Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Mwaka huu ninauita mwaka wa "Hima Zaidi na Kazi Zaidi

«يا مقلّب القلوب و الأبصار. يا مدبّر اللّيل و النّهار» Ewe Mola unayebadilisha nyoyo na macho ya watu. Ewe Mola unayeendesha usiku na mchana. «يا محوّل الحول و الأحوال» Ewe Mola unayebadilisha miaka na hali. «حوّل حالنا الى احسن الحال» Badili hali zetu na uzifanye bora zaidi.

Ninatoa mkono wa idi ya Nouruzi na kuanza mwaka mpya ambako ni kuanza msimu wa machipuo na maisha mapya ya maumbile, kwa wananchi wote azizi nchini kote na kwa Wairani wanaoishi katika maeneo mbalimbali duniani ambao wanaitazama nchi yao kwa matumaini makubwa; hususan vijana, wanaume na wanawake waliojisabilia kwa ajili ya malengo aali ya Mapinduzi ya Kiislamu na nchi yao. Ninatoa mkono wa baraka kwa Wairani waliojitolea na kutoa mhanga vijana wao kwa ajili ya Mapinduzi ya Kiislamu na maendeleo ya nchi yao. Vilevile ninatoa mkono wa baraka na fanaka kwa familia za mashahidi, kwa waliolemazwa katika vita na familia zao zilizojisabilia na wale wote waliojitolewa na wanaofanya jitihada kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa taifa.

Ninatuma sala na salamu kwa roho takasifu ya Imam Khomeini ambaye alikuwa mstari wa mbele wa harakati hiyo kubwa ya wananchi na kinara wa maendeleo na ustawi wa nchi kubwa ya Iran ya Kiislamu.

Sikukuu ya Nouruzi ni mwanzo wa machipuo. Kama ambavyo machipuo hayo yanahisika katika maumbile, yanaweza pia kudhihiri na kuonekana katika nyoyo na nafsi zetu na katika harakati zetu za maendeleo na ustawi. Hebu na tutazame kwa ufupi mwaka unaomaliza wa 1388. Iwapo tunapaswa kuuarifisha mwaka uliopita katika sentensi moja basi ulikuwa mwaka wa taifa la Iran, mwaka wa adhama na ushindi wa taifa hilo kubwa, mwaka wa mahudhurio ya kihistoria na yenye taathira kubwa ya taifa hilo katika nyanya mbalimbali ambayo yatakuwa na nafasi muhimu katika mustakbali wa Mapinduzi ya Kiislamu na mustakbali wa nchi yetu.

Mwanzoni mwa mwaka uliopita wa 1388 wananchi, kwa mahudhurio yao yasiyokuwa na kifani, walitayarisha uchaguzi wa Rais ambao haujawahi kushuhudiwa katika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu na hata katika historia ndefu ya nchi yetu; hiyo ilikuwa hatua kubwa na muhimu. Katika kipindi cha miezi ya baada ya uchaguzi huo wananchi walishiriki katika mtihani mkubwa na katika harakati adhimu na muhimu na kuonesha irada yao, kusimama kwa kidete, azma yao ya kitaifa na maarifa yao.

Tafsiri fupi inayoweza kutolewa kuhusu matukio ya miezi kadhaa ya baada ya uchaguzi wa Rais hapa nchini ni kuwa, baada ya kupita miaka 30 maadui wa nchi na maadui wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu wamekusanya juhudi na nguvu zao zote kwa ajili ya kutoa pigo dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu kutokea ndani ya nchi. Mkabala wa njama hiyo kubwa na harakati hiyo ya kiadui, taifa la Iran limeweza kumshinda adui kwa kuwa na maarifa, azma na kusimama kidete kwa aina yake. Uzoefu wa kipindi cha miezi 8 ya baada ya uchaguzi huo hadi kufikia tarehe 11 Februari mwaka huu kwa taifa la Iran ni uzoefu uliojaa masomo na ibra na sababu ya fahari ya taifa la Iran.

Katika mwaka 1388 taifa la Iran liling'ara sana na viongozi wamefanya juhudi kubwa na zenye thamani. Juhudi hizo zina thamani katika kiwango chake na zinapaswa kushukuriwa. Ni wajibu kwa wachambuzi wote wenye insafu kusifu na kuthamini juhudi, mashaka, kazi na jitihada kubwa zilizofanyika kwa ajili ya ujenzi, ustawi na maendeleo ya nchi katika nyanja mbalimbali. Viongozi wa taifa wamefanya kazi kubwa katika nyanja za sayansi, viwanda, shughuli za kijamii, katika siasa za nje na medani mbalimbali. Namuomba Mwenyezi Mungu awape malipo mema na taufiki ya kufikia maendeleo.

Hata hivyo, tunapotazama hali ya sasa hapa nchini na uwezo mkubwa wa nchi na taifa hili tunaelewa kwamba mambo tuliyofanya na yaliyofanywa na viongozi na wananchi si makubwa yakilinganishwa na uwezo adhimu wa nchi hii kwa ajili ya maendeleo na kufikia uadilifu. Juhudi zaidi zinapaswa kufanyika, na wananchi wote wanapaswa kuwajibika ipasavyo.

Katika dua hii inayosomwa mwanzoni mwa kila mwaka mpya tunasoma kipengee hiki kinachopaswa kupewa mazingatio:  «حوّل حالنا الى احسن الحال» (badili hali yetu na uifanye bora zaidi). Katika dua hii hatuombi siku nzuri au hali nzuri, bali tunamuomba Mola atupe hali bora zaidi, siku bora zaidi nafasi bora na za juu zaidi. Hivi ndivyo inavyopaswa kuwa hima ya Muislamu; yaani kuwa bora zaidi katika nyanja zote.

Ili tuweze kutekeleza yale tuliyofundishwa katika dua hiyo tukufu, na ili tuweze kupiga hatua kwa mujibu wa uwezo na hali ya nchi hii, mwaka huu tunalazimika kuzidisha hima zetu mara kadhaa na kufanya kazi na bidii zaidi. Mwaka huu nauita "Mwaka wa Hima Zaidi na Kazi Zaidi" nikiwa na matarajio kwamba viongozi pamoja na wananchi wataweza kupiga hatua kubwa zaidi na kwa hima kubwa na kazi zaidi katika nyanja mbalimbali za uchumi, utamaduni, siasa, ujenzi, masuala ya jamii na kadhalika na kukaribia zaidi malengo yao makubwa kwa matakwa yake Allah. Tunahitajia mno hima hiyo kubwa, na taifa linahitaji mno kazi hiyo kubwa.

Tunapaswa kumtegemea Mwenyezi Mungu Mtukufu na kumuomba auni na msaada na kuelewa kwamba, nyanja za kazi ni nyingi. Maadui wetu ni maadui wa elimu na imani ya jamii yetu. Tunapaswa kuimarisha zaidi elimu na imani miongoni mwetu na kwa matashi yake Mola njia zote zitatengemaa, vizingiti vitapungua na msaada na nusra Mwenyezi Mungu itakuwa juu ya taifa, nchi na viongozi wetu.

Wassalamu alaykum warahmatullah wabarakatuh

                  

700 /