Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu asema katika ujumbe wake kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Kuangamiza Silaha za Nyuklia:

Serikali ya Marekani pekee ndiyo iliyofanya jinai ya kutumia silaha za nyuklia duniani

Bismillahir Rahmanir Rahim

Kwanza kabisa ninapenda kukukaribisheni wageni waalikwa mliokusanyika hapa. Ni jambo la kufurahisha sana kuona kwamba leo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mwenyeji wa Mkutano wa Kimataifa wa Kutokomeza Silaha za Nyuklia. Ni matumaini yetu kwamba fursa hii itatumiwa vizuri na itakuwa na matunda bora na ya kudumu. Ni matumaini yetu pia kuwa mazungumzo na mashauriano mbalimbali yatakayofanyika katika mkutano huu yatakuwa na faida nzuri kwa jamii ya mwanaadamu.

Utaalamu wa atomiki na sayansi ya nyuklia ni moja ya mafanikio makubwa ya mwanadamu ambayo yanaweza, bali inabidi yatumike kwa ajili ya ustawi wa mataifa ya dunia pamoja na maendeleo na ustawi wa jamii zote za mwanaadamu. Teknolojia yenye faida kubwa ya nyuklia inaweza kukidhi mahitaji ya kitiba, nishati na viwanda ambapo kila kimoja kati ya vitu hivyo kina umuhimu mkubwa. Hivyo tunaweza kusema kwamba teknolojia ya nyuklia ina nafasi muhimu sana katika masuala ya kiuchumi na kadiri siku zinavyosonga mbele na kadiri mahitaji ya kiviwanda, kitiba na kinishati yanavyoongezeka ndivyo umuhimu wa teknolojia hiyo unavyozidi kuwa mkubwa. Kadiri mahitaji yanavyokuwa mengi ndivyo umuhimu wa kufanya juhudi za kumiliki teknolojia ya nyuklia na kutumia vizuri teknolojia hiyo ya kisasa unavyozidi kuwa mkubwa. Mataifa ya Mashariki ya Kati ambayo kama yalivyo mataifa mengine duniani yana kiu ya kuwa na amani, usalama na maendeleo, yana haki pia ya kutumia teknolojia hiyo ili kwa njia hiyo yaweze kuvirithisha vizazi vijavyo nguvu za kiuchumi na nafasi bora duniani. Pengine moja ya sababu za kushuhudiwa upotoshaji katika suala la miradi ya amani ya nyuklia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikawa ni hiyo, yaani kuyafanya mataifa ya eneo hili yasifuatilie kwa nguvu zinazotakiwa, haki yao hiyo isiyopingika na yenye umuhimu mkubwa.

Kichekesho kikubwa ni kwamba mhalifu pekee wa atomiki duniani (Marekani) anaeneza uongo akidai kuwa anapambana na uenezaji na usambazaji wa silaha za atomiki wakati ambapo ni jambo lisilo na shaka hata chembe kwamba hajawahi kuchukua hatua yoyote ya maana katika jambo hilo na kamwe hatachukua hatua yoyote ya maana kuhusu madai yake hayo. Kama madai ya Marekani kuwa inapambana na suala la kusambazwa silaha za atomiki duniani si uongo, basi kwa nini utawala wa Kizayuni unaendelea kukaidi sheria za kimataifa kuhusiana na silaha za atomiki hususan mkataba wa NPT, na kwa nini utawala huo umezibadilisha ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina kuwa viwanda vya kutenengezea korija kwa korija za silaha za nyuklia na kuzirundika huko kwa wingi?

Inasikitisha sana kuona kuwa kama ambavyo atomiki ina maana ya kupatikana maendeleo katika maarifa ya mwanaadamu, ina kumbukumbu mbaya pia ya tukio baya sana katika historia nalo ni la kutumiwa vibaya teknolojia hiyo kuangamiza kizazi cha watu. Ijapokuwa nchi nyingi zimechukua uamuzi wa kujilimbikizia na kuzalisha kwa wingi silaha za nyuklia jambo ambalo lenyewe linaweza kuhesabiwa ni utangulizi wa kufanya uhalifu na kuhatarisha vibaya usalama wa dunia, lakini ni nchi moja tu duniani iliyofanya uhalifu wa kutumia silaha hizo. Ni nchi moja tu ya Marekani ndiyo iliyotumia silaha hizo dhidi ya wananchi madhlumu wa Japan huko Hiroshima na Nagasaki katika vita ambavyo havikuwa vya kiadilifu hata kidogo na havikuwa na chembe ya ubinadamu.

Wakati Marekani ilipotumia silaha za nyuklia kwa mara ya kwanza katika historia dhidi ya miji ya Hiroshima na Nagasaki, nchi hiyo ilisababisha maafa makubwa ambayo hayajawahi kushuhudiwa katika historia na ilihatarisha vibaya sana usalama wa mwanaadamu. Ilitarajiwa kuwa baada ya kufanyika uhalifu huo, jamii ya kimataifa ingelichukua uamuzi madhubuti wa kutokomeza kikamilifu silaha za nyuklia. Matumizi hayo ya silaha za nyuklia si tu yalipelekea kutokea mauaji na uharibifu mkubwa, lakini pia silaha hizo hazikuchagua raia wala mwanajeshi, mtoto mdogo wala mtu mzima, mwanamke wala mwanamme, kijana wala kizee na kwamba athari mbaya zisizo za kibinadamu za matumizi hayo zilivuka mipaka ya kisiasa na kijiografia na kuvitia hasara isiyofidika hata vizazi vilivyokuja baada yake. Hivyo matumizi ya aina yoyote ile, bali hata kutishia tu kutumia silaha za nyuklia ni uvunjaji wa wazi kabisa wa sheria za kibinadamu na ni ushahidi wa wazi wa jinai za kivita. Katika upande wa kijeshi pia na baada ya madola kadhaa kumiliki silaha hizo zilizo dhidi ya ubinadamu, sasa imethibitika kwamba haiwezekani kupata ushindi katika vita vya nyuklia na kwamba kupigana vita kwa kutumia silaha hizo ni jambo ambalo haliwezi kukubalika hata kidogo kiakili, bali kufanya hivyo ni kwenda kinyume kikamilifu na haki za binadamu. Lakini licha ya mambo kuwa wazi kiasi chote hicho kimaadili, kiakili, kibinadamu na hata kijeshi, lakini bado madola yanayomiliki silaha za nyuklia hayataki kusikiliza sisitizo la kila leo la jamii ya kimataifa la kutokomeza na kuangamiza silaha za nyuklia kwani madola hayo yamejenga usalama wao bandia juu ya misingi ya kuhatarisha usalama wa watu wote wengine.

Kung'ang'ania madola hayo misimamo yao ya kuendelea kumiliki, kuongeza nguvu na kuzidisha uwezo wa maangamizi wa silaha za nyuklia hakuna faida yoyote isipokuwa kuzusha vitisho, kufanya mauaji ya umati na kuleta usalama kidhabu uliojengeka juu ya stratijia na mikakati ya kuzuia kushambuliwa ambayo kimsingi imesimama juu ya misingi ya maangamizi ya wote yasiyoepukika. Kunatolewa gharama nyingi kwa ajili ya kudhamini vyanzo nje ya masuala ya kiuchumi na kiubinadamu kwa ajili ya kuendeleza ushindani usio wa kimantiki ili kila dola liweze kupata uwezo bandia wa kuweza kuwaangamiza zaidi ya mara elfu wapinzani wao na wakazi wengine wa sayari ya dunia wakiwemo wao wenyewe. Hapana shaka kuwa, ni kwa sababu hiyo ndio maana stratijia hii ya kuepuka kushambuliwa ikaitwa kuwa na ya kiwendawazimu na imesimama juu ya misingi ya kuangamiza kikamilifu upande mwingine.

Baadhi ya madola yanayomiliki silaha za nyuklia yamekwenda mbali zaidi katika stratijia zao za kuzuia kushambuliwa na madola mengine yanayomiliki silaha za nyuklia kiasi kwamba madola hayo hata yamekuwa yakisisitizia suala la kuendelea kumiliki silaha za nyuklia ili yaweze kukabiliana na vitisho vinavyojulikana kutoka kwa wavunjaji wa mkataba wa NPT. Katika hali ambayo wavunjaji wakubwa wa Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Uenezaji wa Silaha za Nyuklia ni madola hayo makubwa ambayo mbali na kutoheshimu ahadi zao katika kifungu cha sita cha mkataba huo, hata yanaonekana kana kwamba kila mmoja anajaribu kumpiku mwenzake katika kueneza silaha hizo ikiwa ni pamoja na kuupatia silaha hizo utawala wa Kizayuni na kuunga mkono siasa za utawala huo. Madola hayo yanachangia moja kwa moja uenezaji wa silaha za nyuklia na yanakwenda kinyume na ahadi zao kama kinavyosema kifungu nambari 1 cha mkataba huo. Madola hayo yamelitumbukiza eneo la Mashariki ya Kati na dunia nzima kiujumla katika vitisho vikubwa ambapo dola lililo mstari wa mbele katika jambo hilo ni utawala wa kibeberu na kiistikbari wa Marekani.

Mkutano wa kimataifa wa kutokomeza silaha za nyuklia unapaswa sambamba na kuchunguza hatari za kuzalisha na kujilimbikizia silaha za nyuklia duniani, uoneshe njia zinazokubalika na za maana za kukabiliana na hatari hiyo inayomkabili mwanaadamu ili kwa njia hiyo kuweze kupigwa hatua ya maana katika njia ya kulinda usalama na utulivu ulimwenguni.

Sisi tunaamini kwamba mbali na silaha za nyuklia, kuna aina nyingine ya silaha za mauaji ya umati kama za kemikali na vijidudu ambazo ni hatari kubwa kwa mwanaadamu. Kabla ya taifa lolote jingine, taifa la Iran ambalo ni muhanga wa matumizi ya silaha za kemikali, linajua vyema hatari ya kujilimbikizia silaha kama hizo na liko tayari kutumia uwezo wake wote katika njia ya kupambana na silaha hizo.

Sisi tunaamini kwamba ni haramu kutumia silaha hizo na tunaamini ni jukumu la kila mtu kufanya juhudi za kuwalinda wanaadamu kutokana na balaa hiyo kubwa.

Sayyid Ali Khamenei

27/Farvardin 1389 Hijria Shamsia

1/Jamadul Awwal 1431 Hijria Qamariya.

700 /