Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Umoja na mshikamano wa Kiislamu vitashinda njama za maadui

Mapema leo tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal, siku ya Maulidi ya Mtume na kumbukumbu ya kuzaliwa Nabii wa rehma na uongofu, Muhammad (saw) na mjukuu wake, Imam Jafar Swadiq (as), maafisa wa nchi, wageni waalikwa wanaoshiriki katika Mkutano wa 32 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu, mabalozi wa nchi za Kiislamu mjini Tehran na wananchi wa matabaka mbalimbali wameonana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei. 
Katika hotuba yake kwenye hadhara hiyo, Ayatullah Ali Khamenei amesema njia pekee ya saada na ufanisi wa wanadamu ni kufuata dini ya Uislamu na nuru ya Qur'ani. Vilevile ameashiria mwamko unaozidi kupanuka wa Kiislamu na moyo wa mapambano kati ya mataifa ya Waislamu na vilevile kiwewe cha Marekani na waitifaki wake kutokana na hali hiyo na kusema: Kutokana na mapambano na kusimama kidete kwa taifa la Iran katika kipindi chote cha miaka 40 iliyopita, Mapinduzi ya Kiislamu ambayo ni kigezo bora cha kuigwa sasa yamekuwa mti mzuri na imara ambao hauathiriwi na vitisho na harakati habithi za Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel kama ilivyokuwa miaka ya nyuma na hapana shaka kwamba, zitafeli na kushindwa.
Mwanzoni mwa mkutano huo Ayatullah Ali Khamenei amewapongeza Waislamu wote kwa mnasaba wa Maulidi na kumbukumbu ya kuzaliwa Mtume wa rehma Muhammad (saw) na mjukuu wake, Imam Jafar Swadiq (as) na amemtaja Mtume kuwa ni jua linalong'aa ambalo Mwenyezi Mungu mtukufu aliwatunuku wanadamu katika kipindi cha ujahilia na ujinga, na mtukufu huyo akawatayarishia wanadamu uwanja mzuri wa kupata ufanisi na uongofu kwa dini ya mbinguni ya Uislamu na kitabu chenye nuru na mwanga cha Qur'ani.  
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria haja ya siku zote ya wanadamu kwa rehma, uongofu na nuru Mtume wa Uislamu (saw) na kusema: Hii leo pia na kutokana na kuwepo madola ya kibeberu, dhulma inayotokana na matendo yao maovu, ujinga, hadaa na ukosefu wa uadilifu, wanadamu wanasumbuliwa na matatizo na mashaka ya aina mbalimbali ambayo tiba yake pekee inapatikana kwa kuitikia wito wa Nabii Muhammad (saw) na kufuata njia ya uongofu ya Uislamu na Qur'ani. 
Ayatullah Khamenei ametaja harakati ya mapambano na moyo wa mwamko wa Kiislamu katika eneo la Mashariki ya Kati kuwa ni matokeo ya kufuata hidaya na uongufu wa Uislamu an Qur'ani na kusema: Sababu ya madola makubwa ya kibeberu duniani yakiongozwa na Marekani mtenda jinai na shetani mkubwa kuwa na wasiwasi kuhusu eneo la magharibi mwa Asia ni moyo wa watu wa kujielekeza kwenye Uislamu na mwamko wa Kiislamu baina ya mataifa ya eneo hilo. 
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameashiria wasiwasi wa madola ya kibeberu kuhusu mwamko wa mataifa ya Kiislamu na kusema kuwa, mahala popote ambapo Uislamu unadhibiti nyoyo za watu, ubeberu husambaratishwa na kwa mara nyingine mwamko wa Kiislamu katika eneo hili utatoa kipigo kwa ubeberu huo. 
Amewahutubu wanafikra na maulama wa kidini akisema; "Fanyeni kila muwezalo kuimarisha harakati ya mwamko wa Kiislamu na muqawama katika eneo la Mashariki ya Kati kwani njia pekee ya kuliokoa eneo hili ni kueneza moyo na fikra hii."
Ayatullah Khamenei amewambia watawala wa baadhi ya nchi za Kiislamu kwamba: Nasiha zetu kwenu ni kwamba, rudini katika utawala wa Uislamu na muwe chini ya utawala wa Allah kwa sababu utawala wa Marekani na taghuti hautakuwa na faida kwenu.
Kadhalika ameashiria baadhi ya nchi za eneo hili ambazo badala ya kufuata mafundisho ya Uislamu na Qur'ani, zinaifuata Marekani na kusema: Kwa kuzingatia dhati yake ya kibeberu, Marekani inazidhalilisha nchi hizo, na kama ambavyo kila mtu ameshuhudia, Rais mpayukaji wa Marekani amewafananisha watawala wa Saudia na "ng'ombe anayekamuliwa maziwa".
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja udhalilishaji huo wa Rais wa Marekani kuwa unawavunjia heshima raia wa Saudia na mataifa ya Waislamu katika eneo la Mashariki ya Kati na kuongeza kwamba, baadhi ya watawala wa nchi za Kiislamu wanashirikiana na Marekani katika kufanya jinai huko Palestina na Yemeni na kwamba, hata hivyo wananchi madhlumu wa Palestina na Yemen wataibuka washindi, na Marekani na vibaraka wake watafeli na kushindwa katika kadhia hii.
Ayatullah Ali Khameneni amesema kuwa uwezo wa Marekani na utawala haramu wa Israel katika eneo la Mashariki ya Kati umedhoofika zaidi kuliko hapo awali na kuongeza kwamba: Miaka kadhaa iliyopita Israel ilishindwa na harakati ya Hizbullah baada ya vita ya siku 33, miaka miwili baadaye ilistahamili kwa siku 22 tu mbele ya Wapalestina na katika vita na Wapalestina wa eneo la Ukanda wa Gaza haikuweza kustahamili isipokuwa kwa siku nane tu. Ayatullah Khamenei amesema wiki iliyopita Israel ilishindwa na wanamapambano wa Palestina baada ya mapigano ya muda wa siku mbili tu na kushindwa huko kunaonyesha udhaifu endelevu wa utawala huo wa Kizayuni.
Ameashiria suna na kanuni ya Mwenyezi Mungu ya kuyasaidia mataifa yanayokabiliana na kusimama kidete dhidi ya madola ya kibeberu na kusema: Huko Yemen pia taifa la nchi hiyo na harakati ya Ansarullah itapata ushindi licha ya mashaka makubwa na masaibu yanayowapata watu wa nchi hiyo kutokana na jinai zinazofanywa na Aal Saud na washirika wake kwa msaada wa Marekani. 
Vilevile amesisitiza kuwa, kwa mujibu wa kanuni hiyo ya Mwenyezi Mungu, hapana shaka yoyote kwamba, taifa la Palestina litaibuka na ushindi na kuongeza kuwa: Sababu ya kiwewe cha Marekani na washirika wake, bwabwaja, dhulma na jinai zao ni kusimama kidete na mapambano ya mataifa ya Waislamu katika eneo la Mashariki ya Kati na mapambano hayo hatimaye yatapata ushindi. 
Vilevile ameashiria muqawama na mapambano ya miaka 40 ya wananchi wa Iran licha ya matatizo na mashinikizo yote na kusisitiza kwamba, Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel zinakosea kwa kulitisha taifa la Iran.
Ayatullah Ali Khamenei amezungumzia pia kufeli kwa sera za vitisho na vikwazo za Marekani mkabala wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema: Kwa baraka za mapambano yake na chini ya imani yake kwa Mwenyezi Mungu na itikadi yake kuhusu ahadi za Allah SW, taifa la Iran limesimama kidete mbele ya njama zote mithili ya jabali kubwa. Amesema hii leo Jamhuri ya Kiislamu na taifa la Iran ni mti mzuri unaopata maendeleo siku baada ya siku na uwezo wake unaongezeka kila uchao; na hiki ndicho kigezo bora cha maendeleo kwa ajili ya ulimwengu wa Kiislamu. 
Mwishoni mwa hotuba yake, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa umoja, mshikamano na kauli moja ya ulimwengu wa Kiislamu ndiyo njia pekee ya kushinda njama zote za maadui.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Rais Hassan Rouhani pia alihutubia hadhara hiyo akimtaja Mtume Muhammad (saw) kwamba alikuwa mpole na mnyenyekevu kwa watu wote. Amesema kuwa, Mtume (saw) ana haki kubwa ya kihistoria kwa wanadamu wote ikiwemo jamii ya wanawake kwa sababu aliwapa haki ya kutoa maoni ilhali hadi kufikia karne iliyopita wanawake hawakuwa na haki hiyo hata huko Ulaya.
Rais Rouhani ameitaja Madinatun Nabii (mfumo wa jamii ya Kiislamu ya mji wa Madina ulioasisiwa na Bwana Mtume) kuwa ni kigezo bora zaidi cha jamii ya Kiislamu na kusema: Japokuwa makafiri walimkufurisha Mtume na kumuwekea vikwazo vya kiuchumi na kumzingira yeye na masahaba zake, lakini mtukufu huyo alistahamili mashaka hayo yote na katu hakusalimu amri mbele yao.
Rouhani amesema kuwa hii leo baadhi ya watu wanaotumia nara ya kukufurisha Waislamu wenzao wamechafua usalama wa jamii na eneo zima la Mashariki ya Kati na wanatumia jina la Uislamu na Qur'ani kuangamiza roho za watu, usalama na turathi za ustaarabu.
Amesema njama zinazofanywa na mabeberu kwa ajili ya kuvuruga amani na usalama Mashariki ya Kati wakitumia vibaraka wao wa kitakfiri na kutaka kulishinikiza taifa kubwa la Iran kupitia njia ya vikwazo zitafeli na kushindwa. Ameongeza kuwa, wabaguzi wanaendelea kuwaua kwa umati raia wa Palestina kila siku na kuwashambulia kwa mabomu raia wa Yemen.
Vilevile ameashiria ushirikiano uliopo baina ya makundi yenye misimamo mikali ya Kikristo, Kiyahudi na baadhi ya Waislamu na kusema kuwa, maadui wanataka Iran iwe na mwenendo ule ule wa kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini na isiwatetee watu wanaodhulumiwa, lakini Jamhuri ya Kiislamu inayomfuata Mtume Muhammad (saw) haiogopi matakfiri na madola ya kibeberu. 
Rais Rouhani amesisitiza kuwa, Iran inawatambua majirani zake kuwa ni ndugu na kwamba, usalama na amani ya eneo hili ni amani na usalama wake na inanyoosha mkono wa udugu kwa Waislamu wote duniani.

700 /