Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Mudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Wananchi Azizi wa Kurdistan Wanapaswa Kuwatambua Vizuri Maadui Zao

Ayatullah Ali Khamenei ametuma salamu za rambirambi na pongezi kwa wananchi kufuatia tukio la mauaji ya kigaidi la kuuawa shahidi Mamusta Sheikhul Islam, mwakilishi wa wananchi wa mkoa wa Kurdistan katika Baraza la Wataalamu wa Kumchagua Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Matini ya ujumbe wa Kiongozi Muadhamu ni hii ifuatayo:
Kwa jina la Allah, Mwingi wa rehma Mwenye kurehemu.
ومن قتل مظلوما فقد جعلنا لوليه سلطانا
Na mwenye kuuawa kwa kudhulumiwa basi tumempa nguvu mrithi wake (juu ya muuaji….(Israa-33)
Kwa masikitiko na huzuni kubwa nimepokea habari kuwa wahalifu na vibaraka wa ubeberu wasiopenda maendeleo wamemuuwa shahidi mwanazuoni mpiganaji jihadi, alimu na mtumishi hodari janabi Mamusta Sheikhul Islam, mwakilishi wa wananchi wa Kurdistan katika Baraza la Wataalamu wa Kumchagua Kiongozi Muadhamu. Marehemu Mamusta ambaye alikuwa mtu sharifu na mchapakazi, amepata daraja ya juu ya kuuawa shahidi na majeshi ya batili baada ya miongo kadhaa ya kutetea haki. Katika siku kadhaa zilizopita pia wanazuoni wengine azizi akiwemo Imam wa muda wa Sala ya Ijumaa ya Sanandaj na maafisa wawili wa Chombo cha Mahakama wa mkoa huo, walijeruhiwa au kupata fahari ya kuuawa shahidi. Mfululizo huo wa uovu na ufyonzaji damu tena katika mwezi mtukufu wa Ramadhani na katika kipindi cha karibu na maadhimisho ya siku ya kutetea taifa la Palestina, umeonyesha kwamba watenda jinai hao wanaodai kuwa na ghera ya dini na taasubi za kimadhehebu si tu kwamba wameuvunjia heshima mwezi wa Mwenyezi Mungu, bali pia mashambulizi yao kimsingi yanakidhi matakwa ya vyombo vya ubeberu na baadhi ya nchi ovu za eneo hili ambazo zimejifunga kibwebwe na kuvaa mkanda wa uhasama na uadui. Kushikamana barabara na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kutetea thamani za Kiislamu na kadhia ya Quds tukufu ndiyo dhambi isiyosameheka ya mashahidi na majeruhi hawa, katika mtazamo wa vibaraka watenda jinai na mabwana zao wenye sifa za Kifirauni na mwenendo wa Qaruon.
Baada ya safari ya mwezi Ordibehesh mwaka huu (wa Hijria Shamsia) katika mkoa wa Kurdistan ambako sauti ya umoja na mshikamano wa Kiislamu ilirindima na kusikika kuliko wakati wowote mwingine, vyombo vya ubeberu na udikteta vina nia ya kulipiza kisasi kutoka kwa wananchi wema na waliodhulumiwa wa mkoa huo. Maadui hao makatili hawatofautishi baina ya Mkurdi na Mfarsi au kati ya Shia na Suni. Roho zao mbaya na zilizojaa vinyongo zimemfanyia ukatili na unyama hata mwanazuoni mkongwe shahidi aliyedhulumiwa Mamusta Sheikhul Islam. Laana za Mwenyezi Mungu, Mtume Wake na waumini ziwashukie wafyonza damu hao na duru zinazowasaidia na kupanga harakati zao.
Wananchi azizi wa Kurdistan wanapaswa kuwatambua vizuri maadui zao. Vilevile viongozi wa masuala ya usalama wa mkoa wa Kurdistan wanawajibika kukabiliana kwa nguvu zote na makatili hao wauwaji waliotangaza vita na kulipa kipaumbele cha kwanza suala hilo katika mipango yao.
Sambamba na kutoa mkono wa pole na pongezi kwa wananchi wa mkoa wa Kurdistan hususan familia zilizopatwa na msiba, ninawatakia kila la kheri mashahidi hao hasa shahidi mpenzi Mamusta Shaikhul Islam, nikimuomba Mwenyezi Mungu awaridhie na kuwasamehe madhambi yao na kuwaweka katika daraja za juu peponi.
Sayyid Ali Khamenei
26 Shahrivar 1388 ( 18 Septemba 2009)700 /