Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Ujumbe wa Shukran wa Kiongozi Muadhamu kwa Taifa:

Taifa la Iran Limechukua Uamuzi wa Kufikia Kilele cha Maendeleo na Ufanisi

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran Ayatullah Ali Khamenei leo ametoa ujumbe akiwashukuru wananchi wa Iran kwa kushiriki kwa wingi katika maandamano ya kuadhimisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa: "Marafiki na maadui wanapaswa kuelewa kwamba taifa la Iran limetambua njia yake na kuchukua uamuzi wa kufikia kilele cha maendeleo na ufanisi na litaondoa vizuizi vya aina yoyote katika njia hiyo."

Ujumbe kamili wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni huu ufuatao:

Kwa jina la Allah, Mwingi wa rehma, Mwenye kurehemu.

Ewe taifa kubwa na linalofanya maajabu la Iran!

Kamwe usichoke na bendera yako ipepee juu daima. Salama za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya azma na uelewa usiokuwa na kifani wa taifa la Iran ambalo daima limekuwa likitayarisha ushindi wa haki katika medani za kukabiliana na watu waovu na wasiolitakia kheri na kudhihirisha fahari na heshima ya Iran wakati wa haja.

Shukrani ni za Mola Muumba wa ulimwengu ambaye mkono wa uwezo na kudra yake umedhihiri katika azma na imani yenu na kuonesha zaidi na zaidi nguvu na uhai wa mfumo huu unaotegemea imani na kujiamini kwa taifa kwa maadui katika mwaka wa 31 wa kuzaliwa Jamhuri ya Kiislamu.

Je, miaka 31 ya mtihani na makosa ya nchi kadhaa za kibeberu na kidhalimu haitoshi kuziamsha nchi hizo kutoka kwenye usingizi wa mghafala na kuzifahamisha upuuzi wa juhudi zao za kutaka kuidhibiti Iran ya Kiislamu?

Je, mahudhurio ya makumi ya mamilioni ya watu wenye uelewa na ari katika sherehe za kuadhimisha mwaka wa 31 wa Mapinduzi ya Kiislamu hayatoshi kuwazindua maadui na waliohadaiwa na maadui hao ndani ya nchi ambao mara nyingine wanafanya ria kwa kutoa madai ya "kuwatetea wananchi"? Je, mahudhurio hayo hayatoshi kuwaonesha njia na matakwa ya wananchi ambayo ndiyo njia iliyonyooka ya Uislamu halisi wa Mtume Muhammad (SAW) na njia ya Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu?

Marafiki na maadui wanapaswa kuelewa kwamba taifa la Iran limetambua njia yake na kuchukua uamuzi wake na litaondoa vizuizi vyote njiani kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu na kuegamia katika nguvu liliyopewa na Mola Muweza kwa ajili ya kufikia kilele cha maendeleo na ufanisi.

Ninaliombea auni na taufiki ya Mwenyezi Mungu taifa la Iran, na dua za Imam wa Zama Mahdi (AS) zitakuwa pamoja na taifa hili daima.

Sayyid Ali Khamenei

22 Bahman 1388

11 Februari 2010

700 /