuwa mbali na washirikina na mabeberu.
Roho ya Hija ni kumkumbuka na kumtaja Mwenyezi Mungu. Kwa hali yoyote ile, tuzihuishe, tuziimarishe na tuzitie nguvu nyoyo zetu kwa mvua hii ya rehema, na kutawakali Kwake Yeye Ambaye Ndiye chimbuko la nguvu, ustawi, uadilifu na ujamali. Ni kwa njia hii ndipo tutaweza kuzishinda njama za adui. Mahujaji wapendwa! Msisahau kuuombea dua umma wa Kiislamu na watu wanaodhulumiwa katika nchi za Syria, Iraq, Palestina, Afghanistan, Yemen, Bahrain, Libya, Pakistan, Kashmir, Myanmar na maeneo mengine duniani na muombeni Mwenyezi Mungu aukate mkono wa Marekani na mabeberu wengine na vibaraka wao.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullah.
Sayyid Ali Khamenei
28 Mwezi Mordad 1397 (Hijria Shamsia)
Sawa na Mwezi 7, Mfunguo Tatu 1439 (Hijria)
(Agosti 19, 2018).
 

700 /