Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu:

Vita vya sasa duniani ni "Vita vya Irada"

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu mapema leo ameonana na kuhutubia hadhara ya wanamichezo wa Iran waliotwaa medali na washindi wa michezo ya Parasia 2018 iliyofanyika nchini Indonesia. Amewapongeza wanamichezo walemavu na vilema wa vita waliotwaa medali katika michezo hiyo na kusema ushindi huo unaakisi azma kubwa na kutumia uwezo uliojificha. Amewaambia wanamichezo hao kwamba: Kazi kubwa mliyoifanya ni kwamba, mumeonesha kuwa, iwapo uwezo uliopuuzwa ndani ya nafsi ya mwanadamu au ndani ya nchi utatumiwa ipasavyo unaweza kutengeneza mazingira mazuri ya maendeleo na mafanikio makubwa.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema msafara wa wanamichezo vilema na walemavu wa vita wa Iran katika michezo ya Parasia umelifaharisha taifa la Iran na kuongeza kuwa: Mashindano ya michezo yana thamani kwa kila nchi kwa kadiri kwamba, baadhi ya nchi zinaweka masuala ya siasa katika michezo hiyo licha ya kaulimbiu inayosisitiza kuwa, michezo haipasi kutumiwa kisiasa. Amesisitiza kuwa, kupata medali vilema wa vita na walemavu katika mashindano ya michezo kunadhihirisha thamani na azma kubwa.
Ayatullah Khamenei amesifu kitendo cha wanamichezo hao kumshukuru Mwenyezi Mungu pale wanapotunukiwa medali zao na kusisitiza kuwa: Tatizo kuu la watu waovu ni kughafilika na Mwenyezi Mungu, na hapana shaka kwamba, kuona washindi wa medali wa msafara wa michezo ya Parasia wa Iran wakiinua mikono juu au kuanguka chini na kusujudu wakimshukuru Mwenyezi Mungu baada ya kupata ushindi ni hatua yenye thamani kubwa ambayo bila shaka inaanda mazingira mazuri ya kupata ushindi zaidi.  
Ayatullah Khamenei amesema, moyo wa kujiamini walionao wanamichezo majeruhi wa vita na walemavu na hasa wanamichezo wa kike, katika kulinda thamani na tunu zao za kidini na kitaifa ni hatua muhimu sana na ya kupongezwa na akaongezea kwa kusema: Kubebwa bendera ya msafara wa wanamichezo wa Iran na mwanamama aliyevaa hijabu aina ya Chador (buibui la Kiirani), kusimamisha Swala kwa sura ya jamaa na kuhudhuria Swala ya Ijumaa, maana yake ni kusimama imara kwa pamoja kukabiliana na hujuma za mienendo ya maingiliano holela na yasiyo na mipaka ya kijinsia inayozidi kuongezeka duniani na kutosalimu amri mbele ya hujuma hizo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewahutubu wanamichezo hao: Katika hali ambayo, baadhi ya watu wanaoshiriki kwenye medani za kimataifa wanashindwa kusimama kukabiliana na hujuma za matarajio yasiyo na kikomo ya kambi ya ukafiri na uistikbari na kuamua kulegeza misimamo, nyinyi mumesimama imara; na kwa "kuonyesha nguvu za kiutamaduni" mumeilinda hijabu na staha yenu pamoja na vazi lenu la kitaifa na kidini. Kwa sababu hiyo, ninatoa shukurani zangu za dhati na za moyoni kwa msafara wa wanamichezo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
 Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, vita vya sasa duniani ni "Vita vya Irada" na kusisitiza kuwa, kwa harakati yao yenye thamani, wanamichezo majeruhi wa vita na walemavu, wameonyesha kuwa wana uwezo, wanajitegemea kiutamaduni na wana irada na azma imara.
Ayatullah Khamenei amebainisha kuwa, moja ya nukta zenye mafunzo katika ushindi na ubingwa waliopata wanamichezo majeruhi wa vita na walemavu wa Iran ni kutumia uwezo na vipawa vilivyofichika katika nafsi ya mwanadamu na kufafanua kwamba: Miongoni ma matatizo makubwa ya nchi hii katika kipindi cha sasa ni kutotumia vipawa na uwezo mkubwa wa kitaifa kama uwezo wa kijiografia, kibinadamu, rasilimali za chini ya ardhi, biashara na safari za kimataifa.  
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Ikiwa uwezo na vipawa vya taifa vitatumiwa kwa njia sahihi, matatizo mengi ya kiuchumi hapa nchini yatapatiwa ufumbuzi. 
Ayatullah Ali Khamenei amesema: Sisi zote hususan tabaka la vijana tunapaswa kupata ibra na somo kutokana na ushindi wa wanamichezo walemavu na vilema wa vita na tutumie uwezo na vipawa vyetu vilivyojificha ili tuweze kupata maendeleo na ufanisi hapa duniani na huko Akhera.
Amekitaja kitendo cha mwanamichezo vilema wa Iran kushinda medali sita katika mchezo wa kuogelea kuwa kinatoa ilhamu na ni mfano wa wazi wa kutumia uwezo na vipawa vya ndani ya nafsi. 
Msafara wa wanamichezo wa Iran walioshiriki kwenye Michezo ya Tatu ya mashindano ya Parasia 2018 yaliyofanyika nchini Indonesia umejinyakulia jumla ya medali 136, zikiwemo 51 za dhahabu, 42 za fedha na 43 za shaba na kushika nafasi ya tatu katika mashindano hayo.
 

700 /