Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu:

Iran yenye nguvu na iliyostawi ni ishara ya kufifia nguvu za Mare

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu mapema leo katika mkesha wa Tarehe 13 Aban ambayo ni Siku ya Kitaifa ya Kupambana na Ubeberu, amehutubia hadhara ya maelfu ya wanafunzi wa shule na vyuo vikuu na kupongeza mahudhurio makubwa ya wananchi katika shughuli isiyo na kifani na kustaajabisha ya Arubaini ya Imam Hussein (as). Amesema matukio matatu ya mwezi Aban mwaka 1343, 1357 na 1358 Hijria Shamsia ni ishara ya mpambano mkubwa na wa daima baina ya taifa la Iran na Marekani. Ameashiria suala la kufeli 'Shetani Mkubwa' (Marekani) katika njama zake za miaka 40 iliyopita dhidi ya Iran yaani kushindwa kuidhibiti tena Iran kama ilivyokuwa katika kipindi cha utawala wa kidhalimu wa Shah hapa nchini na kusema: Kufifia nguvu za Marekani ni ukweli ambao wataalamu duniani wanakubaliana nao, na katika upande mwingine wa mpambano huo taifa la Iran litakuwa na mustakabali bora na unaong'aa zaidi kutokana na mori, bidii na jitihada za vijana wake.
Mwanzoni mwa mkutano huo Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amewapongeza wale waliopata taufiki ya kushiriki katika shughuli ya Arubaini ya Imam Hussein (as) na kusema: "Wamagharibi wanashindwa kuelewa na kuchambua tukio hilo lisilo la kawaida; kwa miaka kadhaa walikhitari kutumia mbinu ya kunyamaza kimya kuhusu harakati adhimu ya Arubaini lakini mwaka huu wamelazimika kuizungumzia kwa kiasi fulani lakini kwa uchambuzi wa kihasama, usio sahihi na wa kipumbavu."
Amesema kuwa matembezi na maandamano makubwa ya Arubaini ya Imam Hussein (as) yamewatia kiwewe Wamagharibi na kuongeza kuwa: Vyombo vya habari vya Magharibi kama redio ya Uingereza, vimedai kuwa shughuli hiyo inapangwa na serikali lakini swali la kuuliza ni kwamba, ni serikali ya nchi gani inayoweza kuwafanya watu baina ya milioni 10 na milioni 15 watembee masafa yasiyopungua kilomita 80 kwa miguu? 
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, harakati ya Arubaini ya Imam Hussein (as) haiwezi kuwepo bila ya upendo, imani na kuchemka kwa damu ya mashahidi wenye daraja ya juu na hakuna jambo lolote jingine linaloweza kutengeneza harakati adhimu kama hii.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa harakati ya Arubaini ya Imam Hussein (as) inaboreka na kuwa kubwa zaidi mwaka baada ya mwingine na ameishukuru serikali na taifa la Iraq na vilevile wanasiasa na wakuu wa Iraq kutokana na ukarimu wao mkubwa. 
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria matukio matatu ya tarehe 13 Aban ambayo yanahusiana na Marekani kwa njia moja au nyingine na kusema: Tukio la kwanza ni lile la mwaka 1343 Hijria Shamsia linalohusiana na kupelekwa uhamishoni hayati Imam Ruhullah Khomeini baada ya kupinga sheria iliyokuwa ikiwapa kinga raia wa Marekani kufikishwa mahakamani nchini Iran (Bill of Capitulation). Tukio la pili ni la mauaji ya wanafunzi na vijana yaliyofanywa mwaka 1357 Hijria Shamsia na utawala kibaraka kwa Marekani wa Shah, na la tatu ni lile la mwaka 1358 la wanafunzi kuteka na kudhibiti pango la ujasusi la Marekani nchini Iran (ubalozi wa Marekani mjini Tehran), ambalo kwa hakika lilikuwa pigo kubwa la taifa la Iran dhidi ya Marekani. 
Amekitaja kipigo hicho cha taifa la Iran dhidi ya Marekani kuwa ni matokeo ya nguvu na uwezo ambao Mapinduzi ya Kiislamu yamewapa wananchi wa Iran na kuongeza kuwa: Jumla ya matukio hayo matatu ni kielelezo cha changamoto na mpambano uliopo baina ya Iran na Marekani ambao umeendelea katika kipindi chote cha miaka 40 iliyopita, na katika mpambano huo, Wamarekani wametumia harakati na uadui wa aina mbalimbali (dhidi ya taifa la Iran).   
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyataja "mashambulizi ya Tabas", "kumchochea Saddam aingie vitani dhidi ya Iran", "shambulizi la makombora ya Marekani dhidi ya ndege ya abiria ya Iran katika maji ya Ghuba ya Uajemi" na "mashambulizi dhidi ya visima vya mafuta" vya Iran kuwa ni mfano wa vita vya kijeshi vya Marekani katika kipindi hicho cha miaka 40 iliyopita. Ameongeza kuwa: Miongoni mwa harakati za Wamarekani dhidi ya Iran katika kipindi hicho ni kutumia "vita vya kiuchumi"; na madai ya Wamarekani yanayosema kwamba, vikwazo vyao dhidi ya taifa hili ni hatua mpya dhidi ya Iran kwa hakika ni kujidanganya au kulidanganya taifa la Marekani, kwa sababu vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran vimekuwa vikitekelezwa tangu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa, miongoni mwa nyenzo zilizotumiwa na Marekani dhidi ya Iran katika kipindi chote cha miaka 40 iliyopita ni vita vya kipropaganda na vyombo vya habari. Ameongeza kuwa, vita vya vyombo vya habari vya Marekani kwa maana ya kueneza uongo, kuzusha fitina, kueneza ufuska na kuchochea watu vimekuwepo tangu mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran ingawaje hii leo vinatumbia mbinu mpya zaidi kwa kutumia mitandao ya kijamii. 
Amemalizia sehemu hii ya hotuba yake kwa kusisitiza kuwa, katika mpambano wa miaka 40 iliyopita baina ya Marekani na Iran kumekuwepo uhakika muhimu ambao wakati mwingine umefichikana nao ni kwamba, mshindi amekuwa Jamhuri ya Kiislamu, na mshindwa ni Marekani. 
Akieleza sababu ya ukweli huo, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Lengo kuu la Marekani katika kipindi chote cha miaka 40 iliyopita lilikuwa kuidhibiti tena Iran lakini haikuweza kutimiza lengo hilo licha ya juhudi na njama zote zilizofanyika katika uwanja huo.
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, hii leo nchi pekee ambayo Marekani haiwezi kuwa na nafasi ya aina yoyote katika maamuzi yake ni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na suala hili lina maana ya kushindwa kwa Marekani.
Ameitaja sababu kuu ya hatua ya Marekani ya kumchochea Saddam Hussein dhidi ya Iran katika vita vya kutwishwa vilivyoendelea kwa kipindi cha miaka 8 kuwa lilikuwa kutoa pigo na kuvunja hadhi na heshima ya Jamhuri ya Kiislamu duniani na kusisitiza kuwa, katika vita vya miaka 200 iliyopita Iran daima ilikuwa ikishindwa, lakini katika vita vya kutwishwa vya miaka 8 Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliweza kumshinda adui na haikuruhusu hata shibri moja ya ardhi yake itwaliwe na wageni.  
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema lengo la vita vya kiuchumi vya Marekani dhidi ya Iran katika kipindi chote cha miaka 40 ya baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu lilikuwa kuilemaza kabisa nchi na kuibakisha nyuma. Ameongeza kwa kusema: Matokeo ya vita hivi vya kiuchumi pia yalikuwa kinyume na matakwa ya Marekani, kwa sababu harakati ya kuelekea kwenye hali ya kujitosheleza na uzalishaji wa ndani imeshika kasi zaidi na hii leo mamia ya makundi ya vijana wenye ari na fikra nzuri wa vyuo vikuu wanafanya kazi kubwa na muhimu hapa nchini. 
Baada ya hapo ameashiria hali ya sasa ya Marekani duniani na kusema: Katika mtazamo mpana zaidi, uwezo na udhibiti wa Marekani duniani unaelekea kufifia na kusambaratika, na Marekani ya sasa ni dhaifu zaidi mara kadhaa kuliko Marekani ya miongo minne ya kabla yake.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria kukiri kwa idadi kubwa ya wanasiasa na wataalamu wa masuala ya jamii duniani kwamba, ‘nguvu laini’ (soft power) ya Marekani imechakaa na kusambaratika na kusema kuwa: "Nguvu laini ya Marekani' kwa maana ya uwezo wa kuzishawishi na kuzifanya nchi nyingine zikubali mitazamo yako, sasa iko katika hali dhaifu zaidi; na tangu alipoingia madarakani rais wa sasa wa Marekani mataifa mbalimbali hata yale ya Ulaya na pia China, Russia, India, Afrika na Amerika ya Latini yanapinga waziwazi maamuzi ya Marekani."
Ayatullah Ali Khamenei amesema: Hivi sasa si tu kwamba, uwezo wa kiroho na nguvu laini ya Marekani inaelekea kufifia na kutoweka, bali pia hatua za rais mwenye vioja wa sasa wa nchi hiyo zimeufedhehesha mfumo wa demokrasia ya kiliberali ambao ndio msingi wa ustaarabu wa nchi za Magharibi. 
Vilevile ameashiria matamshi yaliyowahi kutolewa na mhakiki maarufu duniani akisema kuwa “hali ya sasa ya Marekani ndio kilele cha ukamilifu wa historia ya mwanadamu” na kusema: "Mtaalamu huyo huyo wa masuala ya jamii sasa ametengua kauli yake ya awali na kutoa matamshi yanayoakisi kudhoofika na kufifia kwa Marekani na demokrasia ya kiliberali.”
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema nguvu ngumu (hard power) ya Marekani katika uwanja wa kijeshi na uchumi pia inafifia na kuongeza kuwa: Wanazo zana za kijeshi lakini kutokana na matatizo ya kinafsi ya askari wao kama msongo wa mawazo, kuchanganyikiwa na kutokuwa na imani thabiti, Wamarekani wanalazimika kutumia makampuni ya watenda jinai kama Blackwater ili kutimiza malengo yao katika nchi nyingine.
Vilevile amelitaja deni la kutisha la Marekani na nakisi ya bajeti ya dola bilioni 800 ya nchi hiyo katika mwaka huu kuwa ni miongoni mwa ishara za kuporomoka uchumi wa nchi hiyo. Ameongeza kuwa, Wamarekani wanaficha na kufunika ukweli huo kwa mambo ya kidhahiri na kwa kutumia nara tupu lakini ukweli huo wa kuporomoka uchumi ungali unashuhudiwa. 
Ayatullah Khamenei amezitaka nchi za eneo la Mashariki ya Kati zitilie maanani ukweli kuhusu suala la kufifia uwezo wa Marekani na kusema: "Wale ambao kutokana na himaya ya Marekani wako tayari kusahau kabisa kadhia ya Palestina waelewe kuwa, uwezo wa Marekani unafifia hata katika eneo lake yenyewe, na mataifa mbalimbali sasa yako hai na yameamka. 
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kuendelea kuwepo moyo wa kupigania uhuru na kujitawala baina ya vijana wenye mielekeo tofauti ya kifikra hapa nchini ni ishara nyingine ya kufeli na kushindwa kwa Marekani. Ameongeza kuwa: Licha ya udhibiti wao mkubwa wa vyombo vya habari na vya kipropaganda, Wamarekani hawakuweza kuondoa hali ya kuchukiwa, moyo wa kupigania uhuru na kujitawala na moyo wa mapambano na kupenda kukabiliana na madola ya kibeberu baina ya vijana wa nchi hii kwa kadiri kwamba, kizazi cha vijana wa sasa kiko mbele zaidi ya kizazi cha awali cha Mapinduzi kwa kuwa na ari na moyo mkubwa zaidi wa kupambana na kusimama kidete.
Ayatullah Ali Khamenei ameashiria suala la kuenea moyo wa kupigania uhuru na kujitawala wa vijana wa Iran katika nchi nyingine na kusema kuwa: Watu na vijana wa Iraq, Syria, Afghanistan, Pakistan na nchi nyingine wanaichukia Marekani kutokana na tabia yake ya kibeberu na udhalilishaji wake, lakini maafisa wa Marekani wasiokuwa na uwezo wa kuelewa sababu ya chuki hiyo, wanaiona kupitia kwenye macho yetu.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema katika uwanja huo kwamba: Wamarekani wanatutisha na kutuma ujumbe kwamba "Iwapo vijana wa nchi fulani watashambulia askari au wafuasi wetu, tutaitambua Iran kuwa ndiyo mkosaji"; hata hivyo sisi tunasema kuwa, mtakuwa mmekosea kuitambua Iran kuwa ndiye mhusika, badala yake mnapaswa kutazama hatua zenu zinazosababisha chuki na hasira katika nchi hizo.  
Ayatullah Khamenei amekumbusha uhakika wa kufifia Marekani kwa wale wenye mielekeo ya kuwa na mapatano na serikali ya Washington na kusisitiza kuwa: Msipoteze wakati wenu kubuni mipango isiyo na msingi wala maana kwa sababu kufifia na kutoweka kwa Marekani ni hakika na kweli. 
Amezitaja sababu za kusambaratika Shetani Mkubwa kuwa ni za muda mrefu na zinazofungamana na utendaji wake wa kibeberu katika kipindi chote cha historia ya nchi hiyo na kusema kuwa: Kwa mujibu wa kanuni za Mwenyezi Mungu, Marekani itaangamia na kutoweka katika uga wa nguvu wa kimataifa. 
Baada ya kuzungumzia hali ya Marekani kama upande mmoja wa mpambano mkubwa na wa siku zote baina ya Iran na Marekani, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Katika upande mwingine wa mpambano huo na bila ya kutia chumvi, tunaweza kushuhudia ishara za maendeleo na kuimarika zaidi katika kipindi chote cha miaka 40 iliyopita. 
Amesema kuwepo mamia ya makundi ya vijana wenye fikra pevu, vipawa vikubwa, wavumbuzi na wenye hima kubwa katika nyanja mbalimbali za kifikra, kivitendo na katika sekta ya teknolojia ni ishara ya wazi ya harakati kubwa ya Jamhuri ya Kiislamu katika njia ya kujitegemea kiviwanda na kisiasa. Ameongeza kuwa, vijana hawa hawafikirii kuwa marais, mawaziri au mawakili na hali hii yenye baraka bado inaendelea.  
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea kwa kuwausia vijana wasisahau uhasama na uadui wa Marekani. Amesema kuna udharura wa kuwa makini na macho mbele ya hadaa na tabasamu za uongo za adui na kuongeza kuwa: Wakati mwingine Wamarekani wanasema kwamba,"hatuna tatizo na wananchi wa Iran na vikwazo si kwa ajili ya wananchi lakini tunakabiliana na serikali ya Iran"; huu ni uongo wa kufedhehesha, kwa sababu serikali ya Iran haiwezi kuwepo bila ya wananchi, hivyo hapana shaka kwamba, wanafanya uadui dhidi ya taifa na idara ya wananchi.
Akijibu swali kwamba, kusimama kidete na uadui wa taifa la Iran na Marekani utaendelea hadi lini, Ayatullah Khamenei amesema: "Pale Marekani itakapositisha sera zake za kibeberu itawezekana kuamiliana nayo kama nchi nyingine lakini hilo ni jambo lisolowezekana kwa sababu dhati ya uistikbari ni kueneza ubeberu na kutaka kuzidhibi nchi nyingine."
Nasaha ya pili ya Ayatullah Ali Khamenei kwa vijana ni kueneza na kufafanua fikra ya muqawama na mapambano. Amesema kuwa fikra ya kupambana na kukabiliana na adui aliyejizatiti na mwenye nguvu ni imara na sahihi kinadharia na kivitendo. Ameongeza kuwa: Vijana wanapaswa kufafanua na kuweka wazi lengo kuu la mabeberu, yaani sera za kutaka kuwadhibiti wengine, katika mazingira mbalimbali ili fikra ya udharura na usahihi wa kupambana na kukabiliana na mabeberu ionekana na kueleweka vyema.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa: “Katika upande wa kivitendo pia sisi tunatambua kuwa, mapambano ni haki ya vijana wa Iraq, Syria, Lebanon, nchi za kaskazini mwa Afrika, Asia na maeneo mengine, na kuimarisha harakati hizo ni kuimarisha kambi ya muqawama na mapambano.”
Agizo la mwisho la Ayatullah Khamenei kwa vijana azizi wa Iran ni kutekeleza majukumu yao kuhusu suala la maendeleo na ustawi wa taifa. 
Amesema kuwa ‘kigezo cha Kiislamu-Kiirani cha maendeleo’ katika kipindi cha miaka 50 ijayo ambacho kimekabidhiwa kwa wasomi na wanafikra kwa ajili ya kukamilishwa, ni mpango uliobuniwa kwa fikra makini. Ameongeza kuwa, vijana wanapaswa kujihesabu kuwa ni sehemu ya mpango huo mpana wa miaka khamsini na wajiweke tayari kwa ajili ya kutoa mchango wao katika nyanja mbalimbali za kisayansi, kiteknolojia, kiuchumi, kijamii na kisiasa kwa kutilia maana hali ya zama zao.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, suala la kukata kabisa utegemezi wa uchumi wa nchi kwa pato la mafuta ni miongoni mwa masuala yanayoshughulisha daima fikra zake na za wataalamu wa uchumi hapa nchini na amewataka vijana wenye imani, fikra pevu na wachapakazi kubuni njia ya ufumbuzi katika uwanja huo.
Ayatullahi Khamenei amesema kuwa, mtindo wa maendeleo na ustawi wa Iran haukuchukuliwa au kuiga vigezo vya ustawi vya Magharibi. Ameongeza kuwa: “Tunatumia teknolojia ya kisasa kwa kiwango kikubwa lakini tunajua kwamba, modeli na mtindo wa Kimagharibi, kinyume na sura na muonekano wake wa kung’aa, una matatizo ya kidhati na batini yake na umezisababishia mashaka na matatizo nchi mbalimbali.”
Amesema kuwa, hima kubwa ya vijana kwa ajili ya kutatua mambo mbalimbali ni miongoni mwa mahitaji muhimu ya nchi na kuongeza kuwa: Vijana wanapaswa kuyapa kipaumbele masuala ya kubuni na kugundua mambo mapya bila ya kuwa na woga wala ugoigoi na watekeleze majukumu yao kwa ari na moyo wa kitaifa kwa ajili ya maendeleo, ufanisi na fahari ya taifa na usalama wa nchi hii.  
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amewataka maafisa wa nchi kuwajali na kuwapa umuhimu vijana wenye ari na kusema: Wakati mwingine kumeonekana kwamba, baadhi ya taasisi husika hazisaidii kazi nzuri, kubwa na zenye ufumbuzi za vijana. 
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amehitimisha hotuba yake kwa kusema: Hapana shaka kuwa, mustakbali wa nchi hii utakuwa wa kung’aa na bora zaidi kuliko ilivyo hivi sasa na iwapo taifa litaendelea mbele kwa moyo na bidii hii, Iran itafika kwenye kilele cha ustawi na maendeleo katika kipindi si kirefu kijacho na kuwa katika nafasi za juu katika mahusiano ya kimataifa; wakati huo vijana wataonja matunda ya maendeleo hayo makubwa ambayo yatapatikana kwa baraka za Uislamu na Mapinduzi ya Kiislamu.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, wawakilishi wa wanafunzi, mabwana Muhammad Saber Baghkhani na Murtadha Azizi walitoa hotuba fupi wakieleza mitazamo yao na kusisitiza udharura wa kusimama kidete na kupambana na njama za ubeberu kwa moyo wa kimapinduzi na kwa kutegemea uwezo wa vijana hapa nchini.   
 

700 /