Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Amiri Jeshi Mkuu:

Jizatitini ili maadui wasithubutu kutoa vitisho dhidi ya Iran

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi Ayatullah Sayyid Ali Khamenei leo amekutana na makamanda na wakuu wa Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema, rasilimaliwatu ya vijana waumini na wenye ari kubwa ndio ufunguo wa kutatulia matatizo katika sekta zote nchini vikiwemo vikosi vya jeshi. Ametilia mkazo udharura wa kufanya kazi kwa bidii na kuzidisha utayarifu wa vikosi vya jeshi na kusema: Jizidisheni uwezo wenu kadiri muwezavyo ili maadui wasithubutu hata kutoa vitisho dhidi ya taifa la Iran. 
Katika mkutano wake na makamanda na wakuu wa jeshi hilo kwa mnasaba wa Siku ya Jeshi la Wanamaji, Ayatullah Khamenei ameashiria jinsi kambi kubwa ya maadui na washindani ilivyojipanga kukabiliana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kueleza kwamba: Kuwepo kwa hali hii halisi sambamba na udharura wa kufidia hali ya kubaki nyuma kimaendeleo, vinadhihirisha ulazima uliopo wa kuchapa kazi kwa kiwango cha juu zaidi ya kawaida katika sekta zote za Jamhuri ya Kiislamu ikiwemo ya Jeshi la Wanamaji.
Amesisitiza kwa kusema: Ongezeni kiwango cha uwezo wenu na utayari wenu kadiri muwezavyo ili maadui wa Iran wasiwe na uthubutu hata wa kutoa vitisho dhidi ya taifa adhimu la Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, kutegemea rasilimaliwatu ya damu changa ya vijana waumini na wenye ari kubwa ndio ufunguo wa kutatulia matatizo katika sekta zote nchini ikiwemo ya vikosi vya ulinzi na akasisitizia ulazima wa kuchapa kazi zaidi na kuongeza kiwango cha utayarifu.
Kiongozi Mudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesema: Mafanikio na hatua lilizopiga jeshi, na hasa vikosi vya majini tangu mwanzoni mwa Mapinduzi ya Kiislamu hadi leo hii ni makubwa na ya kustaajabisha na akaongezea kwa kusema: Kizazi cha sasa cha jeshi la wanamaji kina imani ya dhati kwa ubunifu na vipawa kilivyonavyo; na kujumuishwa manuwari angamizi ya Sahand na nyambizi za Fateh na Ghadir kwenye vyombo vya jeshi la majini kunatoa bishara ya uwezekano wa kupatikana maendeleo zaidi kadiri siku zinavyosonga mbele.
Ayatullah Khamenei amebainisha pia kwamba kuwa tayari zaidi vikosi vya ulinzi vya Iran kutalipa kinga taifa ya kutoweza kushambuliwa na kuwatia hofu maadui. Ameongeza kwa kusema: Jamhuri ya Kiislamu haikusudii kuanzisha vita dhidi ya mtu yeyote lakini inapaswa kuongeza na kuimarisha uwezo wake ili si tu adui awe na woga na hofu ya kuishambulia Iran, lakini kwa baraka za mshikamano, nguvu na uwepo athirifu wa vikosi vya ulinzi katika medani, wingu la vitisho pia liwe mbali na anga ya taifa la Iran.
Kabla ya hotuba ya Amiri Jeshi Mkuu, Kamanda wa Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Admeri Hossein Khanzadi alitoa ripoti kuhusu utayarifu wa manuwari ya Sahand, ukarabati wa manuwari ya Damavand na utengenezaji wa nyambizi ya Fateh unaofanywa na vijana na wataalamu wa Iran na kusema: Jeshi la Majini linafanya jitihada za kusasisha taasisi hiyo na kuwa dhihirisho la uwezo na nguvu ya taifa la Iran la majini. 
Admeri Hossein Khanzadi ameongeza kuwa, Jeshi la Majini la Iran linataka kutoa ilhamu na darsa kwa mataifa huru duniani na kutia kasi katika mwenendo wa kusambaratika mabeberu katika maeneo ya baharini. 
Tarehe 7 Azar (28 Novemba) ni Siku ya Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
 

700 /