Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Vyombo husika viwakamate wahusika wa shambulizi la Ahvaz

Kufuatia shambulio la kigaidi lililofanywa leo asubuhi katika mji wa Ahvaz kusini magharibi mwa Iran, ambalo limepelekea watu kadhaa kuuawa shahidi na kujeruhiwa, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ametuma salamu za rambirambi kwa familia za mashahidi wa tukio hilo chungu.
Matini ya ujumbe wa Kiongozi Muadhamu ni hii ifuatayo:
Tukio chungu na la kusikitisha la kuuliwa shahidi wananchi kadhaa wa Iran huko Ahvaz na magaidi mamluki, limedhihirisha kwa mara nyingine ukatili na uhabithi wa maadui wa taifa la Iran.
Mamluki hawa wenye nyoyo katili wanaowamiminia risasi wanawake, watoto wadogo na watu wasio na hatia ni vibaraka wa watu walewale waongo na wazandiki wanaojidai kila mara kuzungumzia haki za binadamu, wakati nyoyo zao zilizojaa chuki haziwezi kuvumilia kuona nguvu na uwezo wa kitaifa unaoonyeshwa na vikosi vya ulinzi vya Iran.
Jinai za watu hao ni mwendelezo wa njama za tawala vibaraka wa Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati ambazo lengo lao ni kuvuruga usalama ndani ya Iran; hata hivyo watakufa na ndoto yao hiyo, kwani taifa la Iran litaendelea kushikamana na njia yake inayolipa heshima na utukufu, na kama ilivyokuwa huko nyuma litawashinda maadui zake wote.
Ninatoa mkono wa pole na salamu za rambirambi kwa familia za mashahidi watukufu na nawaombea dua ya kuwa na subira na uvumilivu; vilevile nawaombea mashahidi dua ya kupata daraja za juu peponi. 
Vyombo husika vya upelelezi vinawajibika kuwafuatilia watenda jinai hii haraka na kwa makini na kuwafikisha kwenye mikono imara ya vyombo vya mahakama. 
Sayyid Ali Khamenei
31/Shahrivar/1397 (22 Septemba/2018)
 

700 /