Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Salamu za rambirambi za Kiongozi Muadhamu:

Waovu waliotekeleza mauaji hayo wamejitumbukiza katika moto wa ghadhabu za Mwenyezi Mungu

Kwa jina la Allah, Mwingi wa rehma Mwenye kurehemu.

Tukio la kusikitisha la kigaidi nchini Iraq na kuuawa shahidi kidhalimu watu waliokwenda kuzuru haram ya Imam Hussein (as) kumezijeruhi na kuzitia majonzi nyoyo za wapenzi wa Watu wa Nyumba ya Mtume zinazoiona saada na ufanisi katika kumfuata Mtume Muhammad (saw) na Ali zake. Wahalifu waliotekeleza kitendo hicho kiovu na jinai hiyo kubwa wanapaswa kutambua kwamba, wamefadhilisha radhi za mashetani wa majini na watu badala ya ridhaa za mawalii wa Mwenyezi Mungu na kujitumbukiza katika moto wa ghadhabu za Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu na kahari, "Na hakika Jahannamu imewazunguka makafiri" (Tauba:46). Mikono michafu na bongo za shari zilizoasisi ugaidi huo kipofu na usiodhibitika huko Iraq zinapaswa kuelewa kwamba moto huo pia utazikumba na nia yao mbaya itazibana zaidi koo zao kuliko watu wengine, kama ilivyokuwa kwa baadhi ya nchi za Kiislamu.

Mtuhumiwa mkuu wa jinai hizo na mfano wake ni wanajeshi na askari usalama wa Marekani walioivamia kidhalimu na kuikalia kwa mabavu nchi ya Kiislamu ya Iraq kwa kisingizio cha kukabiliana na ugaidi na kuua makumi ya maelfu ya watu nchini humo na kuitumbukiza zaidi kwenye machafuko siku baada ya siku.

Kukua na kustawi kwa nyasi zenye sumu za ugaidi huko Iraq bila shaka kunaandikwa katika faili jeusi la jinai za Marekani na vyombo vya upelelezi vya nchi hiyo na Marekani pamoja na Israel ndio watuhumiwa wakuu wa jinai hizo.

Inatarajiwa kuwa serikali ya Iraq itakabiliana vilivyo na jinai hizo na kudhamini kikamilifu usalama wa watu wanaokwenda kuzuru maeneo matakatifu.

Watu waliouawa katika tukio hilo ni mashahidi wa haram ya Imam Hussein (as) na ujira wao uko kwa Mwenyezi Mungu azizi na mrehemevu inshaallah. Hata hivyo nyoyo za wafiwa na wapenzi wa watu waliouawa shahidi zimejawa na majonzi.

Ninatoa mkono wa pole na salamu za rambirambi kwa watu wote walioathiriwa na tukio hilo hususan familia na waliofiwa. Vilevile namuomba Mwenyezi Mungu Manani awape shifaa majeruhi wa tukio hilo.

Sayyid Ali Khamenei

4/Ordibehest/1388

25 Aprili/2009       

 

700 /