Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Mwenendo wa kuzuru maeneo ya kipindi cha vita vya kujitetea kutakatifu unapaswa kudumishwa

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei leo amehudhuria katika sehemu ya kumbukumbu ya operesheni ya Fat'hul Mubiin katika eneo la Dasht Abbas na kuwakumbuka mashahidi na mashujaa wa Uislamu walioshiriki katika operesheni hiyo mwaka 1361 Hijria. Ayatullah Khamenei amewaombea maghfira na daraja za juu za peponi mashahidi wa operesni hiyo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alihutubia umati wa wananchi waliokuwa katika eneo hilo akipongeza kujitolea, kusimama kidete, kuwa macho na ari kubwa ya kizazi cha vijana wa kipindi cha kujitetea kutakatifu na akasema: "Njia pekee ya saada na ufanisi wa taifa la Iran duniani na akhera ni kudumisha mwenendo huo sambamba na kulinda ushujaa, tadbiri, kuona mbali, azma kubwa na imani ya Kiislamu.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa lengo la kuhudhuria kwake katika maeneo ya operesheni za kipindi cha vita vya kujitetea kutakatifu ni kuadhimisha kujitolea na moyo wa kusimama kidete wa wapiganaji wa Kiislamu na mashahidi watukufu na vilevile kukumbuka kujitolea na ushujaa wa wananchi azizi wa Khuzistan (kusini mwa Iran) katika moja ya vipindi na mazingira magumu mno hapa nchini. Amesema kuwa katika kipindi cha vita vya kujitetea kutakatifu wananchi wa mkoa wa Khuzistan walikuwa katika safu ya kwanza ya wapiganaji wa Kiislamu na walishikamana barabara na Iran ya Kiislamu kwa kadiri kwamba hata vishawishi vya kikaumu na kilugha vya adui wa Kibaathi (utawala wa zamani wa Iraq) havikuweza kudhoofisha mfungamano huo madhubuti.

Ayatullah Ali Khamenei ameyataja maeneo ya operesheni za vita vya kujitetea kutakatifu huko kusini mwa Iran kuwa ni maeneo ya kuzuru. Amesema, moja ya malengo ya safari yake katika maeneo hayo ni kuwapongeza watu wanaoyatembelea na kuyazuru. Amesisitiza kuwa suna na mwenendo huo wa kupongezwa na harakati hiyo yenye baraka tele iliyoanza miaka kadhaa iliyopita, inapaswa kudumishwa.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, taifa la Iran kamwe halipaswi kusahau kipindi nyeti, cha kihistoria na chenye fahari kubwa cha vita vya kujitetea kutakatifu, kwani kipindi hicho ni tajiriba yenye thamani kubwa.

Ayatullah Ali Khamenei ameongeza kuwa iwapo vijana wa kizazi cha sasa wangekuwepo katika kipindi cha kujitetea kutakatifu wangehudhuria katika medani za vita hivyo kwa azma ileile kubwa na hii leo vijana wa sasa wamethibitisha ushujaa wao katika medani za elimu na sayansi, siasa, uchapakazi, mshikamano wa kitaifa na maarifa.

Amesema kuwa lengo la maadui wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kuanzisha vita vya kulazimisha lilikuwa kulidhalilisha taifa la Iran na kuimega sehemu ya ardhi ya Iran. Amesisitiza kuwa katika kipindi hicho Marekani, Urusi ya zamani na baadhi ya nchi za Ulaya zinazotoa madai ya kutetea haki za binadamu, zilimsaidia adui muovu wa Kibaathi ili aweze kuushinda utawala wa Kiislamu hapa nchini; hata hivyo vijana wa taifa hili walizima njama za madola hayo ya kibeberu na kumdhalilisha adui kwa kujitolea, azma kubwa na imani yao madhubuti.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kwamba azma kubwa, kuwa macho, kusimama kidete, msimamo imara na ushujaa wa taifa vinaweza kumshinda adui japokuwa kidhahiri ataonekana mkubwa na mwenye nguvu.

Ayatullah Khamenei amesema kuwa uwezo, nguvu na ushawishi wa taifa la Iran katika dunia ya Kiislamu ni mkubwa na mpana zaidi ikilinganishwa na wakati wa vita vya kujitetea kutakatifu. Ameongeza kuwa njama na hila za maadui leo hii pia ni nyingi lakini taifa la Iran linazikenulia njama hizo.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa vita vya kifikra na kisiasa ni vigumu zaidi kuliko vita vya kijeshi na akasisitiza kuwa taifa la Iran limeonesha kwamba kuona mbali na kusimama kwake kidete katika vita vya medani za kifikra na kiusalama ni kukubwa zaidi kuliko hata kusimama kwake kidete katika kipindi cha vita vya kujitetea kutakatifu.

Amesisitiza tena juu ya udharura wa kuwa na hima zaidi na kuchapa kazi zaidi katika nyanja zote na akasema, taifa la Iran linapaswa kufidia kubakia nyuma kimaendeleo katika kipindi kirefu cha utawala wa kidikteta na uingiliaji wa madola ya kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hii.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa vijana wa sasa wa Iran wana mfano nadra mno katika dunia ya leo. Amesema kuwepo vijana hao kunatoa bishara njema kwa mustakbali wa nchi hii. Ayatullah Khamenei amesema kuwa kwa baraka na rehema zake Mola Mtukufu, itakuja siku ambapo vijana wa nchi hii watajionea kwa macho yao Iran ya Kiislamu ikifika daraja ya juu inayostahiki katika nyanja za sayansi, teknolojia, siasa na ushawishi wa kimataifa.

Katika ziara hiyo Ayatullah Ali Khamenei alifuatana na makamanda kadhaa wa ngazi za juu wa jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.                       

700 /