Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu:

Iraq yenye nguvu na tulivu isimame kidete mbele ya maadui

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei alasiri ya leo amekutana na Rais Barham Ahmed Salih wa Iraq na ujumbe unaoandamana naye hapa mjini Tehran. Ameeleza kufurahishwa kwake na zoezi lililofanyika kwa mafanikio la uchaguzi wa Bunge nchini Iraq, kuchaguliwa Rais na Waziri Mkuu na viongozi wengine na vilevile kurejeshwa amani na utulivu nchini humo na kusisitiza kuwa, njia ya kuvuka matatizo na kukabiliana na njama za wasiotaka mema ni kulinda umoja wa kitaifa wa Iraq, kuwajua vizuri marafiki na maadui na kusimama kidete mbele ya adui muovu, kuwategemea nguvu kazi ya vijana na kulinda na kuimarisha mahusiano na wanazuoni wakuu wa kidini.
Mwanzoni mwa mazungumzo hayo Ayatullah Khamenei amempongeza Barham Salih kutokana na kuchaguliwa kwake kubeba majukumu mazito ya kuwa Rais wa nchi muhimu ya Iraq. Ameashiria uhusiano wenye historia ndefu na wa kina wa mataifa mawili ya Iran na Iraq na akasema: Mahusiano ya mataifa haya mawili hayana kifani na mfano wake wa wazi ni matembezi adhimu ya Arubaini ya Imam Hussein.   
Ayatullah Khamenei ameashiria kushiriki wafanyaziara Wairani wapatao milioni mbili katika matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein AS mwaka huu na kusema kuwa, nyoyo za Wairani waliorejea nyumbani kutoka kwenye matembezi hayo zilijaa shukrani kutokana na ukarimu wa watu wa Iraq. Ameongeza kuwa, hii ni ishara ya ukarimu mkubwa wa Wairaqi wa kuwakaribisha wafanyaziara Wairani na ukarimu huo na mahusiano yanayoandamana na upendo baina ya mataifa haya mawili haviwezi kuelezeka isipokuwa kwa lugha ya sanaa. 
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amemshukuru Rais wa Iraq, Waziri Mkuu na maafisa wengine wa serikali ya nchi hiyo na taifa zima la Iraq kutokana na ukarimu wao mkubwa katika siku za shughuli za Arubaini ya Imam Hussein. Vilevile ameashiria mashaka makubwa ya watu wa Iraq katika miaka iliyopita na kusema kuwa: Kwa sasa ambapo taifa la Iraq limeshika hatamu za nchi na lina haki ya kujiamulia mambo na kuchagua baada ya vipindi vya udikteta, baadhi ya serikali na nchi zisizoitakia Iraq mema zinataka Wairaqi wasionje utamu wa ushindi na mafanukio yao makubwa na wanachotaka wao ni kukosekana utulivu nchini humo na katika eneo hili zima la Mashariki ya Kati.
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, njia pekee ya kukabiliana na njama hizi ni kulinda na kuimarisha umoja miongoni mwa makundi ya Wairaqi, sawa tu wawe Waarabu au Wakurdi au Mashia na Masuni.
Amesema kumjua kwa njia sahihi rafiki na adui ni muhimu sana katika sera za kigeni na kuongeza kuwa, baadhi ya serikali za kanda hii na nje ya eneo zina chuki kubwa sana dhidi ya Uislamu, Ushia, Usuni na nchi ya Iraq, hivyo zinaingilia masuala ya ndani ya Iraq. Amesema, kuna haja ya kusimama kidete na kwa uwazi kupambana na adui muovu.
Kuhusu ushirikiano wa pande mbili baina ya Iran na Iraq, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, wakuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wana azma imara ya kuimarisha uhusiano na Iraq na kuongeza kuwa, yeye binafsi ana imani na suala hilo.
Ameashiria uwezo mkubwa wa nchi mbili hizi wa kupanua zaidi ushirikiano na kusema: "Iraq azizi, yenye nguvu, yenye kujitegemea na iliyostawi ina faida kubwa kwa Iran na sisi tutabaki pamoja na ndugu zetu Wairaqi."
Ametilia mkazo udharura wa kulindwa na kuimarishwa mahusiano na wanazuoni wakuu wa kidini na kusema: Kuwepo mawasiliano na viongozi wa juu wa dini katika vipindi na awamu mbalimbali kunaweza kutatua mambo mengi. 
Ayatullah Khamenei amesema kuwa, tegemea vijana kunajenga mazingira ya kutekelezwa kazi kubwa na kuongeza kuwa: Mfano wa wazi zaidi wa matokeo mazuri ya kuwategemea vijana ni kuundwa harakati ya wananchi ya al Hashdu al Shaabi katika kipindi cha mapambano dhidi ya ugaidi wa makundi ya kitakfiri na kuna haja ya kulindwa harakati hiyo. 
Kwa upande wake Rais Barham Salih wa Iraq amesema katika mazungumzo hayo ambayo pia yamehudhuriwa na Rais Hassan Rouhani wa Iran kwamba ni fahari kubwa kwake kukutana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu. Ameongeza kuwa, amekuja Iran akiwa na ujumbe wa wazi nao ni kwamba, uhusiano na mfungamano wa mataifa mawili ya Iran na Iraq umekita mizizi katika historia na hauwezi kubadilishwa.
Ameashiria mazungumzo yake hapa mjini Tehran na kusema kuwa: "Tunataka kupanua zaidi ushirikiano katika nyanja zote na kuunyanyua juu zaidi hadi kwenye kiwango kinacholingana na hadhi ya uhusiano wa kijamii, kiutamaduni na maslahi ya mataifa haya mawili." 
Rais Barham Salih wa Iraq amesema kuwa, kutoa huduma kwa wafanyaziara katika Arubaini ya Imam Hussein ni fahari kwa serikali na taifa la Iraq. Ameongeza kuwa, Iraq kamwe haitasahau misaada na himaya ya Iran wakati wa utawala wa kidikteta wa Saddam Hussein na katika kipindi cha kupambana na ugaidi wa makundi ya kitakfiri. 
Rais wa Iraq amesema kuwa, kipaumbele cha viongozi wa Iraq katika kipindi kipya ni kuijenga upya nchi na kuhuisha miundombinu, kupambana na ufisadi, kutoa huduma nzuri kwa wananchi, kufanya marekebisho ya ndani na kuimarisha umoja wa kitaifa. 

700 /